Tuesday, June 11, 2013

BAJETI YA SMZ KESHO

  • YATARAJIA KUTUMIA BILIONI 658
  • MASLAHI YA WAFANYAKAZI KUBORESHWA
  • ELIMU, MAJI NA AFYA KUPEWA KIPAUMBELE
Na: Mwinyimvua Nzukwi, Zanzibar
Serikali ya mapinduzi yan Zanzibar inatarajia kutumia jumla ya shilingi bilioni 658.5 katika mwaka wa fedha utakaoanzia Julai mwaka huu.
Akitoa muhtasari wa bajeti kwa waandishi wa habari afisini kwake Vuga mjini hapa Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Fedha na Mipango ya Maendeleo, Omar Yussuf Mzee alisema bajeti hiyo ni ni ongezeko la wastani wa shilingi bilioni 45 ikilinganisha na ya mwaka unaomalizika.
Alisema hali hiyo imetokana na ongezeko la mahitaji ya wananchi na kuimarika kwa pato la taifa ambalo limefikia wastani wa shilingi Milioni moja kwa mwaka kwa kila mwananchi na kupungua kwa mfumko wa bei toka asilimia 14.9 mwaka 2011 hadi asilimia 9 mwaka 2012.
“Serikali inawajibika kutoa huduma za jamii katika hali iliyo bora, kwa kuzingatia hilo na kutokana na kukua kwa hali ya uchumi na kuongezeka kwa pato la taifa tumelazimika kuongeza bajeti ukilinganisha na ya mwaka uluiopita ili kuleta ufanisi katika mipango ya serikali”, alisema.
Alizitaja sekta zilizopewa kipaumbele katika bajeti hiyo ni za afya, maji, kilimo na elimu ambazo amesema zina mchango mkubwa na wa moja kwa moja katika uchumi na ustawi wa jamii.
“Sote tunajua matatizo yaliyopo katika upatikanaji wa maji safi na salama na dawa katika hospitali zetu, hii ndio sababu bajeti hii ikaziweka sekta hizi kuwa ndio kipaumbele chetu”, alisisitiza Waziri Yussuf na kuongeza kuwa serikali inatarajia kujitegemea yenyewe katika suali la upatikanaji wa dawa muhimu baada ya konekana viashiria vya kukoma kwa ufadhili wa mfuko wa pamoja wa sekta ya afya unaofadhiliwa na Global Fund.
Aidha alisema katika kuongeza pato la taifa na mwananchi mmoja mmoja serikali itaelekeza nguvu katika utekelezaji wa mradi mkubwa wa uimarishaji wa mifumo ya umwagiliaji maji ili kukuza uzalishaji wa chakula nchini jambo ambalo amedai litapunguza uagiziaji wa chakula toka nje ya nchi.
“Tutakapozalisha chakula kwa wingi tutapunguza uagiziaji na kuongeza pato la taifa kwani hata nakisi ya bei itakuwa ndogo na kumuwezesha kila mwananchi kupata mahitaji yake muhimu kwa urahisi”, aliongeza Yussuf na kuwataka wananchi kuendeleza hali ya amani na utulivu iliyoko nchini ili kuvutia wawekezaji zaidi ambao watachangia kupunguza tatizo la ajira linaloikabili taifa.
Akizungumzia maslahi ya wafanyakazi katika sekta ya umma Yussuf alisema yataongezeka kama yalivyoahidiwa na Rais katika hutuba ya uzinduzi wa baraza la wawakilishi na Mei Mosi mwaka huu ikiwa na pamoja na kuongeza nafasi za ajira mpya kwa madaktari, mainjinia na kujaza mapengo yaliyowacha wazi na wafanyakazi waliostaafu katia kada mbali mbali.
Kuhusu hali ya uchumi Waziri Yussuf alisema unatarajiwa kukua katika mwaka ujao kutokana na kufanyiwa kwa marekebisho na kuondoshwa kwa baadhi ya kodi na kuimarisha mfumo wa udhibiti wa mapato ya serikali.
“Katika bajeti hii tumependekeza kufanyiwa nmarekebisho, kuondoshwa na kuanzishwa kwa baadhi ya kodi ili kutanua wigo wa ukusanyaji na udhibiti wa mapato ya serikali jambo ambalo naamini litainua hali za wananchi wetu”, alisema.
Kwa mujibu wa waziri huyo kiasi hicho kinachopendekezwa kutumika katika mwaka huu wa fedha, asilimia hamsini inatokana na mapato ya ndani na kiasi kilichobakia kitatokana na ufadhili wa washirika wa maendeleo jambo ambalo amedai linatokana na mipango ya serikali ya kupunguza utegemezi kwa wafadhili katika bajeti.
Bajeti hiyo inatarajiwa kuwasilishwa katika mkutano wa nane wa baraza la wawakilishi unaotarajiwa kuanza kesho (Jumatano) ijayo.
Mwisho.

