Thursday, August 16, 2018

DK. BASHIRU KUZURU ZANZIBAR KUANZIA KESHO KUJITAMBULISHA



NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dk.Bashiru Ally anatarajiwa kufanya ziara ya kikazi ya siku nne visiwani humu Agosti 17 hadi 20 mwaka huu.
Dk.Bashiru anafanya ziara hiyo kwa mara ya kwanza tangu ateuliwe kushika nafasi hiyo Mei mwaka huu baada ya aliyekuwa Katibu Mkuu Abdulrahman Omar Kinana kustaafu.
Akitoa taarifa ya ziara hiyo ya Katibu Mkuu huyo, Katibu wa Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu Taifa(NEC),Idara ya Itikadi na Uenezi CCM, Zanzibar Catherine Peter Nao, alisema CCM Zanzibar tayari kimekamilisha maandalizi yote ya mapokezi ya kiongozi huyo.
Catherine alisema katika ziara yake hiyo pamoja na mambo mengine anatarajia kuzungumza na viongozi mbalimbali wa CCM na jumuiya zake na makundi ya kutoka taasisi za vijana visiwani humu.
Aliongeza kuwa ziara hiyo ya Dk.Bashiru itakuwa ni ya kikazi na kujitambulisha kwa wana-CCM ambapo wanatakiwa kujitokeza kwa wingi katika mapokezi ya Katibu Mkuu huyo ambapo atawahutubia wanachama pamoja na wananchi kwa ujumla katika uwanja wa Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui saa 9 alasiri.
“Tunawaomba wanachama wote tujitokeze kwa wingi kushiriki mapokezi hayo ya kiongozi wetu mpendwa ambaye ni mara ya kwanza kuja tukitambulisha na kuzungumzia sera na masuala mbalimbali ya kuimarisha CCM na Jumuiya zake, alisema Catherine.
Akizungumzia ratiba ya ziara hiyo Katibu huyo wa Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar,Catherine alisema siku ya siku ya kesho Agosti 17 mwaka huu katibu Mkuu huyo atakutana na kuzungumza na Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein.
Katibu huyo aliongeza kuwa Dk.Bashiru anatarajia kukutana na na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa ambaye pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd.
Alisema mchana wa siku hiyo ya ijumaa atazuru Kaburi la Muasisi wa Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar Hayati Mzee Abeid Karume na kuzungumza na watumishi pamoja na Wazee wa CCM Zanzibar ambapo jioni atazungumza na Viongozi na wanachama wa Mikoa minne ya CCM Unguja hapo katika viwanja vya CCM Kisiwandui.
Catherine aliendelea kueleza kuwa jumamosi ya Agosti 18 mwaka huu Katibu Mkuu huyo atazungumza na Wenyeviti wa CCM wa Mikoa na Wilaya, Makatibu wa CCM wa Mikoa na Wilaya, Kamati za siasa za Mikoa na Wilaya, Wabunge, Wawakilishi na madiwani katika ukumbi wa Kamati Maalum Kisiwandui pamoja na kuzungumza na makundi ya vijana katika ukumbi wa CCM Mkoa wa mjini.
Aliongeza kuwa siku ya Jumapili Agosti 19, mwaka huu Katibu Mkuu huyo asubuhi atasafiri kuelekea Pemba kwalengo la kuendelea na ziara yake hiyo ambapo atazungumza na Watumishi wa CCM na  wazee  wa Pemba katika ukumbi wa Ofisi ya CCM Kitengo.
Katibu huyo alisema Dk.Bashiru anatarajia kuzungumza na viongozi na wanachama wa CCM wa Mikoa miwili katika ukumbi wa skuli ya Fidel Castro Mkoa wa Kusini Pemba na jioni anatazungumza na Wenyeviti wa CCM wa Mikoa na Wilaya, Makatibu wa CCM wa Mikoa na Wilaya, Kamati za siasa za Mikoa na Wilaya, Wabunge, Wawakilishi,madiwani na maafisa wadhamini katika ukumbi wa Makonyo Pemba.
Katibu Mkuu huyo atahitimisha ziara yake hiyo siku ya Juma tatu Agosti 20 mwaka huu, kwa kuzuru kaburi la Dk.Omar Ali Juma kisiwani Pemba na kumalizia ziara yake kwa kuzungumza na  makundi ya vijana ambapo jioni atasafiri kuelekea Dar es salaam kuendelea na majukumu mengine.

