Tuesday, May 21, 2013

SAA 24 NA MLEMAVU WA MACHO UDSM


Miongoni mwa mambo yanayopigwa vita na kupigiwa kelele na wanaharakati mbali mbali ni ubaguzi. Kimsingi watu wanazingatia zaidi ubaguzi wa kijinsia na kusahau kuhusu aina nyengine zikiwemo zile zinazowakabili watu wenye mahitaji maalum.
Katika makala haya mwandishi Ado Shaibu anajaribu kuonesha ni jinsi gani mifumu na hata jamii inavyowabagua watu wenye ulemavu wa macho lakini pia changamoto wanazokabiliana nazo pale wanapohitaji kupata huduma muhuimu za kijamii ikiwemo elimu.
Kwa kuwa makala hii imesheheni ushuhuda na uhalisia wa mambo yalivyo katika jamii naiweka mbele yenu ili watu wengi zaidi wapate kunufaika.

Na. Ado Shaibu, Dar es salam
Binafsi sipingi kuanzishwa kwa mfumo shirikishi. Kwa mtazamo wangu, mfumo shirikishi una faida anuai.
Mosi, unawaandaa wanafunzi walemavu kuchanganyika na jamii ambayo kimsingi ndiyo wataishi nayo uraiani. Pili, unawapa fursa wanafunzi wasio walemavu kufahamu changamoto, fursa na mahitaji ya walemavu. Pia mfumo shirikishi unasemwa kuongeza fursa kwa walemavu wengi zaidi kupata elimu kwa sababu una gharama nafuu. Hili la mwisho linahitaji utafiti zaidi.

Jambo la msingi ambalo tunapaswa kujiuliza ni kama wanafunzi wasio na ulemavu na jamuiya za taasisi za elimu kama vile shule na vyuo zimejiandaa kikamilifu kuishi kwa upendo na walemavu na kufahamu vyema mahitaji yao. Nasema hivyo kwa sababu elimu shirikishi haiwezi kufanikiwa kwa kiwango kinachotarajiwa kama jamii itakuwa haijaandaliwa vizuri kisaikolojia kuwapokea, kuwajali na kuwapenda walemavu.
Leo tutazame jinsi mfumo shirikishi unavyofanya kazi kwa mfano halisi; mfano wa maisha yangu. Mwaka 2011 ulikuwa mwaka wa mafanikio makubwa kwangu kwenye siasa za chuo kikuu. Kwanza nilichaguliwa kuwa Katibu wa kitivo cha sheria na baadaye katibu wa bodi ya serikali ya wanafunzi(DARUSO). Kiongozi wa nafasi hiyo, ana fursa kubwa ya kupata sehemu nzuri ya malazi kwenye hosteli za chuo.
Mimi niliamua kuishi chumba kimoja na mlemavu wa macho Vicent Mzena ambaye naye alikuwa waziri wa Jinsia na makundi maalum katika serikali ya wanafunzi (DARUSO).
Kuipokea changamoto ya kuishi chumba kimoja na mlemavu wa macho kumenipa ‘’uamsho’’ mkubwa. Mzena amekuwa mwalimu wangu mkubwa kuhusu mambo ya walemavu.
Somo la kwanza: Hapa tunajifunza kwamba jamii inapaswa kuchukulia kwamba kuishi na walemavu sio tatizo bali ni changamoto inayozalisha fursa ya kujifunza zaidi kutoka kwa walemavu na kuonyesha upendo kwao.
Ni asububuhi kumeshapambazuka. Mzena anaamka mapema. Chumba kimepangiliwa vyema na anafahamu ulipo mswaki, dawa ya meno na maji. Anakwenda mwenyewe bafuni kusafisha mwili. Mimi naamka na kumsaidia kunyoosha nguo zake alizozifua jana. Mzena ana desturi ya kufua nguo mwenyewe na kufuliwa mara chache hasa anapotingwa na majukumu.
Somo la pili: Hapa tunajifunza kwamba katika mfumo shirikishi, kila mmoja ana jukumu la kutekeleza. Walemavu wanapaswa kujizoesha kufanya wenyewe kazi ndogondogo wanazozimudu. Pia wanajamii wanaowazunguka walemavu wanajukumu la kuwasaidia kufanya kazi wasizoweza kuzitekeleza wenyewe.
Namshika mkono Mzena kumpeleka darasani ambaye mkononi ana fimbo nyeupe na begi la vifaa vya shule. Madarasa yako mbali kiasi. Mzena ni mcheshi sana. Tunacheka njia nzima huku akinitania kuwa mimi ni ‘’dereva mahiri’’. UDSM kuna jiografia ya milima lakini Mzena anajitahidi kuyazoea mazingira japo hapa na pale anatatizwa na ngazi.
Somo la nne: Hapa tunajifunza kwamba shule za mchanganyiko wa walemavu na watu wengine ziwe na miundombinu na mazingira rafiki kwa walemavu. Lakini pia walemavu wana jukumu la kuikabili changamoto ya mazingira yao kadiri inavyowezekana.

