NA MWANDISHI WETU
Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Hassan
Ali Kombo amewataka wakaazi wa nyumba za Startling ziliopo Mahonda, Kitope na Mwanakombo
watekeleze agizo la serekali la kuhama katika nyumba hizo na kuzirudisha kwa
kiwanda cha sukari.
Akizungumza na wananchi wanaoishi katika
nyumba hizo Mahonda Kizota DC Hassan aliwataka wananchi hao kutii agizo hilo
kwa kuwa muda waliopewa kujiandaa kuzirudisha nyumba hizo umemalizika.
Alisema ni vyema na busara kwa wakaazi hao
kutekeleza agizo hilo kabla ya kupatwa na matatizo yoyote kwa kuwa taarifa za
kutakiwa kuhama wanazo kwa muda mrefu na kuwataka wawe wamekabidhi nyumba hizo
itakapofika Jumanne ya Machi 13 mwaka huu.
“Tunatarajia hakuna atakaekaidi agizo huili
kwa kuwa limeshatolewa muda mrefu na viongozi mbali mbali hivyo ninawaomba hadi
Jumanne ijayo muwe mmeshahama na kukabidhi funguo katika ofisi ya mkuu wa Wilaya”,
alisisitiza Hassan.
Alisema ameamua kutoa taarifa hiyo kwa mara
nyengine kuwakumbusha ili wasishtuke pindi hatua za kuwahamisha zitakapochukuliwa iwapo watashindwa kuhama kwa
hiari.
Nao wakaazi hao wameiomba serekali kuwapa
muda kwa madai kuwa muda waliopewa ni mfupi kuweza kujitayarisha kuhama na
kutaka wapatiwe ufafanuzi juu ya utolewaji wa taarifa za kuwataka kuhama ambapo
awali waliotakiwa kuhama walikuwa ni wafanyakazi wa serikali.
Aidha walihoji iwapo agizo hilo
litatekelezwa ipi itakuwa hatma za taasisi za kijamii walizozianzisha kama vile
skuli na vyuo vya qur-an viliomo katika eneo hilo.
Taarifa zilizopatika kutoka katika mmoja ya
wakaazi hao kuwa serikali ilitoa notisi kwa wafanyakazi na watendaji wa
serikali wanaoishi katika nyumba hizo 41 miezi mitatu iliyopita na kwamba mtu
mmoja tu kati yao ndie aliyetii agizo hilo.
“Waliopewa barua za kuhama ni wafanyakazi
wa taasisi za serekali na tayari mmoja kati yao amesharudisha funguo lakini sisi
wananchi wa kawaida hakuna aliyepewa taarifa kwa barua ingawa tetesi za kuwa
tuhame zipo kwa muda mrefu sasa”, alieleza mkaazi huyo ambae hakutaka kutajwa
jina lake.
Nyumba za Starling ni miongoni mwa mali za
kilichokuwa kiwanda cha sukari na manukato ambacho kilibinafsishwa na kupatiwa
mmiliki mwengine zinakadiriwa kukaliwa na zaidi ya familia 150 zilijengwa kwa
madhumini ya kukaa wafanyakazi wanaofanyakazi katika kiwanda cha sukari na
manukato katika miaka ya 70.
Muonekano wa jengo la kiwanda cha sukari Mahonda baada ya kuanza upya uzalishaji.
No comments:
Post a Comment