Sunday, September 9, 2018

MALINDI S. C WACHAGUANA, WAMTUNUKU UANACHAMA R. C AYOUB

NA MWINYIMVUA NZUKWI, ZANZIBAR
WAJUMBE wa mkutano mkuu wa klabu ya Malindi inayoshiriki ligi kuu ya Zanzibar wamemchagua Mohammed Abdallah Mohammed ‘Aljabri’ kuwa Mwenyekiti wa klabu hiyo kwa kipindi cha miaka minne ijayo.
Uchaguzi wa viongozi uliofanyika Jumapili Septemba 9, 2018 katika ukumbi wa zamani wa sinema ya Empire Mkunazini, Mwenyekiti huyo aliyebaki peke yake baada ya mgombea mwenzake katika nafasi hiyo Jaffar Hussein Babu ‘Jeff’ kuondoa jina lake, alipata kura 100 kati ya 101 zilizopigwa baada ya kura moja kuharibika.
Akitangaza matokeo Msimamizi wa uchaguzi huo, Katibu Msaidizi wa chama cha soka (ZFA) wilaya ya Mjini Ali Abdullah Mohammed pia alimtangaza ‘Jeff’ kuwa mshindi wa nafasi ya Makamo Mwenyekiti baada ya kupata kura 92 na kumshinda Ramadhan Haji aliyepata kura 5 kati ya kura 100 zilizopigwa na kura 3 ziliharibika.
Katika nafasi ya katibu mkuu wa klabu, Mohammed Masoud aliyegombea peke yake nafasi hiyo alitetea nafasi yake kwa kujinyakulia asilimia 100 ya kura zote 101 zilizopigwa huku kocha Seif Mussa ‘Fagurson’ akichaguliwa kuwa Katibu msaidizi wa klabu hiyo kongwe katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Wajumbe wengine wanaounda Kamati tendaji ya klabu hiyo waliochaguliwa katika uchaguzi huo ni Abdullah Thabit ‘Dula Sunday’ (Katibu Mwenezi), Ali Majid (Mshika fedha), Rajab Said (Msaidizi Mshika Fedha), Amir Saleh (Mhasibu Mkuu) na wajumbe Nassir Seif, Mussa Ramadhan na Mahmoud Hamza.
Aidha mkutano huo umeidhinisha uteuzi wa wajumbe wa baraza la wazee na bodi ya wadhamini wa klabu hiyo na kumthibitisha kiongozi wa muda mrefu wa klabu hiyo Howingkao Hojofat kuwa meneja mkuu wa klabu hiyo yenye mastakimu yake ndani ya Mji Mkongwe wa Zanzibar.
Wanaounda baraza la wazee litakalokuwa na kazi ya ushauri na usuluhishi wa migogoro ndani ya klabu hiyo ni Msadik Abdallah, Abdi Basha, Abdallah Mzee na Ali Mwinyi wakati bodi ya wadhamini inaundwa na mchezaji na kiongozi wa zamani wa klabu hiyo Zahor Salum, sheha wa zamani wa shehia ya Malindi Himid Omar, kiongozi wa zamani wa klabu hiyo Mzee Boti, Ramadhani Haji na mwanachama wa klabu hiyo aliegombea nafasi ya umakamu mwenyekiti katika uchaguzi huo Ali Rajab.
Akitoa shukrani kabla na baada ya kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti Mohammed Abdallah ‘Aljabri’ aliwataka wanachama wa klabu hiyo kuendeleza ushirikiano waliouonesha kabla na wakati wa mkutano huo na kufuata taratibu wakati wa kutekeleza masuala yanayohusiana na klabu yao.
Alisema iwapo mshikamano huo utaimarishwa kuna uwezekano mkubwa wa kufikiwa kwa malengo yaliyowekwa ya kurudisha hadhi ya timu hiyo kama ilivyokuwa katika miaka ya 80 wakati timu hiyo ilipofanikiwa kutwaa ubingwa wa Zanzibar na Tanzania kwa wakati mbali mbali.
Aidha aliahidi kuwa ataendelea kushirikiana na wanachama wote bila ya kujali hadhi au nafasi zao na kwamba ataendelea kusimamia mipango ya kuiendeleza timu hiyo.
Nae Makamu Mwenyekiti Jaffar Hussein ‘Jeff’ aliwashukuru wadau mbali mbali waliofanikisha kukamilia kwa mkutano huo hususan Mkuu wa mkoa wa Mjini Magharibi Ayoub Mohammed mahamoud ambae licha ya kushindwa kuhudhurui katika mkutano huo alitoa baraka za kufanyika ikiwa ni pamoja na ulinzi uliopelekea wanachama wa klabu hiyo kutumia haki yao ya kidemokrasia bila ya hiofu au ukiukwaji wa sheria.
Aliwaasa baadhi ya wanachama, washabiki na wapenzi wa klabu hiyo waliokuwa wakiupinga mkutano huo, kuacha kufanya hivyo na badala yake kuungana na uongozi uliochaguliwa ili kuhimiza maendeleo ya timu hiyo kongwe nchini.
Akiwasilisha mapendekezo ya Kamati hiyo mara baada ya kuchaguliwa Katibu Mkuu Mohammed Masoud alisema watahakikisha kuwa klabu hiyo inakuwa chachu ya maendeleo ya soka nchini na kuzitaka timu nyengine za mitaani kuimarisha timu zao ili kuongeza ushindani.
Alisema iwapo vilabu vikongwe kama Ujamaa, Small Simba, Miembeni na vyenginevyo vitaimarishwa vitaongeza hamasa ya watu wa Zanzibar kwenda viwanjani jambo ambalo litaongeza ushindani kama ilivyokuwa siku za nyuma.
Aidha katibu huyo alikipongeza chama cha soka Zanzibar (ZFA) kwa kurejesha mfumo wa ligi kuu ya pamoja kwa vilabu vya Pemba na Unguja jambo alilosema litasaidia kukuza umoja, ushindani na maelewano miongoni mwa klabu za ligi kuu.
Masoud ambae aliwahi kugombea nafasi ya urais wa Zanzibar na ZFA katika chaguzi zilizopita aliitaka Kamati teule ya chama hicho kukamilisha taratibu za kupatikana kwa viongozi wa chama hicho baada ya viiongozi wake wakuu kujiuzulu na kupelekea Mrajisi wa vyama na klabu za michezo Zanzibar kuunda Kamati ya muda inayosimamia maswala yote ya ZFA taifa.
Mkutano huo wa uchaguzi uliohudhuriwa na wanachama 101 kati ya 126 wa klabu, ulisimamiwa na Kamati maalum ya uchaguzi iliyoongozwa na Makamo Mwenyekiti wa chama cha soka (ZFA) wilaya ya Mjini Juma Mohammed ‘Kocha Juma’ pia wanachama walimtunukia uanachama wa heshima Mkuu wa mkoa wa Mjini Magharibi Ayoub Mohammed Mahmoud kutokana na mchango mkubwa wa kiongozi huyo katika michezo ndani na nje ya mkoa wake.

