Saturday, November 25, 2017

Na Othman Khamis, OMPR
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema Zanzibar na Oman zitaendelea kufanya kazi pamoja  katika lengo la kudumisha uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu kwa maslahi na maendeleo ya wananchi wa nchi mbili hizo.
Alisema Ushirikiano huo umeimarika zaidi kwa Zanzibar  kupokea ufadhili wa Vijana wake wanaopata fursa za kujiunga na Masomo ya juu Nchini Oman katika fani mbali mbali za mafunzo ikiwemo Udaktari, Uhandisi, Kompyuta pamoja na Lugha.
Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati wa mazungumzo yake na Balozi Mpya wa Oman Nchini Tanzania Bwana Ali Abdulla – Al Mahrouq  aliyefika Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar kujitambulisha rasmi akiambatana pia na Balozi Mdogo wa Oman aliyepo Zanzibar Dr. Ahmed Hamood Al - Habsi.
Alisema Zanzibar inafurahia kuendelea kuwepo kwa uhusiano huo wa kipekee na wa kupigiwa mfano ambao umekuwa ukileta faraja na matunda mazuri yanayotowa fursa zaidi kwa Zanzibar kutanua wigo wa Kimaendeleo na kuongeza maeneo mengine ya ushirikiano wa Kisiasa, Kiuchumi na Kiutamaduni.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimueleza Balozi  Ali Abdulla – Al Mahrouq  kwamba uungaji  mkono wa Oman kwa Zanzibar hasa katika utanuzi wa Chuo cha Sayansi ya Afya Mbweni umeleta faraja kwa Wananchi walio wengi kwenye huduma za Afya zinazotarajiwa kuenea katika masafa yasiyozidi Kilomita Tano.
Balozi Seif aliipongeza  Serikali ya Oman kwa msaada wake mkubwa  inayoendelea kutoa kwa Zanzibar hasa kwa kukubali kugharamia matengenezo makubwa ya Majengo ya Kihistoria ya Beit el ajab na Jumba la Makumbusho ya Kifalme yaliyopo Forodhani Mjini Zanzibar.
Alisema msaada huo wa Majengo hayo muhimu umekuja wakati muwafaka kwa vile utasaidia kuhifadhi Historia ya Kiutamaduni na Kiutawala  ya Visiwa vya Zanzibar inayohusisha pia mafungamano  ya Majengo hayo na Oman.
Akigusia ujio wa Meli ya Kifalme ya Fulk Al Salamah kutoka Nchini Oman Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alieleza wazi kwamba Zanzibar imepata faraja  kubwa ya ziara ya Ujumbe wa Serikali ya Oman uliowasili Zanzibar na Meli hiyo ya Kifahari.
 Alisema Wananchi wa Zanzibar wamepata kujifunza mambo mbali mbali kufuatia ujio wa Meli hiyo kwa kupata taaluma ya kuepuka masuala mazima yanayotokana na Sekta ya mafuta ambayo kwa sasa Visiwa vya Zanzibar vimo katika matayarisho ya awali ya kuendesha Miradi inayotokana na Sekta hiyo.
Akigusia suala la Majanga Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  ameishukuru Serikali ya Oman kwa msaada wake wa kuwawezesha Viongozi Wanne Waandamizi wa Zanzibar kupata fursa ya kujifunza  mbinu na Taaluma ya jinsi ya kujikinga na Majanga.
Balozi Seif alisema mafunzo hayo yameleta faida kubwa kiasi kwamba Oman ingefikiria tena kutoa nafasi nyengine kama hizo kwa watendaji wengine wa Taasisi za Majanga Zanzibar  kupata fursa kama hizo katika kipindi chengine kijacho.
Mapema Balozi Mpya wa Oman Nchini Tanzania  Bwana Ali Abdulla – Al Mahrouq  alisema udugu uliopo wa Viongozi  pamoja na hata Wananchi wa kawaida wa Oman na Zanzibar  ni vyema ukaongezeka zaidi katika uhusiano wa masuala ya Kibiashara.
Balozi Al – Mahrouq  alisema pande hizo mbili zimekuwa na historia ndefu ya Kiutamaduni na Kisiasa kiasi kwamba kwa sasa nguvu zikaongezwa katika uimarishaji zaidi wa Kibiashara jambo ambalo linaweza kustawisha kuongeza ukaribu  wa Wananchi wa pande hizo mbili  unaoweza kudumu milele.
Balozi huyo wa Oman Nchini Tanzania alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Serikali ya Oman itaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuhakikisha harakati za Maendeleo na Ustawi wa Jamii wa Wananchi wa Zanzibar unazidi kukua.

Balozi Mpya wa Oman Nchini Tanzania Bwana Ali Abdulla – Al Mahrouq (kushoto)  akijitambulisha rasmi kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi (katikati) alipofika katika Ofisi za Makamu huyo wa Vuga Mjini Zanzibar. Wengine ni Balozi Mdogo wa Oman aliyepo Zanzibar Dr. Ahmed Hamood Al – Habsi (wa kwanza kulia) na Naibu Waziri Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mihayo Juma Nhunga.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi (kulia) akimkabidhi zawadi ya Mlango wa Zanzibar (Zanzibar door) Balozi Mpya wa Oman Nchini Tanzania Bwana Ali Abdulla  Al-Mahrouq kama ishara ya kufungulia Milango ya uwepo wake nchini.

.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi (kulia) akiagana na Balozi Mpya wa Oman Nchini Tanzania Bwana Ali Abdulla  Al - Mahrouq (kushoto) mara baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliyofanyika katika ofisi za balozi Seif Vuga Zanzibar. (Picha na OMPR).