MSEKWA, MAKINDA, KIFICHO KUWANOA WABUNGE VIONGOZI WA BUNGE

NA MWINYIMVUA NZUKWI
SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Yustin Ndugai amewataka wabunge wa bunge hilo kutumia kikamilifu mafunzo wanayopatiwa ili waimarishe utendaji wa chombo hicho.
Amesema bunge kama taasisi inayosimamia utendaji wa seriklia na utungaji wa sheria imekuwa ikitoa mafunzo kwa wabunge mara kwa mara yanayolenga kuwajengea uwezo ili waweze kutekeleza majukumu yao.
Akifungua semina ya Kamati uongozi wa bunge katika ofisi ndogo za bunge hilo Tunguu mkoa wa Kusini Unguja, Ndugai alisema bunge lina wajibu wa kuwaendeleza wabunge na watendaji wa chombo mara kwa mara ili kukifanya kuwa uimara.
Alisema ili kuimarisha utendaji wa bunge na wabunge, ofisi yake imeamua kuitisha mafunzo hayo na mengine yatakayofanyika ndani na nje ya nchi ambayo anaamini yatawaimarisha na kuwataka washiriki wa semina hiyo kutumia kuikamilifu uzoefu wa watoa mada walioteuliwa.
“Hii ni nafasi muhimu kwa kila mshiriki hivyo tutumie nafasi ya kuwa na viongozi wastaafu na wataalamu wengine waliopangwa kuwasilisha mada katika semina hii ili kujifunza namna bora ya kuendesha bunge na Kamati zetu”, alisema Spika Ndugai.
Aidha Spika Ndugai aliwataka viongozi wa Kamati na wabunge wa Zanzibar kuitumia ofisi hiyo kikamilifu katika shughuli zao za kibunge na kusisitiza kuwa ujenzi wa ofisi hiyo ulilenga kuimarisha muungano wa Tanzania.
Akiwakaribisha wajumbe wa semina hiyo ambao ni wenyeviti na makamo wenyeviti wa Kamati za kudumu za bunge, Wenyeviti wa tume ya uajiri ya bunge na wajumbe wa Kamati ya uongozi wa bunge, Spika wa baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid aliupongeza uongozi wa bunge na Kamati ya maandalizi kwa kuchagua watoa mada wenye weledi na uwelewa mpana katika uendeshaji wa mabunge nchini.
Alisema hatua hiyo itawasadia wajumbe kuchota sehemu ya uzoefu wa viongozi hao ambao wamelitumikia bunge la Tanzania, baraza la wawakilishi, serikali na vyombo mbali mbali vya kimataifa.
“Uamuzi wenu kuwaleta mama makinda (anna semamba), mzee Kificho (Pandu Ameir) na mzee Pius Msekwa ni wa kupongezwa kwani naamini katika muda huu wa siku mbili tutaendelea kujifunza mambo mengi ambayo yatasaidia uendeshaji wa bunge kama taasisi muhimu kwa maslahi ya jamii”, alisema Maulid.
Akizungumzia mafunzo hayo makamo mwenyekiti wa Kamati ya ustawi wa jamii inayoshughulikia ukimwi na dawa za kulevya dk. Jasmine tisekwa bunga alisema ubora wa mada zilizopangwa katika semina hiyo utasaidia kukuza uelewa wa wabunge kuhusiana na mambo mbali mbali yanayohusiana na kazi zao.