 Wanachama wakipiga kura wakati wa zoezi la uchaguzi


Makamo Mwenyekiti wa ZFA Wilaya ya Mjini Juma Mohammed (kushoto) akibadilisha mawazo na Sheha wa shehia ya Mkunazini Fuad Abdallah (mwenye kofia) na Makamu Mwenyekiti wa klabu ya Malindi Jaffar Hussein 'Jeff' mara baada ya kuahirishwa mkutano mkuu wa uchaguzi wa klabu ya Malindi.


Wanachama wa klabu ya malindi wakiidhinisha mapendekezo ya kamati tendaji baada ya kuwateua wajumbe wa bodi ya wadhamini, baraza la wazee na meneja wa klabu hiyo mara baada ya kukamilika kwa uchaguzi wa viongozi. 

Sunday, September 2, 2018

BALOZI SEIF KUWATUNZA 'FORM SIX' WA MJINI MAGHARIBI


NA MWINYIMVUA NZUKWI
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla ya ugawaji wa zawadi kwa wanafunzi waliofanya vyema katika mitihani ya kidato cha sita katika mwaka 2018.



Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari ofisini kwake vuga, mkuu wa mkoa wa mjini magharibi Ayoub Mohammed Mahmoud amesema hafla hiyo itafanyika katika viwanja vya kumbu kumbu ya mapinduzi siku ya jumanne Septemba 4, 2018.



Amesema hatua hiyo inafuatia ahadi aliyoitoa wakati alipokutana na wanafunzi wa skuli 17 za mkoa huo waliokuwa wakijiandaa na mitihani mnamo mwezi april mwaka huu ambapo aliahidi kutoa kompyuta mpakato (laptops) watakaopata ufaulu wa daraja la kwanza (Division one) katika mitihani yao.



Amesema ahadi hiyo ililenga kuwahamasisha wanafunzi hao kufanya bidi katika masomo yao na kufanikiwa kupata matokeo mazuri ambayo hajawahi kupatikana katika kipindi kirefu ndani na nje ya mkoa huo.



