Wednesday, June 13, 2018

ROMANIA YAANZA UTAFITI WA MAENEO YA MISAADA MKOA WA MJINI MAGHARIBI


NA MWINYIMVUA NZUKWI
Serikali ya mkoa wa Mjini Magharibi inatarajia kusaini makubaliano na shirika la misaada ya maendeleo la Romania RoAID ili kusaidia maendeleo ya sekta mbali mbali ndani ya mkoa huo.

Mkuu wa mkoa wa Mjini Magharibi  Ayoub Mohammed Mahmoud ameeleza hayo wakati wa kikao cha pamoja kati ya watendaji wa baadhi ya taasisi za Zanzibar na taasisi PRENUIUM AUDIT iliyopewa kazi na serikali ya Romania kufanya utafiti wa awali juu ya maeneo yanayoweza kupatiwa misaada na shirika hilo kwa lengo la kustawisha huduma za jamii nchini.

Amesema hatua hiyo itafikiwa baada ya wataalamu wa sekta mbali mbali nchini kufanya kazi ya kukusanya taarifa kwa pamoja na watendaji wa taasisi ya PREMIUM AUDIT na kasha kufanyiwa upembuzi yakinifu wa taarifa zitazopatikana ambazo zitaainisha ni maeneo gani ya kipaumbele katika kupatiwa misaada hiyo.

Amezitaja baadhi ya sekta zitakazofikiwa na hatua hiyo n ipamoja na sekta ya utalii, sekta ya afya, maji safi na salama, miundombinu ya barabara, nishati ya umeme, uimarishaji wa mji mkongwe  na udhibiti wa takataka katika manispaa za mkoa huo hivyo amewataka watendaji wa taasisi zinazohusikana sekta hizo kukutana haraka na kuainisha maeneo ya vipaumbele yanayoweza kuendelezwa.


Amesema hatua hiyo imekuja kwalengo la kuisaidia serikali katika kukabiliana na changamoto mbali mbali katika sekta za kiuchumi na kijamii na kuishukuru serikali ya Romania kupitia kampuni ya Rom Solution iliyosaidia kufikiwa kwa hatua hiyo ambayo amesema misaada hiyo inaweza kutolelewa mahali pengine popote nje ya mkoa wa Mjini Magharibi.

Awali akiwasilisha mpango wa utekelezaji wa mradi huo, Mtafiti kutoka taasisi ya Premium Audit Cristian Stefenescu ameeleza kuwa shirika la misaada ya maendeleo la Romania linalodhaminiwa na serikali ya Romania limekuwa likitoa misaada ya kibinadaamu na kuimarisha sekta za kijamii katika maeneo mbali mbali ulimwenguni hivyo Zanzibar inaweza kunufaika zaidi  kutokana na kuwa na vigezo vilivyowekwa na shirika hilo.

Akitolea mfano namna shirika lake linavyoweza kuiimarisha sekta ya utalii, Bw. Cristian amesema pamoja na Zanzibar kupokea idadi kubwa ya watalii bado sehemu kubwa ya jamii haijanufaika na soko la sekta hiyo jambo linaloweza kufikiwa kwa kutoa elimu ya kuimarisha ujasiriamali na kutengeneza kituo cha elimu ya utalii ili iweze kuinufaisha jamii nzima.

Katika sekta za afya na miundo mbinu mtafiti huyo ameeleza kuwa wanahitaji kupata taarifa juu ya namna sekta hizo zinavyoweza kuimarishwa kwa kupatiwa vifaa, ujuzi na utaalamu na kuwataka watu watakaokuwemo katika timu ya wataalamu kuwa tayari kufanya kazi inayolenga kutoa matokeo mazuri.

Nae meneja uendeshaji wa kampuni ya Rom Solution LTD George Alexandru amesema kampuni yake imesaidia kupatikana kwa fursa hiyo baada ya kubaini uwepo wa maeneo yanayohitaji msaada na kumshukuru Mkuu a mkoa wa Mjini Magharibi kwa kuiona fursa hiyo na kuitumia jambo alilosema litasidia kuimarisha uhusiano uliopo kati ya serikali ya Zanzibar, Tanzania na ya Romania.

Amesema iwapo mradi huo utakamilika na wataalamu kuainisha maeneo ya utekelezaji utachochochea ukuaji wa uchumi kupitia sekta ya utalii na kuwataka wataalamu watakaohusika katika hatua za awali za utekelezaji wa mradi huo kuzingatia vipau mbele vya sekta ambazo zitapatiwa misaada kwa manufaa ya jamii.

Mradi huo unatarajiwa kuanza kutekelezwa kwa kipindi cha miezi mitatu kuanzia mwezi huu ambapo jumla ya Euro 35,908.15 zilizotolewa na shirika la RoAID zinatarajiwa kutumika kwa kazi ya utafiti wa awali, upembuzi yakinifu na kuandaa miradi itakayofadhiliwa na shirika hilo.









No comments:

Post a Comment