- JUKWAAA LA KUTATHMINI UWAJIBIKAJI KWA WOTE
- TAARIFA SAHIHI NA ZA WAKATI CHACHU YA MAENDELEO YA JAMII
Na: Mwinyimvua Nzukwi, Zanzibar
Septemba 28, kila mwaka inatambuliwa kimataifa kuwa ni siku ya haki ya kujua duniani.
Siku hiyo ilianzishwa mwaka 2002 huko Sofia, Bulgaria kufuatia mkutano wa vyombo na sekta za habari uliojadili namna bora ya kutumikia umma kwa lengo kuongeza uwajibikaji na uelewa wa mtu mmoja mmoja juu ya haki zao kwa serekali pia wajibu wa serekali na vyombo vyake kwa wananchi wake.
Tabaani siku hii ina umuhimu wa pekee kwa pande zote mbili, serikali kwa upande mmoja na wananchi kwa upande mwingine na bila shaka ndipo haja ya kusimikwa na kusimamiwa kwa sheria zinazolazimisha watu kutoa na wengine kupata habari inapoanzia.
Kama zilivyo nchi nyingi duniani Tanzania iliadhimisha siku hii kwa mikutano ya wadau mbali mbali wa habari kwa lengo la kujuzana na kukukmbushana juu ya dhima ya kila mmoja katika jamii ya kufanya juhudi ya kujua hususan mambo ya msingi katika jamii yake.
Mambo hayo yanaweza kuwa ni haki na wajibu wa serikali na vyombo vyake kwa umma, wajibu wa raia kwa serikali na hata wenyewe kwa wenyewe, namna ya uendeshaji wa dola, mipaka ya utawala kati ya ngazi moja na nyengine na kadhalika.
Katika mkutano ulioandaliwa na Baraza la Habari Tanzania ofisi ya Zanzibar, uliofanyika katika hoteli ya Mazson, haki ya kujua imetajwa kuwa ni miongoni mwa haki za msingi za binadamu inayoanzia toka mtu anapokuwa mdogo na kuendelea nayo kadri anavyokuwa.
Akitoa mada juu ya umuhimu wa haki ya kujua Katibu Mtendaji wa tume ya utangazaji ya Zanzibar, Chande Omar Omar aliitaja haki hii kuwa hukua hatua kwa hatua toka katika hali ya mtoto kujitambua maumbile yake, watu anaohusiana nao na kufikia kiwango cha kujua ni kwa nini mambo yako kama yalivyo na si vyenginevyo.
"Tunapofikia hapo ndipo haja ya kujua inakuwa imefikia kiwango cha kuleta mabadiliko katika jamii na hii inatokana na uwezo wa kudadisi na kutafuta ukweli juu ya mambo mbali mbali", alisema Chande.
Aliongeza kuwa hali hii haitokei kwa bahati mbaya bali huwa ni kipaji anachozaliwa nacho mtu na namna alivyokuzwa na familia yake au alivyopata fursa zenye kukuza upeo wa kufikiri na kupembanua mambo.
"Uwezo wa kuhoji unatokana na jinsi makuzi aliyoyapata mtoto ......... iwapo mtoto alikuwa anapatiwa fursa ya kuhoji na kupata majibu yanayostahiki, bila shaka atakuwa na uthubutu wa kutaka kujua kila jambo linalotokea nchini hata kama taarifa zake zitakuwa zimefichwa", aliongeza Chande na kuwataka vijana kutokuwa na hofu ya kuhoji, kudadisi na kutafuta ukweli kwa lengo la kujua kwani kufanya hivyo ni kuitekeleza haki yao kikatiba.
"Msiogope. Section 18 (kifungu cha 18) ya katiba ya Zanzibar ipo wazi juu ya haki ya kutafuta na kupata habari, tafuteni na hamtozuiwa ......... yule atakaewazuia bila shaka atakuwa hajui na mtakapomjulisha mtakuwa mmetekeza wajibu wenu", aliongeza Chande.
Akichangia mada hiyo mtangazaji wa kituo cha redio cha Chuchu FM, Mulhat Yussuf Said alisema tabia ya viongozi wa taasisi za serikali ya kuficha au kubagua kutoa taarifa kwa vyombo vya binafsi inawakosesha wananchi walio wengi haki ya kujua mambo kwa wakati kutokana na vyombo hivyo kuwa na wasikilizaji wengi na kutoa matangazo yao kwa muda mwingi na kwa wakati.
"Baadhi ya viongozi wa taasisi za umma wana tabia ya kuficha habari au kubagua vyombo vya kuzipa habari hasa sisi tunaofanya kazi katika vyombo binafsi.... hii sio sawa kwani kuna kundi kubwa hasa vijana ambao husikiliza vyombo hivi" alisema bi Mulhat.
