Wednesday, March 14, 2018

ZPC YAKUNWA NA UTEUZI WA RAIS DK. SHEIN, KAMATI KUKUTANA MACHI 15

NA MWINYIMVUA NZUKWI

Klabu ya waandishi wa habari Zanzibar (ZPC) imempongeza Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein kwa hatua yake ya kuwateua wanachama wa muda mrefu wa klabu hiyo Dk. Saleh Yussuf Mnemo na Abdullah Hassan Mitawi kuwa Manaibu Makatibu Wakuu katika Wizara ya habari, utamaduni na Mambo ya kale na Ofisi ya Makamo wa pili wa Rais wa Zanzibar hatua inayoonesha imani kwa tasnia ya habari nchini.

Naibu Katibu Mkuu wizara ya Habari, utalii na mambo ya kale (habari) Dk. Saleh Yussuf Mnemo (kulia) akila kiapo mbele ya Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa klabu hiyo Faki Mjaka kwa vyombo vya habari jana, imeeleza kuwa ZPC imeguswa na uteuzi huo na kuutaja kuwa ni nyongeza katika madeni mengi ambayo Dk. Shein ameikopesha tasnia ya habari na wanahabari wa Zanzibar kwa ujumla toka alipoingia madarakani kuiongoza serikali ya awamu ya saba deni ambalo linapaswa kutiliwa maanani na kila mmoja miongoni mwa wanatasnia hiyo.

“Sote ni mashahidi, kama kuna kipindi ambacho tasnia ya habari imepata bahati ya kuonekana moja kwa moja na jicho la kiongozi Mkuu wa nchi basi ni katika awamu ya 7 ya SMZ (Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar) kwani tukiacha mabadiliko makubwa aliyoyaongoza katika vyombo vya habari vya umma tunashuhudia serikali yake inavyoendelea kuwaamini wanahabari kwa kuwateua kushika nafasi mbali mbali serikalini jambo ambalo tunapaswa kumshukuru Mheshimiwa Rais na tumuombea kila la kheri katika utekelezaji wa majukumu yake ya kila siku”, alisema Mjaka na kuwapongeza wateule hao.

Aliwataka wateuliwa hao na wanahabari nchini kufanya kazi kwa kuzingatia weledi, juhudi, maarifa na misingi ya taaluma katika utendaji wa kazi zao ili kuunga mkono juhudi za Rais wa Zanzibar na serikali yake za kuwaletea maendeleo wananchi wa Zanzibar kama moja miongoni mwa njia za kujaribu kulipa sehemu ya deni la imani ambalo Rais amekopesha tasnia ya habari.

Aidha taarifa hiyo pia iliwapongeza Waziri wa Habari, Utamaduni na Mambo ya kale Mahmoud Thabit Kombo, Naibu Waziri Choum Kombo Khamis, Katibu Mkuu wa wizara hiyo Khadija Bakar Juma na Manaibu Makatibu wakuu Dk. Mnemo (habari) na Amina Ameir Issa (utalii na mambo ya kale) kwa kuteuliwa kushika nafasi hizo pamoja na kuwashukuru viongozi wakuu wa iliyokuwa wizara hiyo Rashid Ali Juma na Omar Hassan Omar 'King' na watendaji wengine kwa ushirikano waliokuwa wakiutoa kwa klabu hiyo, vyombo vya habari waandishi wa habari jambo ambalo Mjaka alisema anaamini litaendelezwa na viongozi hao wapya. 
 Katibu mkuu wizara ya habari, utalii na mambo ya kale Khadija Bakar Juma (kulia) akila kiapo.

Katika hatua nyengine Katibu Mjaka alieleza kuwa Kamati Tendaji ya ZPC inatarajia kukutana leo katika kikao chake cha kawaida kitakachofanyika katika ofisi za klabu hiyo Kijangwani mjini Zanzibar kujadili mambo mbali mbali yanayohusu ustawi wa tasnia ya habari, taasisi hiyo na wanachama wake.

