Tuesday, June 11, 2013

KUKATIKA UMEME SASA BASI

DK SHEIN AZINDUA MRADI WA UIMARISHAJI WA MIUNDOMBINU YA UMEME
 
Na: Mwinyimvua Nzukwi, Zanzibar
Shirika la umeme Zanzibar (ZECO) limetakiwa kuwajengea uwezo wafanyakazi wake ili kufanya kazi kwa kiutaalamu na kuachana na tabia ya kufanya kazi kwa mazoea.
 
Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohammed Shein alitoa wito huo katika uzinduzi wa mradi wa uimarishaji wa miundombinu ya usambazaji wa umeme uliofanyika katika kituo kikuu cha kupokelea umeme cha Mtoni, Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja.
 
Dk. Shein amesema vifaa na mfumo uliomo katika miundo mbinu iliyozinduliwa licha ya kuwa na gharama kubwa pia ni ya kisasa hivyo kuna kila haja kwa uongozi wa shirika hilo kuwawezesha kitaaluma watendaji wake ili wawe makini katika uendeshaji wa mitambo hiyo kama moja ya njia za kuutunza mradi huo.
 
"Haitokuwa busara iwapo mradi huu hautodumu kama ilivyokusudiwa, hivyo ipo haja kwa bodi na uongozi wa shirika kuwajengea mazingira mazuri watendaji watakaokuwa wanafanya kazi katika kituo hiki ili wawe makini na kujua kuwa maisha ya Wazanzibari wote yanakuwa mikononi mwao wakati wote", alisema Dk. Shein.
 
Aidha alisema kuwa uzinduzi wa mradi huo unatokana na azma ya Serikali ya Zanzibar katika kuwaletea wananchi wake maendeleo na haja ya ongezeko la mahitaji ya watumiaji wa umeme ambao wamekuwa wakiongezeka mwaka hadi mwaka na kupelekea tatizo la kuzidiwa kwa miundombinu ya awali ya umeme iliyowekwa toka mwaka 1979.
"Idadi ya watu na idadi ya watumiaji wa umeme imekuwa ikiongeza kila kukicha hivyo tusingeliweza kubakia na miundombinu ile ile ambayo ilichakaa na kutoendana na kasi ya maendeleo ya nchi na watu wetu", aliongeza Dk. Shein na kulishukuru Shirika la Maendeleo la Japan (JAICA) kwa kuchangia kukamilika kwa utekelezaji wa mradi huo ambao unatarajiwa kuondosha tatizo la kukatikatika na kupungua nguvu kwa umeme katika kisiwa cha Unguja ambapo katika kipindi cha mwezi mmoja limepungua kwa asilimia 77.3.
Sambamba na hayo Rais Shein alisema serikali yake itaendelea na jitihada za kutafuta vyanzo mbadala vya umeme ili kuweza kupatikana kwa umeme wa uhakika jambo ambalo litaongeza idadi ya wawekezaji kutoka ndani na nje.
 
"Tumefikia hatua nzuri , UNDP (Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa) wametusaidia kuweka mshauri elekezi na katika muda si mrefu tutaamua ni njia ipi tutumie kati ya mawimbi ya bahari na upepo katika kuzalisha umeme mbadala ili ikitokea matatizo kusiwe na matatizo kama ilivyopata kutokea siku za nyuma", aliongeza Dk. Shein ambaye alisema hali hiyo itasaidia kupunguza gharama za uendeshaji wa uzalishaji wa umeme kwa majenereta ya dharura.
 
Mapema akitoa maelezo ya kitaalamu kuhusu mradi huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi Maji, Makaazi na Nishati Al-halil Mirdha alisema mradi huo umekusudia kuimarisha upatikanaji wa huduma za nishati ya umeme kwa kuhusisha ujenzi wa vituo vinne vya kupokelea na kusambazia umeme, ujenzi wa njia za kusafirishia umeme na upatikanaji wa vifaa vya kufanyia kazi.
 
Alisema kuwa jumla ya shilingi Bilioni 57, 342 zimetumika ambapo serikali ya Japani imechangia shilingi Bilioni 55 na serikali ya Zanzibar imechangia kiasi cha shilingi Bilioni 2 laki 342 ambazo zimetumika kwa ununuzi, usafirishaji, ufungaji wa vifaa vya mradi, kumgharamia Mshauri muelekezi na mafunzo ya watendaji wa shirika wakati wa utekelezaji wa mradi.
 
"Makubaliano ya utekelezaji ya mradi huu yaliitaka serikali kugharamia mpango wa kuwahamisha waathirika wa utekelezaji wa mradi, kusamehe kodi ya vufaa vilivyoletwa na upatikanaji wa maeneo ya ujenzi wa vituo na njia za umeme", alisema Katibu Mirdha.
 
Naye Balozi wa Japani nchini Tanzania Masaki Okada alisema serikali ya japani imeamua kufadhili mradi huo kutokana na uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na nchi yake na haja ya kusukuma maendeleo ya watu wa nchi hii.
 
"Japani imesukumwa na hamu ya kutaka kujiendeleleza ya wananchi wa Tanzania na ndio maana tukafadhili mradi huu ili kutoa nafasi kwa wananchi wake waweze kuendelea na kukabiliana na changamoto za kiuchumi na kijamii", alisema Balozi Okada na kuongeza kuwa ni matumaini ya nchi yake kuwa mradi huo utasaidia kupunguza kasi ya umaskini na ongezeko la gesi joto ambalo ni sehemu ya matokeo ya mabadiliko ya tabia nchi.
 
Utekelezaji wa mradi huo unafuatia kukamilika kwa mradi mwengine wa utandazaji wa waya mpya wa umeme wa chini ya bahari kutoka Ras Kiromoni Tanzania Bara hadi Fumba na ujenzi wa kituo cha kupokelea umeme cha Mtoni mwanzoni mwa mwaka huu mradi ambao ulifadhiliwa na mfuko wa changamoto za milenia (MCC).
MWISHO.

No comments:

Post a Comment