Wednesday, November 22, 2017

MASHEHA WA MJINI MAGHARIBI WAPEWA DOZI YA UGATUZI

Na Mwinyimvua Nzukwi

MKUU wa Mkoa Mjini Magharibi Ayoub Mohammed Mahmoud amewataka Masheha wa Mkoa huo kuzingatia katiba, sheria, sera, kanuni na miongozo mbali mbali ya nchi katika utekelezaji wa wajukumu yao ili kuwahudumia wananchi kwa ufanisi.

Akifungua mafunzo elekekezi ya siku mbili kwa masheha wa hao kuhusu dhana ya ugatuzi wa madaraka kutoka serikali kuu kwenda serikali za mitaa yaliyofanyika katika ukumbi wa zamani wa Baraza la wawakilishi Kikwajuni mjini Zanzibar.

Alisema masheha kama watendaji wa awali wa serikali kuu, wana wajibu wa kisheria wa kuhakikisha wanasimamia mipango ya maendeleo na utowaji wa huduma bora kwa wananchi bila ya kujali itikadi zao kisiasa, dini, kabila na rangi kwa maslahi ya shehia zao na taifa kwa ujumla.

Mahmoud alieleza kuwa kupitia mpango wa ugatuzi, masheha wana nafasi ya kuratibu mipango itakayoandaliwa katika ngazi za serikali za mitaa, wilaya na Mkoa, hivyo wanatakiwa kutumia mafunzo hayo kuimarisha utendaji na kuhakikisha mpango huo unafanikiwa.

Akitoa maelezo katika mafunzo hayo Mkurugenzi wa Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa kutoka katika wizara ya nchi ofisi ya rais, tawala za mikoa, serikali za mitaa na idara maalum za serikali ya mapiduzi ya Zanzibar Khalid Abdallah Omari alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea  uwezo masheha kuhusu wajibu na maadili ya kiongozi wa umma.

Aidha alisema mafunzo hayo yamelenga kukumbushana wajibu wa utekelezaji wa majukumu yao watendaji hao ili kuepusha mgongano na muingiliano wa majukumu kati ya serikali kuu na serikali za mitaa.

Nae Mkuu wa Wilaya ya Mjini Unguja Marina Joel Thomas aliwataka masheha hao kuwashajihisha wananchi katika maeneo yao kushiriki katika uuandaji na utekelezaji wa wa miradi mbali mbali ya maendeleo ili kustawisha upatikanaji wa huduma mbali mbali za kijamii.

Mafunzo hayo ya masheha yaliyoandaliwa na wizara ya nchi ofisi ya Rais tawala za Mikoa Serikali za mitaa na idara maalum ni muendelezo wa mafunzo yanayotolewa kwa watendaji wa ngazi mbali mbali za uongozi na utawala ili kuleta ufanisi katika utekelezaji wa mpango wa ugatuzi ulioanza kutekelezwa rasmi katika sekta ya elimu ya awali na msingi, afya na kilimo mnamo mwezi julai mwaka huu.


Katika mafunzo hayo viongozi hao walifundishwa mambo mbali mbali ikiwemo wajibu wa masheha kwa mujibu wa sheria ya Tawala za Mikoa namba 8 ya mwaka 2014 , muelekeo wa mkakati wa upelekaji wa madaraka kwa wananchi, umuhimu wa kuweka kumbukumbu, kanuni za usuluhishi wa migogoro katika ngazi za shehia na sheria za usimamizi wa masuala ya ardhi.  


Mkuu wa wilaya ya Mjini Marina Joel Thomas (kushoto) akimuongoza Mkuu wa mkoa wa Mjini Magharibi Ayoub Mohamed Mahmoud (kulia) kuondoka katika ukumbi wa zamani wa baraza la wawakilishi baada ya kufungua mafunzo ya masheha kuhusu ugatuzi wa madaraka kutoka serikali kuu kwenda serikali za mitaa. Nyuma ya Mahmoud ni mkuu wa wilaya ya Magharibi ‘A’ Capt. Khatib Khamis Mwadini.


MKUU wa mkoa wa Mjini Magharibi Ayoub Mohamed Mahamoud akitoa hutuba ya ufunguzi wa mafunzo kwa masheha wa shehia za mkoa huo kuhusiana na dhana ya ugatuzi wa madaraka kutoka serikali kuu kwenda katika serikali za mitaa. Wa kwanza kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Mjini Marina Joel Thomas

Tuesday, November 21, 2017

KATIBU WA ZAMANI ZFA KUWA MJUMBE WA KAMATI YA CHALENJI

Na Mwinyimvua Nzukwi
Makamo wa Rais wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA - Unguja) Mzee Zam Ali ameteuliwa kuwa mjumbe katika kamati itakayosimamia Mashindano ya Chalenji yaliyoandaliwa na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) yanayotarajiwa kuanza  Disemba 3 hadi 17 mwaka huu nchini Kenya.
Taarifa iliyotolewa na CECAFA imeeleza kuwa Zam ambaye aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa ZFA kwa muda mrefu imeeleza kuwa imefikia uamuzi huo kutokana na uzoefu alionao katika Mashindano mbali mbali yakiwemo mashindano hayo.
Wajumbe wengine waliochaguliwa kuunda kamati hiyo ni Mutasim Gafar kutoka nchini Sudan, Abdigaan Arab Said kutoka Somalia, Jacob Odundo kutoka Kenya, Ashinafi Ejigu wa Ethiopia, Aimable Habimana wa Burundi, Rogers Byamukama wa Uganda, Ajong Domasio Ajong wa Sudan ya Kusini na Ahmed Mgoyi kutoka Tanzania Bara.
Wajumb wengine na nchi wanazotoka katika mabano ni Sunday Kayuni (Tanzania Bara), Mossi Yussuf (Burundi), Celestine Ntangugira (Rwanda), Yigzaw Ambaw (Ethiopia), Bernard Mfubusa (Burundi), Maxim Itur (Kenya), Rogers Mulindwa (Uganda), Bonny Mugabe (Rwanda), Gishinga Njoroge (Kenya), Amir Hassan (Somalia) na Nicholas Musonye (Kenya).
Mashindano hayo yanatarajiwa kushirikisha timu 10 za Tanzania bara, Zanzibar, Kenya, Rwanda na wageni waalikwa Libya zilizopo katika kundi 'A' wakati kundi 'B' linaundwa na timu za Sudani ya Kusini, Ethiopia, Burundi, Uganda na wageni waalikwa Zimbabwe.

