Miongoni mwa
mambo yanayopigwa vita na kupigiwa kelele na wanaharakati mbali mbali ni
ubaguzi. Kimsingi watu wanazingatia zaidi ubaguzi wa kijinsia na kusahau kuhusu
aina nyengine zikiwemo zile zinazowakabili watu wenye mahitaji maalum.
Katika makala
haya mwandishi Ado Shaibu anajaribu kuonesha ni jinsi gani mifumu na hata jamii
inavyowabagua watu wenye ulemavu wa macho lakini pia changamoto wanazokabiliana
nazo pale wanapohitaji kupata huduma muhuimu za kijamii ikiwemo elimu.
Kwa kuwa
makala hii imesheheni ushuhuda na uhalisia wa mambo yalivyo katika jamii
naiweka mbele yenu ili watu wengi zaidi wapate kunufaika.
Na. Ado
Shaibu, Dar es salam
Binafsi
sipingi kuanzishwa kwa mfumo shirikishi. Kwa mtazamo wangu, mfumo shirikishi
una faida anuai.
Mosi,
unawaandaa wanafunzi walemavu kuchanganyika na jamii ambayo kimsingi ndiyo wataishi
nayo uraiani. Pili, unawapa fursa wanafunzi wasio walemavu kufahamu changamoto,
fursa na mahitaji ya walemavu. Pia mfumo shirikishi unasemwa kuongeza fursa kwa
walemavu wengi zaidi kupata elimu kwa sababu una gharama nafuu. Hili la mwisho
linahitaji utafiti zaidi.
Jambo la msingi ambalo tunapaswa kujiuliza ni kama wanafunzi wasio na ulemavu
na jamuiya za taasisi za elimu kama vile shule na vyuo zimejiandaa kikamilifu
kuishi kwa upendo na walemavu na kufahamu vyema mahitaji yao. Nasema hivyo kwa
sababu elimu shirikishi haiwezi kufanikiwa kwa kiwango kinachotarajiwa kama
jamii itakuwa haijaandaliwa vizuri kisaikolojia kuwapokea, kuwajali na
kuwapenda walemavu.
Leo
tutazame jinsi mfumo shirikishi unavyofanya kazi kwa mfano halisi; mfano wa
maisha yangu. Mwaka 2011 ulikuwa mwaka wa mafanikio makubwa kwangu kwenye siasa
za chuo kikuu. Kwanza nilichaguliwa kuwa Katibu wa kitivo cha sheria na baadaye
katibu wa bodi ya serikali ya wanafunzi(DARUSO). Kiongozi wa nafasi hiyo, ana
fursa kubwa ya kupata sehemu nzuri ya malazi kwenye hosteli za chuo.
Mimi
niliamua kuishi chumba kimoja na mlemavu wa macho Vicent Mzena ambaye naye
alikuwa waziri wa Jinsia na makundi maalum katika serikali ya wanafunzi
(DARUSO).
Kuipokea
changamoto ya kuishi chumba kimoja na mlemavu wa macho kumenipa ‘’uamsho’’
mkubwa. Mzena amekuwa mwalimu wangu mkubwa kuhusu mambo ya walemavu.
Somo la
kwanza: Hapa tunajifunza kwamba jamii inapaswa kuchukulia kwamba kuishi na
walemavu sio tatizo bali ni changamoto inayozalisha fursa ya kujifunza zaidi
kutoka kwa walemavu na kuonyesha upendo kwao.
Ni
asububuhi kumeshapambazuka. Mzena anaamka mapema. Chumba kimepangiliwa vyema na
anafahamu ulipo mswaki, dawa ya meno na maji. Anakwenda mwenyewe bafuni
kusafisha mwili. Mimi naamka na kumsaidia kunyoosha nguo zake alizozifua jana.
Mzena ana desturi ya kufua nguo mwenyewe na kufuliwa mara chache hasa
anapotingwa na majukumu.
Somo la
pili: Hapa tunajifunza kwamba katika mfumo shirikishi, kila mmoja ana jukumu la
kutekeleza. Walemavu wanapaswa kujizoesha kufanya wenyewe kazi ndogondogo
wanazozimudu. Pia wanajamii wanaowazunguka walemavu wanajukumu la kuwasaidia
kufanya kazi wasizoweza kuzitekeleza wenyewe.
Namshika
mkono Mzena kumpeleka darasani ambaye mkononi ana fimbo nyeupe na begi la vifaa
vya shule. Madarasa yako mbali kiasi. Mzena ni mcheshi sana. Tunacheka njia
nzima huku akinitania kuwa mimi ni ‘’dereva mahiri’’. UDSM kuna jiografia ya
milima lakini Mzena anajitahidi kuyazoea mazingira japo hapa na pale anatatizwa
na ngazi.
Somo la
nne: Hapa tunajifunza kwamba shule za mchanganyiko wa walemavu na watu wengine
ziwe na miundombinu na mazingira rafiki kwa walemavu. Lakini pia walemavu wana
jukumu la kuikabili changamoto ya mazingira yao kadiri inavyowezekana.
