Friday, March 9, 2018

VIJANA KUADHIMISHA SIKU YA JUMUIYA YA MADOLA KWA BUNGE JUMATATU


NA MWINYIMZUA NZUKWI
Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mgeni Hassan Juma anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Bunge la vijana lililoandaliwa na Chama cha Mabunge ya Jumuiya ya Madola (CPA) Zanzibar tawi la Zanzibar litakalofanyika katika ukumbi wa baraza hilo Jumatatu Machi 12 mwaka huu.
Bunge hilo ambalo ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya Jumuiya ya madola duniani, litahusisha vijana wapatao 50 kutoka wilaya 11 za Unguja na Pemba wenye umri usiozidi miaka 30 wanaotoka katika mabaraza ya vijana wilayani humo.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Chukwani, Mwenyekiti wa chama cha mabunge ya Jumuiya ya Madola tawi la Zanzibar Simai Mohammed Said alisema bunge hilo ni linaitishwa kwa mara ya tatu toka baraza la wawakilishi lianze kuiadhimisha siku hiyo.
Alisema bunge hilo katika kikao hicho cha bunge, vijana watajadili mada mbali mbali, kupitisha maazimio na kutoa maoni juu ya namna kundi hilo linavyoshirikia katika kukuza demokrasia nchini.
"Tunatarajia baada ya bunge hilo maazimio yatakayofikiwa yatawasilishwa wa katika vikao vya Baraza la Wawakilishi kupitia kamati ya maendeleo ya wanawake, habari na utalii kama inavyoelekezwa na kanuni ya 149(3) ya kanuni ya baraza la wawakilishi ili serikali iyatekeleze", alieleza Simai.

Aidha alieleza kuwa bunge hilo linatarajiwa kuongeza uelewa wa jamii na vijana kuhusiana na masuala ya kibunge na kutokana na ufafanuzi wa mada zitakazojadiliwa, kujenga moyo wa kizalendo, ushirikiano na kuibua stadi za uongozi miongoni mwa wabunge hao.
Akizungumzia mafanikio yaliyopatikana toka baraza hilo lijiunge na chama cha mabunge ya jumuiya ya madola (CPA) mwaka 2004, Mwenyekiti huyo alieleza kumekuwa na mabadiliko ya kiutendaji na kimfumo ndani ya baraza jambo linalopelekea chombo hicho kulingana na mabunge mengine duniani.
"Miongoni mwa malengo ya kuanzishwa kwa CPA (Commonwealth Parliamentary Association) ni kutekeleza azma ya maadili chanya ya demokrasia ya kibunge ambayo yanafikiwa kupitia mikutano, semina, ziara za kubadilishana uzoefu na uchapaji wa nyaraka zinazohusiana na jumuiya ambazo baraza la wawakilishi linashiriki kama mwanachama anaejitegemea", aliongeza Simai ambae pia ni mwakilishi wa jimbo la Tunguu, Zanzibar.
Akifafanua jinsi baraza hilo linavyonufaika na muungano huo, Afisa Sheria wa baraza hilo Mussa Kombo Bakar alisema ushiriki wa baraza hilo katika vikao mbali mbali kumepelekea mabadiliko ya kanuni na mfumo wa uendeshaji wa chombo hicho na kukifanya kuaminika zaidi na jamii.
“Mabadiliko mengi katika utekelezaji wa shughuli za baraza yamechochewa na uanachama wetu katika CPA kwani kila yanapotolewa maazimio katika vikao vya bunge la jumuiya ya madola, na sisi tunalazimika kubadili kanuni ili kwenda sambamba na wenzetu”, alisema kombo.
Akitolea mfano wa mabadiliko hayo kuwa ni pamoja na kualikwa kwa makundi mbali mbali ya wadau wanaohusika na fani maalum pale miswaada inapowasilishwa katika kamati za baraza kwa lengo la kupata maoni ya kitaalamu kuhusiana yanayowawezesha wajumbe kuwa na uelewa wa pamoja kuhusu mswada husika.
“Hili ni jambo jipya na limekuja mahsusi ili kuwafanya wajumbe watakapokuwa wanaijadili miswada husika iwe rahisi kwao tofauti na ilivyokuwa katika siku za nyuma”, alifafanua Kombo.
Nae Katibu wa chama hicha ambae pia ni Katibu wa Baraza la wawakilishi Zanzibar Raya Issa Mselem alieleza mashirikiano yaliyopo kati ya chama hicho na kilichopo katika bunge la jamhuri ya muungano wa Tanzania kuwa ni mzuri na kwamba vyombo hivyo vimekuwa vikishirikiana katika utekelezaji wa majukumu yao.
“Bunge la Jamhuri ya muungano wa Tanzania na Baraza la wawakilishi katika muungano wa mabunge tuna hadhi inayofanana na fursa sawa kama wanachama na tunapokuwa na shughuli za kikazi tumekuwa tukishirikiana na kushirikishana ili kuwa na uwiano sawa kama taifa”, alifafanua Raya.
Aliongeza kuwa baraza lake linatarajia kuendele kutoa elimu kwa makundi mbali mbali ili ddamira na hadhi ya baraza la wawakilishi katika kukuza demokrasia na maendeleo ya jamii iweze kufikiwa kwa kiwango kikubwa.
Maadhimisho hayo yanaadhimishwa kwa pamoja kati ya chama cha mabunge ya jumuiya ya madola na chama cha wabunge wanawake wa mabunge ya jumuiya ya madola matawi ya Zanzibar ambapo bunge la vijana litazungumzia masuala ya demokrasia ya kibunge, utawala bora na mambo mengine yanayohusiana na ujumbe wa mwaka huu unaosema ‘kuelekea hatma ya pamoja’.


Mwenyekiti wa Chama cha Mabunge ya Jumuiya ya Madola (CPA) tawi la Zanzibar Simai Mohammed Said (katikati) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu maadhimisho ya siku ya jumuiya ya madola itakayoadhimishwa Jumatatu Machi 12, 2018.


Katibu wa Baraza la Chama cha mabunge ya Jumuiya ya Madola na katibu wa Baraza la Wawakilishi Raya Issa Mselem (kushoto) akieleza jambo wakati wa mkutano wa waandishi kuhusiana na maadhimisho ya siku ya Jumuiya ya Madola. Kushoto kwake ni Mwenyekiti wa chama hicho Simai Mohammed Said na Afisa Sheria wa baraza la wawakilishi Mussa Kombo Bakar.

Baadhi ya waandishi wa habari wa vyombo mbali mbali viliopo Zanzibar wakifuatilia kwa karibu maelezo ya viongozi wa Chama cha Mabunge ya Jumuiya ya Madola tawi la Zanzibar kuhusu maadhimisho ya siku ya Jumuiya ya Madola yatakayofikia kilele chake Jumatatu Machi 12 mwaka huu.

No comments:

Post a Comment