Tuesday, March 20, 2018

ZANZIBAR KUADHIMISHA KWA MARA YA KWANZA SIKU YA MISITU DUNIANI


MWINYIMVUA NZUKWI
'Misitu na miji endelevu; tuhifadhi misitu na miti kwa ustawi wa miji ili tuishi kwa furaha'.

Ni ujumbe wa mwaka huu Kimataifa katika kuadhinmisha siku ya misitu ulimwenguni ianyoadhimishwa kila mwaka ifikapo Machi 21.

Pamoja na ukongwe wake toka ilipoasisiwa na umoja wa mataifa mnamo mwaka 2012, bado siku hii ni ngeni miongoni mwa wananchi wa Zanzibar ambao kwa kiasi kikubwa ni watumiaji wa bidhaa za misitu kwa mahitaji mbali mbali ya kijamii kama vile ujenzi, chakula na dawa.

Uwepo wa siku hii bila shaka kama zilivyo siku nyerngine za kimataifa zinazoangukia katika sekta mbali mbali, umelenga katika jambo mahsusi ambalo linahitaji mazingatia na mikakati madhubuti kwa manufaa ya jamii nzima.

Baada ya miaka 6 toka kuasisiwa kwa siku hiyo, Idara ya misitu na maliasili zisizorejesheka Zanzibar inatarajia kuadhimisha kwa shughuli mbali mbali ikiwemo kongamano la wazi kwa wadau wa misitu na wananchi litakalofanyika katika ukumbi wa zamani wa Baraza la wawakilishi Kikwajuni.

Thursday, March 15, 2018

DK. SHEIN AHIMIZA UTAWALA BORA, AWATAKA WATENDAJI KUACHA MAZOEA


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, amewataka watendaji na wananchi wote kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia misingi ya utawala bora na kuacha kufanya kazi kwa mazoea.
Dk. Shein aliyasema hayo leo, katika uzinduzi wa Semina ya Utawala Bora na Uchumi katika ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi, iliyowashirikisha viongozi wa Wizara na Taasisi mbali mbali za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. 
Katika hotuba yake, Rais Dk. Shein alisema kuwa Utawala Bora ni nguzo muhimu katika jitihada za kupunguza umasikini hivyo, kila mmoja ana wajibu wa kuhakikisha kuwa anajenga na kulinda maadili mema kwa manufaa ya umma na nchi nzima kwa jumla.
Dk. Shein aliongeza kuwa utawala bora ni suala linalozingatia misingi ya ufanisi na tija, utawala wa sheria na haki za binaadamu, ushirikishwaji, kuzingatia maadili, uadilifu uwajibikaji na uwazi na kuzingatia matakwa ya wananchi.

Wednesday, March 14, 2018

ZPC YAKUNWA NA UTEUZI WA RAIS DK. SHEIN, KAMATI KUKUTANA MACHI 15

NA MWINYIMVUA NZUKWI

Klabu ya waandishi wa habari Zanzibar (ZPC) imempongeza Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein kwa hatua yake ya kuwateua wanachama wa muda mrefu wa klabu hiyo Dk. Saleh Yussuf Mnemo na Abdullah Hassan Mitawi kuwa Manaibu Makatibu Wakuu katika Wizara ya habari, utamaduni na Mambo ya kale na Ofisi ya Makamo wa pili wa Rais wa Zanzibar hatua inayoonesha imani kwa tasnia ya habari nchini.

Naibu Katibu Mkuu wizara ya Habari, utalii na mambo ya kale (habari) Dk. Saleh Yussuf Mnemo (kulia) akila kiapo mbele ya Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein.

Tuesday, March 13, 2018

ZALISHENI BIDHAA ZENYE UBORA KUHIMILI USHINDANI - JUMA

NA MWINYIMVUA NZUKWI
WAJASIRIAMALI nchini wametakiwa kuzalisha bidhaa zinazozingatia ubora na viwango ili kukuza mitaji na kuhimili ushindani wa soko la ndani na nje.

Akifungua semina ya udhibiti wa ubora wa viwango kwa wajasiriamali wanaoteneneza sabuni, muda mchachje baada ya kula kiapo cha kuendelea kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya biashara na viwanda Zanzibar Ali Juma Khamis alisema serikali kupitia taasisi ya viawango Zanzibar (ZBS) imeamua kutoa mafunzo hayo kwa lengo la kuwajengea uwezo na kuongeza ubora wa bidhaa zinazozalishwa.

