Sunday, December 24, 2017

MAPINDUZI KUZINDUA MIRADI 49, SHILINGI BILIONI 1.2 KUTUMIKA

Na Mwinyimvua Nzukwi
MIRADI 49 ya kiuchumi, maendeleo na ustawi wa jamii inatarajiwa kuzinduliwa na kuwekewa mawe ya msingi wakati wa shamra shamra za maadhimisho ya miaka 54 ya mapinduzi ya Zanzibar.

Makamu wa pili wa rais wa Zanzibar balozi seif ali iddi ameeleza hayo baada ya kikao cha cha Halmashauri ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa anayoiongoza.

Alisema miongoni mwa miradi hiyo, 33 itazinduliwa rasmi baada ya kukamilika wakati miradi mingine 16 inatarajiwa kuwekewa Mawe ya msingi inayojumuisha miradu ya taasisi za umma, miradi ya Jamii sambamba na  ya Wawekezaji vitega uchumi.

Katika kikao hicho kilichofanyika katika makumbusho ya kasri la Mfalme,   Balozi Seif na wajumbe wa halmashauri hiyo walifikia maamuzi ya kuipunguza miradi mitatu iliyoainishwa katika ratiba ya sherehe hizo baada ya kubaini kuwa haikufikia kiwango kinachokubalika.

Kaimu Kamanda wa Brigedi ya Nyuki Kanali Said Khamis Said ambae ni mjumbe wa kikao hicho, alisema kutakuwa na mabadiliko katika gwaride la mwaka huu kutokana na kilele cha sherehe hizo kuangukia katika siku ya Ijumaa hivyo gwaride hilo litamalizika mapema ili kutoa fursa kwa wananchi na viongozi kujiandaa na ibada ya sala ya Ijumaa.

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Dk. Idriss Muslim Hijja alisema miradi yote iliyopendekezwa kuingizwa katika maadhimisho ya Mwaka huu imefuatiliwa na kutolewa taarifa kwa  sekriterieti  na kufanyiwa marekebisho kwa kiwango kinachohitajika kuingizwa katika ratiba ya sherehe.

Katika hatua nyengine waziri wan chi ofisi ya makamo wa pili wa rais wa Zanzibar Mohammed Aboud Mohammed amewaambia waandishi wa habari ofisini kwake jana kuwa wastani wa shillingi billion 1.2 zinatarajiwa kutumika kwa ajili ya maadhimisho  ya sherehe za miaka 54 ya mapinduzi matukufu ya Zanzibar yatakayofikia kilele chake Januari 12, mwakani.

Aboud amesema serikali imepanga kutumia kiasi hicho cha fedha kulingana na umuhimu wa siku hiyo ambapo  kuelekea katika kilele chake shughuli mbalimbali za kitaifa na kijamii zitafanyika  zikiwemo za kuwekewa mawe ya msini na kuzinduliwa kwa  miradi ya maji, majengo ya skuli, Umeme na Barabara ambapo viongozi wa SMZ na SMT  wanatarajiwa kuizindua kulingana na ratiba zitakazopangwa.

Aidha waziri Aboud alisema katika siku ya kilele serikali itaeleza jinsi ilivyopiga hatua katika kufanikisha huduma muhimu za kijamii na maendeleo kazi ambayo ni mwendelezo wa malengo ya mapinduzi matukufu ya Zanzibar yaliyofanyika  mwaka 1964.

Kilele cha sherehe hizo kinatarajiwa kuadhimishwa 12 Januari Uwanja wa Amaan ambapo viongozi mablimbali wa kitaifa na kimataifa wanatarajiwa kuhudhuria akiwemo Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohammed Shein atakaekuwa mgeni rasmi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idi (kulia) akiongoza kikao cha halmashauri ya sherehe za kitaifa katika ukumbi wa Baraza la Mapinduzi uliopo katika makumbusho ya Kasri ya Mfalme, Forodhani mjini Unguja. (Picha kwa hisani ya OMPR)

Monday, December 18, 2017

FAMILIA ZA WAHANGA WA DRC ZAFARIJIWA

Na Mwinyimvua Nzukwi
Kampuni ya ROM Solution imetoa msaada wa vyakula na fedha taslim kwa familia za askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) waliofariki wakiwa katika ulinzi wa amani nchini DRC mwanzoni mwa mwezi huu.