Mkuu huyo wa mkoa ameeleza kuwa katikam hafla hiyo wanafunzi 96 watapatiwa kompyuta hizo ili ziwasaidie katika shughuli zao za masomo ya juu watakayoendelea nayo.



Ameeleza kuwa katika tukio hilo la kihistoria mbali ya burudani zitakazotolewa na wanafunzi wahitimu, pia wasanii mbali mbali wa kizazi kipya wa Zanzibar na Tanzania bara ambao watatumbuiza ili kuwapongeza wanafunzi hao jambo ambalo litasaidia kuongeza hamasa ya wanafunzi waliopo skuli.



Aidha amewapongeza wadau mbali mbali ikiwemo taasisi ya mimi na wewe kwa kufanikisha upatikanaji wa zawadi hizo  na kwamba wanafunzi wawili waliopata nafasi ya kuingia katika wanafunzi 10 bora kitaifa watapatiwa zawadi ya ziada na ofisi yake ipo tayari kuwasaidia wanafunzi waliofaulu kwa daraja la chini (divisheni 0) pindi wakiwa tayari kurudia mitihani.



Mkuu wa mkoa huyo amewataka wananchi wa ndani na nje ya mkoa huo kujitokeza kwa wingi katika tukio hilo na kuendelea kuunga mnkono juhudi zinazochukuliwa na serikali ya awamu ya saba inayoongozwa na Dk. Ali Mohamed Shein katika kuimarisha sekta na viwango vya elimu nchini.



Katika hatua nyengine RC Ayoub amewataka wanafunzi   waliokosa ufaulu wa daraja la kwanza kutovunjika moyo wa kuendelea na masomo badala yake kuongeza bidii ili kufikia malengo waliojiwekea.



Akizungumza katika sherehe ya kuwaaga wanafunzi wa kidatu cha sita wa skuli ya SOS Mombasa mjini Unguja Ayoub amesema kuna umuhimu kwa wanafunzi hao kujiendeleza ili kupatikana vijana bora zaidi. 



Aidha amewataka wazazi, walezi na walimu wa skuli hiyo kufanya jitihada ya kuhakikisha kuwa wanafunzi wa skuli hiyo wanazingatia zaidi masomo yao ili kupata wasomi zaidi hapa nchini.



Amewapongeza walimu wa skuli hiyo kwa jitihada wanazochukua kwa wanafunzi wao na kuwataka kuendeleza jitihada hizo ili kila mwaka kuwawezesha wanafunzi bora kama ilivyokuwa mwaka huu ambapo skuli hiyom ilifanikiwa kutoa mmoja ya wanafunzi 10 bora kitaifa.



Akisoma risala ya skuli hiyo mwalimu mkuu Ahmed Ali ameeleza kuwepo kwa  changamoto  ya ukosefu wa vifaa mbalimbali  ikiwemo kompyuta na vitabu vya kufundishia na kumuomba mkuu huyo wa mkoa kuwasaidia kutatua changamoto hizo.


KLABU ZA WAANDISHI WA HABARI KUKUTANA ARUSHA


NA MWINYIMVUA NZUKWI
Mkutano Mkuu wa Muungano wa klabu za waandishi wa habari Tanzania (UTPC) unafanyika mkoani Arusha kwa siku mbili kuanzia Septemba 3 ambapo Mkuu wa kitengo cha ushirikano na maendeleo wa Shirika la misaada la Sweden Ulf Kalstig atafungua mkutano huo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa UTPC Aboubakar Karsan mkutano huo utaongozwa na Rais wa Muungano huo Deogratius Nsokolo ambapo pamoja na agenda za kawaida za mkutano huo utaambatana na maadhimisho ya siku ya Daudi Mwangosi ambapo mshindi wa tuzo hiyo atatangazwa na kupatiwa zawadi.

Akizungumzia tuzo hiyo Mkurugenzi huyo alieleza kuwa imewekwa kwa lengo la kukumbuka mchango wa aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa klabu ya waandishi wa habari ya Iringa Daudi Mwangosi aliyeuawa akiwa kazini wakati wa machafuko ya kisiasa kati ya polisi na wafuasi wa chama cha demokrasia na maendeleo (CHADEMA) na kutajwa kuwa ni tukio la kwanza kutokea nchini Tanzania.

“Tuzo hii inatolewa kwa mwandishi au taasisi ya habari kwa kuzingatia umahiri na umakini wa chombo hicho katika kutoa taarifa zenye kuleta mabadiliko chanya kwa jamii na kuendeleza tasnia ya habari nchini”, alieleza Karsan.