KUKATIKA UMEME SASA BASI

DK SHEIN AZINDUA MRADI WA UIMARISHAJI WA MIUNDOMBINU YA UMEME
 
Na: Mwinyimvua Nzukwi, Zanzibar
Shirika la umeme Zanzibar (ZECO) limetakiwa kuwajengea uwezo wafanyakazi wake ili kufanya kazi kwa kiutaalamu na kuachana na tabia ya kufanya kazi kwa mazoea.
 
Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohammed Shein alitoa wito huo katika uzinduzi wa mradi wa uimarishaji wa miundombinu ya usambazaji wa umeme uliofanyika katika kituo kikuu cha kupokelea umeme cha Mtoni, Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja.
 
Dk. Shein amesema vifaa na mfumo uliomo katika miundo mbinu iliyozinduliwa licha ya kuwa na gharama kubwa pia ni ya kisasa hivyo kuna kila haja kwa uongozi wa shirika hilo kuwawezesha kitaaluma watendaji wake ili wawe makini katika uendeshaji wa mitambo hiyo kama moja ya njia za kuutunza mradi huo.
 
"Haitokuwa busara iwapo mradi huu hautodumu kama ilivyokusudiwa, hivyo ipo haja kwa bodi na uongozi wa shirika kuwajengea mazingira mazuri watendaji watakaokuwa wanafanya kazi katika kituo hiki ili wawe makini na kujua kuwa maisha ya Wazanzibari wote yanakuwa mikononi mwao wakati wote", alisema Dk. Shein.
 
Aidha alisema kuwa uzinduzi wa mradi huo unatokana na azma ya Serikali ya Zanzibar katika kuwaletea wananchi wake maendeleo na haja ya ongezeko la mahitaji ya watumiaji wa umeme ambao wamekuwa wakiongezeka mwaka hadi mwaka na kupelekea tatizo la kuzidiwa kwa miundombinu ya awali ya umeme iliyowekwa toka mwaka 1979.
"Idadi ya watu na idadi ya watumiaji wa umeme imekuwa ikiongeza kila kukicha hivyo tusingeliweza kubakia na miundombinu ile ile ambayo ilichakaa na kutoendana na kasi ya maendeleo ya nchi na watu wetu", aliongeza Dk. Shein na kulishukuru Shirika la Maendeleo la Japan (JAICA) kwa kuchangia kukamilika kwa utekelezaji wa mradi huo ambao unatarajiwa kuondosha tatizo la kukatikatika na kupungua nguvu kwa umeme katika kisiwa cha Unguja ambapo katika kipindi cha mwezi mmoja limepungua kwa asilimia 77.3.
Sambamba na hayo Rais Shein alisema serikali yake itaendelea na jitihada za kutafuta vyanzo mbadala vya umeme ili kuweza kupatikana kwa umeme wa uhakika jambo ambalo litaongeza idadi ya wawekezaji kutoka ndani na nje.
 
"Tumefikia hatua nzuri , UNDP (Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa) wametusaidia kuweka mshauri elekezi na katika muda si mrefu tutaamua ni njia ipi tutumie kati ya mawimbi ya bahari na upepo katika kuzalisha umeme mbadala ili ikitokea matatizo kusiwe na matatizo kama ilivyopata kutokea siku za nyuma", aliongeza Dk. Shein ambaye alisema hali hiyo itasaidia kupunguza gharama za uendeshaji wa uzalishaji wa umeme kwa majenereta ya dharura.
 
Mapema akitoa maelezo ya kitaalamu kuhusu mradi huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi Maji, Makaazi na Nishati Al-halil Mirdha alisema mradi huo umekusudia kuimarisha upatikanaji wa huduma za nishati ya umeme kwa kuhusisha ujenzi wa vituo vinne vya kupokelea na kusambazia umeme, ujenzi wa njia za kusafirishia umeme na upatikanaji wa vifaa vya kufanyia kazi.
 
Alisema kuwa jumla ya shilingi Bilioni 57, 342 zimetumika ambapo serikali ya Japani imechangia shilingi Bilioni 55 na serikali ya Zanzibar imechangia kiasi cha shilingi Bilioni 2 laki 342 ambazo zimetumika kwa ununuzi, usafirishaji, ufungaji wa vifaa vya mradi, kumgharamia Mshauri muelekezi na mafunzo ya watendaji wa shirika wakati wa utekelezaji wa mradi.
 
"Makubaliano ya utekelezaji ya mradi huu yaliitaka serikali kugharamia mpango wa kuwahamisha waathirika wa utekelezaji wa mradi, kusamehe kodi ya vufaa vilivyoletwa na upatikanaji wa maeneo ya ujenzi wa vituo na njia za umeme", alisema Katibu Mirdha.
 
