Saturday, January 27, 2018

BALOZI AWATAKA WANANCHI KUACHA MUHALI KATIKA UDHALILISHAJI, KUCHANGIA DAMU KUOKOA MAISHA YA WAHITAJI

NA MWINYIMVUA NZUKWI
Wananchi wa Zanzibar wametakiwa kutofumbia macho vitendo vya ukatili na udhalilishaji dhidi ya wanawake na watoto ili kukomesha vitendo hivyo ndani ya jamii.

Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alitoa wito huo katika tamasha la uchangiaji damu pamoja na uzinduzi wa jumuiya  ya maendeleo ya vijana na wanawake (BIWO)  katika viwanja vya Mnara wa kumbukumbu ya Mapinduzi Michenzani na kueleza kuwa serikali itaendelea kuchukua hatua za kisheria.

 Alisema iwapo jamii itaondoa muhali na kufanya kazi kwa kushirikiana na viongozi wa serikali na asasi za kiraia, tatizo hilo linaweza kukomeshwa na kustawisha maisha ya wananchi na taifa kwa ujumla.

“Tukiwa tayari tunaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa madhara ya vitendo vya udhalilishaji na ukatili wa kijinsia sambamba na matumizi ya dawa za kulevya hivyo naviagiza vyombo vinavyohusika na ufuatiliaji na usimamizi wa sheria ni lazima vifanye kazi kwa haki na kuchukua hatua stahiki kwa watu wanaohusika na uovu huuu”, alieleza Balozi Seif.

Aidha aliipongeza jumuiya ya BIWO kwa uamuzi wao ywa kuanzisha kampeni ya uchangiaji damu kwa hiyari jambo alilosema linaenda sambamba na azma ya Serikali ambayo kupitia misaada na ushirikiano na wafadhili mbalimbali imechukua  juhudi za kuanzisha  benki ya damu  ili kuhakikisha  uhakika wa damu kama moja ya njia za kuimarisha huduma za afya ya jamii.

“Utaratibu wa kuchangia damu  ni wa  duniani kote  hivyo hatua hii itasaidia kupatikana kwa damu ambayo itatumiwa katika  hospitali mbalimbali ambako mahitaji hujitokeza ikiwemo kuwasaidia kina mama wanapotaka kujifungua kwani hupoteza damu nyingi pamoja na panapotokea majanga ya kitaifa au ajali”, alisisitiza Balozi Seif.

Mapema akimkaribisha Mkamo wa pili wa Rais, Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Ayoub Mohammed Mahamoud  alisema  serikali ya Mkoa wake imekuwa ikiunga mkono  jumuiya mbalimbali zenye lengo la kuhakikisha utetezi wa haki, usawa na ustawi wa wananchi kwani kufanya hivyo kunaongeza kasi ya maendeleo taifa.

“Wazo la hili linaenda sambamba na azma ya serikali ya kuimarisha ustawi wa wananchi wetu na ndio maana ndani ya mkoa wetu tulianzisha kampeni ya MIMI NA WEWE ili kuimarisha dhana ya uzalendo kama ilivyokuwa katika miaka ya nyuma”, alisema Mkuu huyo wa mkoa.

 Uzinduzi wa Jumuiya hiyo ulienda sambamba na kampeni ya uchangiaji wa damu kwa hiyari kwa ushirikano na benki ya damu Zanzibar ambapo hadi majira ya saa 6:45 jumla ya chupa 375 za damu zilikwishapatikana kati ya chupa 1000 zilizokadiriwa.


Kwa mujibu wa benki ya damu Zanzibar wastani wa chupa 75 zinakadiriwa kutumika kila siku katika hospitali mbali mbali Zanzibar kwa watu wanaohitaji tiba ya kuongezewa damu ambapo katika kamperni kama hiyo mwaka chupa 500 za damu zilipatiakana.


Mkamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idi akiwakagua baadhi ya watu walijitokeza kuchangia damu katika tamasha la uzalendo lililoandal;iwa kwa pamoja na jumuiya ya maendeleo ya wanawake na vijana (BIWO) na ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi.  anayemfuatia ni Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Ayoub Mohammed Mahmoud.

Friday, January 26, 2018

ZATU KUKUTANA JANUARI 27 - 28, DK. SHEIN ATARIWA KUBARIKI MKUTANO MKUU FEBRUARI

NA MWINYIMVUA NZUKWI
Chama cha Walimu Zanzibar (ZATU) kinatarajia kufanya mikutano mikuu ya ngazi kanda kabla ya kukutana katika ngazi ya taifa baadae mwezi Februari mwaka huu.

Katibu wa chama hicho Mussa Omar Tafurwa amewaambia waandishi wa habari katika makao makuu ya chama hicho Kijangwani mjini Unguja kuwa mkutano wa kanda ya Unguja utafanyika katika ukumbi wa mikutano wa Uhuru Kariakoo wakati mkutano wa kanda ya Pemba utafanyika katika skuli ya sekondari Madungu.

Amesema mikutano yote hiyo uitakayokuwa ya siku mbili pamoja na kufanya kazi zake za kawaida za kupokea, kujadili na kupitisha taarifa mbali mbali zinazohusiana na chama hicho, pia itafanya uchaguzi wa kuwachagua viongozi watakaoziongoza kanda hizo, wajumbe wa mkutano mkuu na baraza kuu la taifa.

“Tunatarajia katika siku mbili hizo wajumbe wa mikutano hiyo watapata nafasi nzuri ya kujadili na kupanga mikakati ya baadae ya chama chetu ikiwa ni pamoja na kuwachagua wenyeviti wa kanda, wajumbe 6 wa baraza kuu taifa, wajumbe wawili wa kamati kuu kutoka kila wilaya na wajumbe wa mkutano mkuu taifa”, alisema Mwalimu Tafurwa.