Kwenye varanda za hosteli na njiani kuelekea darasani tunakutana na wanafunzi wenzetu. Wanaonyesha kutujali na kutupisha njiani upesi. Lakini hapa kuna jambo la kuongeza. Wengi wanaonyesha kutunduwaa kwa mshangao. Baadhi yao wanasimamisha mazungumzo yao. Kwa ufupi,licha ya kuonyesha upendo na kujali, kuna kila dalili kwamba bado hawajaizoea kiukamilifu hali ya kujichanganya na walemavu.
Somo la tano: Hapa tunajifunza umuhimu wa kuijenga jamii kisaikolojia ili iweze kuwapokea walemavu kama sehemu ya jamii. Sasa ni wakati wa kula. Mimi na mzena tunajongea kafeteria kupata staftahi. Kuna msururu mrefu wa wanafunzi. Awali, walemavu walipaswa kupanga foleni kama watu wengine. Baada ya jitihada za viongozi wa walemavu, sasa walemavu wanahudumiwa vizuri na wahudumu wa cafeteria.
Somo la sita: kwenye foleni na misururu inayochosha kama vile benki, migahawani, kwenye vyombo vya usafiri na hospitali, walemavu wapewe kipaumbele.

Ni usiku na giza linachukua sehemu yake. Mimi, Mzena na marafiki wengine tuko chumbani tukibadilishana mawazo. Ghafla anaingia Maingu Nyanjila, mwanamke aliyejitolea vya kutosha kwa ajili ya walemavu. Amekuja kumchukua Mzena akamsomee kitabu cha fasihi, ‘’Autobiography of Malcom X’’.
Ni kitabu kikubwa lakini Mzena hana namna isipokuwa kumsikiliza Maingu akimsomea kurasa moja hadi nyingine. Hakuna vitabu katika maandishi maalumu ya nukta nundu (Braille).
Vingekuwepo Mzena asingehitaji mtu wa kumsomea. Baadhi ya walimu wa chuo wanawapa walemavu notisi zao ambazo Mzena anazisoma kwa vifaa vya kielektroniki vya kutunzia kumbukumbu au kompyuta yenye programu ya sauti.
Darasani anapaswa kwenda na tepurekoda inayonasa mafundisho ya mwalimu. Kwa bahati mbaya, si kila kitu kinasemwa kwa sauti; baadhi ya mambo yanaandikwa ubaoni bila kuzungumzwa.