Alisema pamoja na kuwepo kwa wazalishaji wa bidhaa za sabuni aina mbali mbali bado bidhaa hizo zimeshindwa kuingia katika soko kubwa la utalii kutokana na wingi wa wazaklishaji kutozalisha kwa kuzingatia viwango vya kitaifa na kimataifa.

“Sabuni mnazozalisha ambazo huwa na vionjo vya viungo vya asili ya Zanzibar na kuwavutia watumiaji wengi lakini mara nyingi hukosa kuingia katika soko la kimataifa kutokana na kutozingatiwa kwa ubora na viwango jambo ambalo mnapaswa kulizingatia ili kukuza biashara zenu”, alieleza Khamis.

Aidha aliwataka wazalishaji hao kutumia vyema fursa ya uanzishwaji wa wakala wa viwanda vidogo vidogo (SMIDA) ambayo itawawezesha wajasiriamali wa kila wilaya kupata ujuzi na jmikopo ya kuendeleleza bishara zao.

“Serikali imeanza mchakato wa kuisimamisha hii taasisi ili kuwafanya wajasiriamali wa Zanzibar kuanzisha viwanda vidogo vidogo na kueneza elimu ya ujasiriamali kwa wale watu ambao bado hawajaanzisha biashara ili kuwajengea uwezo wa kujitegemea na kupunguza tatoizo la ajira kwa vijana”, alieleza Khamis.

Mapema akitoa maelezo katika semina hiyo Mkurugenzi Mkuu wa ZBS Mwadini Khatib Mwadini alieleza kuwa semina hiyo ni mwendelezo wa mafunzo yanayotolewa na taaisisi yake kwa wajasiriamali wanaozalisha bidhaa mbali mbali ili kukuza ubora wa bidhaa zao.

“Katika mafunzo haya tumeanza na wazalishaji wa bidhaa za sabuni baada ya kugundua kuwa pamoja na kuwepo kwa uzalishaji mkubwa wa bidhaa hiyo na soko nlake bado bidhaa nyingi hazina alama ya ubora jambo linalochangia kutoingia katika masoko makubwa hasa la utalii ambalo lina firsa nyingi kwa wajasiriamali wetu”, alisema Mwadini.

Akiwasilisha mada katika semina hiyo mkufunzi wa mafunzo hayo George Mang’ala Buchafwe aliwataka wajasiriamali hao mbali ya kuzalisha bidhaa bora kwa kutumia viungo vya asili ya Zanzibar, wafanye kazi kwa kushirikiana ili kuweza kulimudu soko kwa wazalishaji wa bidhaa zinazofanana.

“Wakati mwengine mjifunze kufanya kazi kwa kushirikiana kwani inaweza kutokea mmoja wenu akapata oda ya bidhaa nyingi kuliko uwezo wake sio vibaya kuungana wenzake ili kuweza kulitosheleza soko kuliko kung’ang’ania”, alisisitiza Buchafwe.

Nao washiriki wa semina hiyo waliipongeza taasisi hiyo kwa kuwapatia elimu hiyo na kuitaka kuwa karibu nao ili kuendeleza ujuzi na utaalamu walionao katika utengenezaji wa sabuni.

“Sisi tulizowea kupeleka bidhaa zetu kwa wakala wa chakula, dawa na vipodozi ili kupatiwa ithibati wa ubora wa bidhaa zetu na hatukuelewa kuhusu uwepo wa taasisi hii ambayo ndiyo inayodhibiti ubora wa bidhaa”, alieleza Tatu Suleiman.

Aidha alieleza kuwa mbali ya bidhaa wanazozalisha kuwa na ubora, bado wananchi waliowengi hawapendi kutumia bidhaa zinazozalishwa nchini jambo waliloiomba serikali kuwasaidia kuwapatia masoko ya bidhaa zao.

Mafunzo hayo ya siku tatu yanayowashirikiasha wazalishaji wa sabuni 42 kutoka wilaya 7 za unguja pia yamelenga kuwaunganisha wajasiriamali hao kulitambua na kulifikia soko la bidhaa zao kwa kuzingatia viwango vya Zanzibar, Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla.

