Thursday, April 19, 2018

BAMMATA LATAKIWA KUWAENDELEZA WANAMICHEZO WAKE


NA MWINYIMVUA NZUKWI
Wajumbe wa Kamati Tendaji ya Baraza la Michezo la Majeshi ya Tanzania – BAMMATA wametakiwa kutumia weledi katika uongozi wa michezo ili kuhakikisha wanasimamia shughuli za maendeleo ya michezo katika vyombo vya ulinzi na usalama bila ya kuathiri sheria na kanuni za michezo husika.

Akifungua kikao cha Kamati hiyo katika ukumbi wa mikutano wa idara ya uhamiaji Zanzibar mkuu wa mkoa wa Mjini Magharibi Ayoub Mohammed Mahmoud alisema kufanya hivyo kutathibitisha ubora wa vyombo hivyo katika medani ya michezo na ulinzi wa nchi.

KAMATI YA UONGOZI YA TASAF UNGUJA, WATENDAJI WAOMBA WASHIRIKIANE


NA MWINYIMVUA NZUKWI
Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi ambae pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kamati ya Uongozi ya Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini TASAF III Unguja Ayoub Mohammed Mahmoud amewataka wajumbe wa Kamati hiyo kuzidisha mashirikiano na watendaji wa mpango huo ili utekelezaji wake uoneshe matokeo yanayopimika.

Akizungumza katika Mkutano wa kutathmini utekelezaji wa mpango huo katika kipindi cha mwaka 2017, uliofanyika katika ofisi za TASAF Mazizini Unguja, alisema kufanya hivyo kutasaidia kupunguza changamoto zilizobainika ikiwemo ya kutopatikana kwa matokeo yaliyotarajiwa katika baadhi ya miradi inayotekelezwa.

Monday, April 16, 2018

RC AAGIZA MICHEZO KUHIMIZA AMANI


NA MWINYIMVUA NZUKWI
Mkuu wa mkoa wa Mjini Magharibi Unguja Ayoub Mohammed Mahmoud amewataka washiriki wa mbio za baskeli za Afrika Mashariki kutangaza vivutio vya utalii viliopo na amani ya nchi za afrika mashariki  ili kukuza uchumi wan chi hizo unaotegemea pato la utalii.

Akihutubia wananchi na washiriki wa mbio hizo katika uwanja wa Amaan mjini Zanzibar, RC Ayoub amesema mbio hizo zikitumika kusambaza na kueneza ujumbe wa amani zitasaidia kuwashawishi na kuwakumbusha wananchi juu ya umuhimu wa kulinda amani iliyopo pamoja na uhifadhi wa mazingira kwa lengo la kuimarisha utalii wa ndani wa Zanzibar na Tanzania bara.

Amewataka washiriki hao wanaotoka katika nchi mbali mbali za ukanda wa Afrika Mashariki, Kati na Kusini kutumia muda mchache watakaokuwepo Zanzibar kupitia vivutio vya utalii vilivyopo na kwenda kuvitangaza katika nchi zao sambamba na kuelezea hali ya amani iliyopo nchini.

Aidha aliishukuru wizara ya Habari, Utamaduni na Mambo ya Kale kwa kuamua kushirikiana na taasisi ya Afrika Mashariki Festival kwa kuamua kuanzisha mbio hizo ndani ya mkoa wa Mjini Magharibi mbio ambazo zinatarajiwa kufanyika pia katika mkoa wa Dar es salam ambazo amesema zitasaidia kukuza uwekezaji katika sekta mbali mbali ikiwemo ya utalii.

Mapema akitoa taarifa za mbio hizo katibu mtendaji wa kamisheni ya utalii Zanzibar Dkt. Vuai Idi Lila amezitaja nchi zilizotoa washiriki wa mbio hizo kuwa Tanzania bara, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Ethiopia, afrika kusini na wenyeji Zanzibar.

Amesema mbio hizo ni sehemu ya mikakati ya kamisheni yake ya kuimarisha utalii nchini katika majira yote kama moja ya azma ya serikali ya Zanzibar pamoja na kukuza uhusiano na wadau wengine wa utalii nchini.

Jumla ya washiriki 72 wakiwemo wanawake wawili kutoka nchini Kenya walishiriki mbio hizo za umbali wa kilomita 60 zilizoanzia katika uwanja wa Amaan kupitia Welezo, Mwera, Dunga, Jendele, Unguja Ukuu, Bungi, Tunguu na kurudia  njia ya Mwera hadi uwanja wa Amaan.
Washiriki wa mbio za baskeli za afrika mashariki wakijiandaa kuanza mbio hizo.

