Tuesday, June 26, 2018

BALOZI SEIF ASEMA KILIMO CHA KISASA KIMEPUNGUZA UAGIZAJI WA CHAKULA, MATUNDA NJE


NA OTHMAN KHAMIS – OMPR
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema uagizaji wa baadhi ya bidhaa ikiwamo chakula na matunda nje ya Zanzibar  umepungua kutokana na hamasa kubwa waliyonayo wananchi hasa wakulima katika muelekeo wa kuwekeza zaidi kwenye sekta muhimu ya kilimo.
Alisema sekta ya kilimo ni miongozi mwa maeneo yaliyopewa msukumo wa kwanza na Chama cha Mapinduzi wakati kikiomba ridhaa ya kutaka kuongoza dola nchini Tanzania kwenye kampeni za uchaguzi mkuu kilipokuwa kikitangaza sera na ilani yake.
Balozi Seif alitoa Kauli hiyo wakati alipofanya mahojiano maalum na timu ya wanahabari wa redio Uhuru na Magazeti ya Chama cha Mapinduzi ya Uhuru na Mzalendo waliotaka kujua utekelezaji wa ilani ya CCM kwa upande wa Zanzibar yaliyofanyika kwenye Ofisi ya Uratibu wa shughuli za SMZ Jijini Dar es salaam.
Alisema kutokana na serikali za CCM kusamehe ushuru wa forodha kwenye vifaa vya kilimo vinavyoingizwa nchini sambamba na kuendeleza mafunzo ya kisasa kwa wadau wa kilimo, wakulima wengi nchini hasa wale wanaojishughulisha na kilimo cha matunda wameongeza mara dufu uwezo wa uzalishaji.

Friday, June 22, 2018

RAIS DK. SHEIN AMWAPISHA MWENYEKITI MPYA, WAJUMBE WA ZEC



NA MWANDISHI MAALUM
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein  leo amemuapisha Jaji Mkuu Mstaafu wa Zanzibar Hamid Mahmoud Hamid kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC). 

Wakati huo huo, Rais Dk. Shein amewaapisha Wajumbe wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), ambao aliwateua hivi karibuni kushika nyazifa hizo ambapo Wajumbe walioapishwa ni Mabruki Jabu Makame, Feteh Saad Mgeni, Makame Juma Pandu, Dk. Kombo Khamis Hassan, Jaji Khamis Ramadhan Abdalla na Jokha Khamis Makame. 

Thursday, June 21, 2018

DK. SHEIN KUWAAPISHA WAJUMBE WAPYA WA ZEC KESHO, TAMWA YAMPONGEZA


NA MWINYIMVUA NZUKWI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein kwa kutumia uwezo aliopewa na katiba ya Zanzibar ya 1984 kama ilivyorekebishwa, kifungu cha 119 amefanya uteuzi wa Wajumbe wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC).

Katika uteuzi huo Dkt. Shein amemteua Jaji Mkuu Mstaafu wa Zanzibar Hamid Mahmoud Hamid kuwa Mweyekiti wa tume hiyo pamoja na wajumbe wengine 6 wakiwemo wawakilishi wa vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu.

Walioteuliwa kuwa wajumbe wa tume hiyo ni pamoja na aliewahi kuwa Mkurugenzi wa baraza la manispaa ya Zanzibar Mabruki Jabu Makame, Feteh Saad Mgeni,  Makame Juma Pandu, Dkt. Kombo Khamis Hassan, Jaji Khamis Ramadhan Abdulla na Jokha Khamis Makame ambae anakuwa mwanamke pekee kuteuliwa kuwa mjumbe wa tume hiyo.

Wakati huo huo Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) Zanzibar kimempongeza Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein kwa kuteua mjumbe mwanamke miongoni mwa wajumbe wa ZEC ikiwa ni mara ya kwanza toka na kuwepo kwa asilimia 14.2 ya uwakilishi wa wanawake katika tume hiyo.

Taarifa iliyotolewa na mkurugenzi wa tamwa Zanzibar dk. Mzuri issa ali imeleza kuwa mwaka 2013 tume hiyo haojawahi kuwa na mjumbe mwanamke hali iliyopelekea chama hicho kumuomba Rais Dk. Shein afanye uteuzi wa wajumbe katika tume hiyo hali iliyopelekea kuteuliwa kwa Jokha Khamis Makame.

“Usawa wa kijinsia ni suala muhimu katika kipindi hiki hasa kwa vile kwa miaka mingi wanawake waliachwa nyuma katika ngazi za mbali mbali za uongozi, hivyo kubaki nyuma katika maendeleo, pamoja na kuwa wao wako zaidi ya asilimia 50 ya watu nchini”, imeeleza taarifa hiyo.