Naye Balozi wa Japani nchini Tanzania Masaki Okada alisema serikali ya japani imeamua kufadhili mradi huo kutokana na uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na nchi yake na haja ya kusukuma maendeleo ya watu wa nchi hii.
 
"Japani imesukumwa na hamu ya kutaka kujiendeleleza ya wananchi wa Tanzania na ndio maana tukafadhili mradi huu ili kutoa nafasi kwa wananchi wake waweze kuendelea na kukabiliana na changamoto za kiuchumi na kijamii", alisema Balozi Okada na kuongeza kuwa ni matumaini ya nchi yake kuwa mradi huo utasaidia kupunguza kasi ya umaskini na ongezeko la gesi joto ambalo ni sehemu ya matokeo ya mabadiliko ya tabia nchi.
 
Utekelezaji wa mradi huo unafuatia kukamilika kwa mradi mwengine wa utandazaji wa waya mpya wa umeme wa chini ya bahari kutoka Ras Kiromoni Tanzania Bara hadi Fumba na ujenzi wa kituo cha kupokelea umeme cha Mtoni mwanzoni mwa mwaka huu mradi ambao ulifadhiliwa na mfuko wa changamoto za milenia (MCC).
MWISHO.

Saturday, June 8, 2013

DK. SHEIN KUZINDUA MRADI MKUBWA WA UMEME

Na: Mwinyimvua Nzukwi, Zanzibar
·        ZECO KUPOKEA MRADI WA WAJAPANI WIKI IJAYO
·        NI WA NJIA NA MFUMO MIPYA YA UMEME
·        KUTARAJIWA KUMALIZA KABISA TATIZO LA UMEME VISIWANI
Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) linataraji kuzindua Mradi mpya wa Usambazaji umeme kwa lengo la kuimarisha Miundombinu ya huduma hiyo na kumaliza tatizo la upatikanaji wa Umeme katika kisiwa cha Unguja.
Mradi huo uliogharimu kiasi cha shilingi bilioni 55  ni msaada kutoka nchi ya Japan unatarajiwa kuzinduliwa Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein katika kituo cha Mtoni Unguja Juni 11 mwaka huu.
Akitoa taarifa kwa Waandishi wa habari ofisini kwake, Meneja wa shirika hilo Hassan Ali Mbarouk amesema Mradi huo ulioanza mwaka 2011 tayari  umeshakamilika na kwa sasa wanachosubiri ni uzinduzi unaotarajiwa kufanywa na Rais ahitimishe sherehe hiyo.
Amefahamisha kuwa katika utekelezaji wake Mradi huo ulijumuisha ujenzi wa Vituo vitatu vya kusambazia umeme vya Mtoni, Mwanyanya na Welezo na hivyo utaiwezesha Zanzibar kuwa na umeme wa uhakika bila mgao wa aina yoyote.
Hassan ameongeza kuwa kabla ya Mradi huo mpya baadhi ya maeneo yalikuwa yanakabiliwa na mgao uliosababisha umeme kukatika zaidi ya mara 10 kwa siku lakini tatizo hilo kwa sasa limeondoka kupitia mradi huo.
“Kulikuwa na maeneo ambayo kwa siku umeme ulikuwa unakatika mara 10 au zaidi lakini baada ya kuanza kazi mradi huu tunashukuru hakuna tena mgao  katika maeneo hayo” alibainisha Meneja wa ZECO.
Aidha amewataka Wananchi ambao wanasumbuliwa na matatizo ikiwemo umeme mdogo na kukatika katika umeme katika maeneo yao kutoa taarifa kwa Shirika la Umeme ili kupatiwa ufumbuzi.
Akielezea changamoto zinazolikabili Shirika Meneja Hassan alisema kuwa ni pamoja na uchakavu wa nyaya za kusambazia umeme, kuzidiwa kwa Transfoma kutokana na ongezeko la makaazi na baadhi ya Wananchi kukosa kulipia huduma hiyo.
Hata hivyo alieleza kuwa tayari wameagiza Waya za kutosha, Transfoma na Nguzo kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya upatikanaji wa Umeme wa uhakika katika kila eneo
“Wanachi wasisubiri umeme ukatwe ndio wakalipe, wawe na utamaduni wa kulipa kabla ya muda wa kukatiwa kufika na ikitokezea kuna tatizo basi wawasiliane na ZECO sisi tunafanya kila njia kuwapatia huduma  kwa ufanisi” Alisema Meneja.
Kuhusu utaratibu wa Wananchi kulipia huduma ya umeme kwa njia ya Simu Meneja alisema kuwa wamejadiliana na Kampuni ya Zantel ili kufanikisha utaratibu huo lakini bado kuna kasoro hivyo Wananchi waendelee kuwa na subra.
Amesema wanaendelea kushirikiana kwa karibu na Zanztel kuhakikisha kuwa huduma hiyo inafanya kazi kwa ufanisi bila matatizo yoyote ili kurahisisha utaratibu wa kulipia umeme kwa Wakaazi wa Zanzibar.
Uzinduzi wa Mradi huo mpya wa umeme uliofadhiliwa na Japan utakaofanyika  Jumanne hapo Mtoni Unguja unatarajiwa kuwa suluhisho la tatizo la umeme kwa Kisiwa cha Unguja.
Kwa miezi kadhaa sasa toka kuzinduliwa mradi wa Njia ya Pili ya Umeme wenye Kilowat 100, kutoka Ubungo Dar es Salaam hadi Mtoni Zanzibar, uliofadhiliwa na Shirika la Misaada la MCC la Marekani,Mgao wa umeme haujatokea ambapo uzinduzi huo mpya utalifanya tatizo la mgao wa umeme kuwa la kihistoria Zanzibar.