Mjaka alisema kikao hicho kinachotarajiwa kuongozwa na Mwenyekiti wa ZPC Abdalla Abdulrahman Mfaume kitapokea, kujadili na kupitisha taarifa ya Mkutano Mkuu wa 14 uliofanyika mwishoni mwa mwaka jana, kupitia mpango kazi wa klabu hiyo kwa kipindi cha miezi mitatu ijayo, kupokea taarifa za kiutendaji na maelekezo ya za vikao vya Bodi ya Wakurugenzi ya Muungano wa klabu ya waandishi wa habari Tanzania – UTPC na kupitia maombi wanachama wapya wanaotaka kujiunga na klabu hiyo yaliyopokelewa katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita.

“Hiki ni kikao cha kawaida kama inavyoagizwa na kifungu cha 18 (ii) cha katiba ya ZPC inayoitaka kamati ikutane kila baada ya miezi mitatu na ikizingatiwa kuwa kamati ilikutana mara ya mwisho mwezi Disemba mwaka jana, tumeona haja ya kukutana ili kupitia mambo tuliyoyafanya na kupitisha mipango ya baadae kama ilivyoidhinishwa na mkutano mkuu uliopita”, alieleza Mjaka.

Mwishoni mwa wiki iliyopita Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein alifanya uteuzi wa watendaji wakuu wa baadhi ya wizara za serikali ya Zanzibar na kumteua aliyewahi kuwa Mkuu wa chuo cha habari Zanzibar Dk. Mnemo kuwa Naibu Katibu Mkuu katika wizara ya habari, utalii na mambo ya kale wakati Mitawi aliyekuwa Katibu wa Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu katika ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Mwisho.  




TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
NDUGU WAHARIRI NA WAANDISHI WA HABARI,
Kwa niaba ya Kamati Tendaji wa Klabu ya waandishi wa habari Zanzibar (Zanzibar Press Club – ZPC) ninakuja mbele yenu kuwapa taarifa juu ya mambo mawili muhimu katika ustawi wa ZPC kama taasisi lakini pia tasnia ya habari kwa ujumla.
JAMBO LA KWANZA:
UTEUZI WA WANACHAMA WA ZPC KATIKA NAFASI ZA UNAIBU KATIBU MKUU
Kwa niaba ya wajumbe wa Kamati Tendaji na wanachama wa ZPC, ninatumia waraka huu kuwasilisha pongezi na shukrani zetu kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein kwa kuwateua wanachama wa muda mrefu wa klabu yetu Dk. Saleh Yussuf Mnemo na Ndugu Abdullah Hassan Mitawi kuwa Manaibu Makatibu Wakuu katika Wizara ya habari, utaliii na mambo ya kale na Wizara ya nchi Ofisi ya Makamo wa pili wa Rais wa Zanzibar.

Kwa hakika ZPC imeguswa na uteuzi wa Mheshimiwa Rais na kuuchukulia kuwa ni nyongeza katika madeni mengi ambayo Rais Dk. Shein ameikopesha tasnia ya habari na wanahabari wa Zanzibar toka alipoanza kipindi cha utawala wake deni ambalo linapaswa kutiliwa maanani na kila mmoja miongoni mwa wanatasnia hii.

Nadhani sote ni mashahidi na tutakubaliana ya kwamba kama kuna kipindi ambacho tasnia ya habari imepata bahati ya kuonekana moja kwa moja na jicho la kiongozi Mkuu wa nchi basi ni katika kipindi cha awamu ya 7 ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kwa niaba ya wadau wote wa habari napenda kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa mambo mengi mema aliyoitendea tasnia hii na watendaji wake na tunamuombea kila la kheri katika utekelezaji wa majukumu yake ya kila siku.