Aidha Dk. Mzuri amempongeza mjumbe huyo na wajumbe wengine wa tume hiyo na kuwataka kutekeleza majukumu yao kwa weledi na uaminifu mkubwa.

Akitolea mfano utekelezaji wa itifaki ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) amesema kipengele cha 12 (1) kinazitaka nchi wanachama kuhakikisha zinahakikisha asilimia 50 katika nafasi zote za maaamuzi ifikapo mwaka 2025 na kumuomba rais na jamii kukumbuka wajibu huu wa nchi katika kufikia malengo ya usawa wa kijinsia.

“Ni vyema pia vyama vya siasa kuanza kujitafakari na kuangalia kuwa wanawake ni wadau wa maendeleo kama wanaume hivyo wanahitaji kushika nafasi muhimu za maamuzi ndani ya vyama vyao”, alieleza Mkurugenzi huyo.


Kwa mujibu wa taarifa iliyotiwa saini na Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa baraza la Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee imeeleza uteuzi wa wajumbe hao wanaochukua nafasi ya tume iliyoongozwa na mwenyekiti wake Jecha Salim Jecha umeanza Juni 20, 2018 na wajume hao wanatarajiwa kuapishwa Ijumaa ya Juni 22, 2018 ikulu Mjini Zanzibar.


Thursday, June 14, 2018

"SAIDIENI WENYE MAHITAJI MPATE BARAKA" - RC AYOUB

Mkuu wa mkoa wa Mjini Magharibi Ayoub Mohammed Mahmoud amewataka watu wenye uwezo kusaidia watu wenye mahitaji ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za serikali ya Zanzibar ya kutoa huduma bora za jamii hasa wazee.

Amesema kufanya hivyo licha ya kuongeza baraka katika shughuli zao pia huleta faraja kwa wazee hao ambao baadhi yao wanatunzwa na serikali katika nyumba za kulelea wazee ili waweze kufaidi matunda ya kazi walizozifanya kwa ajili ya nchi wakati wa ujana wao.

Akikabidhi sadaka ya fedha taslim na mavazi vilivyotolewa mfanyabiashara Said Nasser Bopar kwa ajili ya sikukuu ya Eid el fitri kwa wazee wanaoishii kataika nyumba ya kulelea wazee Sebleni mkoa wa Mjini Magharibi alimshukuru mfanyabiashara huyo kwa kuendeleza jambo hilo kila mwaka.

Amesema serikali ya awamu ya saba inayoongozwa na Dk. Ali Mohamed Shein imeongeza maradufu upatikanaji wa huduma muhimu kwa wazee wanaotunzwa katika makaazi maalum  Unguja na Pemba na kuwapatia fedha za kujikimu kila mwezi hivyo misaada inayotolewa na wasamaria wema inapaswa kupongezwa kwani inasaidia kuimarisha huduma hizo.

Wednesday, June 13, 2018

ROMANIA YAANZA UTAFITI WA MAENEO YA MISAADA MKOA WA MJINI MAGHARIBI


NA MWINYIMVUA NZUKWI
Serikali ya mkoa wa Mjini Magharibi inatarajia kusaini makubaliano na shirika la misaada ya maendeleo la Romania RoAID ili kusaidia maendeleo ya sekta mbali mbali ndani ya mkoa huo.

Mkuu wa mkoa wa Mjini Magharibi  Ayoub Mohammed Mahmoud ameeleza hayo wakati wa kikao cha pamoja kati ya watendaji wa baadhi ya taasisi za Zanzibar na taasisi PRENUIUM AUDIT iliyopewa kazi na serikali ya Romania kufanya utafiti wa awali juu ya maeneo yanayoweza kupatiwa misaada na shirika hilo kwa lengo la kustawisha huduma za jamii nchini.

Amesema hatua hiyo itafikiwa baada ya wataalamu wa sekta mbali mbali nchini kufanya kazi ya kukusanya taarifa kwa pamoja na watendaji wa taasisi ya PREMIUM AUDIT na kasha kufanyiwa upembuzi yakinifu wa taarifa zitazopatikana ambazo zitaainisha ni maeneo gani ya kipaumbele katika kupatiwa misaada hiyo.

Amezitaja baadhi ya sekta zitakazofikiwa na hatua hiyo n ipamoja na sekta ya utalii, sekta ya afya, maji safi na salama, miundombinu ya barabara, nishati ya umeme, uimarishaji wa mji mkongwe  na udhibiti wa takataka katika manispaa za mkoa huo hivyo amewataka watendaji wa taasisi zinazohusikana sekta hizo kukutana haraka na kuainisha maeneo ya vipaumbele yanayoweza kuendelezwa.