RAVIA ACHAGULIWA KUWA RAIS WA ZFA

Na. Mwinyimvua Nzukwi, Zanzibar
·        RAVIA RAIS MPYA ZFA
·        APATA ASILIMIA 69.8
·        AWA RAISI WA TATU KATIKA MUHULA MMOJA.
Kitendawili cha nani angelimrithi Amani Ibrahim Makungu baada ya kujiuzulu urais wa chama cha soka Zanzibar ZFA kimepata jibu baada ya mjumbe wa kamati tendaji ya chama hicho kutoka Wilaya ya Kusini Ravia Idarous Faina kuchaguliwa kushika wadhifa huo.
Mkutano huo wa uchaguzi uliofanyika katika ukumbi wa VIP wa uwanja wa Amaan ulimchagua Idarous kwa kura 37 sawa na asilimia 69.8 dhidi ya kura 16 sawa na asilimia 30.2 asilimia za Abdall Juma Mohammed ambaye pia ni mjumbe wa kamati tendaji na Mwanasheria wa chama hicho.
Mgombea mwengine Rajab Ali Rajab hakupata kura hata moja kati ya kura 53 zilizopigwa na hakuna kura iliyoharibika.
Akitoa maelezo mbele ya wajumbe wa mkutano huo kabla na baada ya kuchaguliwa alisistiza kuendelea kusimamia katiba ya chama hicho na kudumisha maelewano miongoni mwa wajumbe wa kamati tendaji na wadau wengine wa soka hapa nchini.
“Naelewa kila kitu kinacholikwamisha soka letu na nazijua shida mlizonazo hivyo naomba mniamini kuwa nitasimamia kanuni na katiba katika kuziondoa na  kwamba mjue wajumbe sote tutakuwa na hadhi sawa na hakuna alie juu ya mwengine kikubwa ni maelewano tu”, alisema Idarous.
Aliongeza kuwa atajitahidi kuhakikisha anasimamia kuwepo kwa maendeleo ya kweli ya soka la Zanzibar huku akiwaomba wajumbe hao na wadau wa soka kufanya kazi kwa bidii katika ngazi zote ili kuhakikisha maendeleo ya kweli na haraka yanapatikana.
Akizungumzia uchaguzi  huo Rajabu alisema licha ya kukosa kura anakubaliana matokeo hayo na kwamba amefarajika sana na jinsi uchaguzi huo ulivyoendeshwa na kamati ya uchaguzi ambayo alisema ilitenda haki na kwamba atakuwa tayari kumuunga mkono rais aliechaguliwa.
“Pamoja na kuwa sikupata kura, hayo ni maamuzi ya wajumbe wa mkutano mkuu lakini kwa ujumla nimeridhika na mchakato ulivyoendeshwa na nakubaliana na matokeo”, alisema Rajabu ambaye ni mwanafunzi wa chuo kikuu cha Zanzibar, Zanzibar University.
Nae Abdalla Juma alimpongeza Ravia na kuahidi kumpa kila ya aina ya ushirikiano na kuwataka wajumbe mengine na wadau kumsaidia ili aweze kutimiza wajibu wake kikamilifu.
“Kimsingi sina pingamizi na matokeo haya zaidi ya kuwashukuru wajumbe kwa kutumia haki yao ya kidemokrasia na ningependa tumsaidie ili aweze kutekeleza majukumu yake.
Mapema mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi ya ZFA Gullam Rashid Abdalla aliwataka wajumbe wa mkutano mkuu kufanya maamuzi bila ya kushawishiwa wala kushinikizwa na kutambua wajibu wao kwa jamii ya wazanzibari ambao wamechoshwa na malumbano katika chama hicho.
“Wajumbe mna wajibu wa kuzingatia matakwa ya wadau wa mchezo wa soka na sio utashi wenu na vyema mkazingatia taratibu za uchaguzi ili kukamilisha mchakato huu”, alisema Mwenyekiti huyo.
Ravia anakuwa Rais wa tatu katika muhula mmoja ulioanzia Oktoba 2010 na kumalizika Disemba 2014, akitanguliwa na Ali Fereji Tamim aliyejiuzulu mnamo mwezi Machi mwaka 2012 na Amani Ibrahim Makungu ambae alijiuzulu mwishoni mwa mwezi Januari mwaka huu kila mmoja akitoa sababu tofauti.  