“Katika siku hizi tutajifunza kuhusu maadili, itifaki na mgongano wa maslahi katika uongozi wa umma mabo ambayo ndiyo changamoto kubwa sio katika uongozi wa bunge lakini hata katika maisha yetu ya kaweaida”, alisema Dk. Jasmine ambae ni mbunge wa viti maalum anaewakilisha vyuo vikuu.
Aliongeza kuwa pamoja na kuwepo kwa mafunzo kama hayo mara kwa mara, semina hiyo imekuwa ya kipekee kutokana na aina ya wawasilishaji wa mada ambao anaamini watasaidia kubadilisha mitazamo ya viongozi wa Kamati na wabunge kwa ujumla.
Nae Mbunge wa Uzini Zanzibar Salum Rehani Mwinyi alipongeza uongozi wa bunge kuandaa semina hiyo na nyengine amabazo zimekuwa zikiwasaidia viongozi wa Kamati na wabunge kuelewa mambo mbali mbali yanayohusiana na sekta wanazozisimamia.
Alisema hatua hiyo mbali ya kuwajengea uwezo, pia inatoa nafasi ya kutanua uelewa juu ya mambo mbali hasa kutokana na mabadiliko yanayotokea katika uendeshaji wa bunge na utekelezaji wa mipango ya serikali.
“Kwa muda mrefu tumekuwa na seminakama hizi lakini hii imekuwa ya kipekee kwani inatukumbusha juu ya umuhimu wa maadili, utawala bora, itifaki na diplomasia pamoja na njia za kuepukana na mgongano wa kimaslahi katika utendaji wetu kama viongozi wa umma ambao tuna wajibu kwa wananchi wetu, vyama vyetu na bunge kwa wakati mmoja”, alifafanua Rehani.
Mapema akitoa taarifa ya semina hiyo katibu wa bunge stepen kigaigai aleleza kuwa semina hiyo inatokana na ombi la wajumbe vwa Kamati za kudumu za bunge walilolitoa baada ya uchaguzi wa Kamati hizo mwezi Machi mwaka huu imelenga kuwawezesha wajumbe wa kutambua wajibu na majukumu yao katika utekelezaji wa kazi zao.
Semina hiyo ya siku mbili imehudhuriwa na viongozi mbali mbali akiwemo Naibu Spika wa bunge hilo Dk. Tulia Akson huku Maspika wastaafu wa bunge na Baraza la Wawakilishi Pius Msekwa, Anna Makinda na Pandu Ameir Kificho wakipangiwa kutoa mada ya uzoefu katika uongozi wa bunge na Kamati za bunge na elimu ya maadili, uongozi na utawala bora na viongozi itakayowasilishwa na mama Makinda kwa niaba ya Uongozi Institute.
Mada nyengine zitakazowasilishwa katika semina hiyo ni mgongano wa maslahi unavyoweza kuathiri maadili ya viongozi wa umma na wabunge itakayowasilishwa na Katibu wa sekretarieti ya maadili ya umma Waziri Kipacha, nafasi ya viongozi wa bunge na wenyeviti wa Kamati za bunge katika ulinzi na usalama wan chi itakayotolewa na Mluli Mahendeka na elimu kuhusu masuala ya diplomasia, itifaki na tabia kwa wabunge na viongozi itakayotolewa na mwalimu mstaafu katika chuo cha Diplomasia Luke Chilambo.
Pamoja na semina hiyo washiriki wa semina hiyo pia watapata nafasi ya kuonana na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein na kufanya ziara katika maeneo mbali mbali ya kihistoria ya mji wa Zanzibar ikiwa ni sehemu ya kuhimiza utalii wa ndani.
MWISHO.

