NA OTHMAN KHAMIS – OMPR
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema
uagizaji wa baadhi ya bidhaa ikiwamo chakula na matunda nje ya
Zanzibar umepungua kutokana na hamasa kubwa waliyonayo wananchi hasa
wakulima katika muelekeo wa kuwekeza zaidi kwenye sekta muhimu ya kilimo.
Alisema sekta ya kilimo ni miongozi mwa maeneo
yaliyopewa msukumo wa kwanza na Chama cha Mapinduzi wakati kikiomba ridhaa ya
kutaka kuongoza dola nchini Tanzania kwenye kampeni za uchaguzi mkuu kilipokuwa
kikitangaza sera na ilani yake.
Balozi Seif alitoa Kauli hiyo wakati alipofanya mahojiano
maalum na timu ya wanahabari wa redio Uhuru na Magazeti ya Chama cha Mapinduzi
ya Uhuru na Mzalendo waliotaka kujua utekelezaji wa ilani ya CCM kwa upande wa
Zanzibar yaliyofanyika kwenye Ofisi ya Uratibu wa shughuli za SMZ Jijini Dar es
salaam.
Alisema kutokana na serikali za CCM kusamehe ushuru wa
forodha kwenye vifaa vya kilimo vinavyoingizwa nchini sambamba na kuendeleza
mafunzo ya kisasa kwa wadau wa kilimo, wakulima wengi nchini hasa wale
wanaojishughulisha na kilimo cha matunda wameongeza mara dufu uwezo wa
uzalishaji.
Balozi Seif alisema katika kipindi cha miaka mitatu
iliyopita mara baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu wakulima wengi wamekuwa
wakilalamikia ufinyu za soko la bidhaa wanazozalisha jambo ambalo imefikia
wakati baadhi ya bidhaa hizo zikisafirishwa kupelekwa upande wa Tanzania bara.
Alisema hatua hiyo imeonyesha mabadiliko makubwa
yaliyokuwa yamezoelekea kwa muda mrefu katika kushuhudia bidhaa nyingi hasa
zile za nafaka, mizizi, mboga mboga pamoja na matunda zikiingizwa
Zanzibar kutokea Mikoa mbali mbali ya Tanzania Bara.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisisitiza
kwamba kwa vile Kilimo ndio uti wa Mgongo wa Taifa Wananchi na hasa Wakulima
wanapaswa kuendelea kuzalisha mazao yao katika kiwango kinachokubalika
Kitaalamu ili Taifa liendelee kupunguza kasi ya kuagiza bidhaa kutoka Nje ya
Nchi.
Balozi Seif alisema Serikali imelazimika kufidia
pembejeo kwa Wakulima na kupunguza bei ya Dawa ili kuhamasisha Wananchi walio
wengi zaidi Vijana kuelekeza nguvu zao katika Sekta ya Kilimo yenye uwezo wa
kutoa ajira pana zaidi na kupunguza umaskini kwa kiwango kikubwa.
Akigusia Sekta nyengine za
Kiuchumi akitolea mfano zile za Utalii, Viwanda, Elimu, Afya pamoja
na Miundombinu ya Mawasiliano ya Bara bara na Anga Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar alisema Serikali chini ya Uongozi mahiri wa Rais wa Zanzibar Dr. Ali
Mohamed Shein imeweza kupiga hatua kubwa katika uimarishaji wa Miundombinu
kwenye maeneo hayo.
Alisema ujenzi wa eneo la Maegesho ya Ndege kwenye
Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, Gati ya Malindi na baadhi
ya Bara bara zinazoelekea katika maeneo ya Utalii ni mfano hai unaothibitisha
utekelezaji wa kasi wa Ilani na Sera ya CCM ya Mwaka 2015/2020 uliofanikiwa
ndani ya Miaka Mitatu.
Balozi Seif aliieleza Timu hiyo ya Wanahabari wa
Redio Uhuru na Magazeti ya Chama ya Uhuru na Mzalendo kwamba lengo la Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar la kupokea Watalii zaidi ya Laki 500,000 ifikapo Mwaka
2020 inaanza kutoa sura zaidi kwa vile hivi sasa inakadiriwa kufikia zaidi la Laki
350,000.
Kwa upande wa makusanyo ya Mapato Balozi
Seif alisema yapo mafanikio makubwa yiliyofikiwa kutokana na
Serikali Kuu kuongeza udhibiti wa matumizi ya fedha za Serikali.
