Thursday, June 21, 2018

DK. SHEIN KUWAAPISHA WAJUMBE WAPYA WA ZEC KESHO, TAMWA YAMPONGEZA


NA MWINYIMVUA NZUKWI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein kwa kutumia uwezo aliopewa na katiba ya Zanzibar ya 1984 kama ilivyorekebishwa, kifungu cha 119 amefanya uteuzi wa Wajumbe wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC).

Katika uteuzi huo Dkt. Shein amemteua Jaji Mkuu Mstaafu wa Zanzibar Hamid Mahmoud Hamid kuwa Mweyekiti wa tume hiyo pamoja na wajumbe wengine 6 wakiwemo wawakilishi wa vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu.

Walioteuliwa kuwa wajumbe wa tume hiyo ni pamoja na aliewahi kuwa Mkurugenzi wa baraza la manispaa ya Zanzibar Mabruki Jabu Makame, Feteh Saad Mgeni,  Makame Juma Pandu, Dkt. Kombo Khamis Hassan, Jaji Khamis Ramadhan Abdulla na Jokha Khamis Makame ambae anakuwa mwanamke pekee kuteuliwa kuwa mjumbe wa tume hiyo.

Wakati huo huo Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) Zanzibar kimempongeza Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein kwa kuteua mjumbe mwanamke miongoni mwa wajumbe wa ZEC ikiwa ni mara ya kwanza toka na kuwepo kwa asilimia 14.2 ya uwakilishi wa wanawake katika tume hiyo.

Taarifa iliyotolewa na mkurugenzi wa tamwa Zanzibar dk. Mzuri issa ali imeleza kuwa mwaka 2013 tume hiyo haojawahi kuwa na mjumbe mwanamke hali iliyopelekea chama hicho kumuomba Rais Dk. Shein afanye uteuzi wa wajumbe katika tume hiyo hali iliyopelekea kuteuliwa kwa Jokha Khamis Makame.

“Usawa wa kijinsia ni suala muhimu katika kipindi hiki hasa kwa vile kwa miaka mingi wanawake waliachwa nyuma katika ngazi za mbali mbali za uongozi, hivyo kubaki nyuma katika maendeleo, pamoja na kuwa wao wako zaidi ya asilimia 50 ya watu nchini”, imeeleza taarifa hiyo.

Aidha Dk. Mzuri amempongeza mjumbe huyo na wajumbe wengine wa tume hiyo na kuwataka kutekeleza majukumu yao kwa weledi na uaminifu mkubwa.

Akitolea mfano utekelezaji wa itifaki ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) amesema kipengele cha 12 (1) kinazitaka nchi wanachama kuhakikisha zinahakikisha asilimia 50 katika nafasi zote za maaamuzi ifikapo mwaka 2025 na kumuomba rais na jamii kukumbuka wajibu huu wa nchi katika kufikia malengo ya usawa wa kijinsia.

“Ni vyema pia vyama vya siasa kuanza kujitafakari na kuangalia kuwa wanawake ni wadau wa maendeleo kama wanaume hivyo wanahitaji kushika nafasi muhimu za maamuzi ndani ya vyama vyao”, alieleza Mkurugenzi huyo.


Kwa mujibu wa taarifa iliyotiwa saini na Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa baraza la Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee imeeleza uteuzi wa wajumbe hao wanaochukua nafasi ya tume iliyoongozwa na mwenyekiti wake Jecha Salim Jecha umeanza Juni 20, 2018 na wajume hao wanatarajiwa kuapishwa Ijumaa ya Juni 22, 2018 ikulu Mjini Zanzibar.


No comments:

Post a Comment