Akitolea mfano wa madhara ya kutojua, afisa kutoka tume ya ukimwi Zanzibar (ZAC) Dk. Sihaba Saadati alisema kukosekana taarifa sahihi na kwa wakati kulichangia kwa kiasi kikubwa kuenea kwa maradhi ya ukimwi katika baadhi ya maeneo nchini jambo ambalo lingeweza kudhibitiwa kama taarifa zingeliwafikia watu kwa muda muafaka.
"Mwanzoni taarifa kuhusu ukimwi zilikuwa hazipatikani kirahisi lakini baada ya kuanza kutolewa tumeona jinsi watu wanavyochukua tahadhari juu ya kuambukizwa au hata tiba yake kwa wale waliambukizwa jambo ambalo limesaidia kwa kiasi kikubwa kudhibiti kasi ya maambukizi mapya", alisema afisa huyo.
Nae mwandishi mwandamizi Salim Said Salim alieleza kuwa ni makosa kwa viongozi wa vyombo na taasisi za serikali kuficha na kukalia taarifa kwa umma na kufanya hivyo ni kwenda kinyume na taratibu na sheriazanchi.
"Zipo taarifa haziwezi kutolewa na kuhojiwa hadharani lakini kwa zile taarifa za kawaida ni makosa kuzikalia au kuweka urasimu katika upatikanaji wake kwani hizi ni taarifa za umma na watu wanahaki ya kujua", alisema Said.
Alitolea mfano wa upatikanaji wa taarifa za tenda zinazotolewa na serikali au taasisi zake katika kutoa huduma mbali mbali kuwa haziwekiwi wazi jambo linalopelekea kuwepo kwa upendeleo na ubadhirifu wa mali za umma huku wanachi wa kawaida wakipata tabu.
"Utakuta kiongozi wa taasisi fulani anakalia taarifa kama vile ni mali yake binafsi, hata wafanyakazi wake hawajui kitu na anakuwa mkali pale anapohojiwa. Huu si uendeshaji mwema wa nchi kwani kila mmoja anawajibu wa kuchangia ujenzi wa taifa sasa kama hawajui namna mambo yalivyo watachangiaje?" , alihoji nguli huyo katika fani ya uandishi wa habari.
Mbali ya ubinafsi na ukiukwaji wa taratibu za utawala wa nchi unaofanywa na viongozi wa taasisi mbali mbali za serikali, wachangiaji wengi katika mkutano huo walilitaka Baraza la Habari Tanzania (MCT) kuchepuza mchakato wa upatikanaji wa sheria ya haki ya kupata habari ambayo katika rasimu yake sehemu ya tatu inaelezea haki ya habari na majukumu ya mamlaka za umma katika kustawisha mwenendo wa utoaji na upatikanaji wa habari.
Bila shaka hapo ndipo nchi itakuwa inatekeleza kwa vitendo azimio la umoja wa mataifa la kuanzishwa kwa siku hii ya haki ya kujua kwa kila mmoja katika jamii kutekeleza wajibu wake ipasavyo kwa kupata, kutoa na kusambaza habari kwa wote na kwa wakati.
Baadhi ya wadau wa habari waliohudhuria maadhimisho ya siku ya haki ya kujua yaliyofanyika 28/9/2012 katika ukumbi wa Hoteli ya Mazson mjini Zanzibar wakifuatilia kwa makini mada ya umuhimu wa kujua iliyotolewa na Katibu Mtendaji wa tume ya utangazaji zanzibar Chade Omar (hayupo pichani). Kutoka kushoto mstari wa mbele ni Mwalim, Juma Seif kutoka idara ya elimu mbadala, Mulhat Said Mtangazaji Chuchu FM redio na Masudi Saanani mwandishi Mwananchi Communication.
Meneja wa Baraza la Habari Tanzania (MCT) ofisi ya Zanzibar, Suleiman Seif Omar akitoa maelezo ya utambulisho kwa wadau wa habari (hawapo pichani) waliohudhuria maadhimisho ya siku ya haki ya kujua yaliyofanyika 28/9/2012 katika ukumbi wa mikutano wa hoteli ya Mazson, Shangani mjini Zanzibar, wengine kutoka kushoto ni Katibu mtendaji wa Tume ya Utangazaji Zanzibar Chande Omar Omar, Makamo mwenyekit mstaafu wa MCT Maryam Hamdan na afisa wa fedha na usuluhishi wa MCT Alan Nlawa
No comments:
Post a Comment