Aidha alieleza kuwa mkutano mkuu wa taifa wa chama hicho utafanyika Februari 10 na 11 mwaka huu unaotarajiwa kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali wa serikali na wadau wengine wa elimu wakiwemo viongozi wa vyama vya walimu na mashirikisho ya vyama vya wafanyakazi kutoka ndani na nje ya nchi.

“Kutakuwa na waalikwa kutoka ndani na nje ya nchi katika mkutano huo ambao tunatarajia utahudhuriwa na wastani watu kati ya 180 na 200 ambapo mbali ya ajenda za kawaida pia utawachagua viongozi wa chama katika ngazi ya taifa”, alifafanua Katibu huyo.

Alizitaja nafasi zinazogombewa katika uchaguzi huo kuwa ni ya Rais, Makamo wa Rais, wajumbe 7 wa Kamati Tendaji taifa, wajumbe wa kukiwakilisha chama katika Baraza Kuu la vyama vya wafanyakazi na wajumbe wa kukiwakilisha chama katika mkutano mkuu wa shirikisho la vyama vya wafanyakazi Zanzibar.

Akizungumzia ujumbe wa mkutano huo Mwalimu Tafurwa alisema mkutano huo utaendeleza ujumbe wa kimataifa wa siku ya walimu unaosema ‘uhuru katika kufundisha hujenga uwezo wa mwalimu’ na kuwataka walimu nchini kuzingatia maadili ya taaluma yao wanapokuwa kazini ili kuongeza tija na kulinda hadhi ya fani hiyo.

Mussa Omar Tafurwa, Katibu Mkuuu wa chama cha walimu Zanzibar (ZATU) akisisitiza jambo katika moja ya mikutano yake na waandishi wa habari.






Wednesday, January 24, 2018

"TUNATAMBUA MCHANGO WA ASASI ZA KIRAIA KATIKA MAENDELEO YA JAMII" - BALOZI SEIF ALI IDI

NA MWINYIMVUA NZUKWI
Serikali ya Zanzibar imeeleza kuwa inatambua na kuthamini mchango unaotolewa na asasi za Kiraia (AZAKI) katika kuisaidia juhudi zake za kukabiliana na umaskini, demokrasia na utawala bora nchini.

Akifungua kongamano la pili la asasi za kiraia Zanzibar katika hoteli ya Zanzibar Beach Resort, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idi alilisema shughuli zinazotekeleza na jumuiya hizo zina mchango mkubwa katika ujenzi wa taifa na kuwataka wasimamizi wa asasi hizo kuzidisha ushirikiana na serikali kwa lengo la kuchochea kasi ya maendeleo ya wananchi kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Balozi Seif alisema ili kufikia maendeleo ya kweli na ya haraka ipo haja kwa pande mbili hizo kushirikiana  na kuzingatia wajibu wa kuijenga nchi kwa mujibu wa katiba ya nchi, sheria na katiba za jumuiya hizo.

“Pamoja na kutambua mchango wenu kwa maendeleo ya nchi yetu, bado nawatahadharisha kuwa serikali  haitokuwa tayari kuziona asasi zenu zinafanya  kazi kinyume  na katiba zao au taratibu zilizojipangia zenyewe kwani uzoefu wa majukumu ya taasisi za kiraia umetoa mafunzo mengi na kupelekea baadhi ya taasisi kukiuka madili yao”, alisema Makamu wa Rais.

Aidha aliwahakikishia washiriki wa kongamano hilo ambalo ni sehemu ya mpango wa kuzisaidia asasi za kiraia Zanzibar (ZANSAP) unaotekelezwa kwa pamoja kati ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) na Umoja wa Ulaya (EU) kwamba serikali ipo tayari kuyafanyia kazi mapendekezo yote yatakayotolewa mwisho wa kongamano hilo.

“Napenda niwahakiishie kuwa serikali ipo tayari kupokea maazimio mtakayoyafikia mwisho wa kongamano hili kwa kuamini kuwa yatasaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha utawala bora sambamba na jamii kupata nguvu za kupambana dhidi ya umaskini kutokana na shughuli za ujasiriamali zinazotekelezwa na baadhi ya azaki”, alisisitiza.

Mapema Mwenyekiti wa Kongamano hilo Dk. Mzuri Issa Ali aliishukuru serikali ya Zanzibar kwa kuweka mazingira mazuri ya utendaji kazi wa asasi za kiraina na kuiomba kuwa na uratibu taasisi zao iliziweze kufanya kazi kwa pamoja na kufokiwa kwa malengo ya kuanzishwa kwao yafikiwe.

Alisema katika muungano wa azaki zinazoshiriki kongamano hilo zipo zinazojihusisha na kazi za kufanya utafiti, kutoa elimu na huduma za jamii ambazo ni chimbuko la mafanikio na maendeleo ya wananchi.

“Katika kongamano hili tutapata fursa ya kupokea na kujadili mada sita muhimu zilizojikita katika utekelezaji wa majukumu yetu ya kila siku ambazo ni zitatoa hali halisi ya taasisi zetu katika utekelezaji wa mipango ya kitaifa kama vile mkakati wa kupunguza umaskini Zanzibar awamu ya tatu (MKUZA III) pamoja na mpango wa kusaidia biashara zinazojitokeza kwa Wajasiriamali”, alisema Dk. Mzuri ambae pia ni mkurugenzi wa chama cha wanahabari wanawake Tanzania (TAMWA) ofisi ya Zanzibar.