Monday, May 27, 2013

RAZA AJITOSA URAIS ZFA

  • AAHIDI KUIMARISHA UMOJA NA MAELEWANO
  • KUONGEZA WADHAMINI, UJENZI WA TAASISI ILIYO IMARA 
Na. Mwinyimvua Nzukwi, Zanzibar
Idadi ya wagombea katika kinyang’anyiro cha uraisi wa Chama Cha Mpira wa Miguu Zanzibar ZFA imefikia watatu baada ya Makamo Mwenyekiti wa zamani wa chama hicho Ibrahim Raza kuchukua na kurejesha fomu katika  afisi za kamati ya ya uchaguzi zilizopo katka uwanja wa Amaan, Zanzibar.

Wengine waliochukua na kurudisha kwa nyakati tofauti siku chache zilizopita ni pamoja na mwanasheria wa chama hicho Abdulla Juma na  mjumbe wa kamati tendaji ya ZFA taifa  kutoka wilaya ya Kusini Unguja,  Ravia Idarous.

Akizungumza na waandishi wa habari afisini kwake Vuga mjini Zanzibar, Raza alisema ameamua  kugombea nafasi hiyo ili kusaidiana na wajumbe wengine kurudisha ari na msimsimko wa wapenzi na wadau wa soka  kama ilivyokuwa katika miaka ya themanini na mwishoni mwa miaka ya tisini.

Alisema kwa muda wapenzi na washabiki wa mchezo huo wamepoteza morali wa kuhudhuria katika mechi za ligi kuu jambo ambalo linarudisha na kushusha ari ya wachezaji  jambo linalopelekea wengine kuhamia katika ligi ya Tanzania bara ambako amedai kuna msisimko wa kutosha.

“Hakuna siri kuwa msisimko wa washabiki kuja viwanjani umepungua na hii inakutokana na mambo mengi ambayo yanapelekea kuporomoka kwa viwango vya wachezaji na soka la Zanzibar”, alisema Raza ambaye pia aliwahi kuwa Makamo Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar (BTMZ) katika miaka ya 90. 

Alisema ili kufikia hali hiyo atahakikisha anaongeza idadi wa wadhamini katika ligi zinazosimamiwa na ZFA Taifa na kusimamia ujenzi wa chama hicho kama taasisi imara yenye kuaminika ili kuvutia wafadhili na wadhamini.

“Tusidanganyane, hakuna mtu anayeweza koungoza peke yake au mdhamini atakayejitokeza kama hakuna umoja na kuaminiana katika chama …….. nashukuru Grand Malt wameanza lakini nitajitahidi kama nikichaguliwa kuongea na mashirika mengine kufanya kuidhamini ligi hiyo na ligi nyengine ili kuongeza ushindani miongoni mwa vilabu vya ligi kuu”, aliongeza kocha wa zamani wa timu ya Mwera Stars iliyowahi kushiriki ligi daraja la kwanza taifa.

Akizungumzia suala la uanachama wa FIFA kwa chama hicho, alisema ataendeleza jitihada zilizofanywa na vyombo husika katika kuipatia Zanzibar uanachama wa shirikisho hilo na kama itashindikana basi atahakikisha chama hicho kinapata mgao unaostahiki kutoka katika shirikisho la mpira wa miguu Tanzania, TFF.

“Hili ni jambo nililolianza toka nikiwa BTMZ kwa kushirikiana na viongozi wa ZFA na wizara ya habari utamaduni na michezo waliokuwepo wakati ule, tulifika hadi France ( Ufaransa) na FIFA wakawa ‘very intresting’ (wakavutiwa) kutaka kujua habari za Zanzibar na ZFA matokeo yake ndio  hadi CAF (shirikisho la vyama vya mpira wa miguu Africa) ikatakiwa na FIFA watupatie uanachama kama wanachama washiriki, sasa naona hili kama sio kubwa sana ni kuendeleza tuu”, aliongeza Raza.

Aidha aliwataka wapiga kura na wanachama wa ZFA kuweka mbele maslahi ya mpira wa Zanzibar kuliko maslahi binafsi na kuondoa tafauti zao kwa kuchagua kiongozi atakayewaunganisha na kupeleka mbele maslahi ya mpira wa miguu wa Zanzibar jambo ambalo amedai kuwa litaongeza kuaminika kwa chama hicho kwa wafadhili na wadhamini.