Kwenye varanda za hosteli na njiani kuelekea darasani tunakutana na wanafunzi
wenzetu. Wanaonyesha kutujali na kutupisha njiani upesi. Lakini hapa kuna jambo
la kuongeza. Wengi wanaonyesha kutunduwaa kwa mshangao. Baadhi yao
wanasimamisha mazungumzo yao. Kwa ufupi,licha ya kuonyesha upendo na kujali,
kuna kila dalili kwamba bado hawajaizoea kiukamilifu hali ya kujichanganya na
walemavu.
Somo la
tano: Hapa tunajifunza umuhimu wa kuijenga jamii kisaikolojia ili iweze
kuwapokea walemavu kama sehemu ya jamii. Sasa ni wakati wa kula. Mimi na mzena
tunajongea kafeteria kupata staftahi. Kuna msururu mrefu wa wanafunzi. Awali,
walemavu walipaswa kupanga foleni kama watu wengine. Baada ya jitihada za
viongozi wa walemavu, sasa walemavu wanahudumiwa vizuri na wahudumu wa
cafeteria.
Somo la
sita: kwenye foleni na misururu inayochosha kama vile benki, migahawani, kwenye
vyombo vya usafiri na hospitali, walemavu wapewe kipaumbele.
Ni usiku na giza linachukua sehemu yake. Mimi, Mzena na marafiki wengine tuko
chumbani tukibadilishana mawazo. Ghafla anaingia Maingu Nyanjila, mwanamke
aliyejitolea vya kutosha kwa ajili ya walemavu. Amekuja kumchukua Mzena
akamsomee kitabu cha fasihi, ‘’Autobiography of Malcom X’’.
Ni kitabu
kikubwa lakini Mzena hana namna isipokuwa kumsikiliza Maingu akimsomea kurasa
moja hadi nyingine. Hakuna vitabu katika maandishi maalumu ya nukta nundu
(Braille).
Vingekuwepo
Mzena asingehitaji mtu wa kumsomea. Baadhi ya walimu wa chuo wanawapa walemavu
notisi zao ambazo Mzena anazisoma kwa vifaa vya kielektroniki vya kutunzia kumbukumbu
au kompyuta yenye programu ya sauti.
Darasani
anapaswa kwenda na tepurekoda inayonasa mafundisho ya mwalimu. Kwa bahati
mbaya, si kila kitu kinasemwa kwa sauti; baadhi ya mambo yanaandikwa ubaoni
bila kuzungumzwa.
Somo la saba: Katika dunia ya leo ya kielektroniki, kuna vifaa vingi ambavyo
vinaifanya elimu ya walemavu iwe rahisi na yenye tija. Jamii na wadau wote wa
haki za walemavu wajitahidi kufadhili upatikanaji wa vifaa muhimu.
Kabla
hawajaondoka chumbani kwenda maktaba au darasani kujisomea, ni desturi ya
Maingu kuibua mjadala kuhusu mada ya kijamii. Ni vijana kutoka fani mbalimbali
na kila mmoja analeta hoja yake. Mzena anatoa hoja kwa mtazamo wa kielimu na
mimi naleta vifungu vya sheria.
Maingu anaingilia
na kutoa hoja ya kifasihi. Mara nyingi wanajua jinsi ya kunishinda. "Nyinyi
wanasheria mna maneno mengi na hamtakwenda mbinguni kwa sababu hamtendi haki"
Maingu angenitania ili kuidhoofisha hoja yangu.
Somo la
nane: Walemavu washiriki kwenye mijadala ya kila siku ya makundirika. Marafiki
wawape walemavu nafasi ya kutoa hoja zao na kuheshimu mitizamo yao. Walemavu
wana tafakuri kama walivyo watu wengine.
Kuna mengi
ya kuyazungumza kuhusu elimu shirikishi. Shule ya Msingi Nanjoka na Sekondari
ya Frankweston nilikuwa swahibu wa mwanafunzi mwenzangu ambaye alikuwa mlemavu
wakusikia. Ndanda nilisoma na walemavu wa macho. UDSM nimekutana na walemavu wa
kila namna. Lakini, darasa maridhawa nimelipata nilipokata shauri kuishi na
vicent Mzena, mlemavu wa macho. Natamani walemavu wote wangekuwa na moyo kama
wa Mzena. Pia, nawausia vijana wenzangu na wanajamii kwa ujumla kuishi, kujenga
urafiki na kuwakaribisha walemavu.
Lakini hali
ikoje kwenye jamii? Utafiti uliofanywa na kituo cha taarifa kuhusu ulemavu (
Information Centre on Disability-ICD) katika Manispaa ya Moshi, Mwanza na
Morogoro kuhusu mchangamano baina ya walemavu na watu wasio na ulemavu,
unaonyesha kuwa bado kuna changamoto katika kufanikisha mfumo shirikishi.
Utafiti
huo unaonyesha kwamba asilimia 57 ya watu kutokuwa na utayari na kukosa hulka
ya upendo kwa walemavu wakati ni asilimia 47 tu ya watu ilionyesha kuwa na moyo
wa kuwajali, kuwapenda na kuwakaribisha walemavu. Shime wanajamii tuibadili
hali hii na kuishi kwa upendo na walemavu.
Inawezekana. Fanya tafakuri ya kina kisha chukua hatua.