Na Mwinyimvua Nzukwi
Kampuni ya ROM Solution imetoa msaada
wa vyakula na fedha taslim kwa familia za askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ)
waliofariki wakiwa katika ulinzi wa amani nchini DRC mwanzoni mwa mwezi huu.
Hafla ya makabidhiano hayo ilifanyika
katika ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, kampuni hiyo ilikabidhi
misaada ya chakula na vifaa vya mayumizi ya nyumbani kwa familia kwa
wawakilishi wa familia za askari 9 waliozikwa Zanzibar unaokisiwa kufikia
shilingi milioni kumi na thelasini elfu.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi
msaada huo Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo George Alexandru alisema wameamua
kutoa msaada huo ili kuungana na wananchi wa Tanzania katika kupunguza ukubwa
wa msiba huo ambao alidai haukupaswa kutokea kutokana na kazi iliyowapeleka
askari hao nchini Congo.
"Vifo vya askari 14 vilitokea wakiwa
wanalinda amani sio vitani. Ni jambo la kushitua sana na ndio maana tulipopata
hii taarifa tukaona haja ya kufanya jambo lolote la kusaidia hasa tukizingatia
jukumu walilokuwa nalo askari hao linafanana na shughuli zetu", alisema
Alexandru ambaye kampuni yake inajihusisha na uuzaji na ufungaji wa kamera za
ulinzi.
Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Uyoub
Mahmoud Mohamed aliuelezea msaada huo kuwa umekuja kwa wakati muafaka ambao
utasaidia kupunguza majonzi kwa familia za askari hao.
Alisema serikali ya Zanzibar na Tanzania
zinafarajika kuona mwitiko wa sekta binafsi katika msiba huo uliohusisha jambo
linaloonesha kukubalika kwa kazi za vikosi vya ulinzi na usalama nchini.
"Wenzetu hawa walienda nchini
DRC sio kulinda amani ya nchi hiyo tu bali pia ya wananchi wa Tanzania na Afrika
kwa ujumla hivyo inapotokea watu wanapoguswa na vifo au madhara waliyoyapata vinaongeza hamasa ya wapiganaji waliobakia
lakini pia familia za walioondokewa na wapendwa wao", alisema Ayoub.
Aidha alieleza kuwa jitihada zinafanywa
kati ya kampuni hiyo na jeshi ili kuhakikisha msaada kama huo unatolewa kwa familia
5 za askari waliozikwa Tanzania bara jambo ambalo alisema litatekelezwa na
kampuni hiyo.
Nae Kaimu Kamanda wa Brigedi ya Nyuki Kanali
Said Khamis Said alisema jeshi limepokea msaada huo kwa furaha na kuahidi kuwa
litaendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia misingi ya uzalendo na
uwajibikaji wa pamoja ili kuhakikisha tanzania na afrika inakuwa na amani.
"Sisi kama wapiganaji tumekuwa
tukifarajika kila tunapoona wananchi wenzetu wameguswa na kupotea kwa maisha ya
wenzetu hawa jambo linalotuongezea nguvu ya kuitumikia nchi yetu kwa uzalendo
wa hali ya juu", alisema Kanali Said.
Akitoa shukrani kwa niaba ya wenzake
mmoja ya wanafamilia za marehemu aliishukuru kampuni hiyo na serikali kwa
kuendelea kushirikiana nao katika mambo mbali ya kifamilia pamoja na misaada ya
hali na mali.
Mkuu wa mkoa wa Mjini wa Magharibi Unguja Ayoub Mohammed Mahmoud (akimkabidhi mmoja ya wanafamilia za askari wa jeshi la wananchi wa tanzania (JWTZ) msaada wa wa vyakula na fedha taslimu uliotolewa na kampuni ya ROM Solution Ltd ya Zanzibar kwa lengo la kuwafariji.
Mkuu wa mkoa wa Mjini wa Magharibi Unguja Ayoub Mohammed Mahmoud (kushoto) akimkabidhi mwanafamilia wa askari wa jeshi la wananchi wa Tanzania (JWTZ) marehemu Nassor Daud Iddi msaada wa vyakula na fedha taslimu uliotolewa na kampuni ya ROM Solution ya Zanzibar kwa lengo la kuwafariji. Wa tatu kutoka kushoto ni Afisa Mtendaji mkuu wa kampuni ya ROM Solution George Alexendru. Anaeshuhudia alivaa miwani ni Katibu Tawala wa mkoa wa Mjini Magharibi Hamida Mussa Khamis.
Kaimu Kamanda ya Brigedi ya Nyuki Kanali Said Khamis Said (wa kwanza kushoto) akimshuhudia Mkuu wa mkoa wa Mjini wa Magharibi Unguja Ayoub Mohammed Mahmoud (kushoto) akimkabidhi mmoja ya wanafamilia askari wa jeshi la wananchi wa Tanzania (JWTZ) aliefariki nchini DRC - Congo bahasha yenye fedha taslimu uliotolewa na kampuni ya ROM Solution ya Zanzibar kwa lengo la kuwafariji kutokana na msiba huo.
No comments:
Post a Comment