Hafla ya makabidhiano hayo ilifanyika katika ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, kampuni hiyo ilikabidhi misaada ya chakula na vifaa vya mayumizi ya nyumbani kwa familia kwa wawakilishi wa familia za askari 9 waliozikwa Zanzibar unaokisiwa kufikia shilingi milioni kumi na thelasini elfu.

Akizungumza mara baada ya kukabidhi msaada huo Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo George Alexandru alisema wameamua kutoa msaada huo ili kuungana na wananchi wa Tanzania katika kupunguza ukubwa wa msiba huo ambao alidai haukupaswa kutokea kutokana na kazi iliyowapeleka askari hao nchini Congo.

"Vifo vya askari 14 vilitokea wakiwa wanalinda amani sio vitani. Ni jambo la kushitua sana na ndio maana tulipopata hii taarifa tukaona haja ya kufanya jambo lolote la kusaidia hasa tukizingatia jukumu walilokuwa nalo askari hao linafanana na shughuli zetu", alisema Alexandru ambaye kampuni yake inajihusisha na uuzaji na ufungaji wa kamera za ulinzi.

Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Uyoub Mahmoud Mohamed aliuelezea msaada huo kuwa umekuja kwa wakati muafaka ambao utasaidia kupunguza majonzi kwa familia za askari hao.

Alisema serikali ya Zanzibar na Tanzania zinafarajika kuona mwitiko wa sekta binafsi katika msiba huo uliohusisha jambo linaloonesha kukubalika kwa kazi za vikosi vya ulinzi na usalama nchini.

"Wenzetu hawa walienda nchini DRC sio kulinda amani ya nchi hiyo tu bali pia ya wananchi wa Tanzania na Afrika kwa ujumla hivyo inapotokea watu wanapoguswa na vifo au madhara waliyoyapata  vinaongeza hamasa ya wapiganaji waliobakia lakini pia familia za walioondokewa na wapendwa wao", alisema Ayoub.

Aidha alieleza kuwa jitihada zinafanywa kati ya kampuni hiyo na jeshi ili kuhakikisha msaada kama huo unatolewa kwa familia 5 za askari waliozikwa Tanzania bara jambo ambalo alisema litatekelezwa na kampuni hiyo.

 Nae Kaimu Kamanda wa Brigedi ya Nyuki Kanali Said Khamis Said alisema jeshi limepokea msaada huo kwa furaha na kuahidi kuwa litaendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia misingi ya uzalendo na uwajibikaji wa pamoja ili kuhakikisha tanzania na afrika inakuwa na amani.

"Sisi kama wapiganaji tumekuwa tukifarajika kila tunapoona wananchi wenzetu wameguswa na kupotea kwa maisha ya wenzetu hawa jambo linalotuongezea nguvu ya kuitumikia nchi yetu kwa uzalendo wa hali ya juu", alisema Kanali Said.

Akitoa shukrani kwa niaba ya wenzake mmoja ya wanafamilia za marehemu aliishukuru kampuni hiyo na serikali kwa kuendelea kushirikiana nao katika mambo mbali ya kifamilia pamoja na misaada ya hali na mali.

Mkuu wa mkoa wa Mjini wa Magharibi Unguja Ayoub Mohammed Mahmoud (akimkabidhi mmoja ya wanafamilia za askari wa jeshi la wananchi wa tanzania (JWTZ) msaada wa wa vyakula na fedha taslimu uliotolewa na kampuni ya ROM Solution Ltd ya Zanzibar kwa lengo la kuwafariji.