 Uchaguzi wa ZFA unafanyika kufuatia kujiuzulu kwa aliyekuwa rais wake amani Ibrahim Makungu kujiuzulu mapema mwaka huu kwa lkile kinachodaiwa kutopewa  ushirikiano na viongozi wakuu wa ZFA wa kisiwa cha Pemba alipokuwa katika ziara ya kichama kisiwani humo na utarajiwa kufanyika Juni 8 mwaka huu.
 

Tuesday, May 21, 2013

SAA 24 NA MLEMAVU WA MACHO UDSM


Miongoni mwa mambo yanayopigwa vita na kupigiwa kelele na wanaharakati mbali mbali ni ubaguzi. Kimsingi watu wanazingatia zaidi ubaguzi wa kijinsia na kusahau kuhusu aina nyengine zikiwemo zile zinazowakabili watu wenye mahitaji maalum.
Katika makala haya mwandishi Ado Shaibu anajaribu kuonesha ni jinsi gani mifumu na hata jamii inavyowabagua watu wenye ulemavu wa macho lakini pia changamoto wanazokabiliana nazo pale wanapohitaji kupata huduma muhuimu za kijamii ikiwemo elimu.
Kwa kuwa makala hii imesheheni ushuhuda na uhalisia wa mambo yalivyo katika jamii naiweka mbele yenu ili watu wengi zaidi wapate kunufaika.

Na. Ado Shaibu, Dar es salam
Binafsi sipingi kuanzishwa kwa mfumo shirikishi. Kwa mtazamo wangu, mfumo shirikishi una faida anuai.
Mosi, unawaandaa wanafunzi walemavu kuchanganyika na jamii ambayo kimsingi ndiyo wataishi nayo uraiani. Pili, unawapa fursa wanafunzi wasio walemavu kufahamu changamoto, fursa na mahitaji ya walemavu. Pia mfumo shirikishi unasemwa kuongeza fursa kwa walemavu wengi zaidi kupata elimu kwa sababu una gharama nafuu. Hili la mwisho linahitaji utafiti zaidi.

Jambo la msingi ambalo tunapaswa kujiuliza ni kama wanafunzi wasio na ulemavu na jamuiya za taasisi za elimu kama vile shule na vyuo zimejiandaa kikamilifu kuishi kwa upendo na walemavu na kufahamu vyema mahitaji yao. Nasema hivyo kwa sababu elimu shirikishi haiwezi kufanikiwa kwa kiwango kinachotarajiwa kama jamii itakuwa haijaandaliwa vizuri kisaikolojia kuwapokea, kuwajali na kuwapenda walemavu.
Leo tutazame jinsi mfumo shirikishi unavyofanya kazi kwa mfano halisi; mfano wa maisha yangu. Mwaka 2011 ulikuwa mwaka wa mafanikio makubwa kwangu kwenye siasa za chuo kikuu. Kwanza nilichaguliwa kuwa Katibu wa kitivo cha sheria na baadaye katibu wa bodi ya serikali ya wanafunzi(DARUSO). Kiongozi wa nafasi hiyo, ana fursa kubwa ya kupata sehemu nzuri ya malazi kwenye hosteli za chuo.
Mimi niliamua kuishi chumba kimoja na mlemavu wa macho Vicent Mzena ambaye naye alikuwa waziri wa Jinsia na makundi maalum katika serikali ya wanafunzi (DARUSO).
Kuipokea changamoto ya kuishi chumba kimoja na mlemavu wa macho kumenipa ‘’uamsho’’ mkubwa. Mzena amekuwa mwalimu wangu mkubwa kuhusu mambo ya walemavu.
Somo la kwanza: Hapa tunajifunza kwamba jamii inapaswa kuchukulia kwamba kuishi na walemavu sio tatizo bali ni changamoto inayozalisha fursa ya kujifunza zaidi kutoka kwa walemavu na kuonyesha upendo kwao.
Ni asububuhi kumeshapambazuka. Mzena anaamka mapema. Chumba kimepangiliwa vyema na anafahamu ulipo mswaki, dawa ya meno na maji. Anakwenda mwenyewe bafuni kusafisha mwili. Mimi naamka na kumsaidia kunyoosha nguo zake alizozifua jana. Mzena ana desturi ya kufua nguo mwenyewe na kufuliwa mara chache hasa anapotingwa na majukumu.
Somo la pili: Hapa tunajifunza kwamba katika mfumo shirikishi, kila mmoja ana jukumu la kutekeleza. Walemavu wanapaswa kujizoesha kufanya wenyewe kazi ndogondogo wanazozimudu. Pia wanajamii wanaowazunguka walemavu wanajukumu la kuwasaidia kufanya kazi wasizoweza kuzitekeleza wenyewe.
Namshika mkono Mzena kumpeleka darasani ambaye mkononi ana fimbo nyeupe na begi la vifaa vya shule. Madarasa yako mbali kiasi. Mzena ni mcheshi sana. Tunacheka njia nzima huku akinitania kuwa mimi ni ‘’dereva mahiri’’. UDSM kuna jiografia ya milima lakini Mzena anajitahidi kuyazoea mazingira japo hapa na pale anatatizwa na ngazi.
Somo la nne: Hapa tunajifunza kwamba shule za mchanganyiko wa walemavu na watu wengine ziwe na miundombinu na mazingira rafiki kwa walemavu. Lakini pia walemavu wana jukumu la kuikabili changamoto ya mazingira yao kadiri inavyowezekana.