Alisema hatua hiyo imeisababishia Serikali kupitia
Taasisi zake kukusanya Mapato yanayokadiriwa kufikia shilingi Bilioni 400,000/-
lengo likiwa kuondokana na utegemezi ambao kwa sasa umefikia Asilimia 7% kutoka
asilimia 20% katika kipindi cha Mwaka 2013 hadi 2016.
Balozi Seif alifahamisha kwamba mianya ya rushwa
imewezeshwa kupungua kwa kiasi kikubwa kutokana na ushirikiano mzuri uliopo
kati ya Serikali, Taasisi za Umma pamoja na Wananchi Wazalendo.
Kuhusu suala la Amani na Utulivu wa Taifa Balozi
Seif kupitia Kipindi hicho Maalum cha Mahojiano aliwanasihi Wananchi
Bara na Zanzibar kuendelea kuitunza Lulu hiyo iliyo adimu kupatikana katika
baadhi ya Mataifa mengi Duniani yakiwemo yale ya Bara la Afrika.
Alisema Viongozi Wakuu kwa kushirikiana na wasaidizi
wao wamekuwa mstari wa mbele katika kuisisitiza Jamii kudumisha Amani na Utulivu
ambayo ndio ngao kubwa ya kuendeleza mshikamo uliojengeka kwa Watanzania walio
wengi Mjini na Vijijini.
Alikumbusha kwamba Serikali zote mbili zitaendelea
kusimamia ulinzi wa Amani iliyopo Nchini muda wote hata wakati unapowadia wa
Taifa kuingia katika harakati za Uchaguzi Mkuu ambazo huonekana baadhi ya
wafuasi wa Vyama vya Siasa wakati mwengine kujaribu kuitikisa Amani hiyo.
Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Balozi Seif Ali Iddi alikutana kwa Mazungumzo na Mkurugenzi wa Idara ya Asia wa
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ya Tanzania Bibi
Justa Matari Nyange Ofisi ya Uratibu wa SMZ Jijini Dar es salaam.
Katika Mazungumzo yao Viongozi hao walizungumzia
hatua zinazoendelea katika maandalizi ya Ushiriki wa Jamuhuri ya Muungano wa
Tanzania katika Maonyesho ya Kimataifa ya Biashara yanayotarajiwa kufanyika
katika Jimbo la Guangzhou Nchini China mnamo Mwezi wa Septemba Mwaka huu.
Balozi Seif alimueleza Mkurugenzi huyo wa Asia
kwamba Jamuhuri ya Watu wa China imekuwa Mashirika mkubwa wa Tanzania katika
masuala ya Utamaduni, Biashara pamoja na Historia mara tuu baada ya Uhuru wa
Tanzania na Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Mwaka 1964.
Alisema uhusiano huo kupitia mialiko na muingiliano
wa ziara za mara kwa mara za pande hizo mbili ni vyema vikaendelea kujengewa
mazingia ya kuimarishwa siku hadi siku kwa faida ya Jamii ya sasa na ile ijayo
ya pande zote mbili.
Nae Mkurugenzi wa Asia wa Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki ya Tanzania Bibi Justa Matari Nyange alisema
kwa vile Kamati za maandalizi ya Maonyesho hayo Chini ya Uratibu wa Wizara ya
Mambo ya Nje zimeshaundwa kwa sehemu zote mbili, ipo haja ya kukutanishwa
pamoja katika njia ya kupata mafanikio ya jumla.
Bibi Justa alisema kinachotarajiwa kwenda
kuwakilishwa katika Maonyesho hayo ya Kibiashara ni ushiriki wa Jamuhuri ya
Muungano wa Tanzania kikamilifu unaojumuisha makusanyo ya Wajumbe wa pande zote
mbili za Muungano.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali
Iddi (katikat)i akifafanua jambo wakati wa mahojiano maalum na Wanahabari wa Redio Uhuru Magazeti ya Chama cha Mapinduzi ya Uhuru na Mzalendo waliotaka kujua
Utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa upande wa Zanzibar kwenye Ofisi ya Uratibu ya
SMZ Jijini Dar es salaam.
Balozi Seif Ali Iddi (kulia) akizungumza na Mkurugenzi wa Idara ya Asia wa Wizara ya Mambo ya Nje
na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ya Tanzania Bi. Justa Matari Nyange katika Ofisi
ya Uratibu wa SMZ Jijini Dar es salaam.
No comments:
Post a Comment