TUTASIMAMIA MAAGIZO KUEPUSHA MIGOGORO YA ARDHI

NA MZEE GEORGE
SERIKALI ya Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja imesema itasimamia maagizo na miongozo ya Serikali kwa kufuata sheria na utaratibu wa matumizi ya ardhi ili kuhakikisha mipango na azma ya kuondosha migogoro ya ardhi katika Mkoa huo inafanikiwa.

Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mhe Ayoub Mohammed Mahmoud ameeleza hayo wakati wa mkutano uliowakutanisha viongozi na watendaji wa Mkoa huo na kamati ya baraza la Mapinduzi inayofuatilia migogoro ya ardhi chini ya Mwenyekiti wake Mhe Haji omar Kheir uliofanyika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la zamani kikwajuni mjini unguja.

Amesema wakati umefika kwa viongozi, watendaji na wananchi wa Mkoa wa Mjini Magharibi kuhakikisha wanafuata taratibu na sheria zilizowekwa  katika matumizi mazuri ya ardhi ili kuona rasilimali hiyo ya taifa inaendelea kutunzwa.

Akitoa  ahadi kwa niaba ya viongozi na watendaji wa Mkoa huo kwa kamati hiyo mhe Ayuob  amesema  yupo tayari kuachia madaraka iwapo atabainika kujihusisha na migogoro ya ardhi kwa maslahi nchi na kutoa indhari kwa  watendaji wakaotajihusisha na migogoro ya ardhi hatosita  kuwachukulia hatua za kinidhamu.

Mapema wajumbe wa Kamati ya Baraza la Mapinduzi inayofuatilia migogoro ya ardhi wamesema utafiti uliofanyika umeonesha baadhi ya viongozi wa wilaya,Jimbo,Wadi na Shehia wamekua wakijipa mamlaka ya kuuza viwanja kinyume na utaratibu hali ambayo inayoibua migororo ya ardhi katika jamii.

Wameongeza kuwa kwa sasa Serikali imedhamiria kuitumia ardhi yake iliyopo kwa matumizi ya maendeleo ya nchi ambapo wamesema kuna haja ya kufanyiwa marekebisho ya sheria za ardhi kutokana na mapungufu yaliopo ambayo ndio chanzo cha matumizi mabaya ya ardhi.

Kamati ya Baraza la Mapinduzi inayofuatilia migogoro ya ardhi imeundwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein kufuatia ripoti ya Kamati iliyofanya utafiti wa migogoro ya ardhi nchini na kubaini ukiukwaji wa sheria za matumizi ya ardhi Kamati ambayo inaongozwa na Mwenyekiti wake Waziri wa ujenzi, mawasiliano na Usafirishaji Zanzibar Dk. Sira Ubwa Mamboya.



