Thursday, March 1, 2018

SMZ YAOMBWA KUWEKEZA ZAIDI KATIKA MRADI WA BAREFOOT COLLEGE KINYASINI UNGUJA


NA MWINYIMVUA NZUKWI
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imetakiwa kutoa msukumo kwa shughuli zinazoendeshwa katika kituo cha kutengenezea vifaa vya umeme wa jua cha ‘Barefoot college’ kilichopo Kinyasini Mkoa wa Kaskazini Unguja ili kizweze kufikia malengo ya kuanzishwa kwake.

Akizungumza na waandishi wa habari kituoni hapo, Mratibu Mkaazi wa ‘Barefoot Collage’ nchini Pendo Yaredi Sambayi alisema mradi huo una lenga kusaidia maendeleo ya jamii kwa kuwawezesha wanawake wa maeneo ya vijijini hivyo ipo haja ya kupewa kipaumbele ili kiweze kuendelea.

Alisema katika utekelezaji wa kazi zake chuo hicho kinatoa mafunzo ya kutengeneza vifaa vya umeme wa jua na kusimamia uunganishaji wa vifaa hivyo kwa wananchi wa vijiji ambavyo havijafikiwa na huduma ya umeme kwa lengo la kuharakisha maendeleo ya jamii sambamba na kutoa elimu ya ujasiriamali.

Alisema kikawaida chuo hicho kinatakiwa kutoa wahitimu mara mbili kwa mwaka lakini kimeshindwa kufanya hivyo kutokana na kukosekana kwa fedha kutoka serikalini jambo hilo limeshindikana na kutishia maendeleo ya mradi huo.

“Wahitimu wa mwisho walimaliza mwezi Aprili mwaka jana (2017) ambapo wanawake 9 walihitimu baada ya wenzao 11 kuhitimu mnamo mwaka mwaka 2016 jambo ambalo ni kinyume na utaratibu unaotakiwa wa kutoa wahitimu kila baada ya miezi mitano”, alieleza Pendo.

Hata hivyo alizipongeza serikali ya Zanzibar na ya India kwa kufikiria kuanzisha mradi huo ambao umesaidia kubadilisha maisha ya baadhi ya wanawake wa vijiji vinavyohusika na utekelezaji wa mradi huu.

“Mradi huu ni miongoni mwa matokeo ya ziara ya Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein alipotembelea nchini India na kutembezwa katika miradi ya huo cha Barefoot ndipo alipoiomba serikali ya nchi hiyo ije kutekeleza mradi huu hapa nchini kwa makubaliano maalum”, alieleza Mratibu huyo.

Aliyataja miongoni mwa makubaliano hayo kuwa ni pamoja na SMZ kugharmia mafunzo, kuratibu upatikanaji wa wanafunzi na eneo lililojengwa chuo hicho huku serikali ya India ikiwezesha ujenzi wa kituo hicho, safari za mafunzo nchini India za wakufunzi miongoni mwa wahitimu 11 wa kituo hicho na uendelezaji wa majengo ya chuo hicho ili kiweze kuchukua wanafunzi wengi zaidi kwa mwaka.

Aidha katika kuendeleza malengo ya mradi huo Pendo alieleza kuwa wameamua kutoa mafunzo ya ushonaji nguo za aina mbali mbali, ufugaji nyuki na kilimo chenye kuzingatia utunzaji wa mazingira ambayo wahitimu wanatakiwa kwenda kuyafanyia kazi pindi wanaporudi katika vijiji vyao sambamba na kukikuza na kuwa cha kimataifa.

"Serikali ya India imeshatoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa makaazi ya wanafunzi na ofisi za kituo, kinachosubiriwa ni kuna hatua za serikali ya zanzibar kurudisha mafunzo yaliyolengwa ambayo mipango inaendelea ili kituo hiki kiweze kutchukua wanafunzi kutoka ndani na nje ya Zanzibar", alisema Mratibu huyo amabae alisema kituo hiko kipo Zanzibar pekee katika Afrika Mashariki.