Wednesday, August 15, 2018

KZU WADHIBITI MOTO MKUNAZINI, RC AYOUB AWATAKA WANANCHI KUCHUKUA TAHADHARI


NA MWINYIMVUA NZUKWI
Kikosi cha Zimamoto na Uokozi Zanzibar (KZU) Agosti 15, 2018 kimefanikiwa kuuzima moto uliozuka majira ya saa moja usiku katika moja ya majengo yaliyopo nyuma ya soko kuu la kuku shehia ya Mkunanizi, mjini Unguja.



Jengo hilo linalotumika kwa biashara na makaazi ya binadamu, linamilikiwa na Haroub Suleiman Nassor ambae amelikodisha kwa hoteli ya Marumaru linatumika kwa makaazi ya wanafunzi wanaofanya mafunzo ya vitendo katika hoteli hiyo pamoja na walimu wao.


Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Ayoub Mohammed Mahmoud (katikati) akizungumza na wanahabari wakati wa shughuli ya uzimaji wa moto. kulia ni Katibu Tawala wa Mkoa huo Hamida Mussa Khamis.

Akizungumza katika eneo la tukio Mkuu wa mkoa wa Mjini Magharibi Unguja Ayoub Mohammmed Mahamoud amewataka wamiliki wa majumba ya mji mkongwe zanzibar kutochanganya matumizi ya nyumba hizo ili kuepusha madhara yanayoweza kutokea pindi majanga ya moto yanapotokea.

Amesema katika jengo hilo lenye maduka ya kawaida na makaazi ya watu, wafanyabiashara wameweka majokofu wanayoyatumia kuhifadhia samaki na vitoweo vyengine jambo lililochangia kutokea kwa moto huo.

Aidha amewashukuru wakaazi wa shehia hiyo kwa hatua za awali walizochukua kuudhibiti moto huo kabla ya kikosi cha Zimamoto na uokozi Zanzibar kufanikiwa kuuzima bila ya kuleta madhara kwa maisha ya waakaazi wa nyumba hiyo.

Akizungumzia tukio hilo mkuu wa kikosi cha zimamoto na uokozi wilaya ya Mjini SSF Suleiman Ahmada Suleiman ameleza chanzo cha moto huo ni kutomika bila kupumzishwa kwa majokofu hayo na kupelekea kutokea kwa hitilafu ya umeme.

SSF Suleiman amesema hali hiyo inasababisha uchakavu na kuwataka watumiaji wa vifaa vya umeme kuzingatia matumizi sahihi ya vifaa hivyo.

Aidha amewatoa hofu wakaazi wa jengo hilo kuwa moto huo umedhibitiwa na kwamba eneo hilo lipo salama kwa matumizi huku akiwataka wananchi kutoa taarifa mapema katika kikosi chao ili kupunguza madhara ya moto au majanga mengine yanapotokea.

Nae sheha wa shehia ya Mkunazini Fuad Mohammed Hussein ameeleza kuwa jengo hilo la ghorofa mbili pamoja na maduka yaliyopo katika eneo la chini, linatumiwa kwa makaazi na wanafunzi wa chuo cha Sillas College waliopo katika mafunzo ya vitendo katika hoteli ya Marumaru iliyopo mjini Zanzibar.

Amesema awali alipewa taarifa ya kutokea kwa moto huo majira ya saa moja usiku na kuanza kutumia vifaa vya kuzimia moto walivyopatiwa na Chama Cha Mapinduzi mkoa wa Mjini hivi karibuni ili kupunguza kasi ya moto huo pamoja na kutoa taarifa polisi na kikosi cha zimamoto na uokozi kwa msaada zaidi.

Kamanda wa polisi mkoa wa Mjini Magharibi Kamishna Msaidizi (ACP) Tobias Sedoyeka aliyefika katika eneo la tukio wakati shughuli za uzimaji zikiendelea aliwapongeza wananchi wa eneo hilo kwa ushirikiano waliouonesha na kuwapa pole watu walioathiriwa na moto huo.

akizungumza kwa niaba ya wenzake mmoja ya wanafunzi hao ambae hakutaka kutajwa jina amesema moto huo ulianzia katika eneo la chini la jengo hilo na kufanikiwa kutoa taarifa kwa watu waliokuwepo maeneo ya jirani na jengo hilo baada ya kuona moshi mkubwa.

"Mimi nilikuwa ndio narudi kutoka kazini ila wenzetu waliokuwepo walisema waliona moshi mwingi ukiingia vymbani huku watu wengine wakipiga kelele za moto ndipo walipotoka ili kupisha watu wa zimamoto lakini tunashukuru sote tupo salama", amesema.

Aidha amewahakikishia wananchi hao kuwa jeshi lake litaendelea kuweka ulinzi katika eneo ili kulinda wananchi hao na mali zao.