Mkuu wa mkoa wa Mjini wa Magharibi Unguja Ayoub Mohammed Mahmoud (kushoto) akimkabidhi mwanafamilia wa askari wa jeshi la wananchi wa Tanzania (JWTZ) marehemu Nassor Daud Iddi msaada wa vyakula na fedha taslimu uliotolewa na kampuni ya ROM Solution ya Zanzibar kwa lengo la kuwafariji. Wa tatu kutoka kushoto ni Afisa Mtendaji mkuu wa  kampuni ya ROM Solution George Alexendru. Anaeshuhudia alivaa miwani ni Katibu Tawala wa mkoa wa Mjini Magharibi Hamida Mussa Khamis. 


Kaimu Kamanda ya Brigedi ya Nyuki Kanali Said Khamis Said (wa kwanza kushoto) akimshuhudia Mkuu wa mkoa wa Mjini wa Magharibi Unguja Ayoub Mohammed Mahmoud (kushoto) akimkabidhi mmoja ya wanafamilia askari wa jeshi la wananchi wa Tanzania (JWTZ) aliefariki nchini DRC - Congo bahasha yenye fedha taslimu uliotolewa na kampuni ya ROM Solution ya Zanzibar kwa lengo la kuwafariji kutokana na msiba huo.                                                                                               

Wednesday, December 6, 2017

DK. SHEIN ATEUA, ABADILISHA WATENDAJI WA SMZ

Na Mwinyimvua Nzukwi
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amefanya uteuzi na kuwabadilisha nafasi baadhi ya viongozi wa Taasisi mbali mbali za Serikali ya Zanzibar akiwemo aliyekua Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Mwanajuma Majid Abdallah.

Mwanajuma alieshika hatamu za uongozi wa Mkoa huo kwa muda mrefu, ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu katika Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Wanawake, Vijana na Watoto anayeshughulikia masuala ya Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto.

Kufuatia mabadiliko hayo, Dk. Shein amemteua Hemed Suleiman Abdullah kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kusini- Pemba, Hassan Khatib Hassan kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kusini,  Unguja kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Dk. Muslih Hija alieteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa wizara ya nchi ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

Aidha katika mabadiliko hayo Rais pia amemteua aliekuwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Magharibi B Hamida Mussa Khamis kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mjini Magharibi na Mohamed Abdulla Ahmed kuwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Magharibi.

Wengine walioteuliwa ni Daima Mohamed Mkalimoto alieteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Mipango, Sera na Utafiti katika  Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora kuchukua nafasi ya Abdulla Issa Mgongo anaekua  Mkurugenzi wa Idara ya Mipango, Sera na Utafiti katika Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ.


Aliekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar (BTMZ) Sharifa Khamis Salim ameteuliwa kuwa Kamishna wa Idara ya Michezo katika Wizara ya Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo na Mohamed Issa Mugheir ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu ya  Zanzibar uteuzi ambao umeanza  Disemba 5, mwaka huu.

RC AYOUB ATAKA MATENGENEZO YA BARABARA, AAGIZA KUZUIWA LESENI YA JAMBO BAR AND GUEST HOUSE

Na Mwinyimvua Nzukwi
Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Ayoub Mohammed Mahmoud ametoa wiki moja kwa Uongozi wa Baraza la Manispaa ya Mjini, Idara ya Utunzaji na Uendelezaji, barabara Zanazibar (UUB) na kampuni ya ZECON kuhakikisha wanaifanyia matengenezo barabara ya kwa Biziredi - Misufini ambayo imechimbwa kwa ajili ya kupitisha waya wa umeme na kusababisha usumbufu kwa watumiaji wake na wakaazi wa maeneo hayo.

RC Ayoub alitoa agizo hilo katika siku ya sita ya ziara zake ndani ya mkoa huo kuzungumza na wananchi kusikiliza kero changamoto zinazowakabili ambapo wananchi wanaoishi katika eneo hilo walilalamikia athari zilizoachwa na ujenzi huo.