Friday, March 9, 2018

WATAKIWA KUKABIDHI NYUMBA ZA KIWANDA CHA SUKARI


NA MWANDISHI WETU
Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Hassan Ali Kombo amewataka wakaazi wa nyumba za Startling ziliopo Mahonda, Kitope na Mwanakombo watekeleze agizo la serekali la kuhama katika nyumba hizo na kuzirudisha kwa kiwanda cha sukari.
Akizungumza na wananchi wanaoishi katika nyumba hizo Mahonda Kizota DC Hassan aliwataka wananchi hao kutii agizo hilo kwa kuwa muda waliopewa kujiandaa kuzirudisha nyumba hizo umemalizika.
Alisema ni vyema na busara kwa wakaazi hao kutekeleza agizo hilo kabla ya kupatwa na matatizo yoyote kwa kuwa taarifa za kutakiwa kuhama wanazo kwa muda mrefu na kuwataka wawe wamekabidhi nyumba hizo itakapofika Jumanne ya Machi 13 mwaka huu.
“Tunatarajia hakuna atakaekaidi agizo huili kwa kuwa limeshatolewa muda mrefu na viongozi mbali mbali hivyo ninawaomba hadi Jumanne ijayo muwe mmeshahama na kukabidhi funguo katika ofisi ya mkuu wa Wilaya”, alisisitiza Hassan.
Alisema ameamua kutoa taarifa hiyo kwa mara nyengine kuwakumbusha ili wasishtuke pindi hatua za kuwahamisha  zitakapochukuliwa iwapo watashindwa kuhama kwa hiari.
Nao wakaazi hao wameiomba serekali kuwapa muda kwa madai kuwa muda waliopewa ni mfupi kuweza kujitayarisha kuhama na kutaka wapatiwe ufafanuzi juu ya utolewaji wa taarifa za kuwataka kuhama ambapo awali waliotakiwa kuhama walikuwa ni wafanyakazi wa serikali.
Aidha walihoji iwapo agizo hilo litatekelezwa ipi itakuwa hatma za taasisi za kijamii walizozianzisha kama vile skuli na vyuo vya qur-an viliomo katika eneo hilo.
Taarifa zilizopatika kutoka katika mmoja ya wakaazi hao kuwa serikali ilitoa notisi kwa wafanyakazi na watendaji wa serikali wanaoishi katika nyumba hizo 41 miezi mitatu iliyopita na kwamba mtu mmoja tu kati yao ndie aliyetii agizo hilo.
“Waliopewa barua za kuhama ni wafanyakazi wa taasisi za serekali na tayari mmoja kati yao amesharudisha funguo lakini sisi wananchi wa kawaida hakuna aliyepewa taarifa kwa barua ingawa tetesi za kuwa tuhame zipo kwa muda mrefu sasa”, alieleza mkaazi huyo ambae hakutaka kutajwa jina lake.
Nyumba za Starling ni miongoni mwa mali za kilichokuwa kiwanda cha sukari na manukato ambacho kilibinafsishwa na kupatiwa mmiliki mwengine zinakadiriwa kukaliwa na zaidi ya familia 150 zilijengwa kwa madhumini ya kukaa wafanyakazi wanaofanyakazi katika kiwanda cha sukari na manukato katika miaka ya 70.

Muonekano wa jengo la kiwanda cha sukari Mahonda baada ya kuanza upya uzalishaji.

VIJANA KUADHIMISHA SIKU YA JUMUIYA YA MADOLA KWA BUNGE JUMATATU


NA MWINYIMZUA NZUKWI
Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mgeni Hassan Juma anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Bunge la vijana lililoandaliwa na Chama cha Mabunge ya Jumuiya ya Madola (CPA) Zanzibar tawi la Zanzibar litakalofanyika katika ukumbi wa baraza hilo Jumatatu Machi 12 mwaka huu.
Bunge hilo ambalo ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya Jumuiya ya madola duniani, litahusisha vijana wapatao 50 kutoka wilaya 11 za Unguja na Pemba wenye umri usiozidi miaka 30 wanaotoka katika mabaraza ya vijana wilayani humo.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Chukwani, Mwenyekiti wa chama cha mabunge ya Jumuiya ya Madola tawi la Zanzibar Simai Mohammed Said alisema bunge hilo ni linaitishwa kwa mara ya tatu toka baraza la wawakilishi lianze kuiadhimisha siku hiyo.
Alisema bunge hilo katika kikao hicho cha bunge, vijana watajadili mada mbali mbali, kupitisha maazimio na kutoa maoni juu ya namna kundi hilo linavyoshirikia katika kukuza demokrasia nchini.
"Tunatarajia baada ya bunge hilo maazimio yatakayofikiwa yatawasilishwa wa katika vikao vya Baraza la Wawakilishi kupitia kamati ya maendeleo ya wanawake, habari na utalii kama inavyoelekezwa na kanuni ya 149(3) ya kanuni ya baraza la wawakilishi ili serikali iyatekeleze", alieleza Simai.