 

Saturday, November 18, 2017

UJUZI MDOGO KATIKA BIASHARA KIKWAZO KWA WAJASIARIAMALI TANZANIA

Na Mwinyimvua Nzukwi
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema Tanzania ina idadi kubwa ya Wajasiriamali lakini ni kidogo kati yao ndio wenye ujuzi wa usimamizi wa biashara, taarifa na maarifa  yanayohitajika  kukuza biashara zao.
Alisema hali hiyo hupelekea biashara nyingi kufa kutokana na kushindwa kuendana na mahitaji halisi ya kisekta na kushindwa kuhimili ushindani wa soko.
Balozi Seif alieleza hayo wakati akifungua Semina ya Mafunzo ya Fursa kwa vijana wajasiriamali yaliyoandaliwa na taasisi ya Fursa Tanzania katika Ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakishi  Kikwajuni Mjini Unguja.
Alisema Serikali ipo tayari kushirikiana na waandaaji wa semina hiyo ili kutengeneza na kutekeleza mikakati itakayojenga mazingira bora na wezeshi kibiashara itakayoweka miundombinu itakayosaidia maendeleo ya wajasiriamali na vijana nchini.
Alisema Tanzania inatekeleza sera ya uchumi wa viwanda azma ambayo katika kufikia hilo, kundi la wajasiriamali lazima lizalishwe kwa wingi ili kuanzisha, kukuza na kuendeleza viwanda hivyo na kutengeneza ajira, kuchochea uvumbuzi na kuhamasisha ushindani wa soko.
 “Fursa imekuwa ikizunguka nchi nzima ili kuzungumza na vijana kuwaonesha namna wanavyoweza kujiendeleza na kuendeleza shughuli zao. Hili ni jambo zuri hasa wakati huu tunapozungumzia uchumi wa viwanda na kuelekea katika uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025”, alisema balozi Seif.
Mapema Muanzilishi wa Taasisi hiyo ambae pia ni msimamizi wa programu ya mafunzo ya iliyolenga kuwakomboa Vijana na Maisha duni Ruge Mutahaba alisema  kuna haja kwa wajasiriamali nchini kubuni maradi au biashara kwa kuzingatia mahitaji ya jamii yake na fursa zinazomzunguka ili kuongeza thamani na kipato cha bidhaa anazozalisha.
Ruge alieleza kuwa wakati umefika kwa jamii kuondokana na mawazo yanayoviza upeo wa ufikiri na kuelewa ku wa mabadiliko yanaanza na mtu binafsi kwa kuzingatia mahitaji yake na mahitaji ya ndani ya jamii.
“Vijana mnaomaliza masomo na wale mlioko vyuoni ni lazima mjuwe kuwa kutokana na ufinyu wa fursa za ajira kitaifa na kimataifa mnalazimika kujitengenezea ajira nyinyi wenyewe zitakazowaongoza kuendesha maisha yenu kwa amani na furaha hapo baadae”, alisema Ruge ambae pia ni mkurugenzi wa Clouds Media Group.
Akitoa salamu za mashirika ya Umoja wa Mataifa (UN) yanayofanyakazi nchini Tanzania, Mratibu Mkaazi wa umoja huo Alvaro Rodriguez alisema Umoja wa Mataifa kupitia taasisi na mashirika yake utaendelea kutoa taaluma kwa makundi mbali mbali ya jamii wakiwemo wanawake kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kujiendesha Kimaisha.
Alisema hakuna taifa lolote ulimwenguni linaloweza kupiga hatua za maendeleo ya kiuchumi bila ya mchango wanawake huvyo ilizitaka serikali za Tanzania kuendelea kutoa msukumo kwa kundi hilo kujiendeleza kiuchumi sambamba na kujengewa mazingira mazuri ya kufikia malengo yao.
“Mashirika ya Umoja wa Mataifa yataendelea kushirikiana na taasisi ya Fursa Tanzania ili kusaidia kupunguza au kuondosha changamoto zinazowakabili vijana na wanawake katika kujikomboa kiuchumi”, alisema Rodriguez.
Awali akimkaribisha mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Ayoub Mahmoud Mohamed aliwakumbusha vijana haja ya kuchangamkia fursa za ajira hasa katika sekta za utalii na uvuvi zinazopatikana kwa wingi katika visiwa vya Unguja na Pemba.
Alisema serikali ya Zanzibar imetekeleza wajibu wake kwa kuimarisha miundombinu ya kuwawezesha vijana kujiajiri kwa kuweka sera na mipango mbali mbali ili waweze kuendesha maisha yao katika misingi ya amani na utulivu.
“Serikali kazi yake kubwa ni kutengeneza mazingira rafiki ili jamii na wageni waendeshe maisha yao kwa kuzingatia misingi ya amani na Utulivuhivyo niwatie moyo na kuwaomba kuzitumia kikamilifu fursa zilizopo mkatika sekta ya utalii ambayo inachangia karibu asilimia 27 ya pato la Taifa na ambayo imezalisha zaidi ya ajira 88,000 ambazo nyingi zimechukuliwa na wageni kutokana na wazawa kutochangamkia fursa”, alieleza Ayoub.