Kwenye varanda za hosteli na njiani kuelekea darasani tunakutana na wanafunzi wenzetu. Wanaonyesha kutujali na kutupisha njiani upesi. Lakini hapa kuna jambo la kuongeza. Wengi wanaonyesha kutunduwaa kwa mshangao. Baadhi yao wanasimamisha mazungumzo yao. Kwa ufupi,licha ya kuonyesha upendo na kujali, kuna kila dalili kwamba bado hawajaizoea kiukamilifu hali ya kujichanganya na walemavu.
Somo la tano: Hapa tunajifunza umuhimu wa kuijenga jamii kisaikolojia ili iweze kuwapokea walemavu kama sehemu ya jamii. Sasa ni wakati wa kula. Mimi na mzena tunajongea kafeteria kupata staftahi. Kuna msururu mrefu wa wanafunzi. Awali, walemavu walipaswa kupanga foleni kama watu wengine. Baada ya jitihada za viongozi wa walemavu, sasa walemavu wanahudumiwa vizuri na wahudumu wa cafeteria.
Somo la sita: kwenye foleni na misururu inayochosha kama vile benki, migahawani, kwenye vyombo vya usafiri na hospitali, walemavu wapewe kipaumbele.

Ni usiku na giza linachukua sehemu yake. Mimi, Mzena na marafiki wengine tuko chumbani tukibadilishana mawazo. Ghafla anaingia Maingu Nyanjila, mwanamke aliyejitolea vya kutosha kwa ajili ya walemavu. Amekuja kumchukua Mzena akamsomee kitabu cha fasihi, ‘’Autobiography of Malcom X’’.
Ni kitabu kikubwa lakini Mzena hana namna isipokuwa kumsikiliza Maingu akimsomea kurasa moja hadi nyingine. Hakuna vitabu katika maandishi maalumu ya nukta nundu (Braille).
Vingekuwepo Mzena asingehitaji mtu wa kumsomea. Baadhi ya walimu wa chuo wanawapa walemavu notisi zao ambazo Mzena anazisoma kwa vifaa vya kielektroniki vya kutunzia kumbukumbu au kompyuta yenye programu ya sauti.
Darasani anapaswa kwenda na tepurekoda inayonasa mafundisho ya mwalimu. Kwa bahati mbaya, si kila kitu kinasemwa kwa sauti; baadhi ya mambo yanaandikwa ubaoni bila kuzungumzwa.

Somo la saba: Katika dunia ya leo ya kielektroniki, kuna vifaa vingi ambavyo vinaifanya elimu ya walemavu iwe rahisi na yenye tija. Jamii na wadau wote wa haki za walemavu wajitahidi kufadhili upatikanaji wa vifaa muhimu.
Kabla hawajaondoka chumbani kwenda maktaba au darasani kujisomea, ni desturi ya Maingu kuibua mjadala kuhusu mada ya kijamii. Ni vijana kutoka fani mbalimbali na kila mmoja analeta hoja yake. Mzena anatoa hoja kwa mtazamo wa kielimu na mimi naleta vifungu vya sheria.
Maingu anaingilia na kutoa hoja ya kifasihi. Mara nyingi wanajua jinsi ya kunishinda. "Nyinyi wanasheria mna maneno mengi na hamtakwenda mbinguni kwa sababu hamtendi haki" Maingu angenitania ili kuidhoofisha hoja yangu.
Somo la nane: Walemavu washiriki kwenye mijadala ya kila siku ya makundirika. Marafiki wawape walemavu nafasi ya kutoa hoja zao na kuheshimu mitizamo yao. Walemavu wana tafakuri kama walivyo watu wengine.
Kuna mengi ya kuyazungumza kuhusu elimu shirikishi. Shule ya Msingi Nanjoka na Sekondari ya Frankweston nilikuwa swahibu wa mwanafunzi mwenzangu ambaye alikuwa mlemavu wakusikia. Ndanda nilisoma na walemavu wa macho. UDSM nimekutana na walemavu wa kila namna. Lakini, darasa maridhawa nimelipata nilipokata shauri kuishi na vicent Mzena, mlemavu wa macho. Natamani walemavu wote wangekuwa na moyo kama wa Mzena. Pia, nawausia vijana wenzangu na wanajamii kwa ujumla kuishi, kujenga urafiki na kuwakaribisha walemavu.
Lakini hali ikoje kwenye jamii? Utafiti uliofanywa na kituo cha taarifa kuhusu ulemavu ( Information Centre on Disability-ICD) katika Manispaa ya Moshi, Mwanza na Morogoro kuhusu mchangamano baina ya walemavu na watu wasio na ulemavu, unaonyesha kuwa bado kuna changamoto katika kufanikisha mfumo shirikishi.
Utafiti huo unaonyesha kwamba asilimia 57 ya watu kutokuwa na utayari na kukosa hulka ya upendo kwa walemavu wakati ni asilimia 47 tu ya watu ilionyesha kuwa na moyo wa kuwajali, kuwapenda na kuwakaribisha walemavu. Shime wanajamii tuibadili hali hii na kuishi kwa upendo na walemavu.
Inawezekana. Fanya tafakuri ya kina kisha chukua hatua.
Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa namba ya simu 0653619906. Barua pepe adoado75@hotmail.com

