Na. Othman Khamis, OMKPR
Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema nia ya Serikali ya kuanzisha wizara inayosimamia
sekta ya kazi ni kuhakikisha kwamba inapambana na
tatizo la ajira linaloonekana kuathiri nguvu kubwa ya vijana nchini.
Kauli hiyo
aliitoa wakati akizindua Chuo cha Ushoni na ujasiriamali
kilichoanzishwa na Jumuiya ya Vijana ya Kibweni ya Kibweni Yourth Organization KYO iliyopo Kibweni
kwa Botoro,Jimbo la Bububu, wilaya ya Magharibi Unguja.
Alisema hatua hiyo pia
inakwenda sambamba na utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010
inayoelezea umuhimu wa kuundwa kwa vikundi vya ujasiri amali
ambavyo hutoa fursa ya ajira miongoni mwa wananchi.
Alisema kazi hizo zimekuwa
zikisaidia kupunguza umaskini na serikali itajitahidi kuhakikisha
inavijengea nguvu vikundi hivyo vya ili viweze kutekeleza majukumu vilivyojipangia.
Aidha aliipongeza
jumuiya hiyo kwa uamuzi wa kuanzisha kikundi
hicho ambacho kinatarajiwa kuwa mkombozi kwa wanajumuiya na vijana wa jimbo hilo
kwa ujumla.
Balozi Seif
aliwahimiza viongozi na wana jumuiya hiyo kuwa wastahamilivu na kuvumiliana
katika harakati zao za kila siku hatua ambayo itafanikiwa endapo kutakuwa na utaratibu wa kufuata kanuni walizojiwekea.
“ Nimefurahi
kuona vijana mmejikusanya kuanzisha mfumo wa ajira ambao serikali kuu kadri ya
hali itakavyoruhusu itazingatia na kutoa msaada unaostahiki ili kukiendeleza
kikundi chenu”, alisisitiza Balozi Seif.
Aliwahimiza kuendelea
na mpango waliouanzisha wa kupanda miti ili kukabiliana na upungufu wa maji
uliyoikumba nchi kutokana na tabia za baadhi ya watu kukata miti ovyo.
Katika
kuunga mkono juhudi za vijana hao za kuanzisha chuo hicho Makamu huyo wa Rais
alikabidhi vyarahani vitano kama mchango wake katika kukipa nguvu chuo hicho.
Vile vile aliahidi
kuchangia kompyuta moja na mashine ya kudarizi kwa chuo hicho hatua
ambayo imeungwa mkono na Mwakilishi wa jimbo hilo Hussein Ibrahim Makungu
‘BHAA’ aliyetoa mchango wa shilingi Milioni 2 wakati Mbunge wa Jimbo hilo
Masoud Sururu ambaye ni mlezi wa jumuiya hiyo akIahidi kuchangia vyarahani vitano,
pasi na vifaa vingine vidogo vidogo.
Akisoma
risala kwa niaba ya wanajumiya wenzake Farida Juma Haji alisema vijana wa
Kibweni wameamua kuanzisha jumuiya hiyo wakitambua kwamba serikali kuu haina
fursa ya kutoa ajira kwa watu wote.
Alisema
elimu ya ujasiri amali ambayo ni muhimu kwa taifa lolote Duniani ndio
itakayowapa nafasi pekee ya kukabiliana na tatizo la ajira na kwamba jumuiya
yao imelenga kwenda sambamba na mpango
wa taifa wa kupunguza umaskini Zanzibar (MKUZA).
Mapema akikikagua
chuo hicho Mwalimu wa chuo hicho Subira Haji Yahya alimueleza Balozi Seif
kwamba lengo la kuanzishwa kwa chuo hicho ni kuwajengea mazingira ya ajira
vijana wa Shehia hiyo.
Subira
alieleza kwamba mfumo huo wa mafunzo mbali ya kutengeneza kazi za ajira lakini
pia utasaidia kupunguza wimbi la vitendo viovu wanavyojihusisha zaidi vijana
ndani ya mitaa na kuleta kero na fadhaa kwa jamii.
Chuo cha
ushoni cha ujasiri amali cha Kwa Botoro kilichoanzishwa takribani miezi tisa
iliyopita kina wanafunzi 16 wa rika mbali mbali ambao mbali ya kujifunza
ushonaji wa nguo kwa hatua mbali mbali pioa hupata wasaa wa kujifunza lugha ya
Kiingereza pamoja na upandaji miti katika maeneo ya vianzio vya maji vya
Mwanyanya.
No comments:
Post a Comment