Semina hiyo ya kiuchumi ni mwendelezo wa majukwaa yaliyofanyika katika mikoa 13 ya Tanzania bara na Zanzibar kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa makundi mbali ya jamii juu ya namna ya kutumia fursa zinazowazunguka kuzalisha ajira a kukuza uchumi wao ambapo kwa mwaka huu imebebe ujumbe wa anzia sokoni.
Baadhi ya washiriki wa Semina ya  Mafunzo ya kuwajenge uwezo vijana wa kupata fursa za ajira wakiimba wimbo wa Taifa kabla ya kufunguliwa kwa semina hiyoiliyofanyika katika ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi Kikwajuni Zanzibar.
 Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akihutubia washiriki wa Semina ya Mafunzo ya Fursa kwa Vijana Wajasiriamali iliyoandaliwa na taasisi ya Fursa Tanzania alipokuwa akiifungua rasmi.
Muanzilishi ambae pia ni msimamizi wa programu ya mafunzo wa taasisi ya Fursa Tanzania Ruge Mutahaba  akitoa darsa kwa Vijana walioshiriki wa Semina ya Mafunzo ya Fursa kwa Vijana Wajasiriamali Zanzibar.
Mratibu nmkaazi wa Umoja wa Mataifa (UN) nchini Tanzania Alvaro Rodriguez akitoa salamu katika ufunguzi wa Semina ya Mafunzo ya Fursa kwa Vijana Wajasiriamali Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akishikili nembo ya taasisi ya Fursa Tanzania inayotoa ujumbe wa 'Nipo Tayari katika Kampeni ya Kitaifa ya usafi wa Mazingira' mara baada ya kufungua semina ya kutambua fursa za ajira kwa vijana. Kuliakwake ni Mratibu Mkaazi wa Umoja wa Mataifa (UN) nchini Tanzania Alvaro Rudreguez, Mbunge wa Jimbo la Mpendae Salum Turky (mwenye kofia) na Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Ayoub Mahmoud Mohamed. (Picha kwa hisani ya OMPR).

UJENZI WA JENGO LA ABIRIA UWANJA WA NDEGE WA KIMATAIFA ZANZIBAR KUENDELEA MWEZI UJAO

Na Mwinyimvua Nzukwi, Zanzibar
UJENZI wa jengo jipya la abiria  katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Abeid Amani Karume Zanzibar unatarajiwa kuendelea mwezi ujao baada ya kukamilika kwa mazungumzo kati ya serikali ya Zanzibar na serikali ya China ili kurahisisha upatikanaji wa huduma bora za usafiri wa anga  kwa abiria  wanaotumia  uwanja huo.
Akitoa taarifa ya serikali kwa Waandishi wa Habari mjini Unguja, Waziri wa Fedha na Mipango zsanzibar Dk. Khalid Salum Mohammed amesema ujenzi huo ambao ulisisima kwa muda mrefu, unatarajiwa kuendelea kuanzia katikati ya mwezi Disemba kufuatia serikali ya watu wa china kutoa dhamana ya mkopo wa ziada kwa serikali ya Zanzibar kugharamia ujenzi huo kutoka katika benki ya Benki ya Exim ya China.
Alisema kusimama kwa mradi ambao ni miongoni mwa miradi ya uimarishaji wa uwanja huo, ulitoakana na kubadilika kwa muundo wa ujenzi wa jengo hilo uliozingatia mahitaji mapya ya shirika la usafiri wa anga dulinani (ICAO) hali iliyopelekea kuongezeka kwa gharama za ujenzi zilizopangwa awali.
Alisema awali mradi huo ulipangwa kutumia dola milioni 70.4 za marekani ambazo ni mkopo wa masharti nafuu ambazo ziliongezeka na kufikia dola million 128.7 ambazo serikali ya Cina ilishauri zitafutwe mahali pengine na kupelekea kusimama kwa ujenzi huo uliohusisha ujenzi wa jengo hilo, upanuzi wa eneo la maegesho kwa zaidi ya mita za mraba 38,000 na maegesho ya magari ya watumiaji wa uwanja huo.
“Tatizo kubwa lililojitokeza ni upatikanaji wa huizo fedha za ziada, lakini baada ya mashauriano ya muda mrefu kati ya SMZ (Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar), SMT (Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania) na serikali ya jamhuri ya watu wa china yaliyochukua muda mrefu hatimae benki ya exim imekubali kudhamini mkopo wote wa kugharamia ujenzi huo kwa taratibu za mkopo wa masharti nafuu badala ya masharti ya kibiashara kama ilivyopendekeza awali”, alieleza Dk. Khalid na kuwashukuru wadau wote waliofanikisha kutatua changamoto hizo.
Alisema serikali imepigania kutatua changamoto zilizojitokeza kwa kuamini kuwa kukamilika kwa ujenzi huo utapelekea kuimarika kwa  huduma za kusafirisha abiria na mizigo sanjari na kuzihudumia ndege zitakazotua uwanjani hapo kwa kuzingatia viango vya kimataifa.
“Katika miradi iliyotangulia, tuliimarisha huduma za kiusalama kwa kununua magari mapya ya zimamoto pamoja na kuweka vifaa vya ulinzi na usalama  ili kuimarisha  hali ya usalama katika  eneo hilo  hususani watalii  ambao wana mchango muhimu  katika uchumi wa Zanzibar”, alisisitiza wazir Khalid.
Nae Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Balozi Ali Abeid Karume alisema Wizara yake itahakikisha inasimamia kikamilifu ujenzi huo ili uweze kumalizika kwa wakati na kwa ubora uliokusudiwa kwa lengo la kukuza uchumi wa Zanzibar.
Alisema ili kufanikisha hilo imeanza mawasiliano na wizara nyengine ili kuweka mazingira mazuri ya upatikanaji wa rasimilali za ujenzi na kwamba wameshapatiwa maeneo yatakayotumika kwa ajili ya upatikanaji wa mchanga na kifusi ili kuharakisha ujenzi huo.
“Kwa mujibu wa makubaliano mapya, wizara yangu ndiyo itakuwa mwajiri katika mradi huu na tumeshajipanga kuona ni kwa namna gani mradi huu unakamilika kwa wakati na kwa viwango vilivyokusudiwa kwa kuweka wasimamizi wa kazi mbali ya mshauri elekezi, hivyo hakuna kazi itakayotekelezwa na mkandasi au kukubaliwa kabla na sisi kujiridhisha”, alieleza balozi karume.
Aidha alieleza kuwa uwanja huo utakapokamilika unatarajiwa kuwa na uwezo wa kuhudumia abiria  million 1.6 kwa mwaka na  kukabiliana kwa kiasi kikubwa na tatizo la kuchelewa kuhudumiwa kwa abiria wanaowasili au kuondoka kutokana na jengo linalotumika sasa kuwa na uwezo wa kuhudumia watu laki 5 kwa mwaka.
Akifafanua baadhi ya hoja za waandishi, katibu mkuu wa wizara ya fedha na mipango Zanzibar khamis mussa khamis alisema kuendelea kwa ujenzi huo kutapelekea uwanja huo kuweza kupokea ndege za aina zote isipokuwa air bus 3 na kwamba hadi sasa mkandarasi kampuni ya Beijing Construction & Engineering Group ameshalipwa kiasi cha dola 35.2 milioni kwa kazi alizofanya awali.
“Sisi (serikali ya Zanzibar) tulisita kukubali kuingia katika mkopo wenye masharti ya kibishara kwa kujua kuwa usingekuwa na nafuu kama huu ambao ndani yake una ruzuku lakini pia una riba ya asilimia 2 lakini pia una muda mrefu wa malipo ambao ni miaka 25 baada ya kumalizika kwa kipindi cha kujizuia kulipa ambacho kinadhaminiwa na serikali ya china”, alifafanua Katibu Mkuu huyo.