Mtakumbuka kuwa mwishoni mwa wiki iliyopita Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein alifanya uteuzi wa watendaji wakuu wa baadhi ya wizara za serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kuwateua mwanahabari (kitaaluma) aliyewahi kuwa Mkuu wa chuo cha habari Zanzibar (ZJMMC) Dk. Saleh Yussuf Mnemo kuwa Naibu Katibu Mkuu katika wizara ya habari, Utalii na Mambo ya kale anayeshuhulikia masuala ya habari na Ndugu Abdullah Hassan Mitawi aliyekuwa Katibu wa Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuwa Naibu Katibu Mkuu katika Wizara ya nchi ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

Ni imani yangu na ya ZPC kwamba wateuliwa hao wataendelea kushirikiana na wanahabari wenzao kufanya kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni, miongozo, weledi, juhudi, maarifa na misingi ya taaluma zao ili kuunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na serikali yake za kuwaletea maendeleo wananchi wa Zanzibar lakini pia kujaribu kulipa sehemu ya deni la imani ambalo mheshimwa Rais ametukopesha.

Aidha kwa niaba ya wadau wa habari ninapenda kuwapongeza kwa dhati Waziri wa Habari, Utalii na Mambo ya kale Mahmoud Thabit Kombo, Naibu Waziri Choum Kombo Khamis, Katibu Mkuu Khadija Bakar Juma na Manaibu Makatibu wakuu Dk. Mnemo (habari) na Amina Ameir Issa (utalii na mambo ya kale) kwa kuteuliwa kushika nafasi hizo pamoja na kuwashukuru viongozi wakuu wa iliyokuwa wizara ya habari utamaduni, utalii na michezo mhe; Rashid Ali Juma na ndg; Omar Hassan Omar 'King' na watendaji wengine kwa ushirikano waliokuwa wakiutoa kwa klabu yetu, vyombo vya habari waandishi wa habari jambo ambalo naamini litaendelezwa na viongozi wapya wa wizara hii.

Vile vile tunawatakia viongozi hao utendaji uliotukuka katika maeneo waliyopangiwa kufanya kazi na kwamba ZPC haitosita kuwapatia kila aina ya msaada na ushirikiano pale watakapouhitajia.  
JAMBO LA PILI:
KIKAO CHA KAMATI TENDAJI YA ZPC;
KAMATI Tendaji ya klabu ya waandishi wa habari Zanzibar (ZPC) inatarajia kukutana katika kikao chake cha kawaida leo (kesho machi 15, 2018) katika ofisi za klabu hiyo Kijangwani mjini Zanzibar kujadili mambo mbali mbali yanayohusu ustawi wa tasnia ya habari nchini, taasisi yetu na wanachama wake.

Kwa mujibu wa KATIBA ya ZPC, Mwenyikiti wa klabu ndie anaeongoza vikao vyote vya Kamati Tendaji hivyo kikao hicho kinatarajiwa kuongozwa na ndugu Abdalla Abdulrahman Mfaume - Mwenyekiti wa ZPC ambapo kikao hicho kitapokea, kujadili na kupitisha taarifa ya Mkutano Mkuu wa 14 uliofanyika Disemba 30, 2017 na kupitisha mpango kazi wa klabu hiyo kwa kipindi cha miezi mitatu ijayo kuanzia mwezi April 2018.

Aidha kikao hicho pia kitapokea taarifa za kiutendaji na maelekezo ya vikao vya Kamati na bodi ya Wakurugenzi wa Muungano wa klabu za waandishi wa habari Tanzania – UTPC na kupitia maombi wanachama wapya walioomba kujiunga na klabu katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita.

Kikao hiki ni cha kawaida kama inavyoagizwa na kifungu cha 18 (ii) cha katiba ya ZPC inayotaka Kamati Tendaji ikutane kila baada ya miezi mitatu, hivyo kwa kuwa kamati ilikutana mara ya mwisho mwezi Disemba mwaka jana, ipo haja ya kukutana ili kupitia mambo tuliyoyafanya na kupitisha mipango ya baadae kama ilivyoidhinishwa na Mkutano Mkuu uliopita ili iingie katika utekelezaji.

Nawatakia majukumu mema.

FAKI MJAKA,
KATIBU MKUU,
KLABU YA WAANDISHI WA HABARI ZANZIBAR – ZPC,
14, MACHI 2018.

No comments:

Post a Comment