Tuesday, August 14, 2018

DK. SHEIN AHIMIZA USAFI UIMARISHWE 'CHAWL BUILDING', AIPA TANO ZSSF

NA MWINYIMVUA NZUKWI
Rais wa Zanzibar na Baraza la Mapindunzi na Mwenyekiti wa Baraza la Mapindunzi Dk. Ali Mohamed Shein amewataka wafanyabiashara watakaopata nafasi ya kufanya biashara katika jumba la Chawal (jumba la treni) kudumisha usafi ili liweze kutumika kwa muda mrefu.

Akihutubia wananchi katika uzinduzi wa jengo hilo liliopo Darajani Mjini Unguja baada ya kufanyiwa matengenezo makubwa, Dk. Shein amesema jengo hilo lina historia kubwa hivyo kuimarishwa kwa usafi kutaongeza sifa ha haiba ya mji wa Zanzibar.

Amesema uamuzi wa serikali kulifanyia matengenezo jumba hilo yaliyosimamiwa na mfuko wa hifadhi ya jamii Zanzibar (ZSSF) Dk. Shein amesema umelaenga kuweka mazingira mazuri ya ufanyaji biashara na kutunzwa historia ya jingo hilo ambalo ni sehemu ya urithi wa kimataifa.

"Tulipoamua kulijenga upya jengo hili tulikuwa tunadhamira ya dhati ya kulinda na kuhifadhi historia ya nchi yetu katika masuala ya biashara bila ya kuathiri uhalisia wake na ndio maana kabla ya kuanza kujenga tulihakikisha tunazingatia maelekezo ya UNESCO", amesema.

Ameupongeza uongozi na wafanyakazi wa wizara ya Fedha na Mipango, Mfuko wa hifadhi ya jamii (ZSSF) na Mshauri mwelekezi wa mradi huo kwa kusimamia kikamilifu ujenzi wa jengo hilo uliotekelezwa na kampuni ya CRJE ya China kwa kufuata vigezo vilivyowekwa na shirika la kimataifa la sayansi na utamaduni (UNESCO) na kusimamia uendeshaji.

"Kama tulivyotekeleza mradi huu, tutakeleza miradi mingine ukiwepo huu wa ujenzi wa maduka ya kisasa hapa Darajani mara baada ya kukamilisha taratibu zilizowekwa na UNESCO kwani eneo hilo lipo katika ukanda wa urithi wa kimataifa", amesema Dk. Shein.

Nae Waziri wa Fedha na mipango Zanzibar Dk. Khalid Salum Mohammed amempongeza Rais Dk. Shein kwa kusimamia maelekezo yake kila mara yaliopelekea kupatikana kwa mafanikio ya mfuko huo katika uwekezaji wa miradi mbali mbali ya maendeleo nchini.

Amesema katika kipindi cha miaka 20 ya uhai wa mfuko huo, umeweza kutekeleza miradi ya ujenzi na uwekezaji kiuchumi iliyolenga kuiamarisha uwezo wa mfuko huo ili kutoa huduma kwa wanachama wake.

Amaitaja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni ujenzi wa mnara wa kumbu kumbu ya mapinduzi, ujenzi wa viwanja vya kufurahishia watoto vya Kariakoo mjini Unguja na Tibirinzi kisiwani Pemba, ujenzi wa nyumba za makaazi na ukarabati wa jengo hilo  na katika muda mchache ujao ZSSF itaanza ujenzi wa maduka ya kisasa katika eneo la Michenzani.

Aidha Dk. Khalid amewapongeza wafanyabiashara waliokuwa wakifanyabiashara na wakaazi wa jengo hilo kwa kukubali kuhama ili kupisha ujenzi huo na kuwahakikishia kuwa serikali itaendelea kujenga miundombinu rafiki ya kukuza biashara nchini ikiwa ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM na ahadi ra Rais alizozitoa wakatiki wa kampeni.

Mapema akitoa taarifa kuhusu ujenzi huo, Mkurugenzi Mwedeshaji wa ZSSF Sabra Issa Machano amesema ujenzi huo ulihusisha makampuni mbali mbali utasaidia kukuza uchumi wa nchi kutokana na shughuli zitakazoendeshwa ndani ya jengo hilo pamoja na kuwa kivutio cha utalii.