Katika mwaka uliopita kampuni ya Clouds Media Group ilitwaa tuzo hiyo pamoja na fedha taslim shilingi milioni 10 za Tanzania kutokana na uwezo waliouonesha kukabiliana na changamoto za weledi katika uandishi wa habari. 

Alisema klabu wajumbe wa mkukano huo kutoka klabu zote 28 za waandishi wa habari Tanzania zinashiriki mkutano huo utakaofanyika katika hoteli ya Lush Garden ambapo taarifa mbali mbali zinazohiusiana na taasisi hiyo na tasnia ya habari kwa ujumla zitawasilishwa na kujadiliwa.

Mkurugenzi huyo alieleza kuwa miongoni mwa agenda za mkutano huo ni pamoja na taarifa ya utekelezaji wa shughuli za muungano huo kwa mwaka uliopita hadi mwezi uliopita na kupitisha makadirio ya mipango na matumizi kwa mwaka ujao.

“Kwa ujumla maandalizi yamekamilika kwani toka mwanzoni mwa mwaka huu sekretarieti ilikuwa Arusha kwa maandalizi ya vikao vya kamati na bodi ya wadhamini ambavyo vimefanyika kwa mafanikio makubwa”, alieleza Karsan.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi akiwa njiani kuelekea Arusha mmoja ya wajumbe wa mkutano huo Katibu mkuu wa klabu ya waandishi wa habari Zanzibar (ZPC) Faki Mjaka alieleza kuridhishwa kwake na maandalizi ya mkutano huo kutokana na kupatiwa taarifa zote mapema.

“Tunaamini mkutano wa mwaka huu utakuwa na mafanikio makubwa kwani licha ya kuwa na shughuli nyingi, kutakuwa na matumizi mazuri ya muda hasa ikizingatiwa wajumbe wote tulipatiwa nyaraka zitakazowasilishwa mkutanoni mapema na kupata muda wa kuzijadili na wajumbe wenzetu ambao hawatokuwepo Arusha”, alisema Mjaka.

Katika mkutano huo ZPC kama zilivyo klabu nyengine inawakilishwa na mwenyekiti wa klabu hiyo Abdallah mafaume amabae bia ni mjumbe wa bodi ya UTPC na Mweka hazina wake Halima Tamim ambao waliondoka mjini Zanzibar Jumamosi wa wiki iliyopita kuelekea Arusha kwa ajili ya mkutano huo.