Somo la saba: Katika dunia ya leo ya kielektroniki, kuna vifaa vingi ambavyo vinaifanya elimu ya walemavu iwe rahisi na yenye tija. Jamii na wadau wote wa haki za walemavu wajitahidi kufadhili upatikanaji wa vifaa muhimu.
Kabla hawajaondoka chumbani kwenda maktaba au darasani kujisomea, ni desturi ya Maingu kuibua mjadala kuhusu mada ya kijamii. Ni vijana kutoka fani mbalimbali na kila mmoja analeta hoja yake. Mzena anatoa hoja kwa mtazamo wa kielimu na mimi naleta vifungu vya sheria.
Maingu anaingilia na kutoa hoja ya kifasihi. Mara nyingi wanajua jinsi ya kunishinda. "Nyinyi wanasheria mna maneno mengi na hamtakwenda mbinguni kwa sababu hamtendi haki" Maingu angenitania ili kuidhoofisha hoja yangu.
Somo la nane: Walemavu washiriki kwenye mijadala ya kila siku ya makundirika. Marafiki wawape walemavu nafasi ya kutoa hoja zao na kuheshimu mitizamo yao. Walemavu wana tafakuri kama walivyo watu wengine.
Kuna mengi ya kuyazungumza kuhusu elimu shirikishi. Shule ya Msingi Nanjoka na Sekondari ya Frankweston nilikuwa swahibu wa mwanafunzi mwenzangu ambaye alikuwa mlemavu wakusikia. Ndanda nilisoma na walemavu wa macho. UDSM nimekutana na walemavu wa kila namna. Lakini, darasa maridhawa nimelipata nilipokata shauri kuishi na vicent Mzena, mlemavu wa macho. Natamani walemavu wote wangekuwa na moyo kama wa Mzena. Pia, nawausia vijana wenzangu na wanajamii kwa ujumla kuishi, kujenga urafiki na kuwakaribisha walemavu.
Lakini hali ikoje kwenye jamii? Utafiti uliofanywa na kituo cha taarifa kuhusu ulemavu ( Information Centre on Disability-ICD) katika Manispaa ya Moshi, Mwanza na Morogoro kuhusu mchangamano baina ya walemavu na watu wasio na ulemavu, unaonyesha kuwa bado kuna changamoto katika kufanikisha mfumo shirikishi.
Utafiti huo unaonyesha kwamba asilimia 57 ya watu kutokuwa na utayari na kukosa hulka ya upendo kwa walemavu wakati ni asilimia 47 tu ya watu ilionyesha kuwa na moyo wa kuwajali, kuwapenda na kuwakaribisha walemavu. Shime wanajamii tuibadili hali hii na kuishi kwa upendo na walemavu.
Inawezekana. Fanya tafakuri ya kina kisha chukua hatua.
Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa namba ya simu 0653619906. Barua pepe adoado75@hotmail.com

Thursday, May 9, 2013

VIFAA TASWA-ZANZIBAR



TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Kampuni ya Ocean Group of  Hotel ( OGH) ya Zanzibar ambayo inayomiliki  hoteli za kitalii za PEMBA MISALI SUNSET BEACH HOTEL,  AMANI BANGALOWS na ZANZIBAR OCEAN VIEW HOTEL, Ijumaa 10/05/2013  saa 7.00 mchana inatarajiwa kukabidhi vifaa vya michezo kwa timu ya mpira wa miguu ya CHAMA cha WAANDISHI wa HABARI za MICHEZO wa TANZANIA ZANZIBAR, TASWA-ZANZIBAR.

Makabidhiano hayo yanayotarajiwa kufanyika katika ukumbi wa mikutano wa hoteli ya Zanzibar Ocean View utaenda sambamba na kutiliana saini mkataba wa udhamini wa timu hiyo kati ya TASWA-ZANZIBAR na kampuni ya OGH ambao umelenga katika kuimarisha malengo ya chama hicho ya kuleta maendeleo ya michezo nchini.

Itakumbukwa kuwa toka kuzinduliwa kwa timu hiyo mwanzoni mwa mwezi Januari mwaka huu, imekuwa ni kiungo muhimu kati ya wanachama wa chama hicho na wadau wengine wa michezo wa ndani na nje ya Zanzibar.

Msaada na udhamini huo bila shaka utaongeza kasi ya wanachama katika kustawisha michezo nchini kupitia mpango wa chama hicho wa kufanya ziara maeneo mbali mbali kuhamasisha vijana kushiriki katika michezo.

Mkakati huo unaotambulika kama ‘OPERAESHENI SAKA VIPAJI’ ulioanza mwezi April mwaka huu kwa ziara ya kimichezo katika Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Unguja ambapo timu hiyo ilicheza na mabingwa wa ligi daraja la vijana “central league”, itaendelea na ziara hiyo katika Wilaya ya Kaskazini ‘A’ siku ya Jumamosi wakati TASWA-ZANZIBAR  F. C itakapoumana na makamo bingwa wa ligi daraja la vijana wilayani humo timu ya DOGODOGO STARS.