Akimkaribisha Mgeni ulifungua Kongamano hilo Kaimu Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar  Maaalim Haroun Ali Suleiman alisema serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya (EU) imeanzisha Mradi wa kuzizaidia taasisi za kiraia nchini (ZANSAP) ili zifanye kazi zake kwa ufanisi na kuchangia maendeleo ya jamii.

“Mradi huu wenye kutekelezwa kwa mfumo wa Mkataba ulibuniwa kwa lengo la kuimarisha demokrasia na utawala bora, kuongeza ushiriki wa wananchi katika shuguli zinazowahusu, ushiriki wa azaki katika utekelezaji wa sera, sheria sambamba na kufuatilia utekelezaji wa mipango ya kitaifa na kimataifa nchini na tunatarajia hadi kukamilika kwa mradi, taasisi hizi zitakuwa zimeimarika na kuibua maeneo mapya ya utekelezaji”, alisema Maalim Haroun ambae pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utawala Bora na Utumishi wa Umma.


Zaidi ya asasi za kiaraia 200 zinashiriki kongamano hilo lililoanza januari 24 hadi 25 mwaka huu kutoka Unguja na Pemba ambalo ni la pili baada ya lililofanyika mwaka uliopita ambalo lilitumika kuutambulisha mradi wa ZANSAP kabla ya kuanza utekelezaji wake kwa kuzijengea uwezo asasi na makundi mbali mbali ya kijamii.

Balozi Seif akinusa ili kuridhika na kiwango cha utengenezaji wa Mafuta ya asili ya nazi yaliyosarifiwa na wajasiriamali wa Zanzibar wakati alipokuwa akikagua maonesho ya kazi za asasi za kiraia Zanzibar. Kushoto yake ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utawala Bora na Utumishi wa Umma Haroun Ali Suleiman na kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Ayoub Mohammed Mahmoud.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi (alievaa miwani) akipata maelezo juu ya moja ya bidhaa zilizotengenezwa na Wajasiriamali wa asasi za Kiraia alipotembelea maonesho ya kazi za wajasiriamali kabla ya kufungua Kongamano la pili la Asasi za Kiraia za zanzibar linalofanyika katika hoteli ya Zanzibar Beach Resort  Mazizini. 
 
Balozi Seif akihutubia washiriki wa kongamano la pili la asasi za kiraia zanzibar (hawapo pichani) linalofanyika katika Ukuimbi wa Mikutano wa hoteli ya Zanzibar Beach Resort Mazizini Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idi (katikati walioketi) akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Kamati ya Maandalizi ya Kongamano la asasi za Kiraia Zanzibar (waliosimama) mara baada ya kulifungua rasmi Kongamano hilo. Wengine katika picha hiyo kutoka kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Ayoub Mohammed Mahmoud, Mkuu wa timu ya wataalamu wa mradi wa kuziwezesha asasi za kiraia Zanzibar (ZANSAP) Fergal Ryan, Mwenyekiti wa kongamano hilo Dk. Mzuri Issa Ali, Kaimu Waziri wa Fedha na Mipango Maalim Haroun Ali Suleiman, Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango Zanzibar Juma Khamis Reli na Kamishna wa Fedha za nje katika wizara ya fedha na mipango Zanzibar Hindi Nassor Khatib.  

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif (katikati walioketi) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wawakilishi wa asasasi za kiraia zinazoshiriki Kongamano la pili la asasi za Kiraia Zanzibar (waliosimama) mara baada ya kulifungua rasmi Kongamano hilo linalofanyika katika hoteli ya Zanzibar Beach Resort Mzizini. wa kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya watu wenye ulemavu Zanzibar Abeda Rashid mara baada ya kulingua rasmi Kongamano hilo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idi akiagana na Mwenyekiti wa Kongamano la asasi za Kiraia mara baada ya kulifungua rasmi Kongamano hilo linalofanyika katika hoteli ya Zanzibar Beach Resort Mzizini. anaeshuhudia ni Mkuu wa timu ya wataalam wa mradi wa kuziwezesha asasi za kiraia Zanzibar (ZANSAP) Fergal Ryan.
(PICHA KWA HISANI YA OMPR)



Wednesday, January 10, 2018

DK. SHEIN KUWEKA JIWE LA MSINGI UJENZI WA MJI KISASA WA FUMBA

NA MWINYIMVUA NZUKWI
Ikiwa imesalia siku moja kabla ya kilele cha sherehe za mapinduzi ya Zanzibar,leo asubuhi Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la mapinduzi Dk. Ali Mohammed Shein anatarajiwa kuwa Mgeni rasmi katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa mji wa kisasa wa Fumba itakayofanyika Nyamanzi, wilaya ya Magharibi B.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Halmashauri ya sherehe na maadhimisho ya kitaifa shughuli hiyo ambayo awali ilipangwa kufanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Magufuli itafanyika chini ya usimamizi wa wizara ya Fedha na Mipango Zanzibar.

Mradi huo unaotekelezwa na kampuni ya CPS-Lives LTD ikiwa ni sehemu ya miradi 35 iliyopangwa kuzinduliwa na kuwekewa mawe ya msingi katika kipindi cha maadhimisho hayo yanayofikia kilele chake Januari 12, 2018.

Akizungumzia tukio hilo Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya CPS-Lives Tobius Dietzold aliishukuru serikali ya Zanzibar kwa Kuuhusisha mradi huo katika maadhimisho ya sherehe za mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka huu ambayo  yanayotimiza miaka 54 toka yalipoasisiwa Januari 12, 1964.