Monday, August 20, 2018

DK. BASHIRU AHIMIZA CCM KUJITEGEMEA, AONYA UBADHIRIFU NA MATUMIZI MABAYA YA MALI ZA CHAMA

NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Dk.Bashiru Ally amesema Chama hicho kinadhibiti mianya ya ubadhilifu wa rasilimali fedha na mali zake ili kijitegemee kiuchumi.
 Alisema endapo rasilimali hizo zitatumika vizuri na kuanzishwa kwa miradi mingine mikubwa ya uzalishaji wa kipato katika ngazi mbali mbali za chama na jumuiya kwa  kuwanufaisha  wanachama wote badala ya watu wachache.
Kauli hiyo aliitoa jana katika mwendelezo wa ziara yake kisiwani Pemba wakati akizungumza na viongozi na wanachama wa Chama cha Mapinduzi wa Mikoa Miwili katika ukumbi wa Fidel Castro uliopo, Mkoa wa Kusini Pemba.
Dk.Bashiru alieleza kuwa lengo la kusimamia dhana ya ukuaji wa uchumi ndani ya chama kupitia vyanzo vyake vya mali na fedha ni kukiondosha chama katika mazoea ya kutegemea ufadhili wa watu wenye fedha wanaokuwa na malengo ya kujinufaisha wenyewe kisiasa.
Pia aliyataja malengo mengine kuwa ni uimarishaji wa maslahi ya watumishi wa CCM na jumuiya zake kwani bado maslahi yao ni ya kiwango cha chini ambayo hayaendani na hadhi ya taasisi yenyewe.
“ Kwa miaka mingi chama chetu kimeondoka katika misingi ya kujitegemea na badala yake kujitokeza kwa watu wenye fedha kukichangia chama wakati wa uchaguzi na mazoezi mengine ya kitaasisi, sasa katika mageuzi haya ya kimuundo tuna dhamira ya chama chetu kukiondosha uko na tukaweza kutumia mali zetu wenyewe kujiendesha kitaasisi.” Alifafanua Dk.Bashiru.
Alieleza kuwa malengo hayo yakifanikiwa utakuwa ni ushindi mkubwa kwa wanachama wa CCM wote kwani tabia za rushwa na makundi ya kusaka nafasi za uongozi kwa kutumia fedha yatakuwa yamedhibitiwa.
Aliwataka viongozi wote wa taasisi hiyo kuunga mkono malengo hayo kwa kuhakikisha wanapunguza matumizi holela ya fedha na badala yake waanzishe miradi itakayowasaidia kujiendesha ili kulinda heshima na hadhi ya CCM mbele ya jamii.
Pamoja na hayo alizitaka jumuiya zote hasa ya umoja wa vijana (UVCCM) kuhakikisha wanakuwa wabunifu kwa kutumia rasilimia walizonazo kwa kuanzisha miradi mikubwa ya kilimo, uvuvi na viwanda vidogo vidogo ili vijana wajiajiri wenyewe.
Katibu Mkuu huyo Dk.Bashiru aliweka wazi msimamo wa Chama Cha Mapinduzi kuwa wale wote waliohusika na kutapeli na kujimilikisha mali za taasisi hiyo kinyume na utaratibu wote watachukuliwa hatua za kisheria.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Mabodi alisema wanachama wote wana haki ya kuunga mkono mambo mema yanayotekelezwa na taasisi hiyo kwa nia ya kuongeza ufanisi.
Alisema wakati wa vyama vya ukombozi vya ASP na TANU viongozi wa wakati huo walifanikiwa kupanga mambo ya maendeleo yaliyodumu kwa muda mrefu kutokana na umoja na mshikamano waliokuwa nao hasa katika masuala ya kuvijenga kimaendeleo vyama vyao.
Dk. Mabodi alieleza kuwa suala la uzalendo katika kusimamia maslahi ya kitaifa ni jambo muhimu hasa kwa viongozi wanaoaminiwa na kupewa dhamana za kuongoza jamii.
Akizungumzia ushindi wa CCM visiwani Zanzibar mwaka 2020 alisema mpaka sasa Zanzibar hakuna upinzani bali kuna vikundi vidogo vidogo vya watu wanaojivisha joho la upinzani wakati wao ni madalali wa kisiasa waliofilisika kifikra.
Naibu Katibu Mkuu huyo alisema CCM itashinda kisayansi kutokana na serikali zake kutekeleza mahitaji ya wananchi wa mijini na vijijini kupitia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015/2020.

BALOZI SEIF AWATIA MOYO WANAFUNZI KUSAKA ELIMU KWA MAENDELEO YAO, TAIFA


NA MWINYIMVUA NZUKWI
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema wakati Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inazidi  kuimarisha miundombinu ndani ya Sekta ya Elimu, wanafunzi wanalazimika kujikita kutafuta elimu itakayowajengea maisha ya furaha wao na familia zao.

Alisema wanafunzi wakisoma kwa juhudi, maarifa na kufikia kiwango cha elimu ya juu ya katika vyuo vikuu watakuwa na nafasi kubwa ya kujihakikishia za ajira zilizozoweya kufanywa na Wataalamu wa Kigeni.

Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati akisalimiana na wananchi wa kijiji cha Mwambe katika ziara yake ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa majengo mapya ya skuli za sekondari zinazojengwa kwa pamoja kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mshirika wa Maendeleo Mfuko wa Kimataifa wa jumuiya ya maendeleo ya petroli ulimwenguni (OPEC).

Alisema Taifa linahitaji wataalamu wake watakaotokana na wanafunzi ambao wanapaswa kuweka malengo ya kusoma kwa bidii kwa lengo la kuwahudumia Wananchi kwa kiwango cha uzalendo zaidi.

Balozi Seif aliwahimiza watoto wa kike nchini kusoma kwa ziada ili zile kazi za Kitaalamu zinazofanywa na Wanaume akatolea mfano za huduma za Afya wazifanye wenyewe katika azma ya kulinda na kuheshima mila, sila, Tamaduni na hata imani za Kidini.

Katika kutilia mkazo nafasi ya mtoto wa kike kusoma kwa malengo Balozi Seif  ameagiza Wazazi wowote watakaohusika na kitendo cha kuwaozesha  Watoto wao wa Kike wakati wanasoma Uongozi wa Serikali ya Mkoa usimamie katika kuona Vyombo vya Dola vinawachukulia hatua za Kisheria mara moja Wazazi hao ikiwa ni pamoja na kuwaweka ndani.

