Monday, October 29, 2012

ZIARA YA MAKAMO WA 2 WA RAIS SMZ

 
                                                                                                                                                                                                  NAKAGUA:
Mnamo oktoba 28, 2012 Makamo wa pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alifanya ziara ya siku moja kwa ajili ya kukagua miradi ya maendeleo iliyoanzishwa kwa nguvu za wananchi na kufadhiliwa na serikali au washirika wa maendeleo.
Ziara hiyo ilihusisha vijiji vya Bweleo, Fumba na Bwefum viliopo wilaya ya Magharibi, Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja. Haya ni baadhi ya matukio katika ziara hiyo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiangalia majengo ya skuli ya Bwefum iliyoko Wilaya ya Magharibi, Mkoa wa  Mjini Magharibi ambayo Mapaa yake yako katika hali ya uchakavu akiwa na Mwalimu Mkuu wa Skuli hiyo Kesi Mwinyi Shomari pamoja na baadhi ya wanafunzi wa darasa la kwanza wa skuli hiyo.
 
 Mwalimu mkuu wa skuli ya Bwefum, Kesi Mwinyi Shomari (wa kwanza kushoto aliyevaa kofia) akimuongoza Makamo wa pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi kukagua majengo na eneo la skuli hiyo siku kiongozi huyo alipotembelea vijiji vya Bweleo na Fumba kukagua miradi ya maendeleo na chanagamotozinazowakabili wananchi wa vijiji hivyo.
 
 
Mmiliki wa eneo lenye  Magofu ya Bwefum, Bwana Chandra (wa kwanza kulia) akitoa maelezo kwaa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi kufuatia mgogoro wa muda mrefu kati yake na Wananchi wa Kijiji Hicho. Balozi Seif alizitaka pande hizo kuwa na subra wakati Serikali inafanya utafiti utakaopelekea kupatikana kwa maamuzi sahihi ya kusuluhisha mgogoro huo.
 
Mwenyekiti wa Kamati ya ujenzi wa Uwanja wa kisasa wa mpira wa miguu wa kijiji cha  Bweleo, Hassan Gharib (wa pili kushoto) akitoa maelezo kwa  Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi juu ya changamoto wanazoipambana nazo katika kutimiza azma yao. Wa kwanza kulia alievaa miwani ni mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Zanzibar (BTMZ) Sharifa Khamis.
 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akifurahia bidhaa zilizotengenezwa na Kikundi cha Ushirika cha Ukweli ni Njia Safi cha Kijiji cha Bweleo. Kikundi hicho kinazalisha bidhaa mbali mbali za matumizi ya urembo na kawaida kwa kutumia mwani na mazao mengine ya baharini hali iliyomshawishi makamo huyo wa Rais kununua baadhi ya bidhaa hizo.




Wednesday, October 17, 2012

HAKI YA KUJUA

SIKU YA HAKI YA KUJUA DUNIANI
  • JUKWAAA LA KUTATHMINI UWAJIBIKAJI KWA WOTE
  • TAARIFA SAHIHI NA ZA WAKATI CHACHU YA MAENDELEO YA JAMII

Na: Mwinyimvua Nzukwi, Zanzibar

Septemba 28, kila mwaka inatambuliwa kimataifa  kuwa ni siku ya haki ya kujua duniani.

Siku hiyo ilianzishwa mwaka 2002 huko Sofia, Bulgaria kufuatia mkutano wa vyombo na sekta za habari uliojadili namna bora ya kutumikia umma kwa lengo kuongeza uwajibikaji na uelewa wa mtu mmoja mmoja juu ya haki zao kwa serekali pia wajibu wa serekali na vyombo vyake kwa wananchi wake.

Tabaani siku hii ina umuhimu wa pekee kwa pande zote mbili, serikali kwa upande mmoja na wananchi kwa upande mwingine na bila shaka ndipo haja ya kusimikwa na kusimamiwa kwa sheria zinazolazimisha watu kutoa na wengine kupata habari inapoanzia.

Kama zilivyo nchi nyingi duniani Tanzania iliadhimisha siku hii kwa mikutano ya wadau mbali mbali wa habari kwa lengo la kujuzana na kukukmbushana juu ya dhima ya kila mmoja katika jamii ya kufanya juhudi ya kujua hususan mambo ya msingi katika jamii yake.

Mambo hayo yanaweza kuwa ni haki na wajibu wa serikali na vyombo vyake kwa umma, wajibu wa raia kwa serikali na hata wenyewe kwa wenyewe, namna ya uendeshaji wa dola, mipaka ya utawala kati ya ngazi moja na nyengine na kadhalika.

Katika mkutano ulioandaliwa na Baraza la Habari Tanzania ofisi ya Zanzibar, uliofanyika katika hoteli ya Mazson, haki ya kujua imetajwa kuwa ni miongoni mwa haki za msingi za binadamu inayoanzia toka mtu anapokuwa mdogo na kuendelea nayo kadri anavyokuwa.