"Toka tumeanza kutekeleza mradi wetu tumekuwa na mashirikiano ya karibu sana na serikali ya Zanzibar na viongozi wake, hii ni kwa sababu tunajenga mji huu hapa Zanzibar kwa ajili ya Wazanzibari hivyo tunaamini kuingizwa katika ratiba ya sherehe hizi kunaongeza thamani ya kile tunachokifanya na ari ya wafanyakazi wetu", alisema Tobius.

Mradi wa ujenzi wa mji wa kisasa wa Fumba (Fumba Town Development) ni miongoni kwa miradi miwili mikuu ya makaazi inayotekelezwa katika ukanda wa maeneo huru ya kiuchumi ya Fumba yaliyotangazwa mnamo miaka ya 90.

Mbali na shughuli hiyo, mchana wa januari 11 Dk. Shein atatunuku nishani maalum za mapinduzi kwa watu mbali mbali waliotoa mchango na kutumikia jamii katika nyadhifa matukio mbali mbali wakati Rais mstaafu wa awamu ya sita Dk. Amani Abeid Karume atafungua kituo cha kutotolea vifaranga vya samaki huko Beit el Ras, Wilaya ya Magharibi 'A' Unguja.

Wakati wa mchana Waziri wa nchi ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Mohammed Aboud Mohammed anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika bonanza la mashindano ya michezo mbali mbali ya miaka 54 ya mapinduzi yakakayofanyika katika viwanja vya maisara kabla ya vikosi vya ulinzi na usalama kurusha fashifashi za maadhimisho hayo itakapofika saa 6:00 usiku mkesha ambao utatawaliwa na burudani mbali mbali za ngoma asilia, muziki wa dansi na muziki wa kiizazi kipya shughuli zitakazofanyika katika viwanja vya Maisara Mjini Unguja na Gombani kisiwani Pemba.




Muonekano wa moja ya nyumba za mfano zinazojengwa katika mradi wa mji wa kisasa wa Fumba unaotekelezwa na kampuni ya CLS-Lives LTD ambae utawekewa jiwe la msingi na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohammed Shein ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 54 ya mapinduzi ya Zanzibar.

Monday, January 8, 2018

BALOZI SEIF AWATAKA WAKANDARASI KUZINGATIA UADILIFU

NA OTHMAN KHAMIS, OMPR
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewaomba Wakandarasi na wasimamizi wanaopata kazi za Ujenzi katika Taasisi za Serikali kufanya kazi zao kwa uadilifu wa hali ya juu kinyume chake Serikali haitokubali kukabidhiwa majengo yasiyokuwa na kiwango.

Alisema Serikali italazimika kutumia sheria za ujenzi zilizopo katika njia na Utaratibu wa  kukataa kazi yoyote ile iliyokuwa chini ya kiwango kinachokubalika kimikataba.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa ombi hilo wakati akiweka Jiwe la Msingi wa Ofisi Tatu Pacha za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambazo ni za Wizara ya Kazi Uwezeshaji, Vijana, Wazee, Wanawake na Watoto, Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora zilizofanyika Mtaa wa Gombani Chake Chake Pemba.

Alisema haikubaliki kuona muda  mfupi tu baada ya kukamilika kwa Ujenzi na kukabidhiwa Majengo hayo yanaanza kuharibika, kuvuja, kupasuka, kupoteza haiba na hadhi inayokusudiwa.

Balozi Seif alieleza kwamba hivi sasa yapo Mjengo mengi hasa yake ya Skuli katika maeneo tofauti Nchini yaliyojengwa chini ya kiwango zimeanza kuvuja kama chungio jambo ambalo Serikali Kuu tayari imepata fundisho kutoka kwa baadhi ya Wakandarasi na hivyo hapana budi sasa kuchukuwa tahadhari.

Alieleza kuanzishwa kwa ujenzi wa majengo pacha kwa ajili ya matumizi ya Ofisi za Wizara Tatu za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambao zote ni muhimu kumefungua fursa za ujenzi wa jengo jengine kwa ajili ya matumizi ya Ofisi ya Bodi ya Mapato Zanzibar litakalokuwepo Mkabala na Majengo hayo.

Balozib Seif alisema ujenzi huo utazidi kulifanya eneo hilo la Gombani kuwa na haiba nzuri zaidi na  ni matarajio ya Wananchi wanaoishi jirani na maeneo hayo wanaweza kunufaika kwa kuitumia fursa hiyo kwa kuanzisha biashara ndogo ndogo.

Alisema biashara hiyo itakayosaidia kutoa ajira kwa Wananchi hao itaweza kuwahudumia Wafanyakazi wengi watakaokuwa wanapita katika maeneo yao wakati wakielekea au kutoka kazini.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwapongeza Wananchi na Vijana wote waliokuwa wakilitumia eneo hilo kwa uamuzi wao wa kizalendo waliouonyesha  wa kuamua kuondoka wenyewe kwa hiari yao ili kupisha shughuli hizo za ujenzi wa Ofisi za Serikali.

“Kulikuwa na Vijana waliolitumia eneo hilo kibiashara, uoshaji wa Magari pamoja na Wakulima waliojishughulisha na kilimo cha mboga mboga ambao walikubali kuhama kupisha mradi wa maendeleo bila ua usumbufu”. Alisema Balozi Seif.

Alitoa wito kwa Wananchi wa maeneo mengine  Pemba na Unguja ambao wanatumia ardhi ya Serikali kwa kufanya shughuli zao binafsi wanapaswa  kujifunza kutoka kwa Wananchi wa Gombani kwa kuondoka bila ya malalamiko kupisha ujenzi wa Serikali.

