Na: Mwinyimvua Nzukwi, Zanzibar
· ZECO KUPOKEA MRADI WA WAJAPANI WIKI IJAYO
· NI WA NJIA NA MFUMO MIPYA YA UMEME
· KUTARAJIWA KUMALIZA KABISA TATIZO LA UMEME VISIWANI
Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) linataraji kuzindua Mradi mpya wa Usambazaji umeme kwa lengo la kuimarisha Miundombinu ya huduma hiyo na kumaliza tatizo la upatikanaji wa Umeme katika kisiwa cha Unguja.
Mradi huo uliogharimu kiasi cha shilingi bilioni 55 ni msaada kutoka nchi ya Japan unatarajiwa kuzinduliwa Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein katika kituo cha Mtoni Unguja Juni 11 mwaka huu.
Akitoa taarifa kwa Waandishi wa habari ofisini kwake, Meneja wa shirika hilo Hassan Ali Mbarouk amesema Mradi huo ulioanza mwaka 2011 tayari umeshakamilika na kwa sasa wanachosubiri ni uzinduzi unaotarajiwa kufanywa na Rais ahitimishe sherehe hiyo.
Amefahamisha kuwa katika utekelezaji wake Mradi huo ulijumuisha ujenzi wa Vituo vitatu vya kusambazia umeme vya Mtoni, Mwanyanya na Welezo na hivyo utaiwezesha Zanzibar kuwa na umeme wa uhakika bila mgao wa aina yoyote.
Hassan ameongeza kuwa kabla ya Mradi huo mpya baadhi ya maeneo yalikuwa yanakabiliwa na mgao uliosababisha umeme kukatika zaidi ya mara 10 kwa siku lakini tatizo hilo kwa sasa limeondoka kupitia mradi huo.
“Kulikuwa na maeneo ambayo kwa siku umeme ulikuwa unakatika mara 10 au zaidi lakini baada ya kuanza kazi mradi huu tunashukuru hakuna tena mgao katika maeneo hayo” alibainisha Meneja wa ZECO.
Aidha amewataka Wananchi ambao wanasumbuliwa na matatizo ikiwemo umeme mdogo na kukatika katika umeme katika maeneo yao kutoa taarifa kwa Shirika la Umeme ili kupatiwa ufumbuzi.
Akielezea changamoto zinazolikabili Shirika Meneja Hassan alisema kuwa ni pamoja na uchakavu wa nyaya za kusambazia umeme, kuzidiwa kwa Transfoma kutokana na ongezeko la makaazi na baadhi ya Wananchi kukosa kulipia huduma hiyo.
Hata hivyo alieleza kuwa tayari wameagiza Waya za kutosha, Transfoma na Nguzo kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya upatikanaji wa Umeme wa uhakika katika kila eneo
“Wanachi wasisubiri umeme ukatwe ndio wakalipe, wawe na utamaduni wa kulipa kabla ya muda wa kukatiwa kufika na ikitokezea kuna tatizo basi wawasiliane na ZECO sisi tunafanya kila njia kuwapatia huduma kwa ufanisi” Alisema Meneja.
Kuhusu utaratibu wa Wananchi kulipia huduma ya umeme kwa njia ya Simu Meneja alisema kuwa wamejadiliana na Kampuni ya Zantel ili kufanikisha utaratibu huo lakini bado kuna kasoro hivyo Wananchi waendelee kuwa na subra.
Amesema wanaendelea kushirikiana kwa karibu na Zanztel kuhakikisha kuwa huduma hiyo inafanya kazi kwa ufanisi bila matatizo yoyote ili kurahisisha utaratibu wa kulipia umeme kwa Wakaazi wa Zanzibar.
Uzinduzi wa Mradi huo mpya wa umeme uliofadhiliwa na Japan utakaofanyika Jumanne hapo Mtoni Unguja unatarajiwa kuwa suluhisho la tatizo la umeme kwa Kisiwa cha Unguja.
Kwa miezi kadhaa sasa toka kuzinduliwa mradi wa Njia ya Pili ya Umeme wenye Kilowat 100, kutoka Ubungo Dar es Salaam hadi Mtoni Zanzibar, uliofadhiliwa na Shirika la Misaada la MCC la Marekani,Mgao wa umeme haujatokea ambapo uzinduzi huo mpya utalifanya tatizo la mgao wa umeme kuwa la kihistoria Zanzibar.
No comments:
Post a Comment