Amesema ujenzi huo uliochukua miezi 20 hadi kukamilika kwake, umegharimu shilingi bilioni 11.5 ambapo mbali ya milango ya 52 ya maduka, ndani ya jengo hilo kutakuwa na nyumba 10 za makaazi, mgahawa, ukumbi wa mazoezi na vyumba vya mashine za kielektroniki za kutolea fedha (ATM).

Akizungumzia ujenzi huo Mkuu wa mkoa wa Mjini Magharibi Ayoub Mohammed Mahmoud amemshukuru rais wa Zanzibar kwa kusisitiza uadilifu miongoni mwa wafanyabiashara na wasimamizi wa mradi huo ili uweze kuleta mafanikio.

Aidha amemshukuru Dk. Shein kwa kuridhia kuendelea kuishi katika jengo hilo bila ya malipo mmoja ya wakaazi wa awali wa jengo hilo bi. Zuwena ambae alikuwa mtu wa mwisho kuhama katika jengo hilo kabla ya kukabidhiwa kwa mkandarasi kwa ajili ya ujenzi.

Amesema mama huyo licha ya kuwa na vielelezo vilivyomhalalisha kuishi katika jengo hilo alivyopatiwa na serikali ya awamu ya kwanza iliyoongozwa na mzee abeid Amani karume, mama huyo alikubali kupisha ujenzi huo na kupelekwa katika makaazi ya kulelea wazee Sebleni.

"Mama huyu alikuwa ni miongoni mwa wakaazi wa jengo hili alieishi kwa muda mrefu zaidi ya mtu mwengine yeyote lakini alikubali kuondoka na kupisha ujenzi kufanyika lakini leo Mheshimiwa Rais ameagiza mama huyu apatiwe nyumba miongoni mwa nyumba zilizomo humu na aishi kwa muda wake wote bila ya malipo yeyote", amesema Ayoub.   

Dk Ali Mohamed Shein Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi akifungua pazia kuashiria uzinduzi wa jengo la Chawl (Jumba la treni) baada ya kufanyiwa matengenezo makubwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF).
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein (alievaa miwani) akihutubia wananchi wakati uzinduzi wa jengo la Chawl (Jumba la treni) baada ya kufanyiwa matengenezo makubwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF).
 Mkurugenzi Mwendeshaji wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) Sabra Issa Machano (kulia)  akitoa maelezo ya utekelezaji wa mradi wa matengenezo ya jengo la Chawl (Jumba la treni).
 Muonekano wa jengo la Chawl (jumba la treni) baada ya kufanyiwa matengenezo makubwa na na kuzinduliwa ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 20 ya
Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF). PICHA KWA HISANI YA IDARA YA HABARI MAELEZO, ZANZIBAR.

Monday, August 13, 2018

RC AYOUB AKABIDHIWA KOMYUTA ZA WAFAULU WA KIDATO CHA SITA



Na Mwinyimvua Nzukwi

WADAU wa sekta ya elimu na wananchi wa Zanzibar, wametakiwa kuunga mkono juhudi zinazochukuliwa na Serikali ili kuimarisha elimu nchini kwa kiwango kilicho bora.

Akizungumza baada ya kupokea kompyuta 96 aina ya laptop kutoka kampuni ya ROM Solutions, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Ayoub Mohammed Mahmoud, amesema kufanya hivyo kutatanua wigo wa mafanikio katika sekta hiyo.

Amesema serikali kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, imekuwa ikitekeleza shughuli mbalimbali zikiwemo za ujenzi wa madarasa na kuondoa michango kwa wanafunzi wa ngazi zote ili kuondoa changamoto zinazoikabili sekta ya elimu ambazo huchangia kupatikana matokeo yasiyoridhisha.

