Tuesday, October 16, 2012

NIPENI MUDA KUTATUA MGOGORO HUU - BALOZI SEIF


  • MGOGORO WA ARDHI KATI YA JWTZ, WANANCHI NGOMA BADO MBICHI
  • TUME YA TAKRIMA YASHINDWA KUTOA RIPOTI
Na: Mwinyimvua Nzukwi, Zanzibar.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeeleza kuwa inakusudia kutoa uamuzi wa moja kwa moja katika kutafuta suluhu juu ya mgogoro wa ardhi uliopo kati ya Wananchi wa Vijiji vya Fuoni, Maungani , Kombeni na Diiman kwa upande mmoja na Kambi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kambi ya Kisaka saka wilaya ya magharibi, unguja.

Kauli hiyo imetolewa na makamo wa pili wa rais wa Zanzibar, Balozi Seif Aili Iddi alipokuwa akizungumza na wananchi wa Maeneo hayo katika Kituo cha Afya cha Fuoni Kibondeni baada ya Tume aliyoiunda mwezi Julai mwaka huu kushindwa kuwasilishwa ripoti yake tokea mwishoni mwa mwezi Agosti.

Balozi Iddi aliwataka Wananchi hao kuendelea kuwa na subra wakati Serikali inalitafakari suala hilo kwa ajili ya kulipatia ufumbuzi wa kudumu utakaoleta afueni kwa pande zote mbili.

Aidha aliekleza kusikitishwa kwake kwa kutotekelezwa kwa maagizo aliyoyatowa katika Kikao cha pamoja kati ya pande mbili za mzozo huo mnamo  Julai 7 mwaka huu ambapo mbali na kuunda kamati ya kuchunguza na kupendekeza hatua za kutatua mgogoro huo pia aliuagiza Uongozi wa Kambi ya Kisakasaka kulirejesha Bambo waliloliondoa mahali walipokubaliana na Wananchi katika mazungumzo ya awali.
“ Hakukuwa na haja ya kutoa maamuzi ya haraka kuhusiana na Mgogoro huo, ndio maana nikaunda Tume hiyo lakini cha kusikitisha hadi sasa sijaletewa ripoti hiyo kama nilivyoagiza kuletewa mwishoni mwa Mwezi wa Agosti mwaka huu.” Aliswema Balozi Seif.

Alieleza kuwa Serikali isingependa kuona Jeshi lililoundwa kwa ajili ya kutumikia Jamii linaendelea kuwa na mifarakano na Wananchi katika utekelezaji wa majukumu yake.
Makamu huyo wa Rais wa Zanzibar ambaye ndiye mtendaji na msimamizi mkuu wa shughului za serikali ya Zanzibar aliwaahidi Wananachi hao kwamba mambo yote waliyokubaliana na Uongozi wa Jeshi yanatekelezwa kikamilifu huku ufumbuzi wa kudumu ukitafutwa.
“Nipeni muda, hivi sasa nimetingwa na shughuli za Baraza la Wawakilishi na nadhani mnaelewa kuwa mimi ndie msimamizi mkuu wa kazi za serikali shughuli za Serikali …….. nikimaliza tu jibu la suala hili nitajuka kulitoa hapa hapa”. Alifafanua Balozi Seif.
Mapema Mwenyekiti wa Kamati ya Wananchi hao Khamis Vuai Makame, aliiomba Serikali kuyachukulia hatua za haraka mambo waliyokubaliana na uongozi wa jeshi hilo ili kutatua mgogoro huo na kuepusha madhara yanayoweza kutokea.
Khamis alisema bado wataendelea kulalamikia kutokuwepo kwa uhalali wa ramani ya kambi hiyo wakati wananchi hao ndio wenye hati ya umiliki wa ardhi hiyo kwa mujibu wa sheria na taratibu za mamlaka inayohusika na ardhi hapa nchini walizopatiwa miaka kadhaa iliyopita.
Mwenyekiti huyo alimuelezea Balozi Seif kuwa jeshi hilo limeingia katika mgogoro huo kwa utashi wa baadhi ya watu maslahi yao na si maslahi ya jeshi au jamii inayolizunguka kambi hiyo.
Khamis alisema wanaamini kuwa utatuzi wa mgogoro huo utapatikana kwa kutumia vikao halali na kumpongeza Balozi Seif kwa hatua anazoendelea kuchukuwa katika kutafuta ufumbuzi wa mgogoro huo toka ulipozuka.
“Hapa hapana tatizo kubwa kama tutatumia vikao na kulizungumza kwani mwisho wa yote naamini suluhu itapatikana ”, alisema mwenyekiti huyo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliunda tume ya kuufuatilia Mgogoro huo wa ardhi kati ya JWTZ  kambi ya Kisakasaka na wananchi wanayoizunguuka kambi hiyo Julai mwaka huu chini ya uenyekiti wa Mkuu wa Wilaya ya Magharibi, tume ambayo imeshindwa kuwasilisha ripoti yake katika muda uliopangwa kama iliyoagizwa. .
Mgogoro huo umezuka baada ya wananchi wa vijiji hivyo kulalamikia ramani mpya ya JWTZ inayoonesha maeneo hayo kuwa ni sehemu ya jeshi hilo kambi ya Kisakasaka huku wananchi hao wakiwa na hati halali za umiliki jambo linalodaiwa ni utashi wa baadhi ya watu kwa maslahi yao na si ya taasisi hiyo, madai ambayo yanapingwa na viongozi wa jeshi.
 
551.jpg569.jpgBaadhi ya wananchi wa vijiji vya Fuoni, Maungani , Kombeni na Dimani Wilaya ya Magharibi, Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja wakimsikiliza Makamo wa pili wa Rais wa Zanzibar (hayupo pichani) katika mkutano ulioandaliwa kwa lengo la kutafuta suluhu ya mgogoro wa ardhi kati ya wananchi wa vijiji hivyo na JWTZ kambi ya Kisakasaka.

Balozi Seif akisisitiza jambo kwa wananchi wa vijiji vya Fuoni, Maungani, Kombeni na Dimani Wilaya ya Magharibi, Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja katika mkutano wa kutafuta suluhu ya mgogoro wa ardhi kati ya wananchi wa vijiji hivyo na JWTZ kambi ya Kisakasaka. (Picha na OMKPR)

No comments:

Post a Comment