“Jamii inahitaji kuwa na Ewataalamu wa Kike ambao watahusika kushughulikia huduma zinazofanywa na Wanaume Kitaalamu ambazo hazistahiki kutokana na Tamaduni na Imani wa Kidini”. Alisisitiza Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alionya kwamba tabia hii inayoonekana kuendelea kwa baadhi ya Mitaa Nchini inarejesha nyuma maendeleo ya Mtoto wa kike aliyekandamizwa kwa muda mrefu kutokana na mfume Dume uliozoeleka kwa kipindi kirefu kilichopita.

Alieleza kwamba matukio hayo  ni miongoni mwa matendo yanayoonyesha muendelezo wa unyanyasaji wa Kijinsia uliomgubika Mtoto wa Kike unaopswa kuondolewa hivi sasa kutokana na mabadiliko makubwa ya Sayansi na Teknolojia yaliyoanza kumfunulia njia Mtoto wa Kike.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwapongeza Wazazi na Wananchi wa Mwambe kutokana na mwamko wao mkubwa wa kuwapelekea Skuli Watoto wao jambo ambalo linafaa kuigwa na Wazazi wengine Nchini.

Alisema Mikondo Mitatu ya Wanafunzi wanaoingia na kusoma kwenye Skuli ya Mwambe ni ushahidi tosha wa Wazazi hao kutambua uhumihu wa Elimu licha ya Idadi kubwa ya Wakaazi wake ambao Watoto wake walikuwa wakipenda sana kufanya kazi za U vuvi.

Mapema Mkuu wa Mkoa Kusini Pemba Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdullah alisema ziara zake za Majimbo Tisa akijumisha na maskuli yaliyombo kwenye Majimbo hayo  zimemthibitishia kukithiri kwa utoro kwenye Skuli nyingi za Mkoa huo.

Mh. Suleiman alisema bila ya Elimu hakuna Daktari, Mwalimu na hata Mhandisi, na katika kutambua umuhimu huo Serikali ya Mkoa imeamua kwa makusudi Mzazi ambae mtoto wake atatoroka Skuli atakamatwa na kushtakiwa kwa kosa la kumkosesha haki ya Elimu Mtoto wake.

Mkuu huyo wa Mkoa Kusini Pemba amewapongeza Swananchi wa Mwambe  kwa uwamuzi wao wa kuimarisha Ulinzi Shirikishi katika Shehia yao kitendo kilicholeta faraja na Amani katika eneo hilo.

Mh. Hemed alisema Kijiji cha Mwambe kilikuwa kikitajika kwa vitendo vya wizi wa mazao na ulevi vilivyosababishwa na baadhi ya Vijana waliokosa muelekeo kutokana na kukosa Taaluma ya Kimaisha.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alikagua Maendeleo ya ujenzi wa Skuli za Sekondari za Mwambe na Wara Ndugukitu na kuridhika na hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa Skuli hizo.

Balozi Seif aliwahimiza Wahandisi wa ujenzi wa Majengo hayo kuongeza jitihada ili kuhakikisha kwamba Miradi hiyo inakamilika katika wakati uliowekwa pamoja na kiwango cha hadhi inayokubalika ya kimajengo.

Mapema asubuhi Balozi Seif  alikagua Bara bara mpya inayojengwa kwa kiwango cha Lami katika Kijiji cha Ole hadi Kianga inayokadiriwa kuwa na urefu wa Kilomita 10.

Afisa Mdhamini Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Hemed Baucha alimueleza Balozi Seif  kwamba kipande kilichobaki cha Bara bara hiyo kimechelewa kumalizika kutokana na Nyumba Nne zilizolazimika kuvunjwa kupisha ujenzi huo ambazo mwanzoni hazikuwamo.

Hata hivyo  Baucha alisema Wataalamu wa Wizara hiyo wameshafanya tathmini na taratibu za malipo ya Fidia kwa Wananchi wanaohusika na Nyumba hizo zikamilike.
Balozi Seif alipongeza Wataalamu wa Idara ya Utunzaji na Ujenzi wa Bara bara {UUB} kwa kazi kubwa na nzuri waliyoifanya ambapo Serikali Kuu imeridhika na Taaluma waliyonayo Wahandisi hao wazalendo.

Alisema wakati Serikali inajitahidi kuangalia uwezekano wa kuwapatia vifaa zaidi vya ujenzi Wahandisi wa Idara hiyo lakini bado wana dhima ya kuhakikisha kazi wanazopewa wanazikamilisha kwa wakati muwafaka.