Alielezea matumaini yake kwamba kukamilika kwa ujenzi wa Ofisi hizo Tatu Pacha na kuanza kutumika kwake kunatarajiwa kuimarisha huduma zinazotolewa na Wizara hizo Kisiwani Pemba.

Alisema katika kuimarishwa huduma hizo kwa Wananchi Serikali imepanga kuweka mifumo ya Kisasa ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ambayo kwa kiasi kikubwa huwa inachochea utendaji kazi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwahakikishia Wananchi wote wa Zanzibar kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendeleza na malengo yote ya Mapinduzi ambao ni kutoa huduma bora kwa Wananchi.

Mapema  akitoa Taarifa ya ujenzi wa Majengo pacha ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Gombani Chake chake Pemba Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Zanzibar Nd. Khamis Mussa Omar alisema Serikali kupitia Wizara ya Fedha iliandaa Programu ya ujenzi wa Majengo ya Taasisi za Serikali Unguja na Pemba.

Nd. Mussa alisema hatua hiyo imekuja kufuatria Ofisi nyingi za Serikali kukumbwa na changamoto ya uhaba wa Ofisi jambo ambalo lilisababisha watendaji wa Taasisi hizo kusoma uwajibikaji unaotakiwa.

Alisema ujenzi wa Ofisi Tatu Pacha za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Gombani Pemba umezingatia uhaba huo wa Ofisi ambapo zaidi ya Wafanyakazi 186 wa Wizara hizo walikuwa wakifanya kazi zao katika mazingira mabovu  ambayo Ofisi nyingi tayari zimechakaa.

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango alieleza kwamba ujenzi wa Ofisi pacha za SMZ Gombani umeanza mara baada ya kutiwa saini Mkataba wa Mradi huo mapema mwezi Julai Mwaka 2017 na ujenzi wake kuanza rasmi Oktoba Mwaka huo.

Alisema maendeleo ya ujenzi wa Mradi huowa sasa umeshafikia asilimia 52% ambapo hatua iliyofikiwa inakwenda na mkataba wa Ujenzi. Hata hivyo alisema wakati ujenzi ukiendelea Wizara hiyo kwa kuzingatia mfumo wa uwajibikaji wa ongezeko la Ofisi ilishauri kuwepo kwa Ofisi ya Tume ya Mipango wazo lililokubaliwa na Swerikali Kuu na hatimae kuongezwa kwa Ghorofa Moja zaidi ya Majengo hayo.

Ndugu Khamis Mussa Omar kwa niaba ya Wizara ya Fedha aliwaomba radhi Wananchi ambao ndio walipa kodi Wakuu kufuatia changamoto iliyotokea ya ujenzi wa Jengo la Wizara hiyo liliopo Tibirinzi Chake chake Pemba ambalo halikuwa katika kiwango kilichokubalika cha Ujenzi.

Alisema Taratibu za kisheria dhidi ya Mkandarasi wa ujenzi wa jengo hilo zimechukuliwa na tayari ameshafikishwa kwenye vyombo vya Sheria na kuilipa fidia Serikali kutokana na uzembe huo ambao aliahidi kwamba hautatokea tena.

Akimkaribisha Mgeni rasmi kwenye hafla hiyo ya uwekaji wa Jiwe la Msingi la Majengo Pacha ya SMZ Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar  Dr. Khalid Salum Mohamed alisema Teknolojia ya Kisasa inayokwenda kwa kasi tayari imeshakuwa haioani na Majengo mengi ya Taasisi za Serikali zilizopo hivi sasa.

Dr. Khalid alisema inapendeza kuona Taasisi nyingi za Serikali hivi sasa zimeanza kuelekea kwenye mfumo wa kisasa wa majengo yanayokwenda na mfumo wa dunia wa Mawasiliano ya Habari na Teknolojia.

Aliishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohamed Shein kwa kuridhia ujenzi wa Jengo Jipya la Bodi ya Mapato Zanzibar {ZRB} jirani na Mjego Pacha ya Ofisi za Serikali yaliyopo Gombani Mpya Chake Chake Pemba.

Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar alisema ujenzi wa Ofisi Mpya za Serikali uliomo ndani ya Utekelezaji wa Programu maalum inayosimamiwa na Wizara ya Fedha umekuja kutokana na kuongezeka kwa Mapato ya Taifa katika kiwango kinachokubalika.

Alisema hali ya kuongezeka huo kumechangia pia ongezeko la huduma kwa Wananchi hasa katika Sekta ya Afya, Elimu Kilimo na miradi mengine inayolenga kupunguza ukali wa maisha wa Wananchi walio wengi Visiwani Zanzibar.

Ujenzi wa Majengo Pacha ya Ofisi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar unaogharamiwa kwa asilimia 100% na Serikali ambao uko chini ya ujenzi na Wasimamizi Wakandarasi Wazalendo utararajiwa kugharimu zaidi ya Shilingi za Kitanzania Bilioni Saba, Milioni Mia Nane na 24.

Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idi akifungua pazia kuashiria kuweka jiwe la msingi la jengo litakalotumiwa na ofisi mbali mbali za serikali ya Zanzibar kisiwani Pemba.



 Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idi akikagua ujenzi wa jengo litakalotumiwa na wizara mbali mbali za serikali ya zanzibar  mara baada ya kuweka jiwe la msingi.


baadhi ya wananchi waliohudhuria na kushuhudia uwekaji wa jiwe la msingi wa majengo pacha yatakayotumiwa na wizara mbali mbali za serikali ya zanzibar ujenzi ambao unasimamiwa na Wizara ya Fedha na Mipango Zanzibar.