Mradi huo unatarajiwa  kugharimu  Jumla ya Dola za marekani Million 128 utakamilika baada ya kipindi cha miezi 18 kuanzia mwezi ujao, unatarajiwa kuanza majaribio ya awali mnamo mwezi agosti 2019 kabla ya kukabidhiwa rasmi serikalini mwezi disemba mwaka huo.
Waziri wa fedha na Mipanzo Zanzibar Dk. Khalid Salum Mohamed

Tuesday, November 14, 2017

RC MAHMOUD AHITIMISHA ZIARA YAKE KWA KUHIMIZA UWAJIBIKAJI

Na Mwinyimvua Nzukwi
WATENDEJI na viongozi wa Mkoa wa Kaskazini wametakiwa kubadilika na kutumia falsafa za ‘hapa kazi tu’ na ‘kutofanya kazi kwa mazowea’ ili kuongeza kasi ya upatikanaji wa huduma za jamii mkoani humo.

Akizungumza na wajumbe wa kamati za ulinzi na usalama, watendaji wa serikali za wilaya, mkoa na halmashauri za wilaya za mkoa huo baada ya ziara yake ya  siku 5 Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Ayoub Mahmoud Mohammed alisema ipo haja kwa watendaji hao kutumia ziara hiyo kutathmini utendaji wao na mahitaji ya wananchi wa mkoa huo.

Alisema ili kuongeza imani ya wananchi kwao, hawana budi kuzingatia muda, wajibu na majukumu yao kwa umma ili kupunguza malalamiko ya jamii jamboa alilisema litaongeza imani ya wananchi kwa serikali yao.

Alisema katika ziara hiyo amegundua kuwa kero nyingi zilizokuwa zikitolewa na wananchi dhidi ya serikali na sekta binafsi mkoani humo ni matokeo ya upungufu wa uwajibikaji jambo ambalo lilipunguza imani ya wananchi kutumia huduma zinazotolewa na taasisi hizo kiasi cha kuibua kwa malalamiko miongoni mwa wananchi.

Alisema wananchi wengi waliopata nafasi ya kueleza kero zao walionesha kutoridhishwa na huduma zinazotolewa na watendajiwa serikali za wuilaya, halmashauri na shehia  hivyo kwa pamoja wamekubaliana kubadilika na kufanya kazi kwa juhudi, maarifa na kujituma.

“Ninawaomba tubadilike, kwani wananchi walio wengi na kwa muda mrefu walikosa imani na sisi (serikali) kwa kudhani kuwa hata wakija hatutoweza kuwahudumia ima kwa tofauti zao za kimaeneo au kikanda au kisiasa au kidini jambo ambalo sio dhamira ya serikali zote mbili ambazo zipo kwa ajili ya mkoa ni kuwahudumia wananchi”, alisema RC Ayoub.

Aidha aliawakata kuwa na ujasiri wa kuamua na kutekeleza wajibu waonda watasaidia kuongeza kasi ya maendeleo na kupunguza kiwango cha umaskini wa wananchi wa mkoa huo.

Kabla ya kikao hicho, Mkuu huyo wa Mkoa alikutana na na kamati za ulinzi na usalama za Wilaya na mkoa huo na kukubaliana kuundwa kwa kamati maalum ya kufuatilia maagizo na maelekezo yaliyotolewa wakati wa ziara ambayo yalielekezwa katika maeneo mbali mbali ya kiutendaji.

