Thursday, June 14, 2018

"SAIDIENI WENYE MAHITAJI MPATE BARAKA" - RC AYOUB

Mkuu wa mkoa wa Mjini Magharibi Ayoub Mohammed Mahmoud amewataka watu wenye uwezo kusaidia watu wenye mahitaji ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za serikali ya Zanzibar ya kutoa huduma bora za jamii hasa wazee.

Amesema kufanya hivyo licha ya kuongeza baraka katika shughuli zao pia huleta faraja kwa wazee hao ambao baadhi yao wanatunzwa na serikali katika nyumba za kulelea wazee ili waweze kufaidi matunda ya kazi walizozifanya kwa ajili ya nchi wakati wa ujana wao.

Akikabidhi sadaka ya fedha taslim na mavazi vilivyotolewa mfanyabiashara Said Nasser Bopar kwa ajili ya sikukuu ya Eid el fitri kwa wazee wanaoishii kataika nyumba ya kulelea wazee Sebleni mkoa wa Mjini Magharibi alimshukuru mfanyabiashara huyo kwa kuendeleza jambo hilo kila mwaka.

Amesema serikali ya awamu ya saba inayoongozwa na Dk. Ali Mohamed Shein imeongeza maradufu upatikanaji wa huduma muhimu kwa wazee wanaotunzwa katika makaazi maalum  Unguja na Pemba na kuwapatia fedha za kujikimu kila mwezi hivyo misaada inayotolewa na wasamaria wema inapaswa kupongezwa kwani inasaidia kuimarisha huduma hizo.


Ameeleza kuwa wazee hao wamelitumikia taifa kwa moyo na uzalendo wa hali ya juu hivyo wanapaswa kutunzwa na kila mmoja miongoni mwa jamii na kuwataka wazee hao kupokea misaada na sadaka zinazotolewa kwao na kuitumia kama ilivyokusudiwa.

"Mnapopokea misaada hii msijisikie unyonge kwani hii ni haki yenu na ni wajibu wa kiola mmoja wetu kuhakikisha mnamalizia maisha yenu kwa heshima kubwa kama mlivyoiletea nchi yetu heshima wakati wa ujana wenu hivyo nawaomba sana mvitumie vitu mlivyokabidhiwa ili mfaidi matunda ya jasho mlilolitoa kwa ajili ya maendeleo ya nchi yenu", alisema Ayoub.

Nae Mwakilishi wa Mfanyabiashara huyo, Sheikh Mohammed Suleiman 'Tall' aliwashukuru wazee hao kwa kukubali kupokea sadaka hiyo na kutoa shukurani kwa mku huyo wa mkoa kwa juhudi anazaochukua za kutafuta njia za kuhakikisha ustawi bora wa jamii ndani na nje ya mkoa wake.

Alieleza kuwa iwapo viongozi wa ngazi mbali mbali watachukua juhudi za kutatua matatizo yanayowakabili wananchi wao kama ilivyo kwa kiongozi huyo, kuna uwezekano mkubwa wa kuimarika kwa mapenzi, imani na amani iliyopo nchini na kuchochea kuimarika kwa huduma za jamii pamoja na uchumi wa nchi.

"Juhudi unazochukua za kufika kila mahali ambapo watu wana mahitaji kunaongeza imani ya wananchi hata pale unapokosa uwezo wa kusaidia moja kwa moja jambo ambalo naamini kama kila kiongozi akilizingatia litasaidia kukuza umoja na mshikamano wa watu wetu", alisema.

Aidha Sheikh Suleiman amewahimiza vijana na makundi mbali mbali ya jamii kuona umuhimu wa kuwatendea wema wazee wanaoishi mitaani na wanaotunzwa katika vituo maalum ili kupata radhi na fadhila nyingi kutoka kwa Mwenyezi Mungu zitakazowanufaisha duniani na akhera.

Akizungumza kwa niaba ya wazee wenzake Bi. Asaa Ali Issa alimshukuru Mkuu wa mkoa na mfanyabiashara huyo kwa sadaka hiyo na kuwaomba kutosita kufanya hivyo kila mara uwezo unapowaruhusu ili kuwawezesha kumudu gharama za maisha.

Mama huyo pia alimshukuru Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein kwa juhudi zake za kuimarisha huduma kwa wazee katika kituo hicho jambo linalowavutia wasamaria wema wengine na viongozi mbali mbali kutoa misaada ambayo alisema inawaongezea furaha na kutambua thamani yao kwa serikali na nchi yao.

Katika hafla hiyo wazee hao walikabidhiwa nguo za kike na kiume, mashuka na fedha taslimu kwa ajili ya kujikimu katika sikukuu ya Eid itakayoanza Ijumaa au Jumamosi wiki hii baada ya kukamilika kwa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani ambao ni moja ya nguzo katika nguzo tano za uislamu.






MKUU wa mkoa wa mjini magharibi Ayoub Mohammed Mahmoud (alievaa kanzu na kofia) akiwakabidhi miongoni mwa wazee wanaoishi katika nyumba ya kulelea wazee Sebleni msaada wa nguo na fedha taslim uliotolewa na mfanyabiashara Said Nasser Bobar kwa ajili ya sikukuu ya Eid el Fitri hafla iliyofanyika katika makaazi ya wazee hao Sebleni, mkoa wa Mjini Magharibi Unguja. (Picha na Mwinyimvua Nzukwi).

No comments:

Post a Comment