Na: Mwinyimvua
Nzukwi, Zanzibar
Makamu wa Pili
wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema maendeleo ya haraka kwa mataifa
machanga yatapatikana iwapo suala la matumizi ya mtandao wa kisasa wa mawasiliano
ya habari na mawasiliano yatapewa msukumo unaostahiki.
Alisema mfumo
huo unaweza kuunganisha na kurahisisha utekelezeji wa majukumu ya taasisi pia unaweza
kutoa ajira zaidi maeneo katika maeneo ya vijijini ambayo huduma za mawasiliano hazijafika au ziko katika kiwango
hafifu.
Balozi Seif alisema
hayo alipokuwa akiifungua warsha kuhusu
mawasiliano vijijini iliyoandaliwa na mfuko wa mawasiliano kwa wote wenye makao
makuu yake Nchini Uholanzi inayofanyika katika ukumbi wa hoteli ya Melia
iliyopo Pwani Mchangani Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Alizitaja sekta
za kilimo, biashara na elimu kuwa ni miongoni mwa sekta za zinazopaswa kupewa
kipau mbela na kuendelezwa kwa kutumia
mfumo huo ili kuleta tija inayostahiki
Balozi Seif
alifahamisha kuwa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Mapinduzi ya
Zanzibar zimeanza kuchukua hatua za kufuata mfumo huu ili kutengeneza mazingira
bora yatakayowezesha kukuza uchumi wa taifa
Alielezea kuwa kutokana
na warsha hiyo kufanyika nchini Tanzania ni vyema washiriki wakatumia fursa
hiyo kikamilifu ambayo alidai itasaidia
kuunganisha nguvu za pamoja katika kukabiliana na changamoto zilizomo kwenye mfumo
huo.
“ Tumeshuhudia
Mataifa kama vile Chile, Uturuki na Malaysia yalivyopiga hatua kubwa na ya
haraka katika kuimarisha uchumi wao baada ya kuamua kutumia mfumo huo wa
mawasiliano “. Alisema Balozi Seif.
Aliwataka
washiriki wa warsha hiyo kufikiria njia zitakazowezesha kuongezeka kwa
watumiaji wa teknolojia ya kisasa na kuwafikia wananachi walio wengi hasa wale
walioko vijijini mara watakaporejea katika Mataifa yao.
Aliongeza kuwa licha
ya Zanzibar kutajwa kuwa imepiga hatua katika matumizi ya teknolojia ya habari
na mawasiliano (TEHAMA), bado Serikali
inaendelea na mikakati ya kusimamia upatikanaji wa huduma hizo ziwafikie
wananchi wote mijini na vijijini.
Mapema akimkaribisha
balozi iddi, Katibu mkuu wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia wa
Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Florens Martin Turuka alisema
lengo la warsha hiyo ni kujenga nguvu zitakazosaidia kufikisha mawasiliano
sehemu zisizo na huduma hizo.
Dr. Turuka aliongeza
kuwa mfumo huu mpya ambao unaanza kuelekezwa katika mataifa machanga unakusudia
kuanzisha mpango maalum wa mafunzo maskulini kwa kutumia mtandao wa mawasiliano
ya moja kwa moja kati ya sehemu moja hadi nyengine.
Alisema hatua
hiyo itakwenda sambamba na utolewaji wa huduma za mawasiliano ambazo
zitawahusisha baadhi ya wasimamizi waliojiandaa kutoa huduma hizo kwa kupatiwa
ruzuku katika maeneo ya vijijini.
“ Tumefarajika
kuona wataalamu wa mfuko wa mawasiliano kwa wote wameamua kuifanya warsha hii
hapa Zanzibar, hii ni kufuatia visiwa hivi
kupiga hatua ya maendeleo katika matumizi ya mawasiliano ya simu za mkononi “ .
Alisisitiza Dr. Turuka.
Warsha hiyo ya
siku tano ni ya sita ambayo inashirikisha Mataifa 12 ya Bara la Afrika wakiwemo
wawakilishi wa mataifa ya India, Malaysia na Marekani nchi zinazotajwa kupiga hatua kubwa katika uvumbuzi
na matumizi ya teknolojia ya mawasiliano imedhaminiwa na wa Mfuko wa
mawasiliano kwa wote wa Uholanzi.
No comments:
Post a Comment