·
SMZ
YAFUNGUA MILANGO KWA KAMPUNI YA KIOMANI
·
YENEWE
YAAHIDI KUWEKEZA KUKUZA UCHUMI WA NCHI NA WATU WAKE
Na. Mwinyimvua Nzukwi, Zanzibar
Kampuni ya Kimataifa ya Shanfar & Partners Co. L.L.C yenye Makao makuu
yake Mjini Salala, Nchini Oman imeonyesha nia ya kutaka kuwekeza vitega uchumi
vyake hapa Zanzibar.
Nia hiyo imekuja kufuatia Visiwa vya Zanzibar kubarikiwa kuwa na
rasilmali kadhaa ambazo bado hazijatumika katika kusaidia kuendeleza uchumi wa
Taifa sambamba na kuongeza vipato kwa wananchi.
Mwakilishi wa Kampuni hiyo Ali Omar Al–Sheikh akiuongoza ujumbe wa
Viongozi watano wa Kampuni hiyo alieleza hayo wakati akizungumza na Makamu wa pili
wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi katika ofisi za Makamo huyo Vuga,
Mjini Zanzibar.
Omar amesema ujumbe wake
umeridhika na rasilmali kadhaa zilizomo ndani ya Visiwa vya Zanzibar baada ya
kupata fursa ya kutembelea maeneo mbali mbali mijini na vijijini katika ziara
hioyo.
Alifahamisha kwamba taasisi yake inaangalia maeneo inayoweza kuwekeza
baada ya kufanya uchambuzi wa kina wakilenga zaidi katika sekta ya utalii ambayo
tayari imefikia hatua kubwa baada ya serikali kujitahidi kuimarisha miundo
mbinu inayochochea ukuaji wa haraka wa sekta hiyo.
“ Zanzibar tayari imeshafanikiwa vyema katika uwekezaji wa Hoteli za daraja
linalokubalika Kimataifa, kinachohitajika kwa wakati huu ni namna gani wanaweza
kushajiisha makampuni ya kitalii kuweza kuitumia zaidi fursa hiyo” alifafanua Omar.
Aliongeza kuwa “ Tumeliangalia hata zao la karafuu linalotegemewa kwa
Uchumi wa Zanzibar ambalo pia linaweza kuimarishwa mauzo yake katika soko la
Kimataifa kwa kutumiwa zaidi utaalamu wa kisasa” na kusisitiza kuwa kampuni
yake yenye makao makuu yake nchini Oman na matawi katika nchi kadhaa duniani.
Naye Ofisa Mkuu wa Kampuni hiyo S.
Srihar alimueleza Balozi Seif kuwa katika
jitihada za kusaidia maendeleo ya Zanzibar Kampuni yao ina uwezo wa
kuyashawishi mashirika na Makampuni ya Kimataifa ya watembezaji Watalii
kulitumia soko la utalii la Zanzibar katika kutembeza wateja na wageni wao.
Srihar alisema kufanikiwa kwa
mpango huo kunaweza kutoa nafasi ya ajira kwa wazalendo waliowengi nchini hasa
vijana wanaomaliza masomo yao.
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali
Iddi aliueleza ujumbe huo kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar bado
inaendelea na juhudi za kuimarisha miundo mbinu katika sekta mbali mbali za kiuchumi
hapa nchini ili kuinua uchumi wan chi na watu wake.
Balozi Seif alisema kuwa uimarishaji wa kiwanja cha ndege cha kimataifa cha
Zanzibar ni miongoni mwa hatua hizo zilizolenga kujenga mazingira mazuri ya
uwekezaji.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliushauri Ujumbe huo kuitumia fursa
hiyo ili kusaidia uchumi wa Zanzibar sambamba na kuimarisha uhusiano wa
Kihistoria uliopo kati ya Zanzibar na Oman.
Kampuni ya Kimataifa ya Kibiashara ya Shanfar & Patners Co. L.L.C ya
Salala Nchini Oman imekuwa na ubia wa kibiashara na zaidi ya Makampuni saba ya kimataifa
katika nyanja za viwanda, usafiri wa anga, utalii, huduma za Umeme, ujenzi na uchapishaji
duniani kote.
No comments:
Post a Comment