BAUSI ATAJA NYOTA WA CHALLENJI
Na. Mwinyimvua Nzukwi, Zanzibar
Na. Mwinyimvua Nzukwi, Zanzibar
Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Zanzibar ‘Zanzibar Heroes’,
Salum Bausi amewaita nyota 30 kuunda kikosi cha timu hiyo kinachojiandaa na
michuano ya Chalenji inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi mjini Nairobi Kenya
baadae mwaka huu.
Aliyataja mambo hayo kuwa ni nidhamu ya mchezaji,
uwezo wa mchezaji binafsi, nafasi ya mchezaji katika timu yake na ukubwa wa
mashindano wanayojiandaa nayo jambo ambalo amesema litawapa nafasi wachezaji
hao kuongeza juhudi na kujituma wakiwa katika timu hiyo.
“Pamoja na mambo yote hayo mkazo mkubwa kwangu ni
katika nidhamu ya mchezaji, ndani na nje ya uwanja kwani naamini ni vigumu kama
mwalimu kuwa na timu yenye matokeo mazuri bila ya wachezaji wanaozingatia
nidhamu wakati wote”, alisema Bausi.
Bausi ambaye
awali alitangaza kujiuzulu timu kuifundisha timu hiyo mara baada ya kushika
nafasi ya tatu katika mashindano yaliyopita yaliyofanyika Kampala, Uganda na
alirudishiwa jukumu hilo na ZFA (chama cha soka Zanzibar) baada ya kushauriwa
wa Rais wa Zanzibar Dk. Ali mohammed Shein. Aliwataka wadau wa mchezo huo
kujitokeza na kumpa ushirikiano na kwamba yeye atakua tayari kupokea ushauri
wowote ule.
“Hii timu hii si yangu wala ZFA ni yetu sote, sasa
kila mmoja anaruhusiwa kutoa mchango, maoni, ushauri na kila aina ya msaada
ambao anahisi utasaidia katika kuleta matokeo mazuri ya timu hii”, aliongeza.
Wachezaji watakaounda timu hiyo na timu zao kwenye
mabano ni walinda milango Mwadini Ali Mwadini (Azam fc), Abdalla Rashid ‘Babu’ (Ruvu
Shooting) na Ali Suleiman Abdi (KMKM) wakati walinzi ni Mohammed Azan ‘Brown’ (Polisi
- Zanzibar), Waziri Salum (Azam ), Shafii Hassan (Malindi) na Mohammed Faki (Zimamoto).
Wengine katika nafasi hiyo ni Salum Haji Juma (Miembeni),
Said Yussuf (Mtende Rangers), Mohammed Othman Mmanga (Jamhuri), Mussa Said
Magarawa (Chwaka Stars) na Nassor Masoud ‘Cholo’ (Simba).
Viungo wa timu hiyo ni pamoja na Abdulhalim Humuod (Simba),
Sabri Ali Makame (Oljoro JKT), Adeyoum Saleh (Simba) na Is-haka Othman (JKU).
Wengine ni Ali Kani Mkanga (JKT Ruvu), Hamadi
Mshamata (Chuoni), Hamadi Juma Issa na Masoud
Ali Mohammed (Mtibwa Sugar).
Washambuliaji katika kikosi hicho kinachotarajiwa
kuanza mazoezi Alhamisi ijayo baada ya kukamilika kwa zoezi la upimaji wa afya
siku ya Jumatano ni Seif Abdalla Rashid na Khamis Mcha Khamis ‘Viali’ wa Azam,
Suleiman Kassim Suleiman ‘Solembe’ (Coastal Union), Amour Omar Mohammed ‘Janja’
(Miembeni) na Amir Omar Hamad (Oljoro JKT).
Wachezaji wengine katika safu ya ushambuliaji ni Jaku
Joma Jaku (Mafunzo), Faki Nahoda (Kimbunga F. C), Hassan Seif Ali (Mtibwa) na mfungaji bora wa mashindano ya kombe copa
cola yaliyomalizika hivi karibuni Juma Ali Yussuf anaechezea timu ya New Vission inayoshiriki
ligi daraja la central wilaya ya Mjini, Unguja.
Akizungumzia uteuzi huo mjumbe wa Kamati Tendaji ya ZFA
Taifa Maalim Masoud Attai aliwataka wapenzi wa mpira wa miguu visiwani hapa wakubaliane
nao kutokana na kuwa umezingatia vigezo vya kitaaluma na waisaidie ili kuwatia
moyo wachezaji na viongozi wa timu hiyo.
“Huu ni uteuzi wa mwalimu na wenzake na sisi sote
hatuna budi kuunga mkono kwa sababu wao ndio tuliwakabidhi kazi hivyo ni vyema
tukawasaidia kutekeleza majukumu yao”, alisema Maalim Attai.
Timu hiyo ambayo inatarajiwa kucheza mechi mbali mbali
za mchujo ili kupata wachezaji 20 watakaoenda Nairobi, ipo chini ya Bausi anayesaidiwa
na Hafidh Muhidin na Malale Hamsini huku Saleh Ahmed Seif akipewa jukumu la
kuwanoa makipa wa timu hiyo na daktari wa timu ni Mohammed Mwinyi na mtunza
vifaa (kit manager) ni Mohammed Said ‘Mdudu’.
No comments:
Post a Comment