UTPC YAANZA KUWANOA WAANDISHI WA HABARI, WANACHAMA WA KLABU ZA WAANDISHI WA HABARI


NA MWINYIMVUA NZUKWI
Muungano wa klabu za waandishi wa habari Tanzania (UTPC) umeanza kutekeleza mpango wa mafunzo kwa wanachama wa klabu za waandishi wa habari nchini Tanzania kuanzia leo.

Taarifa iliyotolewa na Afisa programu za mafunzo, utafiti na machapisho wa UTPC Victor Maleko kwa klabu za waandishi wa habari Tanzania imeeleza kuwa mafunzo hayo yamelenga kuimarisha uwezo wa kitaaluma wa waandishi wa habari na kuleta mabadiliko katika jamii.

Alisema hatua hiyo inafuatia kukamilika kwa uchambuzi wa maombi ya wanachama wa klabu hizo yaliyofanywa miezi miwili iliyopita na kwamba waandishi hao watapatiwa mafunzo mbali mbali kuanzia mwezi wa Agosti 2018

“Mafunzo haya ni sehemu ya utekelezaji wa mpango mkakati wa UTPC wa 2016 - 2020 ambapo waandishi watapatiwa mafunzo kisha kupatiwa mikataba ya kufanya kazi ili kutathmini ufanisi wa mafunzo yanayotolewa”, alieleza.

Aliongeza kuwa kundi la kwanza la waandishi hao linatarajiwa kuanza kupatiwa mafunzo ya uandishi wa habari za mazingira yatakayofanyika mkoani Morogoro kuanzia Agost13 - 27 mwaka huu wakati kundi la pili litashiriki mafunzo ya uchambuzi wa sera na ufuatiliaji wa bajeti yatakayofanyika mkoani Pwani na kufuatiwa na mafunzo ya habari za uchunguzi kati ya Agosti 14 na 17 mwaka huu.

Maleko alieleza kuwa kwa mwaka 2018 mbali na mafunzo hayo, wanachama wa klabu za waandishi wa habari Tanzania watajengewa uwwzo wa uandika  habari za jinsia, habari za afya, habari za haki za binadamu na utawala bora, misingi na maadili ya uandishi wa na mafunzo ya utangazaji.

Afisa huyo amewataka waandishi waliobahatika kupata nafasi hiyo kuitumia kikamilifu na kujifunza kwa lengo la kubadilisha uandishi wao unaotarajiwa kuleta mabadiliko katika jamii.

Akizungumzia hatua hiyo Katibu Mkuu wa klabu ya waandishi wa habari Zanzibar (ZPC) Faki Mjaka mbali ya kuwapongeza wanachama wa klabu hizo kwa kuteuliwa kuhudhuria mafunzo hayo na kuwataka kuitumia vyema fursa hiyo ili kutimiza ndoto zao za kujiimarisha katika taaluma ya uandishi wa habari.

Alisema iwapo waandishi hao watashiriki na kuzingatia mafunzo hayo kuna uwezekano wa kupatikana mabadiliko makubwa katika tasnia ya habari na taifa kwa ujumla.

Aidha aliipongeza sekretarieti ya UTPC kwa kutekeleza majukumu yao kwa kufuata mipango iliyoidhinishwa na vikao vya juu vya taasisi hiyo na kuwaomba wakuu wa vyombo vya habari nchini kuwaruhusu waandishi wao ili washiriki mafunzo hayo yatakayosaidia kuimarisha utendaji wa vyombo vyao.

"Kutokana na utaratibu wa UTPC mwandishi anaomba mwnyewe aina ya mafunzo, unaongeza uthubutu, uwajibikaji na kubadililisha mitazamo ya wanachama wetu hivyo ninawaomba wawe wepesi kutumia hizi fursa", alisisitiza Mjaka.

Zaidi ya wanachama 50 wa klabu za waandishi wa habari nchini wakiwemo wanachama 6 wa klabu ya waandishi wa habari Zanzibar (ZPC) wanatarajiwa kushiriki mafunzo ya uandishi wa habari za uchunguzi, habari za mazingira na habari za uchambuzi wa sera na ufuatiliaji wa bajeti kuanzia Agosti 13, 2018 yatakayofanyika katika mikoa Morogoro, Pwani na Dodoma.