Mchezo huo unatarajiwa kufanyika katika kiwanja cha skuli ya Mkwajuni ambapo mbali na mchezo huo waandishi hao watapata nafasi ya kutembelea ofisi za chama cha mpira wa miguu Wilaya ya Kaskazini ‘A’ na kupata nafasi ya kubadilishana mawazo na uzoefu na uongozi wa chama hicho.

TASWA-ZANZIBAR inaamini kuwa udhamini huu na ziara hizi zitasaidia kuibua vipaji vipya ili mamlaka husika na wadau wengine waweze kuviendeleza na bila shaka wadau wote hawatasita kutoa ushirikiano na misaada yao kila itakapohitjika.

Aidha TASWA-ZANZIBAR inaamini kuwa kwa pamoja tunaweza kusaidia maendeleo ya jamii yetu kupitia michezo kwani michezo mbali ya kuwa ni burudani, katika siku za karibuni imekuwa ni ajira ambalo soko lake ni pana linaloweza kuajiri watu wengi kwa wakati mmoja na kupunguza tatizo la ajira nchini. Basi tushirikiane, ‘kwa pamoja kidogo kidogo tutafika’.
Imetolewa na;       MWINYIMVUA A. NZUKWI
          Mwenyekiti, TASWA-ZANZIBAR
09/05/2013 – ZANZIBAR.

Monday, May 6, 2013

BALOZI SEIF AKUTANA NA UJUMBE WA KAMPUNI YA SHANRAF AND PARTNERS YA OMAN


·        SMZ YAFUNGUA MILANGO KWA KAMPUNI YA KIOMANI
·        YENEWE YAAHIDI KUWEKEZA KUKUZA UCHUMI WA NCHI NA WATU WAKE
Na. Mwinyimvua Nzukwi, Zanzibar
Kampuni ya Kimataifa ya Shanfar & Partners Co. L.L.C yenye Makao makuu yake Mjini Salala, Nchini Oman imeonyesha nia ya kutaka kuwekeza vitega uchumi vyake hapa Zanzibar.

Nia hiyo imekuja kufuatia Visiwa vya Zanzibar kubarikiwa kuwa na rasilmali kadhaa ambazo bado hazijatumika katika kusaidia kuendeleza uchumi wa Taifa sambamba na kuongeza vipato kwa wananchi.

Mwakilishi wa Kampuni hiyo Ali Omar Al–Sheikh akiuongoza ujumbe wa Viongozi watano wa Kampuni hiyo alieleza hayo wakati akizungumza na Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi katika ofisi za Makamo huyo Vuga, Mjini Zanzibar.
 Omar amesema ujumbe wake umeridhika na rasilmali kadhaa zilizomo ndani ya Visiwa vya Zanzibar baada ya kupata fursa ya kutembelea maeneo mbali mbali mijini na vijijini katika ziara hioyo.
Alifahamisha kwamba taasisi yake inaangalia maeneo inayoweza kuwekeza baada ya kufanya uchambuzi wa kina wakilenga zaidi katika sekta ya utalii ambayo tayari imefikia hatua kubwa baada ya serikali kujitahidi kuimarisha miundo mbinu inayochochea ukuaji wa haraka wa sekta hiyo.

“ Zanzibar tayari imeshafanikiwa vyema katika uwekezaji wa Hoteli za daraja linalokubalika Kimataifa, kinachohitajika kwa wakati huu ni namna gani wanaweza kushajiisha makampuni ya kitalii kuweza kuitumia zaidi fursa hiyo” alifafanua Omar.

Aliongeza kuwa “ Tumeliangalia hata zao la karafuu linalotegemewa kwa Uchumi wa Zanzibar ambalo pia linaweza kuimarishwa mauzo yake katika soko la Kimataifa kwa kutumiwa zaidi utaalamu wa kisasa” na kusisitiza kuwa kampuni yake yenye makao makuu yake nchini Oman na matawi katika nchi kadhaa duniani.

