TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Kampuni ya Ocean Group of Hotel ( OGH) ya Zanzibar ambayo inayomiliki hoteli za kitalii za PEMBA MISALI SUNSET BEACH
HOTEL, AMANI BANGALOWS na ZANZIBAR OCEAN
VIEW HOTEL, Ijumaa 10/05/2013 saa
7.00 mchana inatarajiwa kukabidhi vifaa vya michezo kwa timu ya mpira wa miguu
ya CHAMA cha WAANDISHI wa HABARI za MICHEZO wa TANZANIA ZANZIBAR, TASWA-ZANZIBAR.
Makabidhiano hayo yanayotarajiwa kufanyika katika
ukumbi wa mikutano wa hoteli ya Zanzibar Ocean View utaenda sambamba na
kutiliana saini mkataba wa udhamini wa timu hiyo kati ya TASWA-ZANZIBAR na
kampuni ya OGH ambao umelenga katika kuimarisha malengo ya chama hicho ya
kuleta maendeleo ya michezo nchini.
Itakumbukwa kuwa toka kuzinduliwa kwa timu hiyo
mwanzoni mwa mwezi Januari mwaka huu, imekuwa ni kiungo muhimu kati ya
wanachama wa chama hicho na wadau wengine wa michezo wa ndani na nje ya Zanzibar.
Msaada na udhamini huo bila shaka utaongeza kasi ya
wanachama katika kustawisha michezo nchini kupitia mpango wa chama hicho wa kufanya
ziara maeneo mbali mbali kuhamasisha vijana kushiriki katika michezo.
Mkakati huo unaotambulika kama ‘OPERAESHENI SAKA VIPAJI’
ulioanza mwezi April mwaka huu kwa ziara ya kimichezo katika Wilaya ya Kaskazini
‘B’ Unguja ambapo timu hiyo ilicheza na mabingwa wa ligi daraja la vijana “central
league”, itaendelea na ziara hiyo katika Wilaya ya Kaskazini ‘A’ siku ya Jumamosi
wakati TASWA-ZANZIBAR F. C itakapoumana
na makamo bingwa wa ligi daraja la vijana wilayani humo timu ya DOGODOGO STARS.
Mchezo huo unatarajiwa kufanyika katika kiwanja cha
skuli ya Mkwajuni ambapo mbali na mchezo huo waandishi hao watapata nafasi ya
kutembelea ofisi za chama cha mpira wa miguu Wilaya ya Kaskazini ‘A’ na kupata
nafasi ya kubadilishana mawazo na uzoefu na uongozi wa chama hicho.
TASWA-ZANZIBAR inaamini kuwa udhamini huu na ziara
hizi zitasaidia kuibua vipaji vipya ili mamlaka husika na wadau wengine waweze
kuviendeleza na bila shaka wadau wote hawatasita kutoa ushirikiano na misaada
yao kila itakapohitjika.
Aidha TASWA-ZANZIBAR inaamini kuwa kwa pamoja
tunaweza kusaidia maendeleo ya jamii yetu kupitia michezo kwani michezo mbali
ya kuwa ni burudani, katika siku za karibuni imekuwa ni ajira ambalo soko lake ni
pana linaloweza kuajiri watu wengi kwa wakati mmoja na kupunguza tatizo la
ajira nchini. Basi tushirikiane, ‘kwa pamoja kidogo kidogo tutafika’.
Imetolewa na;
MWINYIMVUA A. NZUKWI
Mwenyekiti,
TASWA-ZANZIBAR
09/05/2013
– ZANZIBAR.
No comments:
Post a Comment