Wakati huo huo Balozi Seif  alifika Pagali kuangalia maendeleo ya ujenzi wa Nyumba za Makaazi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Ujenzi unaofanywa  chini ya Wahandisi wa Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo Zanzibar (KMKM).

Mshauri Muelekezi Mkuu  wa Ujenzi huo Mhandisi Ramadhan Mussa Bakari alimueleza Balozi Seif kwamba Ujenzi huo ulioanza Rasmi Juni 23 mwaka huu unaendelea vyema licha ya changamoto ya upatikanaji wa huduma za Maji.

Mhandisi Ramadhan alisema ili kazi hiyo iendelee kama ilivyopangwa na kukusudiwa upo umuhimu wa kuchimbwa Kisima ndani ya eneo hilo ili kuwa na uhakika wa upatikanaji wa huduma hiyo muhimu.

Akikagua baadhi ya Majengo ya Nyumba hizo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliridhika na kiwango pamoja na uharaka wa Wahandisi hao wanaouendeleza na kujenga matumaini yake ya kumalizika Mradi huo kwa wakati uliopangwa.

PICHA NA MAELEZO YAKE
Wananchi wa Kijiji cha Mwambe kisiwani Pemba wakisimkiliza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi (hayupo pichani) baada ya kukagua Mradi wa Ujenzi wa Skuli ya Sekondari ya Mwambe inayojengwa kijijini hapo.


Mhandisi wa Ujenzi wa Skuli ya Sekondari ya Wara Ali Khamis Shaibu (alienyoosha mkono) akitoa maelezo kwa Balozi Seif (mwenye miwani) kuhusiana na maendeleo ya ujenzi wa majengo ya Skuli hiyo unaokwenda kwa wakati uliopangwa. Wa kwanza kulia ni Naibu Waziri katika ofisi ya Makamu wa pili wa Rais Mihato Juma N'hunga.

Balozi Seif Ali Iddi (kushoto) akimchum mtoto Sulhia Ali wa Kijiji cha Mwambe huku Mama Mzazi wa mtoto huyo (kulia) akitabasamu mara baada ya kusalimiana na wananchi wa kijiji hicho kukagua maendeleo ya ujenzi wa skuli ya Sekondari ya Wara.


Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Maalim Abdulla Mzee Abdulla (wa pili kulia) akiteta jambo na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  kwenye majengo ya Skuli Mpoya ya Sekondari inayojengwa katika Kijiji cha Wara Chake Chake Pemba.

Balozi Seif akikagua baadhi ya Majengo ya nyumba za makaazi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar zinazojengwa katika eneo la Pagali Wilaya ya Chake chake Pemba.
PICHA KWA HISANI YA OMPR.

Sunday, August 19, 2018

"HATUKURUPUKI KUWEKEZA KATIKA MIRADI YA MAENDELEO" - DK. SHEIN


NA MWINYIMVUA NZUKWI, ZANZIBAR

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameeleza kuwa uwekezaji unaofanywa katika maeneo mbali mbali unalenga kukuza uchumi na kunguza tatizo la ajira kwa wananchi wa Zanzibar.

Akizindua biashara katika mji mdogo wa Fumba unaojengwa na kampuni ya CPS-lives katika shehia ya Nyamanzi wilaya ya Magharibi ‘B’ Unguja, Dk. Shein alisema hatua hiyo inachukuliwa na kutekelezwa kwa umakini kati ya serikali na sekta binafsi.

Alisema katika kuekeleza dhana ya uhusiano kati ya serikali na sekta binafsi (PPP), serikali yake imeweka miundombinu rafiki ya kuiwezesha sekta binafsi kutekeleza miradi mbali mbali ikiwemo ya makaazi badala ya serikali kutekeleza miradi hiyo.



Alisema miongoni mwa hatua hizo ni pamoja na kuanzisha ukanda wa maeneo huru ya kiuchumi na kuipa juklumu mamlaka ya ukuzaji vitega uchumi Zanzibar (ZIPA) inatekeleza mipango mbali mbali na ilani ya uchaguzi wa CCM ili kuongeza kasi ya maendeleo ya jamii.

Aliitaja mipango hiyo kuwa ni dira ya Maendeleo 2020, mkakati wa kukuza uchumi na kupunguza umaskini Zanzibar (MKUZA III) na ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambayo ilirithi ilani ya chama cha Afro Shiraz Party (ASP) iliyoitumia wakati wa uchaguzi mkuu wa Zanzibar wa mwaka 1961 na 1962.