Thursday, May 9, 2013

VIFAA TASWA-ZANZIBAR



TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Kampuni ya Ocean Group of  Hotel ( OGH) ya Zanzibar ambayo inayomiliki  hoteli za kitalii za PEMBA MISALI SUNSET BEACH HOTEL,  AMANI BANGALOWS na ZANZIBAR OCEAN VIEW HOTEL, Ijumaa 10/05/2013  saa 7.00 mchana inatarajiwa kukabidhi vifaa vya michezo kwa timu ya mpira wa miguu ya CHAMA cha WAANDISHI wa HABARI za MICHEZO wa TANZANIA ZANZIBAR, TASWA-ZANZIBAR.

Makabidhiano hayo yanayotarajiwa kufanyika katika ukumbi wa mikutano wa hoteli ya Zanzibar Ocean View utaenda sambamba na kutiliana saini mkataba wa udhamini wa timu hiyo kati ya TASWA-ZANZIBAR na kampuni ya OGH ambao umelenga katika kuimarisha malengo ya chama hicho ya kuleta maendeleo ya michezo nchini.

Itakumbukwa kuwa toka kuzinduliwa kwa timu hiyo mwanzoni mwa mwezi Januari mwaka huu, imekuwa ni kiungo muhimu kati ya wanachama wa chama hicho na wadau wengine wa michezo wa ndani na nje ya Zanzibar.

Msaada na udhamini huo bila shaka utaongeza kasi ya wanachama katika kustawisha michezo nchini kupitia mpango wa chama hicho wa kufanya ziara maeneo mbali mbali kuhamasisha vijana kushiriki katika michezo.

Mkakati huo unaotambulika kama ‘OPERAESHENI SAKA VIPAJI’ ulioanza mwezi April mwaka huu kwa ziara ya kimichezo katika Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Unguja ambapo timu hiyo ilicheza na mabingwa wa ligi daraja la vijana “central league”, itaendelea na ziara hiyo katika Wilaya ya Kaskazini ‘A’ siku ya Jumamosi wakati TASWA-ZANZIBAR  F. C itakapoumana na makamo bingwa wa ligi daraja la vijana wilayani humo timu ya DOGODOGO STARS.

Mchezo huo unatarajiwa kufanyika katika kiwanja cha skuli ya Mkwajuni ambapo mbali na mchezo huo waandishi hao watapata nafasi ya kutembelea ofisi za chama cha mpira wa miguu Wilaya ya Kaskazini ‘A’ na kupata nafasi ya kubadilishana mawazo na uzoefu na uongozi wa chama hicho.

TASWA-ZANZIBAR inaamini kuwa udhamini huu na ziara hizi zitasaidia kuibua vipaji vipya ili mamlaka husika na wadau wengine waweze kuviendeleza na bila shaka wadau wote hawatasita kutoa ushirikiano na misaada yao kila itakapohitjika.

Aidha TASWA-ZANZIBAR inaamini kuwa kwa pamoja tunaweza kusaidia maendeleo ya jamii yetu kupitia michezo kwani michezo mbali ya kuwa ni burudani, katika siku za karibuni imekuwa ni ajira ambalo soko lake ni pana linaloweza kuajiri watu wengi kwa wakati mmoja na kupunguza tatizo la ajira nchini. Basi tushirikiane, ‘kwa pamoja kidogo kidogo tutafika’.
Imetolewa na;       MWINYIMVUA A. NZUKWI
          Mwenyekiti, TASWA-ZANZIBAR
09/05/2013 – ZANZIBAR.