Muonekano wa majengo pacha yanayojengwa na serikali ya Zanzibar kwa ajili ya iofisi za wizara mbali mbali kisiwani Pemba. (Picha kwa hisani ya OMPR)

DK. KARUME ATAKA MIUNDO MBINU IINAYOJENGWA ITUNZWE, AITAKA WIZARA YA FEDHA KUWASAIDIA WAMILIKI WA MAJENGO YA MJI MKONGWE

NA MWINYIMVUA NZUKWI
Rais mstaafu wa Zanzibar Dk. Amani Abeid Karume amewataka wananchi wa Zanzibar kutunza na kuhifadhi miundombinu ya kiuchumi inayotengenezwa na serikali ili kukuza uchumi wa nchi na jamii kwa ujumla.

Akihutubia wananchi na watendaji mbali mbali wa taaisisi za serikali, binafsi na kisiasa katika uzinduzi wa ukuta wa bahari wa mizingani Dk. Karume aliyeiongoza serikali ya awamu ya sita, alisema kutotunzwa kwa miradi hiyo kutaisababishia hasara serikali na wananchi kwa ujumla.

Alisema mradi huo ambao ulibuniwa wakati wa uongozi wake, ulilenga kuondoa hatari iliyokuwa inayoukabili ukuta wa awali amabao ulijengwa mnamo mwaka 1920, kupunguza madhara ya maji ya mvua katika maeneo ya makaazi na kuipa haiba nzuri miji mikuu ya Zanzibar.

“Mradi huu umetekelezwa kwa fedha amabazo ni mkopo, hivyo msiposhiriki katika utunzaji wake licha ya kuwa tutaendelea kupata madhara lakini mjue kuna siku sote tutahusika katika malipo ya mkopo huu”, alitahadharisha Dk. Karume.

Aidha aliishauri wiraza ya fedha kuandaa mradi utakaolenga kuwasaidia wamiliki wa majengo yaliyomo ndani ya eneo la Mji Mkongwe wasio na uwezo wa kuyajenga au kuyafanyia ukarabati majengo yao ili kuuweka mji huo katika haiba na usalama zaidi.

“Nimefurahi kusikia kuwa awamu ijayo ya mradi huu (uimarishaji wa huduma za miji ya Zanzibar – ZUSP) kuwa utahusisha ukarabati wa jengo la Beit El Jaib, basi muongee na hawa wakubwa (benki ya dunia) kuona uwezekano wa kuwasaidia wamiliki wa majengo yaliyomo ndani ya Mji Mkongwe wawajengee uwezo wa kuyajenga upya majengo yaliyoanguka na kuyafanyia ukarabati yaliyokonga ili kuuongezea haiba na thamani mji huu ambao ni urithi wa kimataifa”, alisisitiza Dk. Karume.

Awali akimkaribisha Dk. Karume, Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar Dk. Khalid Salum Mohammed mbali ya kuishukuru benki ya dunia kwa kufadhili mradi huo, pia aliishukuru kwa kukubali kutoa fedha dola za marekani 55 milioni kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa ZUSP awamu ya pili utakaohusisha ujenzi wa jaa la kisasa litakalojengwa katika eneo la Kibele wilaya ya Kati Unguja.

“Miongoni mwa kazi nyengine ni pamoja na ujenzi wa njia za waenda kwa miguu katika barabara za Malindi – Darajani, Mkunazini – Kariakoo, uwekaji wa taa za barabarani katika barabara ya Mwanakwerekwe – Uwanja wa ndege na ujenzi wa mtaro mkubwa wa maji ya mvua utakaoanzia katika bwawa la Mwanakwerekwe – Magogoni – Sebleni – Kwa Abasi Hussein – Kinazini”, alisema Dk. Khalid.

Aidha aliishukuru benki ya dunia kwa misaada yake kwa serikali ya Zanzibar ambayo alisema imesaidia na kuchochea kasi ya maendeleo ya Zanzibar na wananchi wake na kuwapongeza wakandarasi na wasimamizi wa ujenzi wa ukuta huo kwa kumaliza kazi hiyo kwa ufanisi na kwa wakati uliopangwa.

“Hakika umahiri uliooneshwa na mjenzi, mshauri mwelekezi na msimamizi wa ujenzi wa mradi huu wa kumaliza kazi kwa viwango na wakati uliopangwa umeongeza Imani ya serikali kwenu na hakika mmejiwekea akiba njema katika kumbukumbu za ujenzi hapa Zanzibar”, alieleza Dk. Khalid.

Akitoa maelezo ya kitaalamu kuhusiana na ujenzi wa ukuta huo sambamba na utekelezaji wa mradi wa ZUSP katibu mkuu wa wizara ya fedha na mipango Zanzibar alisema mradi huo uliosainiwa mwaka 2009 na kuanza utekelezaji wake april 2010, kwa kuhusisha maeneo manne makuu ya ujenzi wa ukuta huo wenye urefu wa mita 312 kuanzia bustani ya forodhani hadi mizingani.

Maeneo mengine ya mradi huo ni ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami yenye urefu wa mita 308 na upana wa mita 6, ujenzi wa njia za waenda kwa miguu, vibaraza vya kupumzikia, uekaji wat aa za barabarani na ujenzi wa njia za maji ya mvua kuelekea katika bahari ya hindi kazi iliyokamilika na kukabidhiwa serikalini mwezi septemba mwaka uliopita.