 “ASP iliweka ahadi ya kujenga na kuyaendeleza makaazi ya wananchi wa Zanzibar ambao wengi wao walikuwa na makazi duni azma ambayo inaendelezwa na CCM (Chama Cha Mapinduzi) baada ya mapinduzi ya 1964 na hadi sasa kupitia ilani ya uchaguzi ambayo zinaelekeza serikali zake kwa kushirikiana na sekta binafsi”, alieleza Dk. Shein.

Alisema licha ya uwezo mdigo ilionao serikali yake itaendelea kujenga na kuiiimarisha miji midogo na mji mikongwe wa Zanzibar na kutoa ushirikiano na wawekezaji sambamba na kuzingatia usafi ili kuwavutia wageni na kujikinga na maradhi.



Aidha Dk. Shein aliipongeza kampuni ya CPS-Lives kwa kufanikisha ujenzi wa mradi kwa kasi na kiasi cha kukamilisha nyumba hizo katika kipindi kifupi na kwa kutumia teknolojia inayozingatia uhifadhi wa mazingira.

“Tulipokuja kuuwekea jiwe la msingi mwezi Januari mwaka huu hali haikuwa hivi. Hivyo sina budi kuwapongeza wawekezaji wa mradi huu kwa kutimiza ahadi waliyoiweka wakati ule kuwa wangekabidhi sehamu ya nyumba hizi kwa wateja wao na leo tumeshuhudia wateja 60 waliokamilisha malipo wamekabidhiwa nyumb zao”, alisema Rais Dk. Shein.

Mapema akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar Dk. Khalid Salum Mohammed alisema mradi huo ni miongoni mwa miradi ya uwekezaji inayotekelezwa  kwa faida nchini kutokana kodi inayolipwa serikalini na faida nyengine ikiwemo ya upatikanaji wa ujuzi.

Alisema mradi huo una lenga kuweka haiba ya Zanzibar na kuongeza fursa za ajira kwa wananchi, utasaidia kupunguza msongamano katika maeneo ya mji wa Zanzibar.

“Wawekezaji katika mradi huu ni walipa kodi wazuri na wametoa ajira za kudumu 250 na ajira za muda zaidi ya 500 sambamba na fursa za mafunzo ya utunzaji wa mazingira jambo ambalo limesaidia kutimiza malengo ya kuhimiza uwekezaji nchini mwetu”, alisema Dk. Khalid.

Nae Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya CPS-Lives Sebastian Dietzold alimshukuru Dk. Shein kwa kuendelea kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa mradi huo na kuahidi kuwa kampuni yake itaendelea kushirikiana na serikali ya mapinduzi Zanzibar.

Amesema toka kuasisiwa kwa mradi huon jumla ya nyumba 400 za awamu ya kwanza zimeshauzwa na 60 katin ya hizo zimekabidhiwa kwa wenyewe katika uzinduzi huo kazi ambayo inatarajiwa kufanyika kila mwezi.

“Mradi wetu umekuwa na manufaa makubwa sio kwetu bali pia kwa vijiji vya karibu yetu vya nyamanzi na dimani kwa kusaidia upatikanaji wa huduma za jamii i pamoja na kuwapatia ajira watu kutoka maeneo mbali mbali ya Zanzibar”, alieleza.


Aliongeza kuwa baada ya kukamilika kwa awamu ya kwanza ya ujenzi huo baadae mwaka huu, awamu ya tatu ya utekelezaji wa mradi huo utaanza ambao utahusisha ujenzi wa majengo ya huduma za jamii na viwanda.

Awali Mkurugenzi mtendaji wa mamlaka ya ukuzaji vitega uchumi Zanzibar (ZIPA) Salum Khamis Nassor alieleza kuwa uendelezaji wa eneo hilo ni sehemu ya utekelezaji wa mpango ulioasisiwa na serikali ya awamu ya 5 iliyoyatangaza maeneo ya Fumba na Micheweni kuwa ni maeneo huru ya uchumi mwaka 1992.

Alieleza kuwa uamuzi huo ulilenga kuimarisha uchumi wa Zanzibar kwa kushirikiana na sekta binafsi kazi ambayo inaendelea kutekelezwa na mamlaka yake kwa kuzingatia sera na sheria za nchi.

Makabidhiano ya nyumba hizo umekuja baada ya kukamilika kwa awamu ya kwanza ya ujenzi huo ambapo nyumba 400 za awali kati ya 2000 zilizokusudiwa kujengwa katika awamu hiyo inayotarajiwa kukamilika baadae mwaka huu.
Mwisho.