Baadhi ya maeneo hayo  ni pamoja na kuendelezwa kwa vita dhidi ya dawa za kulevya katika maeneo yote ya mkoa huo, kushughulikiwa kikamilifu kwa migogoro ya ardhi, kufuatiliwa na kuwekewa mkakati wa ajira za wakaazi wa maeneo ya jirani na hoteli za kitalii, udhalilisha wa kijinsia na kudhibitiwa kwa watembeza watalii wasio rasmi katika fukwe za mkoa huo.

Mambo hayo ni miongoni mwa kero zilizotolewa na wananchi wa maeneo mbali mbali ya mkoa huo katika mikutano 11 ya hadhara iliyofanyika katika shehia za Bumbwini Makoba, Mahonda, Nungwi, Kivunge, Kiwengwa, Kinyasini, Upenja, Donge Pwani, Matemwe na Tumbatu uvuvini ambayo ilijumuisha wananchi wa shehia nyengine za jirani nazo.

Ziara ya RC Ayoub ilianza Novemba 7 mwaka huu katika shehia ya Bumbwini Makoba wilaya ya Kaskazini ‘B’ na kuhitimishwa katika shehia ya Tumbatu Uvuvini  wilaya ndogo ya Tumbatu Novemba 12 mwaka huu ambapo wananchi zaidi ya 100 walipata nafasi ya kueleza kero na changamoto zinazowakabili katika maeneo yao zilizohusiana na utendaji wa serikali na sekta binafsi na kupatiwa ufumbuzi wa papo kwa papo na mengine kuelekezwa taasisi husiuka kuzishughulikia.

MAELEZO YA PICHA: Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Ayoub Mahmod Mohammed (katikati) akisisitiza jambo katika mkutano wa majumuisho baada ya ziara yake ya siku 5 mkoani humo. kushoto ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja na kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini 'A' Unguja.

Monday, November 13, 2017

UVCCM MFENESINI KUJIEPUSHA NA MIGOGORO

Na Is-haka Omar,.

KAIMU Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM Zanzibar, Abdulghafar Idrissa Juma amewataka viongozi wa Baraza kuu la UVCCM Wilaya ya Mfenesi kuwa sehemu muhimu ya kuwaunganisha vijana na sio kuwagawa katika makundi yatakayoweza kuleta migogoro ndani ya Umoja huo.

Rai hiyo ameitoa leo wakati akifungua Kikao cha kwanza cha Baraza hilo tangu kumalizika kwa Uchaguzi wa ngazi ya Wilaya hiyo  kilichofanyika katika Ofisi za UVCCM Mfenesini zilizopo Bububu Unguja.

Alisema wajumbe wa Baraza hilo wanatakiwa kuwa mstari wa mbele kushughulikia matatizo yanayotokea kwa Vijana ili waendelee kuishi katika misingi ya malezi bora ya Chama cha Mapinduzi.

 “Viongozi mliochaguliwa kupitia Uchaguzi wa Umoja wetu msipofanya vizuri mtakuwa mmeharibu mfumo wa maisha yenu ya kisiasa, lakini mkifanya vizuri itakuwa ni njia ya kupata fursa mbali mbali za kiungozi na kiutendaji ndani ya Chama na Jumuiya  ”, alisema Abdulghafar.

Aliwambia kuwa matarajio ya UVCCM ni kuona Baraza hilo linakuwa ni shamba darasa la kuwapata viongozi imara wenye uwezo wa kujenga hoja zenye nguvu ya kuleta mabadiliko ya kimaendeleo nchini.

Abdulighafar alisisitiza kuwa wajibu wa kila kiongozi ndani ya umoja huo ni kuongoza vizuri sambamba na kuzisoma kwa kina kanuni ya UVCCM na Katiba ya CCM ili maamuzi yoyote yatakayofanyika yaweze kuzingatia matakwa ya Kikatiba.

Aidha Kaimu Katibu Mkuu huyo, Abdulghafar umefika wakati wa kuwa na UVCCM huru yenye nguvu kiuchumi na kiutendaji hivyo viongozi wa umoja huo wanatakiwa kubuni miradi endelevu itakayosaidia vijana kujiajiri wenyewe.

“Vijana tutakapokuwa na uhakika wa kipato kupitia miradi tunayoisimamia wenyewe basi hata hao baadhi ya wanasiasa wenye fedha waliozoea kututumia kwa maslahi yao watakuwa hawana nafasi hiyo tena bali tutasimama wenyewe kutetea maslahi ya chama na jumuiya kwa ujumla.”, alieleza Kaimu Katibu Mkuu huyo.


Mapema  Katibu wa Hamasa na Chipukizi wa Wilaya hiyo aliyemaliza muda wake, Mussa Khamis Mzee  alijiuzulu wadhifa wake ili kupisha kikao hicho kutekeleza utaratibu wa kikanuni  wa kumdhibitisha Katibu atakayeshika nafasi hiyo kwa miaka mitano ijayo.

MAELEZO YA PICHA:
Picha no.9- Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM Zanzibar, Abdulghafar Idrissa Juma akifungua Kikao cha Baraza Kuu la UVCCM Wilaya ya Mfenesini Unguja.

Picha no.11 na 14 Baadhi ya Wajumbe walioudhuria  kikao hicho kilichofanyika katika Ofisi za UVCCM Wilaya ya Mfenesini zilizopo Bububu Unguja.