Kwa upande wa gharama za Ujenzi jumla ya Shilingi za Kitanzania bilioni 7,636,056,400/- zilitumika. Fedha hili ni bila ya ongezeko la thamani ambalo linakisiwa kuwa ni shilingi za Kitanzania milioni 763,605,640 na kwa upande wa malipo ya mkandarasi, malipo yote stahiki tayari yamelipwa na malipo yaliyobakia ni ya mwisho (retention payment), malipo hayo hufanywa baada ya kumalizika kwa muda wa uangalizi wa ubora yaani “Defect Liability Period”, alisema na kuongeza kuwa fedha hizo ni mkopo wa masharti nafuu kutoka benki ya dunia.

Akitoa salamu za benki ya dunia, mwakilishi wa benki hiyo nchini Tanzania Andre Bald alisema taasisi yake imeridhishwa kufikiwa kwa viwango katika ujenzi wa ukuta huo na utekelezaji wa mradi mzima hivyo itaendelea kuisaidia Zanzibar na Tanzania ili kuweka viwango bora vya maisha ya watu wake.

“Benki ya dunia kila mara huzingatia upatikanaji wa huduma bora za maisha ya watu hivyo kila mtakapofikiria njia bora za kuimarisha maisha ya watu sisi hatutosita kusaidia hasa pale kunapokuwa na utekelezaji unaoashiria matokeo bora kama ilivyo katika mradi huu wa uimarishaji wa huduma za miji ya Zanzibar”, alisema Bald.

Uzinduzi wa ukuta huo ulifanyika katika eneo la Mizingani na bustani ya Forodhani ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya sherehe za miaka 54 ya mapinduzi ya Zanzibar ambapo mbali ya Dk. Karume viongozi wengine waliohudhuria hafla hiyo ni waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala bora maalim Haroun Ali Suleiman, mke wa Dk. Karume Mama Shadya Karume, Naibu Waziri wa Ujenzi, mawasiliano na uchukuzi Mohammed Ahmada Salum, wenyeviti wa chama cha mapinduzi (CCM) mikoa ya Mjini na Magharibi (kichama) na viongozi wa dini akiwemo katibu wa mufti wa Zanzibar sheikh Fadhil Suleiman Soraga.


Rais Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dk. Aman Abeid Karume akikata utepe kuashiria Uzinduzi wa matumizi ya eneo la Ukuta wa kuzuia maji ya bahari katika eneo la  Mizingani Mjini Zanzibar ikiwa ni shamra shamra za Maadhimisho ya kutimia  Miaka 54 ya Mapinduzi ya Zanzibar. Kulia yake ni Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Khalid Salum Mohammed na kushoto ni Mwakilishi wa Benki ya Dunia Andre Bald.     

Rais Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dk. Aman Abeid Karume (Kushoto) akipata maelezo kutoka kwa  Mratibu wa Mradi wa Huduma za Jamii Mijini (ZUSP) Makame Ali Makame kuhusiana na ujenzi wa ukuta wa Baharini katika uzinduzi wa ukuta huo katika eneo la Mizingani Mjini Zanzibar.

  Rais Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dkt,Aman Abeid Karume  (katikati) akitembea kwa miguu baada ya uzinduzi wa  Ukuta wa Baharini Mizingani kuelekea katika Bustani ya Forodhani  Mjini Zanzibar. Wengine kutoka kulia ni Mratibu wa mradi wa ZUSP Mkame Ali Makame, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Ayoub Mohammed Mahmoud, Waziri wa fedha na mipango Zanzibar Dk. Khalid Salum Mohammed na Katibu Mkuu wizara ya fedha na mipango Khamis Mussa Khamis.


Mwakilishi wa Benki ya Dunia Andre Bald akitoa salamu za taasisi yake juu ya utekelezaji wa miradi mbali nchini inayofadhiliwa na beki hiyo ukiwemo ujenzi wa ukuta wa Baharini katika eneo la Mizingani sherehe zilizofanyika katika Bustani ya Forodhani Mjini Zanzibar.


Rais Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dk. Aman Abeid Karume akisisitiza jambo alipokuwa akihutubia hadhara (haipo pichani) wakati wa uzinduzi wa ukuta wa baharini wa Mizingani sherehe zilizofanyika katika Bustani ya Forodhani Zanzibar. Kulia ni waziri wa fedha na mipango Zanzibar Dk. Khalid Salum Mohammed na kushoto ni Mwakilishi wa Benki ya Dunia nchini Andre Bald.




1. Baadhi ya wafanyakazi wa Wizara ya fedha na Mipango Zanzibar na wageni waalikwa waliohudhuria katika uzinduzi wa ukuta wa baharini wa Mizingani sherehe zilizofanyika katika Bustani ya Forodhani Mjini Zanzibar zikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Miaka 54 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Friday, January 5, 2018

DK. SHEIN AZINDUA SOKO JIPYA LA TIBIRINZI, PEMBA

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema kuwa miongoni mwa malengo ya Mapinduzi matukufu ya Januari 12, 1964 ni kufanya hali za maisha ya Wazanzibari kuwa bora na ujenzi wa soko la Tibirinzi ni miongoni mwa malengo hayo na sio kichocheo cha kubaguana kwa vyama, dini, jinsia au mahala mtu anapotokea.

Dk. Shein amesisitiza kuwa jengo hilo jipya la soko ni ukombozi kwa wakulima, wafanyabiashara, wafugaji, wavuvi na wajasiriamali pamoja na wananchi wote kwa jumla kwa kuweza kuongeza kipato chao ili maisha yao yaweze kuwa bora.
Rais Dk. Shein aliyasema hayo leo mara baada ya kulizindua soko jipya la Tibirinzi Chake Chake Pemba.