Aidha alieleza kuwa bunge hilo linatarajiwa kuongeza uelewa wa jamii na vijana kuhusiana na masuala ya kibunge na kutokana na ufafanuzi wa mada zitakazojadiliwa, kujenga moyo wa kizalendo, ushirikiano na kuibua stadi za uongozi miongoni mwa wabunge hao.
Akizungumzia mafanikio yaliyopatikana toka baraza hilo lijiunge na chama cha mabunge ya jumuiya ya madola (CPA) mwaka 2004, Mwenyekiti huyo alieleza kumekuwa na mabadiliko ya kiutendaji na kimfumo ndani ya baraza jambo linalopelekea chombo hicho kulingana na mabunge mengine duniani.
"Miongoni mwa malengo ya kuanzishwa kwa CPA (Commonwealth Parliamentary Association) ni kutekeleza azma ya maadili chanya ya demokrasia ya kibunge ambayo yanafikiwa kupitia mikutano, semina, ziara za kubadilishana uzoefu na uchapaji wa nyaraka zinazohusiana na jumuiya ambazo baraza la wawakilishi linashiriki kama mwanachama anaejitegemea", aliongeza Simai ambae pia ni mwakilishi wa jimbo la Tunguu, Zanzibar.
Akifafanua jinsi baraza hilo linavyonufaika na muungano huo, Afisa Sheria wa baraza hilo Mussa Kombo Bakar alisema ushiriki wa baraza hilo katika vikao mbali mbali kumepelekea mabadiliko ya kanuni na mfumo wa uendeshaji wa chombo hicho na kukifanya kuaminika zaidi na jamii.
“Mabadiliko mengi katika utekelezaji wa shughuli za baraza yamechochewa na uanachama wetu katika CPA kwani kila yanapotolewa maazimio katika vikao vya bunge la jumuiya ya madola, na sisi tunalazimika kubadili kanuni ili kwenda sambamba na wenzetu”, alisema kombo.
Akitolea mfano wa mabadiliko hayo kuwa ni pamoja na kualikwa kwa makundi mbali mbali ya wadau wanaohusika na fani maalum pale miswaada inapowasilishwa katika kamati za baraza kwa lengo la kupata maoni ya kitaalamu kuhusiana yanayowawezesha wajumbe kuwa na uelewa wa pamoja kuhusu mswada husika.
“Hili ni jambo jipya na limekuja mahsusi ili kuwafanya wajumbe watakapokuwa wanaijadili miswada husika iwe rahisi kwao tofauti na ilivyokuwa katika siku za nyuma”, alifafanua Kombo.
Nae Katibu wa chama hicha ambae pia ni Katibu wa Baraza la wawakilishi Zanzibar Raya Issa Mselem alieleza mashirikiano yaliyopo kati ya chama hicho na kilichopo katika bunge la jamhuri ya muungano wa Tanzania kuwa ni mzuri na kwamba vyombo hivyo vimekuwa vikishirikiana katika utekelezaji wa majukumu yao.
“Bunge la Jamhuri ya muungano wa Tanzania na Baraza la wawakilishi katika muungano wa mabunge tuna hadhi inayofanana na fursa sawa kama wanachama na tunapokuwa na shughuli za kikazi tumekuwa tukishirikiana na kushirikishana ili kuwa na uwiano sawa kama taifa”, alifafanua Raya.
Aliongeza kuwa baraza lake linatarajia kuendele kutoa elimu kwa makundi mbali mbali ili ddamira na hadhi ya baraza la wawakilishi katika kukuza demokrasia na maendeleo ya jamii iweze kufikiwa kwa kiwango kikubwa.
Maadhimisho hayo yanaadhimishwa kwa pamoja kati ya chama cha mabunge ya jumuiya ya madola na chama cha wabunge wanawake wa mabunge ya jumuiya ya madola matawi ya Zanzibar ambapo bunge la vijana litazungumzia masuala ya demokrasia ya kibunge, utawala bora na mambo mengine yanayohusiana na ujumbe wa mwaka huu unaosema ‘kuelekea hatma ya pamoja’.


Mwenyekiti wa Chama cha Mabunge ya Jumuiya ya Madola (CPA) tawi la Zanzibar Simai Mohammed Said (katikati) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu maadhimisho ya siku ya jumuiya ya madola itakayoadhimishwa Jumatatu Machi 12, 2018.


Katibu wa Baraza la Chama cha mabunge ya Jumuiya ya Madola na katibu wa Baraza la Wawakilishi Raya Issa Mselem (kushoto) akieleza jambo wakati wa mkutano wa waandishi kuhusiana na maadhimisho ya siku ya Jumuiya ya Madola. Kushoto kwake ni Mwenyekiti wa chama hicho Simai Mohammed Said na Afisa Sheria wa baraza la wawakilishi Mussa Kombo Bakar.