Alifahamisha kuwa utaratibu wa kukata barabara hiyo haukukamilishwa hivyo aliwataka wahusika wote kuhakikisha wanaifanyia marekebisho barabara haraka na kulitaka baraza la manispaa kufuatilia majukumu yao kwa wakati pindi wanapotoa ruhusa ili kuhakikisha azma ya serikali ya kuimarisha miundombinu inafikiwa kama ilivyokusudiwa.

Aidha Mkuu hoyo wa Mkoa alilitaka Baraza la Sanaa, Sensa ya filamu na Utamaduni kufuta kibali cha kupiga muziki katika ukumbi wa Maisara CCM Social Hall baada ya wananchi wanaoishi jirani na ukumbi huo kulalamikia sauti za muziki jambo ambalo linakiuka agizo la Serikali ya Mkoa Mjini Magharibi la kutopigwa katka siku za katikati ya wiki.

Katika hatua nyengine, Ayoub amelitaka baraza la Manispaa ya Mjini, Kamisheni ya Utalii na Bodi ya vileo kutotoa kibali na leseni ya biashara kwa nyumba ya kulala wageni ya Jambo iliyopo Migombani mjini Unguja kutokana na kusababisha kero mbali mbali kwa wananchi wa maeneo hayo likiwemo la kutumika kama danguro.

“Kwa hili la jambo guest house, taasisi zinazohusika na kutoa vibali na lesini ya biashara naagiza visitolewe hadi tutakapoelewana mwacheni amalizie muda wake lakini kisitolewe kibali kwa ajili yam waka ujao kwani hatuwezi kumwacha mtu mmoja anakera wengine kwa kisingizio cha mapato”, alisema.

Awali akiwasilisha malalamiko yake kwa niaba ya wananchi wenzake mkaazi wa shehia ya Migombani ali khamis mwinyi alieleza kuwa nyumba hiyo ambayo iana baa ndani yake imekuwa kero kwa wakaazi na wageni wa eneo hilo kiasi cha kusababisha maafa.

“Kinachotusikitisha watu wanaokwenda katika hiyo gesti kwa ajili ya ufska baadhi yao hutumia misikiti uliopo jirani na hiyo nyumba kwa kuoga lakini hutupa mipira ya kiume iliyokwishatumika tunategemea kuwa na jamii gani?”, alihoji mwananchi huyo.

Akitoa ufafanuzi juu ya malalamiko ya wananchi kuhusu usafiri wa bodaboda Zanzibar, Katibu wa bodi ya usafiri wa barabarani Mohammed Simba alisema usafiri huo haujaruhusiwa kwa mujibu wa sheria namba 7 ya mwaka 2003 kwa ajili ya kusafirisha abiria na kuwepo kwake ni kinyume na sheria za nchi.


Hata hivyo alieleza kuwa sheria imetoa ruhusa kwa bodi yake kumshauri waziri anaehusika na masuala ya usafirishaji juu ya vyombo vinavyowea kutumika kwa ajili ya usafiri na usafishaji wa abiria hivyo wanaendelea kufuatilia kuona kama ipo haja ya aina hiyo ya usafiri kuruhusiwa.

Mkuu wa Mkoa wa Majini Mgharibi Unguja Ayoub Mohammed Mahamoud (kushoto) akitoa maelekezo  baada ya kupokea malalamiko ya wananchi katika uwanja wa Komba wapya mjini Unguja.

katibu wa biodi na mahakama ya vileo zanzibar  (katikati) akijibu hoja na kutoa ufafanuzi kuhusiana na Baa na nyumba ya kulala wageni ya Jambo iliyopo Migombani baada ya wananchi wa shehia hiyo kuilalamikia. kulia ni mwananchi alietoa malalamiko hayo ali khamis mwinyi na wa kwanza kushoto waliosimama ni mkurugenzi wa manispaa ya Mjini Abou Serenge. (PICHA KWA HISANI YA OFISI YA MKUU WA MKOA).