Dk. Shein alisemakuwa soko hilo si vyema likahusishwa na masuala ya kisiasa kwani ni soko la watu wote wa vyama vyote, dini zote na jinsia zote huku akiwataka wafanyabiashara watakaolitumia soko hilo kuleta bidhaa zenye ubora zitakazolingana na hadhi ya soko hilo.
Alisema kuwa ujenzi wa soko hilo ni katika hatua za kutafsiri Mapinduzi ya mwaka 1964 kwa vitendo kwa kuwaletea wananchi maendeleo zaidi bila ya ubaguzi.

Alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatekeleza Sera mbali mbali zikiwemo zinazolenga kuinua kipato cha wananchi na kupunguza umasikini.

Sambamba na hayo, Dk. Shein alisisitiza haja ya kulitunza na kulienzi soko hilo ikiwa ni pamoja na kudumisha usafi wa soko hilo kwani usafi ni jambo la lazima na halina mbadala.

Dk. Shein alitumia fursa hiyo kueleza mafanikio sambamba na azma ya Mapinduzi Matukufu ya Januri 12, 1964 ambayo yamewakomboa wananchi wa Zanzibar na kukata minyororo ya chuki na udhalimu sambamba na kunyanyaswa.

Alieleza madhumuni makubwa ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kuwa huru na hatua ambayo imepekea kupanga mambo bila ya kuingiliwa na mtu na kuweza kuongoza nchi sambamba na kuandaa mipango ya muda mrefu na muda mfupi na wakati.

Alieleza kuwa Zanzibar imepata maendeleo makubwa katika kukuza uchumi wake ndani ya kipindi cha miaka 54 huku akieleza kuwa mabadiliko makubwa ya kiuchumi, sera ya serikali maisha ya watu ambayo yote hayo ni maendeleo.

“Leo naambiwa ndege zinazokuja Pemba hivi sasa hazitoshi, meli hazitoshi watu wanasafiri kila leo hayo yote ni maendeleo na kukua kwa uchumi.. jengo hilo ni lazima tulipe heshima yake” Alisema Dk. Shein.

Nae Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Hamad Rashid Mohammed alieleza kuwa kuna kila sababu ya kumuenzi na kumuombea dua Rais Dk. Shein kwa maendeleo makubwa sambamba na juhudi anazozichukua katika kuwaletea maendeleo wananchi wa Zanzibar.

Waziri Rashid alisema kuwa maendeleo yanayoonekana na kwa mara ya kwanza katika historia wafanyakazi wameweza kulipwa mshahara mara mbilili wanaopata, kuzalisha mpunga tani 39 elfu, kuwepo na mchele kutoka Zanzibar pamoja na maendeleo mengineyo ikiwemo kuimarika kwa miundombinu.

Aliongeza kuwa Rais Dk. Shein kuwa Zanzibar imebaki salama kutokana na hekima yake na hakuna mpasuko na kumekuwa na amani kubwa kwani huwezi kupata maendeleo kama hakuna amani ya nchi.

Alieleza kuwa Dk. Shein ni kiongozi anaetaka kila mmoja kutoa maamuzi na kumshirikisha kufanya hivyo na ndicho kilichomfanya Dk. Shein kuweza kuwatumikia watu tena bila ya ubaguzi.

“Kina Mzee Karume wasingeweza kupindua nchi kama wasingekuwa na nia nzuri… Mwenyezi Mungu peke yake ndie anaechagua kiongozi.. kwani katika mazingira haya nani angelijua kuwa Hamad Rashid angekuwa Waziri wa Kilimo…unapomkuta kiongozi anajenga fitna kwa watu anajenga fitna kwa watu, unapomkuta kiongozi anajenga makundi hata salamu alaykum haitikiii ni kweli huyu mtu wa peponi?”,aliuliza Hamad Rashid.

Waziri Rashid aliwataka baadhi ya wananchi kisiwani humo kuwacha siasa na badala yake washughulikie mambo ya msingi na yenye kuleta maendeleo huku akieleza kuwa Serikali inalengo la kujenga masoko makubwa mawili huko Malindi mjini Zanzibar na soko jengine litajengwa huko kiswani Pemba.

Mapema Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Joseph Abdalla Meza alieleza kuwa soko hilo ni kati ya masoko manne yaliojengwa Zanzibar kupitia Programu ya Miundombinu ya Masoko, Uongezaji Thamani na Huduma za Kifedha Vijijini (MIVAP) inayogharamiwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aliongeza kuwa program hiyo inasimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi kwa Zanzibar na kueleza kuwa ujenzi wa soko hilo ulianza mwezi wa Aprili 2016 ambapo wazabuni 12 waliomba kufanya kazi hiyo na baada ya tathmini Kampuni ya ZECCON LIMITED ya Zanzibar ndiyo iliyoibuka mshindi na kupata tenda hiyo na kuingia mkataba wa ujenzi kwa gharama za TZS Milioni 972.2 ambapo kati ya hizo milioni 48.6 zimetolewa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Alisema akuwa soko hilo lina vibaraza 76 vitakavyokabidhiwa kwa wafanyabiashara ambapo soko hilo lina chumba cha baridi kwa ajili ya kuhifadhia samaki na chumba maalum kilichotengwa kuwekewa mtambo wa kutengenezea barafu ambao utawasaidia wavuvi kutumia barafu hizo wakati wakiwa baharini.
CHANZO: Ikulu - Zanzibar

Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohammed Shein akihutubia wananchi walihudhuria kushuhudia uzinduzi wa soko la kisasa liliopo Tibirinzi. Kulia ni Mhamoud Thabit Kombo waziri wa Afya Zanzibar.


Muonekano wa soko jipya la Tibirinzi baada ya kukamilika kwa ujenzi wake katika eneo la Chake chake mkoa wa Kusini Pemba,