Baadhi ya waandishi wa habari wa vyombo mbali mbali viliopo Zanzibar wakifuatilia kwa karibu maelezo ya viongozi wa Chama cha Mabunge ya Jumuiya ya Madola tawi la Zanzibar kuhusu maadhimisho ya siku ya Jumuiya ya Madola yatakayofikia kilele chake Jumatatu Machi 12 mwaka huu.

Thursday, March 1, 2018

SMZ YAOMBWA KUWEKEZA ZAIDI KATIKA MRADI WA BAREFOOT COLLEGE KINYASINI UNGUJA


NA MWINYIMVUA NZUKWI
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imetakiwa kutoa msukumo kwa shughuli zinazoendeshwa katika kituo cha kutengenezea vifaa vya umeme wa jua cha ‘Barefoot college’ kilichopo Kinyasini Mkoa wa Kaskazini Unguja ili kizweze kufikia malengo ya kuanzishwa kwake.

Akizungumza na waandishi wa habari kituoni hapo, Mratibu Mkaazi wa ‘Barefoot Collage’ nchini Pendo Yaredi Sambayi alisema mradi huo una lenga kusaidia maendeleo ya jamii kwa kuwawezesha wanawake wa maeneo ya vijijini hivyo ipo haja ya kupewa kipaumbele ili kiweze kuendelea.

Alisema katika utekelezaji wa kazi zake chuo hicho kinatoa mafunzo ya kutengeneza vifaa vya umeme wa jua na kusimamia uunganishaji wa vifaa hivyo kwa wananchi wa vijiji ambavyo havijafikiwa na huduma ya umeme kwa lengo la kuharakisha maendeleo ya jamii sambamba na kutoa elimu ya ujasiriamali.

Alisema kikawaida chuo hicho kinatakiwa kutoa wahitimu mara mbili kwa mwaka lakini kimeshindwa kufanya hivyo kutokana na kukosekana kwa fedha kutoka serikalini jambo hilo limeshindikana na kutishia maendeleo ya mradi huo.

“Wahitimu wa mwisho walimaliza mwezi Aprili mwaka jana (2017) ambapo wanawake 9 walihitimu baada ya wenzao 11 kuhitimu mnamo mwaka mwaka 2016 jambo ambalo ni kinyume na utaratibu unaotakiwa wa kutoa wahitimu kila baada ya miezi mitano”, alieleza Pendo.

Hata hivyo alizipongeza serikali ya Zanzibar na ya India kwa kufikiria kuanzisha mradi huo ambao umesaidia kubadilisha maisha ya baadhi ya wanawake wa vijiji vinavyohusika na utekelezaji wa mradi huu.

“Mradi huu ni miongoni mwa matokeo ya ziara ya Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein alipotembelea nchini India na kutembezwa katika miradi ya huo cha Barefoot ndipo alipoiomba serikali ya nchi hiyo ije kutekeleza mradi huu hapa nchini kwa makubaliano maalum”, alieleza Mratibu huyo.

Aliyataja miongoni mwa makubaliano hayo kuwa ni pamoja na SMZ kugharmia mafunzo, kuratibu upatikanaji wa wanafunzi na eneo lililojengwa chuo hicho huku serikali ya India ikiwezesha ujenzi wa kituo hicho, safari za mafunzo nchini India za wakufunzi miongoni mwa wahitimu 11 wa kituo hicho na uendelezaji wa majengo ya chuo hicho ili kiweze kuchukua wanafunzi wengi zaidi kwa mwaka.

Aidha katika kuendeleza malengo ya mradi huo Pendo alieleza kuwa wameamua kutoa mafunzo ya ushonaji nguo za aina mbali mbali, ufugaji nyuki na kilimo chenye kuzingatia utunzaji wa mazingira ambayo wahitimu wanatakiwa kwenda kuyafanyia kazi pindi wanaporudi katika vijiji vyao sambamba na kukikuza na kuwa cha kimataifa.

"Serikali ya India imeshatoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa makaazi ya wanafunzi na ofisi za kituo, kinachosubiriwa ni kuna hatua za serikali ya zanzibar kurudisha mafunzo yaliyolengwa ambayo mipango inaendelea ili kituo hiki kiweze kutchukua wanafunzi kutoka ndani na nje ya Zanzibar", alisema Mratibu huyo amabae alisema kituo hiko kipo Zanzibar pekee katika Afrika Mashariki.