RC AYOUB AWATAKA VIJANA KUTUMIA MAZINGIRA YAO KUZALISHA AJIRA

Na Mwinyimvua Nzukwi
VIJANA nchini wametakiwa kutumia fursa zinazopatikana katika mazingira yao ili kuzalisha ajira kwa lengo la kujiendeleza kimaisha.

Kaimu mkuu wa mkoa wa Kaskazini Unguja, Ayoub Mahmoud Mohammed alitoa kauli hiyo katika vijiji vya Nungwi, Bumbwini na Matemwe wakati wa mwendelezo wa ziara zake mkoani humo kusikiliza kera na changamoto zinazowakabili wananchi iliyoanza Novemba 7 mwaka huu.

Alisema kutokana na nafasi chache za ajira zinazopatikana serikalini, vijana wanatakiwa kujikusanya pamoja na kutumia fursa za uwezeshaji kwa kubuni kazi au miradi itakayowapatia kipato.

Aidha Ayoub ambae pia ni Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, aliwataka vijana wachache wanaobahatika kuajiriwa katika sekta mbali mbali  kupenda kufanya kazi badala ya kupenda kuajiriwa ili kuongeza uzalishaji utakaoongeza kipato katika taasisi hizo na kuzijengea uwezo wa kutoa malipo mazuri.

"Tutakapotumia vizuri mazingira na fursa zinazotuzunguka tunaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la ajira kwani tutakuwa na shughuli nyingi za kufanya za kuzalisha mali na kupunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la ajira hasa kwa vijana na wana nwake badala ya sote kusubiri kuajiriwa katika sekta rasmi ambayo ina uwezo mdogo wa kuajiri", alieleza Ayoub na kuwataka kujiendeleza kielimu na kitaaluma.

Wakitoa malalamiko yao mbele ya Mkuu huyo aliyeambatana na Mkuu wa wilaya ya Kaskazini ‘A’ Unguja Hassan Ali Kombo na watendaji mbali mbali wa serikali ya wilaya ya Kaskazini ‘A’ na viongozi wa CCM mkoani humo, wananchi wa maeneo hayo walidai kuwa hawanufaiki na uwepo wa mahoteli mengi ya kitalii kwa mambo mbali mbali ikiwemo ajira.

"Kwa idadi ya hoteli ziliopo katika shehia yetu, hatupaswi kuwa tuna lalamikia ajira kwa vijana wetu kwani kicha ya kuwa baadhi yao hawana sifa za kufanya kazi za kitaalamu lakini basi washindwe kufanya hata  kazi ya kuwa mtunza bustani?", alihoji Mbarawa Sheha Haji mkaazi wa shehia ya Nungwi Banda kuu.

Malalamiko hayo pia yalijitokeza katika mikutano ya Mkuu huyo wa Mkoa iliyofanyika katika shehia za Kiwengwa, Matemwe, Donge Mchangani, Kinyasini na Mahonda hali iliyopelekea Mahmoud kumuagiza Afisa wa idara ya Kazi Mkoani humo kushirikiana na masheha wa shehia za ukanda huo kuwabaini wananchi wanaotoka katika shehia zao ambao wameajiriwa katika hoteli hizo.

Aidha Mahmoud aliagiza kukamatwa kwa wanyama watakaoachiwa bila ya udhibiti baada ya wiki moja kuanzia juzi ili kuuweka mji mdogo wa Nungwi katika haiba nzuri.

"Hili la wanyama, viongozi wenzangu lazima ifike wakati tusimamie sheria ya udhibiti wa wanyama kikamilifu. Hivyo natoa wiki moja kila mwenye mbuzi au ng'ombe wake ajue vya kumdhibiti na baada ta muda huo halmashauri kwa kushirikiana na jeshi la polisi ni lazima mchukue hatua kwa mujibu wa sheria", alisisitiza Mahmoud.

Aidha aliitaka halmashauri ya wilaya ya Kaskazini ‘A’ kufanya kazi kwa mashirikiano na wananchi wa shehia zilizomo ndani ya wilaya hiyo kupitia kwa masheha wanapofanya kazi zinazohitaji nguvu ya ziada ili kuepusha upinzani kama ilivyotokea katika ujenzi wa vibaraza vya kuhifadhia taka taka katika shehia za Nungwi, wilayani humo.

Katika ziara hizo Mkuu huyo amekutana na wananchi ambao walieleza kero na changamoto zinazowakabili ambazo baadhi yao zilipatiwa majibu na utatuzi papo hapo na nyengine kutolewa maelekezo kwa watendaji wa taasisi mbali mbali za serikali na binafsi kuzishughulikia katika muda mfupi jambo lililopongezwa na wananchi walio wengi wa mkoa huo .
Mwisho


Saturday, November 11, 2017

PARALEGAL WATAKIWA KUZINGATIA WELEDI, MIONGOZO

Na Mwinyimvua Nzukwi
WASAIDIZI wa sheria – ‘Paralegal’ wa wilaya za Magharibi ‘A’ na Kaskazini ‘B’ Unguja wametakiwa kufanya kazi zao kwa kufuata miongozo wanayopatiwa na weledi ili kuongeza tija kwa jamii.

Mwenyekiti wa Umoja wa Watu Wenye ulemavu Zanzibar (UWZ) Salma Saadat alitoa rai hiyo alipokuwa akifunga mafunzo ya siku 3 ya kuwajengea uwezo Paralegal wa Unit za wilaya ya Magharibi A na Kaskazini B Unguja.

 Alisema kufanya hivyo kutasaidia kufikiwa kwa malengo ya kueneza elimu ya sheria na huduma za kisheria kwa wananchi wengi wa wilaya hizo.

Alisema iwapo elimu na huduma za kisheria zitapatikana kwa uhakika na wakati stahiki miongoni mwa jamii, kuna uwezekano mkubwa wa kupungua kwa migogoro ya kisheria na kijamii nchini.