Akielezea mafanikio ya kituo hicho mratibu huyo alieleza kuwa idadi ya vijiji wanavyovihudumia imeongezeka na kufikia vinane Unguja na Pemba ambapo zaidi ya nyumba 1,000 zimeshafungwa vifaa vya umeme huo.

“Kwa sasa tupo katika vijiji 6 unguja na 2 pemba ambap kinamama wapaooondoka hapa kila mmoja hupatiwa vifaa vya umeme jua 50 ili akaviunganishe na kuwavungia watu 50 na kuwasimamia katika malipo ambayo ni madogo kulingana na vifaa vyenyewe lakini pia fedha hizo huwa ni mali yao kama kikundi au jamii”, alieleza.

Nae kiongozi wa timu ya kijamii wa kituo hicho aboubakar khalid alieleza licha ya kufanikiwa kuwa na wahitimu 20 hadi kufikia 2017, bado chuo hicho kinakabiliwa na uhaba wa fedha za kuendeshea mafunzo, vifaa vya kufanyia kazi baada ya masomo na ugumu wa kuwapata wanafuzi kutokana na sababu mbali mbali.

“Mradi huu umelenga kuwawezesha wanawake hasa wale wa vijijini ambao hawakusoma au wana elimu ndogo ambao wana umri kati ya miaka 35 na 55, hivyo baadhi ya wakati inakuwa ngumu kuwapata ili waweze kuhudhuria mafunzo kutokana na kutoruhusiwa na waume au jamaa zao”, alieleza Khalid.

Alisema ugumu wa waume na jamaa za wanawake wanaotamani kujiunga na masomo hayo unatokana na mwanafunzi kutakiwa kubakia chuoni kwa muda wa miezi mitano bila ya kuondoka jambo ambalo linakuwa gumu.

Akizungumzia mafunzo ya ufugaji nyuki yanayotolewa na kituo hicho Mratibu wa ufugaji nyuki Zanzibar Hassan Faraji Ali alisema mafunzo hayo yanaenda sambamba na mafunzo ya utunzaji wa mazingira ili kurahisisha upatikanaji wa mavuno mengi.

“Tumeamua kuliingiza somo hili ili kuwafanya wahitimu wetu wawe na ujuzi tofauti tofauti utakaowasaidia kuendeleza maisha yao kwani licha ya kupatiwa nyenzo za kuanzishia miradi yao pia tunawapatia ujuzi wa kutafuta masoko ya bidhaa wanazozalisha”, alifafanua.

Kituo hicho ambacho ni sehemu ya miradi ya chuo cha Barefoot unaotekelezwa katika nchi mbali mbali duniani kwa lengo la kueneza matumizi ya nishati mbadala kama njia ya kutunza mazingira na kuwawezesha wanawake ulizinduliwa na Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein miaka mitano iliyopita.   

   

Mratibu Mkaazi wa ‘Barefoot Collage’ nchini Pendo Yaredi Sambayi (Kulia) akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) walikitembelea chuo cha kufundishia utengenezaji wa vifaa vya umeme wa jua (sola power) kilichopo Kinyasini, Unguja. Kushoto ni Fatma Juma  Haji mwalimu wa uunganishaji wa vifaa vya sola aliyepata mafunzo nchini India . 
 

Mmmoja ya wahitimu na mwalimu wa kituo cha utengezaji wa vifaa vya umeme wa jua Amina Saleh Shamata (kushoto) akiwaelekeza waandishi wa habari waliotembelea kituo hicho namna vifaa vya umeme jua kabla ya kuanza kutumika.


Mwalimu wa somo la ufugaji nyuki na mazingira Elia Filbert Msuha (kushoto) akiwaonesha waandishi wa habari jinsi ya kutengeneza mbolea ya mboji inayotokana na mabaki ya vyakula na majani ya miti. Kulia ni Mratibu wa ufugaji nyuki Zanzibar Hassan Faraji Ali.


Mwalimu wa somo la ufugaji nyuki na mazingira Elia Filbert Msuha (kushoto) akitoa maelezo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu ufugaji wa nyuki.

No comments:

Post a Comment