Sunday, September 2, 2018

KLABU ZA WAANDISHI WA HABARI KUKUTANA ARUSHA


NA MWINYIMVUA NZUKWI
Mkutano Mkuu wa Muungano wa klabu za waandishi wa habari Tanzania (UTPC) unafanyika mkoani Arusha kwa siku mbili kuanzia Septemba 3 ambapo Mkuu wa kitengo cha ushirikano na maendeleo wa Shirika la misaada la Sweden Ulf Kalstig atafungua mkutano huo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa UTPC Aboubakar Karsan mkutano huo utaongozwa na Rais wa Muungano huo Deogratius Nsokolo ambapo pamoja na agenda za kawaida za mkutano huo utaambatana na maadhimisho ya siku ya Daudi Mwangosi ambapo mshindi wa tuzo hiyo atatangazwa na kupatiwa zawadi.

Akizungumzia tuzo hiyo Mkurugenzi huyo alieleza kuwa imewekwa kwa lengo la kukumbuka mchango wa aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa klabu ya waandishi wa habari ya Iringa Daudi Mwangosi aliyeuawa akiwa kazini wakati wa machafuko ya kisiasa kati ya polisi na wafuasi wa chama cha demokrasia na maendeleo (CHADEMA) na kutajwa kuwa ni tukio la kwanza kutokea nchini Tanzania.

“Tuzo hii inatolewa kwa mwandishi au taasisi ya habari kwa kuzingatia umahiri na umakini wa chombo hicho katika kutoa taarifa zenye kuleta mabadiliko chanya kwa jamii na kuendeleza tasnia ya habari nchini”, alieleza Karsan.

Katika mwaka uliopita kampuni ya Clouds Media Group ilitwaa tuzo hiyo pamoja na fedha taslim shilingi milioni 10 za Tanzania kutokana na uwezo waliouonesha kukabiliana na changamoto za weledi katika uandishi wa habari. 

Alisema klabu wajumbe wa mkukano huo kutoka klabu zote 28 za waandishi wa habari Tanzania zinashiriki mkutano huo utakaofanyika katika hoteli ya Lush Garden ambapo taarifa mbali mbali zinazohiusiana na taasisi hiyo na tasnia ya habari kwa ujumla zitawasilishwa na kujadiliwa.

Mkurugenzi huyo alieleza kuwa miongoni mwa agenda za mkutano huo ni pamoja na taarifa ya utekelezaji wa shughuli za muungano huo kwa mwaka uliopita hadi mwezi uliopita na kupitisha makadirio ya mipango na matumizi kwa mwaka ujao.

“Kwa ujumla maandalizi yamekamilika kwani toka mwanzoni mwa mwaka huu sekretarieti ilikuwa Arusha kwa maandalizi ya vikao vya kamati na bodi ya wadhamini ambavyo vimefanyika kwa mafanikio makubwa”, alieleza Karsan.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi akiwa njiani kuelekea Arusha mmoja ya wajumbe wa mkutano huo Katibu mkuu wa klabu ya waandishi wa habari Zanzibar (ZPC) Faki Mjaka alieleza kuridhishwa kwake na maandalizi ya mkutano huo kutokana na kupatiwa taarifa zote mapema.

“Tunaamini mkutano wa mwaka huu utakuwa na mafanikio makubwa kwani licha ya kuwa na shughuli nyingi, kutakuwa na matumizi mazuri ya muda hasa ikizingatiwa wajumbe wote tulipatiwa nyaraka zitakazowasilishwa mkutanoni mapema na kupata muda wa kuzijadili na wajumbe wenzetu ambao hawatokuwepo Arusha”, alisema Mjaka.

Katika mkutano huo ZPC kama zilivyo klabu nyengine inawakilishwa na mwenyekiti wa klabu hiyo Abdallah mafaume amabae bia ni mjumbe wa bodi ya UTPC na Mweka hazina wake Halima Tamim ambao waliondoka mjini Zanzibar Jumamosi wa wiki iliyopita kuelekea Arusha kwa ajili ya mkutano huo.

No comments:

Post a Comment