Sunday, September 2, 2018

BALOZI SEIF KUWATUNZA 'FORM SIX' WA MJINI MAGHARIBI


NA MWINYIMVUA NZUKWI
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla ya ugawaji wa zawadi kwa wanafunzi waliofanya vyema katika mitihani ya kidato cha sita katika mwaka 2018.



Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari ofisini kwake vuga, mkuu wa mkoa wa mjini magharibi Ayoub Mohammed Mahmoud amesema hafla hiyo itafanyika katika viwanja vya kumbu kumbu ya mapinduzi siku ya jumanne Septemba 4, 2018.



Amesema hatua hiyo inafuatia ahadi aliyoitoa wakati alipokutana na wanafunzi wa skuli 17 za mkoa huo waliokuwa wakijiandaa na mitihani mnamo mwezi april mwaka huu ambapo aliahidi kutoa kompyuta mpakato (laptops) watakaopata ufaulu wa daraja la kwanza (Division one) katika mitihani yao.



Amesema ahadi hiyo ililenga kuwahamasisha wanafunzi hao kufanya bidi katika masomo yao na kufanikiwa kupata matokeo mazuri ambayo hajawahi kupatikana katika kipindi kirefu ndani na nje ya mkoa huo.



Mkuu huyo wa mkoa ameeleza kuwa katikam hafla hiyo wanafunzi 96 watapatiwa kompyuta hizo ili ziwasaidie katika shughuli zao za masomo ya juu watakayoendelea nayo.



Ameeleza kuwa katika tukio hilo la kihistoria mbali ya burudani zitakazotolewa na wanafunzi wahitimu, pia wasanii mbali mbali wa kizazi kipya wa Zanzibar na Tanzania bara ambao watatumbuiza ili kuwapongeza wanafunzi hao jambo ambalo litasaidia kuongeza hamasa ya wanafunzi waliopo skuli.



Aidha amewapongeza wadau mbali mbali ikiwemo taasisi ya mimi na wewe kwa kufanikisha upatikanaji wa zawadi hizo  na kwamba wanafunzi wawili waliopata nafasi ya kuingia katika wanafunzi 10 bora kitaifa watapatiwa zawadi ya ziada na ofisi yake ipo tayari kuwasaidia wanafunzi waliofaulu kwa daraja la chini (divisheni 0) pindi wakiwa tayari kurudia mitihani.



Mkuu wa mkoa huyo amewataka wananchi wa ndani na nje ya mkoa huo kujitokeza kwa wingi katika tukio hilo na kuendelea kuunga mnkono juhudi zinazochukuliwa na serikali ya awamu ya saba inayoongozwa na Dk. Ali Mohamed Shein katika kuimarisha sekta na viwango vya elimu nchini.



Katika hatua nyengine RC Ayoub amewataka wanafunzi   waliokosa ufaulu wa daraja la kwanza kutovunjika moyo wa kuendelea na masomo badala yake kuongeza bidii ili kufikia malengo waliojiwekea.



Akizungumza katika sherehe ya kuwaaga wanafunzi wa kidatu cha sita wa skuli ya SOS Mombasa mjini Unguja Ayoub amesema kuna umuhimu kwa wanafunzi hao kujiendeleza ili kupatikana vijana bora zaidi. 



Aidha amewataka wazazi, walezi na walimu wa skuli hiyo kufanya jitihada ya kuhakikisha kuwa wanafunzi wa skuli hiyo wanazingatia zaidi masomo yao ili kupata wasomi zaidi hapa nchini.



Amewapongeza walimu wa skuli hiyo kwa jitihada wanazochukua kwa wanafunzi wao na kuwataka kuendeleza jitihada hizo ili kila mwaka kuwawezesha wanafunzi bora kama ilivyokuwa mwaka huu ambapo skuli hiyom ilifanikiwa kutoa mmoja ya wanafunzi 10 bora kitaifa.



Akisoma risala ya skuli hiyo mwalimu mkuu Ahmed Ali ameeleza kuwepo kwa  changamoto  ya ukosefu wa vifaa mbalimbali  ikiwemo kompyuta na vitabu vya kufundishia na kumuomba mkuu huyo wa mkoa kuwasaidia kutatua changamoto hizo.


No comments:

Post a Comment