Naye Ofisa Mkuu wa Kampuni hiyo  S. Srihar alimueleza Balozi Seif kuwa  katika jitihada za kusaidia maendeleo ya Zanzibar Kampuni yao ina uwezo wa kuyashawishi mashirika na Makampuni ya Kimataifa ya watembezaji Watalii kulitumia soko la utalii la Zanzibar katika kutembeza wateja na wageni wao.

 Srihar alisema kufanikiwa kwa mpango huo kunaweza kutoa nafasi ya ajira kwa wazalendo waliowengi nchini hasa vijana wanaomaliza masomo yao.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliueleza ujumbe huo kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar bado inaendelea na juhudi za kuimarisha miundo mbinu katika sekta mbali mbali za kiuchumi hapa nchini ili kuinua uchumi wan chi na watu wake.

Balozi Seif alisema kuwa uimarishaji wa kiwanja cha ndege cha kimataifa cha Zanzibar ni miongoni mwa hatua hizo zilizolenga kujenga mazingira mazuri ya uwekezaji. 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliushauri Ujumbe huo kuitumia fursa hiyo ili kusaidia uchumi wa Zanzibar sambamba na kuimarisha uhusiano wa Kihistoria uliopo kati ya Zanzibar na Oman.

Kampuni ya Kimataifa ya Kibiashara ya Shanfar & Patners Co. L.L.C ya Salala Nchini Oman imekuwa na ubia wa kibiashara na zaidi ya Makampuni saba ya kimataifa katika nyanja za viwanda, usafiri wa anga, utalii, huduma za Umeme, ujenzi na uchapishaji duniani kote.

Thursday, May 2, 2013

MAWASILILIANO VIJIJINI YAIMARISHE SEKTA MTAMBUKA


Na: Mwinyimvua Nzukwi, Zanzibar
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema maendeleo ya haraka kwa mataifa machanga yatapatikana iwapo suala la matumizi ya mtandao wa kisasa wa mawasiliano ya habari na mawasiliano yatapewa msukumo unaostahiki.
Alisema mfumo huo unaweza kuunganisha na kurahisisha utekelezeji wa majukumu ya taasisi pia unaweza kutoa ajira zaidi maeneo katika maeneo ya vijijini ambayo huduma  za mawasiliano hazijafika au ziko katika kiwango hafifu.
Balozi Seif alisema hayo alipokuwa  akiifungua warsha kuhusu mawasiliano vijijini iliyoandaliwa na mfuko wa mawasiliano kwa wote wenye makao makuu yake Nchini Uholanzi inayofanyika katika ukumbi wa hoteli ya Melia iliyopo Pwani Mchangani Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Alizitaja sekta za kilimo, biashara na elimu kuwa ni miongoni mwa sekta za zinazopaswa kupewa kipau mbela na  kuendelezwa kwa kutumia mfumo huo ili kuleta tija inayostahiki
Balozi Seif alifahamisha kuwa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Mapinduzi ya Zanzibar zimeanza kuchukua hatua za kufuata mfumo huu ili kutengeneza mazingira bora yatakayowezesha kukuza uchumi wa taifa
Alielezea kuwa kutokana na warsha hiyo kufanyika nchini Tanzania ni vyema washiriki wakatumia fursa hiyo kikamilifu ambayo alidai  itasaidia kuunganisha nguvu za pamoja katika kukabiliana na changamoto zilizomo kwenye mfumo huo.
“ Tumeshuhudia Mataifa kama vile Chile, Uturuki na Malaysia yalivyopiga hatua kubwa na ya haraka katika kuimarisha uchumi wao baada ya kuamua kutumia mfumo huo wa mawasiliano “. Alisema Balozi Seif.
Aliwataka washiriki wa warsha hiyo kufikiria njia zitakazowezesha kuongezeka kwa watumiaji wa teknolojia ya kisasa na kuwafikia wananachi walio wengi hasa wale walioko vijijini mara watakaporejea katika Mataifa yao.
Aliongeza kuwa licha ya Zanzibar kutajwa kuwa imepiga hatua katika matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA),  bado Serikali inaendelea na mikakati ya kusimamia upatikanaji wa huduma hizo ziwafikie wananchi wote mijini na vijijini.
Mapema akimkaribisha balozi iddi, Katibu mkuu wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Florens Martin Turuka alisema lengo la warsha hiyo ni kujenga nguvu zitakazosaidia kufikisha mawasiliano sehemu zisizo na huduma hizo.
Dr. Turuka aliongeza kuwa mfumo huu mpya ambao unaanza kuelekezwa katika mataifa machanga unakusudia kuanzisha mpango maalum wa mafunzo maskulini kwa kutumia mtandao wa mawasiliano ya moja kwa moja kati ya sehemu moja hadi nyengine.
Alisema hatua hiyo itakwenda sambamba na utolewaji wa huduma za mawasiliano ambazo zitawahusisha baadhi ya wasimamizi waliojiandaa kutoa huduma hizo kwa kupatiwa ruzuku katika maeneo ya vijijini.
“ Tumefarajika kuona wataalamu wa mfuko wa mawasiliano kwa wote wameamua kuifanya warsha hii hapa Zanzibar, hii ni  kufuatia visiwa hivi kupiga hatua ya maendeleo katika matumizi ya mawasiliano ya simu za mkononi “ . Alisisitiza Dr. Turuka.
Warsha hiyo ya siku tano ni ya sita ambayo inashirikisha Mataifa 12 ya Bara la Afrika wakiwemo wawakilishi wa mataifa ya India, Malaysia na Marekani  nchi zinazotajwa kupiga hatua kubwa katika uvumbuzi na matumizi ya teknolojia ya mawasiliano imedhaminiwa na wa Mfuko wa mawasiliano kwa wote wa  Uholanzi.