Alisema katika jamii ya Zanzibar kuna migogoro ya kisheria ambayo inaweza kutatuliwa au kufikia hukumu nzuri iwapo wahusika wangepatiwa usauri wa kisheria katika hatua za awali kabla ya mashauri hayo kufikishwa katika vyombo hivyo.

"Siku zote mnapaswa kutambua kuwa jamii yetu inakabiliwa na mahitaji makubwa ya elimu na huduma za kisheria, hivyo ni vyema mkafanye kazi hizo kwa jamii yetu kwa kutumia ujuzi mliopatiwa kwa moyo wa kujitolea, uwajibikaji, uwazi na ushirikiano wa hali ya juu ili kupunguza muda mwingi unaotumika na watu wetu kufuatilia masdhauri yao katika vyombo vya sheria", alieleza Mwenyekiti huyo.

Aidha aliwataka wasaidizi hao kutumia mafunzo hayo kwa lengo la kuziimarisha taasisi zao ili ziweze kujitegemea baada ya kukamilika kwa mradi uliolenga kuiwezesha jamii ya Zanzibar kuwa na uelewa mkubwa wa sheria na kupatiwa msaada wa huduma za sheria unaosimamiwa na UWZ chini ya ufadhili wa shirika la Legal Services Facilities - LSF la Tanzania bara.

“licha ya mradi huu kulenga katika kuongeza idadi ya wananchi wanaopatiwa huduma na elimu za sheria katika shehia zenu, pia ipo haja ya kuutumia kujijengea uwezo ili muweze kuendelea na kazi hiyo hata baada ya mradi kumaliza muda wake kwa manufaa ya jamii yetu”, alisema Salma.

Mapema Mkurugenzi Mtendaji wa UWZ Asya Abdulsalam alieleza kuwa katika tathmini ya awali ya utekelezaji wa mradi huo, taasisi wanazosimamia zimeonesha muelekeo mzuri licha ya kutofikiwa kwa malengo ya wananchi waliotarajiwa kufikiwa katika robo ya kwanza ya utekelezaji wa mradi huo iliyoanza mwezi Julai mwaka huu.

“Kwa ujumla robo ya kwanza baadhi ya ‘units’ zimeonesha mwelekeo mzuri wa kulifikia lengo la mradi japo kuna changamoto mbali mbali ikiwemo ya idadi ndogo ya wateja mliowafikia”, alieleza Mkurugenzi huyo.

Aliongeza kuwa kila ‘Unit’ imewekewa lengo la kuhakikisha asilimia 35 ya wakaazi wa wilaya husika inapatiwa elimu ya sheria na asilimia 30 ya wakaazi hao wanapatiwa huduma za sheria ifikapo mwisho wa mradi hivyo wasaidizi hao wanapaswa kuwa na mikakati imara ya kuyafikia malengo hayo.

Aidha alieleza umuhimu wa ‘units’ hizo kuzitumia kamati za ushauri za wilaya (TAGP) zinazoongozwa na wakuu wa wilaya na kamati za ushauri za viongozi wa kijamii (CAT) zinazowajumuisha masheha ili kurahisisha utendaji kazi wa wasaidizi hao.

Katibu Mkuu wa ‘unit’ ya wasaidizi wa sheria wa wilaya ya Kaskazini ‘B’ Unguja (NBPU) mwalimu Ali Salim Ali alieleza kuwa katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita walifanikiwa kuwafikia jumla ya watu 487 kinyume na lengo lililowekwa la kuwafikia watu 1,787 katika kipindi hicho.

“Tulijitahidi kuitisha mikutano katika shehia mbali mbali kupitia wasaidizi wa sheria wetu, lakini mara nyingi tulipata idadi ndogo kutokana na sababu mbali mbali zikiwemo za harakati za maisha na mwamko mdogo wa jamii katika maswala ya sheria katika maeneo mengi ya wilya zetu”, alieleza mwalimu Ali.

Nae Katibu Msaidizi wa ‘unit’ ya wasaidizi wa sheria wa wilaya ya Magharibi ‘A’, Makame Mwadini alieleza kuwa mafunzo hayo yatasaidia kuimarisha utekelezaji wa kazi zao na kuahidi kuyafanyia kazi mapungufu yote yaliyoonekana katika tathmini hiyo.

“Kikubwa tulichojifunza ni kwamba tulikuwa tunafanya kazi bila ya kujiwekea malengo, hivyo tutajitahidi kuyafanyia kazi mapungufu yaliyoainishwa ili tuwe na matokeo mazuri jambo ambalo ndio madhumuni ya kuanzisha jumuiya yetu”, alisema mwadini na kuwashukuru wadau wote kwa usaidizi waliowapatia.

Mafunzo hayo yaliyolenga kutoa tathmini na kurekebisha makosa yaliyogundulika katika utekelezaji wa mradi huo unaotekelezwa katika maeneo yanayosimamiwa na umoja huo ambazo ni wilaya za Kaskazini Unguja ‘A’, Kaskazini ‘B’, Mjini na Magharibi ‘A’ Unguja ili kuleta ufanisi kwa jamii.
MWISHO.

PICHANI: Katibu Mkuu wa Unit ya Wasaidizi wa sheria (Paralegal) ya wilaya ya Kaskazini 'B' Unguja Omar Khamis (kushoto) akimsikiliza Mwenyekiti wa Umoja wa watu wenye ulemavu Zanzibar (UWZ) Salma Saadat (hayupo pichani) alipokuwa akifunga mafunzo kwa Paralegal hao yaliyotolewa na UWZ kwa ufadhili wa Legal Services Facility - LSF.