Na. Mwinyimvua Nzukwi, Zanzibar
· RAVIA RAIS MPYA ZFA
· APATA ASILIMIA 69.8
· AWA RAISI WA TATU KATIKA MUHULA MMOJA.
Kitendawili cha nani angelimrithi Amani Ibrahim Makungu baada ya kujiuzulu urais wa chama cha soka Zanzibar ZFA kimepata jibu baada ya mjumbe wa kamati tendaji ya chama hicho kutoka Wilaya ya Kusini Ravia Idarous Faina kuchaguliwa kushika wadhifa huo.
Mkutano huo wa uchaguzi uliofanyika katika ukumbi wa VIP wa uwanja wa Amaan ulimchagua Idarous kwa kura 37 sawa na asilimia 69.8 dhidi ya kura 16 sawa na asilimia 30.2 asilimia za Abdall Juma Mohammed ambaye pia ni mjumbe wa kamati tendaji na Mwanasheria wa chama hicho.
Mgombea mwengine Rajab Ali Rajab hakupata kura hata moja kati ya kura 53 zilizopigwa na hakuna kura iliyoharibika.
Akitoa maelezo mbele ya wajumbe wa mkutano huo kabla na baada ya kuchaguliwa alisistiza kuendelea kusimamia katiba ya chama hicho na kudumisha maelewano miongoni mwa wajumbe wa kamati tendaji na wadau wengine wa soka hapa nchini.
“Naelewa kila kitu kinacholikwamisha soka letu na nazijua shida mlizonazo hivyo naomba mniamini kuwa nitasimamia kanuni na katiba katika kuziondoa na kwamba mjue wajumbe sote tutakuwa na hadhi sawa na hakuna alie juu ya mwengine kikubwa ni maelewano tu”, alisema Idarous.
Aliongeza kuwa atajitahidi kuhakikisha anasimamia kuwepo kwa maendeleo ya kweli ya soka la Zanzibar huku akiwaomba wajumbe hao na wadau wa soka kufanya kazi kwa bidii katika ngazi zote ili kuhakikisha maendeleo ya kweli na haraka yanapatikana.
Akizungumzia uchaguzi huo Rajabu alisema licha ya kukosa kura anakubaliana matokeo hayo na kwamba amefarajika sana na jinsi uchaguzi huo ulivyoendeshwa na kamati ya uchaguzi ambayo alisema ilitenda haki na kwamba atakuwa tayari kumuunga mkono rais aliechaguliwa.
“Pamoja na kuwa sikupata kura, hayo ni maamuzi ya wajumbe wa mkutano mkuu lakini kwa ujumla nimeridhika na mchakato ulivyoendeshwa na nakubaliana na matokeo”, alisema Rajabu ambaye ni mwanafunzi wa chuo kikuu cha Zanzibar, Zanzibar University.
Nae Abdalla Juma alimpongeza Ravia na kuahidi kumpa kila ya aina ya ushirikiano na kuwataka wajumbe mengine na wadau kumsaidia ili aweze kutimiza wajibu wake kikamilifu.
“Kimsingi sina pingamizi na matokeo haya zaidi ya kuwashukuru wajumbe kwa kutumia haki yao ya kidemokrasia na ningependa tumsaidie ili aweze kutekeleza majukumu yake.
Mapema mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi ya ZFA Gullam Rashid Abdalla aliwataka wajumbe wa mkutano mkuu kufanya maamuzi bila ya kushawishiwa wala kushinikizwa na kutambua wajibu wao kwa jamii ya wazanzibari ambao wamechoshwa na malumbano katika chama hicho.
“Wajumbe mna wajibu wa kuzingatia matakwa ya wadau wa mchezo wa soka na sio utashi wenu na vyema mkazingatia taratibu za uchaguzi ili kukamilisha mchakato huu”, alisema Mwenyekiti huyo.
Ravia anakuwa Rais wa tatu katika muhula mmoja ulioanzia Oktoba 2010 na kumalizika Disemba 2014, akitanguliwa na Ali Fereji Tamim aliyejiuzulu mnamo mwezi Machi mwaka 2012 na Amani Ibrahim Makungu ambae alijiuzulu mwishoni mwa mwezi Januari mwaka huu kila mmoja akitoa sababu tofauti.
No comments:
Post a Comment