Friday, March 15, 2013

KAMATI ZA MAAFA, SHEREHE ZAKUTANA ZANZIBAR


·          BALOZI SEIF AONGOZA VIKAO
·        Zapongezwa, wananchi watakiwa kufuatilia taarifa za hali ya hewa
Kamati ya sherehe na maadhimisho ya kitaifa Zanzibar
imekutana kutathmini maadhimisho ya sherehe za miaka 49 ya Mapinduzi ya Zanzibar zilizofanyika mwezi Januari mwaka huu katika ukumbi wa nyuma wa Jumba la Wananchi Forodhani Mjini Zanzibar.
Kikao hicho kilichokuwa  ya Mwenyekiti wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kilipokea taarifa ya tathmini ya maadhimisho hayo toka kwa kaimu Katibu wa Sekriterieti ya Kamati hiyo ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  Said Shaaban ambae alisema kamati zote zilitekeleza vyema majukumu waliyopangiwa.
Said aliwaeleza wajumbe hao kuwa licha ya ufanisi ulioshuhudiwa pia zipo changamoto zilizojichomoza ndani ya utekelezaji wa majukumu ya kamati hizo ambayo ni pamoja na ufinyu wa bajeti kulingana na shughuli zilivyopangwa na ushiriki mdogo wa maafisa wa serikali na masheha kwa dhana ya kuwa sio wahusika.
Alisema katika kufanikisha maadhimisho ya mwakani ambapo Zanzibar
itakuwa inatimiza nusu sekriterieti imependekeza kuvishikisha na kuvitumia ipasavyo vyombo vya habari hasa vya serikali ili kushajiisha umma kuelewa umuhimu wa kushiriki katika maadhimisho.
Aidha Mwenyekiti wa Kamati hiyo alizipongeza kamati zote kwa kufanikisha vyema sherehe hizo na kufahamisha kwamba zilifanikiwa kutokana na ushirikiano mzuri uliokuwepo baina ya viongozi na wafanyakazi wa taasisi za umma, binafsi na wananchi.
“Wakati tunafanya tathmini ya sherehe za miaka 49 ya Mapinduzi ya Zanzibar
tunapaswa kuanza safari kubwa ya sherehe hizi kutimia nusu karne hapo mwakani”. Alisema Balozi Seif.
Nao wajumbe wa kamati hiyo walishukuru ushirikiano waliopatiwa na serikali na kuazimia kukutana tena katika kipindi cha mwezi mmoja ujao ili kupanga mikakati ya maandalizi kwa ajili ya maadhimisho ya mwakani.
Mapema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alikiongoza kikao cha kamati ya Maafa Zanzibar kujadili namna ya taifa linavyoweza kujiandaa dhidi ya maafa au matatizo  yoyote yanayoweza kutokea katika kipindi hichi cha mvua za masika zilizokwishaanza.
Kikao hicho kilichojumuisha wajumbe wa kamati hiyo toka Unguja na Pemba kilifanyika katika ukumbi wa Ofisini kwa Makamu huyo wa Rais iliyopo Vuga Mjini Zanzibar.
Akiwasilisha taarifa juu ya mwelekeo wa mvua za masika katika kipindi cha kuanzia mwezi wa Machi hadi Mei, Mkurugenzi wa Idaya ya Maafa Zanzibar Ali Juma Hamad alisema kuwa pamoja matarajio ya mvua kuwa za wastani katika maeneo mengi, bado upo uwezekano wa kutokea miripuko ya magonjwa.
Hamad alisema taasisi zinazohusika na maafa zinapaswa kuchukuwa  hatua za tahadhari kufanya maandalizi ya kukabiliana na madhara yanayoweza  kusababishwa na mvua za masika.
Akizungumzia sekta ya kilimo na usalama wa chakula Hamad alisema maeneo mengi ya ukanda wa pwani ya kaskazini pamoja na Visiwa vya Zanzibar yanatarajiwa kuwa na unyevu unyevu wa kutosha wa udongo hali ambayo wakulima wanashauriwa  kuendelea na taratibu za kawaida za kilimo cha msimu huu wa mvua za masika.
Akikiahirisha Kikao hicho Balozi Iddi aliiagiza Idara hiyo kwa kushirikiana na wataalamu wa taasisi washirika kuandaa utaratibu mahsusi wa kutoa taarifa rasmi kwa wananchi kuanzia wiki ijayo ili kuisaidia jamii kuchukua tahadhari dhidi ya majanga yoyote yanayoweza kutokea katika mvua za masika.
Alisema serikali na wananchi wote wanapaswa kujitayarisha kukabiliana na majanga au maafa ili kuepusha madhara yatakayosababishwa na mvua za masika zilizoanza mapema mwezi huu.
Wakichangia wajumbe wa kamati hiyo walisema wananchi wengi  hadi sasa hawajawa na utamaduni ya  kufuatilia mienendo ya mifumo ya hali ya hewa nchini ambayo ni muhimu katika maisha yao ya kila siku licha ya taasisi zinazohusika na hali ya hewa kutoa taarifa hizo mara kwa mara.

Monday, February 18, 2013

ASKOFU MUSHI KUZIKWA KITOPE

ASKOFU MUSHI KUZIKWA JUMATANO

MAZISHI ya marehemu Askofu Veratus Gabriel Mushi wa kanisa katoliki jimbo la zanzibar aliyweuawa kwa kupigwa risasi jana asubuhi yanatarajia kufanyika Jumatano katika makaburi ya Kitope mkoa wa Kaskazini Unguja.

Akizungungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Shangani mjini Zanzibar, Askofu Mkuu wa Kanisa hilo jimbo la Zanzibar Agostino Shao alisema kanisa lake limepokea kwa mshtuko tukio hilo na kwamba linaendelea na maandalizi ya mazishi yanayotarajiwa kufanyika katika makaburi ya viongozi wa kanisa hilo katika kijiji cha Kitope, wilaya ya Kaskazini 'B', Unguja.

Alisema kanisa lake linafanya mawasiliano na ndugu wa marehemu ili kujua ni watu gani wataotaka kuhudhuria katika mazishi hayo pamoja na wageni.