Akielezea mafanikio ya kituo hicho mratibu huyo alieleza kuwa idadi ya vijiji wanavyovihudumia imeongezeka na kufikia vinane Unguja na Pemba ambapo zaidi ya nyumba 1,000 zimeshafungwa vifaa vya umeme huo.

“Kwa sasa tupo katika vijiji 6 unguja na 2 pemba ambap kinamama wapaooondoka hapa kila mmoja hupatiwa vifaa vya umeme jua 50 ili akaviunganishe na kuwavungia watu 50 na kuwasimamia katika malipo ambayo ni madogo kulingana na vifaa vyenyewe lakini pia fedha hizo huwa ni mali yao kama kikundi au jamii”, alieleza.

Nae kiongozi wa timu ya kijamii wa kituo hicho aboubakar khalid alieleza licha ya kufanikiwa kuwa na wahitimu 20 hadi kufikia 2017, bado chuo hicho kinakabiliwa na uhaba wa fedha za kuendeshea mafunzo, vifaa vya kufanyia kazi baada ya masomo na ugumu wa kuwapata wanafuzi kutokana na sababu mbali mbali.

“Mradi huu umelenga kuwawezesha wanawake hasa wale wa vijijini ambao hawakusoma au wana elimu ndogo ambao wana umri kati ya miaka 35 na 55, hivyo baadhi ya wakati inakuwa ngumu kuwapata ili waweze kuhudhuria mafunzo kutokana na kutoruhusiwa na waume au jamaa zao”, alieleza Khalid.

Alisema ugumu wa waume na jamaa za wanawake wanaotamani kujiunga na masomo hayo unatokana na mwanafunzi kutakiwa kubakia chuoni kwa muda wa miezi mitano bila ya kuondoka jambo ambalo linakuwa gumu.

Akizungumzia mafunzo ya ufugaji nyuki yanayotolewa na kituo hicho Mratibu wa ufugaji nyuki Zanzibar Hassan Faraji Ali alisema mafunzo hayo yanaenda sambamba na mafunzo ya utunzaji wa mazingira ili kurahisisha upatikanaji wa mavuno mengi.

“Tumeamua kuliingiza somo hili ili kuwafanya wahitimu wetu wawe na ujuzi tofauti tofauti utakaowasaidia kuendeleza maisha yao kwani licha ya kupatiwa nyenzo za kuanzishia miradi yao pia tunawapatia ujuzi wa kutafuta masoko ya bidhaa wanazozalisha”, alifafanua.

Kituo hicho ambacho ni sehemu ya miradi ya chuo cha Barefoot unaotekelezwa katika nchi mbali mbali duniani kwa lengo la kueneza matumizi ya nishati mbadala kama njia ya kutunza mazingira na kuwawezesha wanawake ulizinduliwa na Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein miaka mitano iliyopita.   

   

Mratibu Mkaazi wa ‘Barefoot Collage’ nchini Pendo Yaredi Sambayi (Kulia) akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) walikitembelea chuo cha kufundishia utengenezaji wa vifaa vya umeme wa jua (sola power) kilichopo Kinyasini, Unguja. Kushoto ni Fatma Juma  Haji mwalimu wa uunganishaji wa vifaa vya sola aliyepata mafunzo nchini India . 
 

Mmmoja ya wahitimu na mwalimu wa kituo cha utengezaji wa vifaa vya umeme wa jua Amina Saleh Shamata (kushoto) akiwaelekeza waandishi wa habari waliotembelea kituo hicho namna vifaa vya umeme jua kabla ya kuanza kutumika.


Mwalimu wa somo la ufugaji nyuki na mazingira Elia Filbert Msuha (kushoto) akiwaonesha waandishi wa habari jinsi ya kutengeneza mbolea ya mboji inayotokana na mabaki ya vyakula na majani ya miti. Kulia ni Mratibu wa ufugaji nyuki Zanzibar Hassan Faraji Ali.


Mwalimu wa somo la ufugaji nyuki na mazingira Elia Filbert Msuha (kushoto) akitoa maelezo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu ufugaji wa nyuki.