NA MWINYIMVUA NZUKWI
Katibu Tawala wa Mkoa Mjini
Magharibi Hamida Mussa Khamis amewataka wajumbe wa shirikisho la vikundi
vya ushirika na maendeleo vya mkoa huo kuwahimiza wananchi juu ya umuhimu wa
uchimbaji na matumizi sahihi ya vyoo ili kuijiepusha na maradhi ya mripuko.
Akifungua mafunzo ya kuwajengea
uwezo viongozi wa shirikisho hilo kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa mjini magharibi
Ayoub Mohammed Mahmoud alisema wana vikundi hao wana wajibu wa kueneza elimu
hiyo kwa wananchi wenzao wa shehia zilimo ndani ya mkoa huo.
“Umefika wakati kwa wananchi
kujenga utamaduni wa kujenga vyoo na kuvitumia ili kuondokana na maradhi mbali
mbali yanayosababishwa na uchafu yakiwemo ya kipindupindu”, alisema Katibu huyo.
Alieleza kuwa baadhi ya maeneo
ya mkoa huo mazingira yake hayaridhishi kutokana na kukosa vyoo vya kisasa
hivyo ni vyema wanachama wa shirikisho hilo wakawa mabalozi wazuri kwa wananchi
waliowazunguka ndani ya wilaya za mkoa huo.
Aidha aliwaasa wanaushirika hao
kuendelea kujitolea kwa ajili ya maendeleo ya vikundi vyao ili
viweze kuondokana na umasikini uliokithiri nchini unaochangiwa na ukosefu
wa ajira.
“Kutokana na sababu mbali mbali
zikiwemo za ongezeko la watu, serekali haina uwezo wa kuwaajiri wananchi wote
hivyo ni vyema mkajikusanya katika vikundi na kuanzisha miradi ya maendeleo
ili muweze kusaidiwa kupitia mfuko wa
uwezeshaji ulioanzishwa na serikali kwa madhuimuni hayo”, alisema Hamida na
kuahidi kuwa serikali ya mkoa huo itaendelea kuwasaidia ili wafikie malengo
waliyojiwekea.
Akitoa maelezo kabla ya ufunguzi
wa mafunzo hayo Mratibu wa Shirikisho la vikundi hivyo Sadfa Othman Kaswela ameeleza
kuwa lengo la kuazishwa shirikisho hilo ni kuwasaidia wananchi kujikwamua
kimaisha kupitia miradi ya maendeleo wanayoiendeha.
Alisema katika kukabiliana na
umaskini wananchi wa maeneo mbali mbali ya mkoa huo wameanzisha vikundi vya
ushirika kwa lengo la kukabiliana na changamoto za maisha hivyo shirikisho hilo
linakusudia kuviunganisha vikundi hivyo ili kupata nguvu ya pamoja.
“Vikundi vyetu huwa
vianakabiliwa na changamoto kadhaa zikiwemo za uwezo mdogo wa kujiendeleza
hivyo kupitia shirikisho hili tunaamini tutaweza kukabiliana na changamoto hizo
na kuimarisha utekelezaji wa kazi zetu”, alieleza.
Nao baadhi ya viongozi wa
shirikisho hilo kutoka katika wiliya za mkoa huo waliwahimiza wanawake wa mkoa
wa Mjini Magharibi kujitokeza na kujiunga katika vikundi vya maendeleo ili
kupata mafunzo yatakayowajengea uwezo wa kujitegemea na kuepukana na utengemezi
katika jamii zao.
Walisema panmoja na idadi kubwa
ya vikundi hivyo kuundwa na wananwake, bado kundi hilo la jamii linapaswa kuwa
mstari wa mbele katika kuimarisha ushirika kama njia mojawapo ya kupambana na umaskini
wa kipato ndani ya familia zao.
Mafunzo hayo yaliyofanyika
katika ukumbi wa skuli ya sekondari ya Haile Selassie yaliandaliwa na
shirikisho hilo kwa lengo la kujengeana uwezo ili kuvisaidia vikundi hivyo kuwa
endelevu kwa lengo la kuimarisha maendeleo ya jamii.