"Tunachokifanya toka jana baada ya kukabidhiwa mwili wa marehemu majira ya saa kumi jioni ni kuratibu juu ya namna ya mazishi yatakavyokuwa pamoja na wageni tunaotarajia kuwapokea katika mazishi hayo", alisema Askofu Shao.

Pamoja na kuelezwa kuridhishwa kwake na hatua zilizochukuliwa na jeshi la polisi toka kutokea kwa tukio hilo, Askofu Shao alisema ipo haja kwa jeshi hilo kuhakikisha linawajibika ipasavyo ili kukomesha vitendo vya uhalifu si tu kwa viongozi wa dini na maeneo yao ya ibada bali pia kwa raia wote.

Akionesha kutoridhika na kutofanyiwa kazi kwa taarifa za kutokea kwa matukio mbali mbali dhidi ya kanisa na viongozi wake, askofu huyo alisema kuna haja maalum kwa Rais kufanya marekebisho ya uongozi wa jeshi hilo kwa upande wa Zanzibar ili lifanye kazi kwa kuzingatia sheria na kufanya juhudi katika kuzuia uhalifu kabla ya kutokea.

"Kuna taarifa nyingi tumekuwa tukitoa kwa jeshi la polisi lakni taarifa hizi zimekuwa hazifanyiwi kazi kikamilifu na kuwa ndio chanzo cha matukio mengi ya kihalifu ndani ya nchi", alisema Askofu Shao.


SMZ YATOA TAMKO

SERIKALI ITWASAKA WALIOMUUA ASKOFU MUSHI
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imewataka wananchi wa imani zote kutoa ushirikiano kwa vyombo vya ulinzi na usalama ili kuviwezesha kufanya uchunguzi wa kifo cha Askofu  Varistus Gabriel Mushi kilichotokea jana asubuhi.

Akitoa taarifa ya serikali, Waziri wa nchi Afisi ya Makamo wa Kwanza wa Rais Muhammed Aboud Muhammed ofisini kwake Vuga, alisema serikali italiwezehsa jeshi la polisi na vyombo vyengine ulinzi na usalama ili kubaini chanzo cha matukio hayo yanayoonekana kushamiri siku hadi siku.

Abuod alisema katika wakati huu wa majonzi wananchi na waumini wa dini zote wanapaswa kutulia na kuviacha vyombo hivyo vifanye kazi zao kwa utaalamu na mafunzo yao.

"Serikali haiwezi kuacha matukio kama haya yaendelee kwani yanaibua hofu kwa jamii na kuathiri jina la nchi yetu na uchumi wetu kwa ujumla", alisema Aboud.

Aliongeza kuwa serikali ya Zanzibar inaunga mkono tamko lililotolewa na serikali ya muungano linalovitaka vyombo vya usalama vya ndani na nje ya nchi ili kubaini chanzo cha matukio hayo na kama kuna watu au kundi lolote linalofadhili matukio hayo.

Kuhusu suala la uwezekano wa kuzagaa kwa silaha, Aboud alisema hali hiyo inatokana na mazingira ya Zanzibar yanayowezesha kuwepo kwa bandari zisizo rasmi (bubu) jambo ambalo serikali inalifanyia kazi na kuwataka wananchi kutoa taarifa juu ya watu wanaowatilia shaka kuhusika na vitendo vya uhalifu.

Aidha aliwataka viongozi wa dini kuendelea kuhubiri amani , utulivu na kuvumiliana miongoni mwa waumini wao ili kuiepusha nchi na matatizo ya kijamii na kiuchumi.

"Kwa miaka mingi watu wa dini tofauti wamekuwa wakiishi pamoja kwa mafahamiano na mshikamano hivyo bado kila mmoja wetu anapaswa kutimiza wajibu wake ili kuendeleza mshikamano uliodumu kwa muda mrefu", aliongeza Aboud.

Askofu Mushi aliuawa kwa kupigwa risasi tatu kichwani asubuhi ya Jumapili wakati akienda kuendesha misa ya Jumapili katika kanisa la mtakatifu Theressa liliopo Beit el Ras nje kidogo ya mji wa Zanzibar ambalo ni sehemu ya kanisa Katholiki jimbo kuu la Zanzibar.