RAIS wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, amewataka watendaji na
wananchi wote kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia misingi ya utawala bora na
kuacha kufanya kazi kwa mazoea.
Dk. Shein aliyasema hayo leo, katika uzinduzi wa Semina ya
Utawala Bora na Uchumi katika ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi,
iliyowashirikisha viongozi wa Wizara na Taasisi mbali mbali za Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar.
Katika hotuba yake, Rais Dk. Shein alisema kuwa Utawala Bora ni
nguzo muhimu katika jitihada za kupunguza umasikini hivyo, kila mmoja ana
wajibu wa kuhakikisha kuwa anajenga na kulinda maadili mema kwa manufaa ya umma
na nchi nzima kwa jumla.
Dk. Shein aliongeza kuwa utawala bora ni suala linalozingatia
misingi ya ufanisi na tija, utawala wa sheria na haki za binaadamu,
ushirikishwaji, kuzingatia maadili, uadilifu uwajibikaji na uwazi na kuzingatia
matakwa ya wananchi.
Aliwataka washiriki wa Semina hiyo wakiwa ni viongozi ni lazima
wajiamini kwamba wanao uwezo wa kutosha wa kuleta mabadiliko ya haraka katika
nafasi walizokabidhiwa kwa kutumia rasilimali zilizopo na kuwataka kuacha dhana
kwamba nchi yao ni changa na haiwezi kufanya mambo makubwa yanayofanywa na nchi
nyengine.
Rais Dk. Shein aliwaeleza viongozi hao kuwa semina hiyo ni
miongoni mwa juhudi za Serikali za kuimaruisha utawala bora, kama alivyoahidi
pamoja na kutoa elimu juu ya mipango mikuu ya maendeleo ya nchi na viongozi
wote ni vyema wakaifahamu mipango hiyo na kushirikiana katika kuitekeleza kwa
mujibu wa malengo ya Serikali na matarajio ya wananchi.
Dk. Shein alisema kuwa Zanzibar imekuwa na historia ya muda
mrefu ya kufuata misingi ya utawala bora; historia ambayo ilianza tangu
Mapinduzi Matukufu ya Zanzar ya 1964. Alifahamisha kwamba baada ya Uchaguzi
Mkuu wa Mwaka 2000, Serikali ilianzisha Wizara maalum ya kushughulikia masuala
ya Utawala bora.
Alieleza kuwa mafanikio makubwa yamepatikana katika jitihada za
kukuza na kuendeleza utawala bora; ambapo Zanzibar imepiga hatua kwa kuanzisha
Taasisi zenye jukumu la kusimamia utendaji wa Wizara, Idara na Taasisi za
Serikali kama vile Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali,
Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu wa Uchumi (ZAECA) Tume ya Maadili ya
Viongozi wa Umma, Ofisi ya Mkurugenzi Mashtaka (DPP).
Aidha, alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatambua
kwamba ili mafanikio yapatikane katika kuimarisha utawala bora ni lazima
Serikali ishirikiane na sekta binafsi, hivyo kwa kutambua hilo Serikali
itaendelea kuhakikisha inaweka mazingira bora yatakayoiwezesha sekta binafsi
kufanya shughuli zake kwa urahisi na ufanisi mkubwa.
Dk. Shein pia, aliwataka viongozi hao kuendelea kupanga na
kutekeleza mikakati inayolenga katika kuondoa urasimu usio wa lazima na aina zote
za uzembe ambazo zinakuwa ni vikwazo katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Alisisitiza dhamira ya Serikali katika kuendeleza matumizi ya
TEHAMA kwa kuweka mifumo imara ya elektroniki katika uendeshaji wa shughuli na
utoaji wa huduma mbali mbali.
Kwa upande wa watumishi wa umma, Rais Dk. Shein alieleza kuwa
bado wapo wafanyakazi wanaochelewa kwenda kazini na pia, wapo wanaotoroka
kazini na ambao viwango vyao vya kufanya kazi haviridhishi na baadhi yao
mkabala wao na maneno yao si mazuri pale wanapowahudumikia wananchi.
Alisema kuwa Serikali imebaini kuwepo vitendo vinavyofanywa na
baadhi ya wafanyakazi ambavyo vinavunja misingi ya utawala bora vikiwemo
rushwa, ghilba, hadaa, wizi na vyenginevyo ambavyo vyote hivyo vinapelekea
wananchi kuanza kuilalamikia Serikali yao.
Pia, Rais Dk. Shein alisema kuwa Serikali imebaini baadhi ya
matatizo ya udanganyifu kwenye mishahara ya wafanyakazi katika baadhi ya Wizara
za Serikali, ulipelekea mishahara kulipwa kinyume na utaratibu.
Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein alieleza kuwa kila kiongozi wa
Serikali ana wajibu wa kuyafahamu mambo yaliyoelezwa kwenye MKUZA III, Ilani ya
CCM ya Uchaguzi Mkuu ya mwaka 2015-2020, Dira ya Maendeleo 2020, Malengo ya
Maendeleo Endelevu pamoja na Sheria mbali mbali zilizobainishwa kwenye Katiba
na zile zinazohusu sekta wanazozisimamia.
Rais Dk. Shein alitaka
kila kiongozi kuhakikisha kuwa anazo nakala za nyaraka hizo muhimu katika ofisi
yake kama nyenzo za kufanyia kazi.
Hata hivyo, Rais Dk. Shein aliwaakumbusha viongozi hao kuweka
mkazo maalum katika sekta ya mafuta na gesi katika mipanago ya maendeleo
itakayoanza mwaka 2020.
Katika uzinduzi huo, pia, Rais Dk. Shein alizindua jarida la
Utawala Bora pamoja na kuzinudia Jarida la Mkakati wa Kuzuia Ruswa.
Nae Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi wa
Umma na Utawala Bora Haroun Ali Suleiman alipongeza juhudi za Rais wa Zanzibar
katika kuendeleza Utawala Bora hapa nchini.
Mapema Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk.
Abdulhamid Yahya Mzee alieleza kuwa ili kutekeleza mipango ya maendeleo utawala
bora unahitajika kwa kiasi kikubwa hatua ambayo pia inapelekea kuwa na uchumi
imara.
Katika Semina hiyo mada mbali mbali zilitolewa zikiwemo Dhana ya
Utawala Bora, Katibu Tume ya Maadili ya Viongozi wa Ummma, Dhana ya Utawala
Bora Katika Mtizamo wa Dini, Utawala Bora na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu
wa Hesabu za Serikali, Mgngano wa Maslahi katika Utumishi wa Umma, MKUZA III
2016-2020, Ufuatiliaji wa Tathmini ya MKUZA III na Mwenendo wa Uchumi wa
Zanzibar kuelekea mwaka 2020.
CHANZO: IKULU ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment