NA MZEE GEORGE
SERIKALI ya Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja imesema itasimamia maagizo na miongozo ya Serikali kwa kufuata sheria na utaratibu wa matumizi ya ardhi ili kuhakikisha mipango na azma ya kuondosha migogoro ya ardhi katika Mkoa huo inafanikiwa.
Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mhe Ayoub Mohammed Mahmoud ameeleza hayo wakati wa mkutano uliowakutanisha viongozi na watendaji wa Mkoa huo na kamati ya baraza la Mapinduzi inayofuatilia migogoro ya ardhi chini ya Mwenyekiti wake Mhe Haji omar Kheir uliofanyika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la zamani kikwajuni mjini unguja.
Amesema wakati umefika kwa viongozi, watendaji na wananchi wa Mkoa wa Mjini Magharibi kuhakikisha wanafuata taratibu na sheria zilizowekwa katika matumizi mazuri ya ardhi ili kuona rasilimali hiyo ya taifa inaendelea kutunzwa.
Akitoa ahadi kwa niaba ya viongozi na watendaji wa Mkoa huo kwa kamati hiyo mhe Ayuob amesema yupo tayari kuachia madaraka iwapo atabainika kujihusisha na migogoro ya ardhi kwa maslahi nchi na kutoa indhari kwa watendaji wakaotajihusisha na migogoro ya ardhi hatosita kuwachukulia hatua za kinidhamu.
Mapema wajumbe wa Kamati ya Baraza la Mapinduzi inayofuatilia migogoro ya ardhi wamesema utafiti uliofanyika umeonesha baadhi ya viongozi wa wilaya,Jimbo,Wadi na Shehia wamekua wakijipa mamlaka ya kuuza viwanja kinyume na utaratibu hali ambayo inayoibua migororo ya ardhi katika jamii.
Wameongeza kuwa kwa sasa Serikali imedhamiria kuitumia ardhi yake iliyopo kwa matumizi ya maendeleo ya nchi ambapo wamesema kuna haja ya kufanyiwa marekebisho ya sheria za ardhi kutokana na mapungufu yaliopo ambayo ndio chanzo cha matumizi mabaya ya ardhi.
Kamati ya Baraza la Mapinduzi inayofuatilia migogoro ya ardhi imeundwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein kufuatia ripoti ya Kamati iliyofanya utafiti wa migogoro ya ardhi nchini na kubaini ukiukwaji wa sheria za matumizi ya ardhi Kamati ambayo inaongozwa na Mwenyekiti wake Waziri wa ujenzi, mawasiliano na Usafirishaji Zanzibar Dk. Sira Ubwa Mamboya.
No comments:
Post a Comment