Mkuu wa mkoa wa mjini magharibi Ayoub Mohammed Mahmoud akipeperusha bendera ya jumuiya ya afrika mashariki kuashiria kuanza kwa mbio za baskeli za Afrika Mashariki


Mmoja kati ya wanawake wawili walioshiriki mbio hizo kutoka nchini Kenya.


Sunday, April 15, 2018

BALOZI SEIF AONYA UKATAJI WA MITI, AIPONGEZA ZAFRED KUCHIMBA VISIMA


NA OTHMAN KHAMIS, OMPR
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameinasihi jamii kuepuka kukata miti ovyo na badala yake irejee katika utamaduni ya kuotesha miti katika maeneo wanayoishi ili ardhi iendelee kubakia katika maumbile yake ya kawadia.
Alisema hivi sasa kiwango cha maji katika ardhi kinaendelea kupungua kutokana na tabia ya wanaadamu kuchafua mazingira ikiwemo ukataji ovyo wa misitu jambo ambalo ni hatari kwa maisha ya viumbe.
Balozi Seif Ali Iddi ambae pia ni Mwakilishi wa jimbo la Mahonda alitoa nasaha hizo wakati wa sherehe za uzinduzi wa visima viwili vya maji safi na salama vilivyochimbwa katika kituo cha afya jimbo la Donge na skuli ya msingi na sekondari za Mahonda jimbo la Mahonda.

'ZANZIBAR OLD STARS' YATAKA WENYE MAMLAKA YA SOKA LA ZANZIBAR WAWATUMIE


Na Salum Vuai, MAELEZO
TIMU ya soka ya wachezaji wa zamani Zanzibar Old Stars, imemuomba Mkuu wa Mkoa wa Mjini  Magharibi Ayoub Mohammed Mahmoud, kusaidia kuwaelimisha wadau  na mamlaka za michezo juu ya umuhimu wa kutunza kumbukumbu zinazohusiana na mchezo huo nchini.

Akizungumza wakati uongozi wa timu hiyo ulipokwenda kumshukuru Mkuu huyo na kumkabidhi kikombe cha ushindi wa mechi ya ‘Karume Day’, Katibu Mkuu wa kikosi hicho Salum Hamduni, alisema inasikitisha kuona wanasoka walioiletea sifa Zanzibar hawathaminiwi hata kwa kutakiwa ushauri.

Alisema tafauti na nchi nyengine, Zanzibar haina utaratibu wa kutunza historia za wanamichezo wake wa zamani ambao waliiwakilisha kimataifa na kuifanya itambuliwe na kuheshimiwa ndani na nje ya nchi.

Saturday, April 14, 2018

WANACHAMA CCM WAHIMIZWA KULINDA MISINGI YA VYAMA VYA ASP NA TANU


Na Is-Haka Omar, Zanzibar.
WANACHAMA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wameshauriwa kuendeleza harakati za kulinda, kutetea na kusimamia misingi ya taasisi hiyo ili kuenzi kwa vitendo juhudi za waasisi wa ASP na TANU.
Hayo ameyasema Katibu Mwenezi CCM Wilaya ya Dimani Hassan Suleiman  Jaku,  katika ziara ya Makatibu uenezi wa CCM ngazi za matawi hadi Wilaya ya Dimani walipotembelea  maeneo ya historia ya kumbukumbu ya aliyekuwa Rais wa kwanza wa Zanzibar marehemu Abeid Aman Karume,  Kisiwandu Unguja. 
Makatibu wenezi wakipata maelezo ndani ya chumba alichouawa muasisi wa mapinduzi ya Zanzibar Sheikh Abeid Aman Karume.
Amesema nguvu za Chama Cha Mapinduzi zinatokana na wanachama wazalendo wanaolinda na kuthamini urithi wa Chama hicho toka enzi za vyama vya ASP na TANU.

WAZEE ZANZIBAR WAMPONGEZA DK. SHEIN KWA KUENDELEZA PENCHENI JAMII, WAMUOMBA KUPUNGUZA UMRI WA WANUFAIKA WANAWAKE



Na Mwinyimvua Nzukwi
Jumuiya ya Wazee Zanzibar (JUWAZA) imeiomba serikali ya mapinduzi ya Zanzibar kupunguza umri wa wazee wanawake wanaopokea pencheni jamii kutoka  miaka  75 hadi 55 ili kuliwezesha kundi hilo kunufaika na pencheni hiyo.

Wakizungumza na waandishi wa habari ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya kutimiza miaka miwili toka kuanza kutolewa kwa pencheni hiyo, wazee hao walimshukuru Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein kwa kuanzisha pensheni hiyo waliyosema imesaidia kuimarisha hali zao na kuondokana na utegemezi.