Akitoa mada juu ya umuhimu wa haki ya kujua Katibu Mtendaji wa tume ya utangazaji ya Zanzibar, Chande Omar Omar aliitaja haki hii kuwa hukua hatua kwa hatua toka katika hali ya mtoto kujitambua maumbile yake, watu anaohusiana nao na kufikia kiwango cha kujua ni kwa nini mambo yako kama yalivyo na si vyenginevyo.

"Tunapofikia hapo ndipo haja ya kujua inakuwa imefikia kiwango cha kuleta mabadiliko katika jamii na hii inatokana na uwezo wa kudadisi na kutafuta ukweli juu ya mambo mbali mbali", alisema Chande.

Aliongeza kuwa hali hii haitokei kwa bahati mbaya bali huwa ni kipaji anachozaliwa nacho mtu na namna alivyokuzwa na familia yake au alivyopata fursa zenye kukuza upeo wa kufikiri na kupembanua mambo.

"Uwezo wa kuhoji unatokana na jinsi makuzi aliyoyapata mtoto ......... iwapo mtoto alikuwa anapatiwa fursa ya kuhoji na kupata majibu yanayostahiki, bila shaka atakuwa na uthubutu wa kutaka kujua kila jambo linalotokea nchini hata kama taarifa zake zitakuwa zimefichwa", aliongeza Chande na kuwataka vijana kutokuwa na hofu ya kuhoji, kudadisi na kutafuta ukweli kwa lengo la kujua kwani kufanya hivyo ni kuitekeleza haki yao kikatiba.

"Msiogope. Section 18 (kifungu cha 18) ya katiba ya Zanzibar ipo wazi juu ya haki ya kutafuta na kupata habari, tafuteni na hamtozuiwa ......... yule atakaewazuia bila shaka atakuwa hajui na mtakapomjulisha mtakuwa mmetekeza wajibu wenu", aliongeza Chande.

Akichangia mada hiyo mtangazaji wa kituo cha redio cha Chuchu FM, Mulhat Yussuf Said alisema tabia ya viongozi wa taasisi za serikali ya kuficha au kubagua kutoa taarifa kwa vyombo vya binafsi inawakosesha wananchi walio wengi haki ya kujua mambo kwa wakati kutokana na vyombo hivyo kuwa na wasikilizaji wengi na kutoa matangazo yao kwa muda mwingi na kwa wakati.

"Baadhi ya viongozi wa taasisi za umma wana tabia ya kuficha habari au kubagua vyombo vya kuzipa habari hasa sisi tunaofanya kazi katika vyombo binafsi.... hii sio sawa kwani kuna kundi kubwa hasa vijana ambao husikiliza vyombo hivi" alisema bi Mulhat.

Akitolea mfano wa madhara ya kutojua, afisa kutoka tume ya ukimwi Zanzibar (ZAC) Dk. Sihaba Saadati alisema kukosekana taarifa sahihi na kwa wakati kulichangia kwa kiasi kikubwa kuenea kwa maradhi ya ukimwi katika baadhi ya maeneo nchini jambo ambalo lingeweza kudhibitiwa kama taarifa zingeliwafikia watu kwa muda muafaka.

"Mwanzoni taarifa kuhusu ukimwi zilikuwa hazipatikani kirahisi lakini baada ya kuanza kutolewa tumeona jinsi watu wanavyochukua tahadhari juu ya kuambukizwa au hata tiba yake kwa wale waliambukizwa jambo ambalo limesaidia kwa kiasi kikubwa kudhibiti kasi ya maambukizi mapya", alisema afisa huyo.

Nae mwandishi mwandamizi Salim Said Salim alieleza kuwa ni makosa kwa viongozi wa vyombo na taasisi za serikali kuficha na kukalia taarifa kwa umma na kufanya hivyo ni kwenda kinyume na taratibu na sheriazanchi.

"Zipo taarifa haziwezi kutolewa na kuhojiwa hadharani lakini kwa zile taarifa za kawaida ni makosa kuzikalia au kuweka urasimu katika upatikanaji wake kwani hizi ni taarifa za umma na watu wanahaki ya kujua", alisema Said.

Alitolea mfano wa upatikanaji wa taarifa za tenda zinazotolewa na serikali au taasisi zake katika kutoa huduma mbali mbali kuwa haziwekiwi wazi jambo linalopelekea kuwepo kwa upendeleo na ubadhirifu wa mali za umma huku wanachi wa kawaida wakipata tabu.

"Utakuta kiongozi wa taasisi fulani anakalia taarifa kama vile ni mali yake binafsi, hata wafanyakazi wake hawajui kitu na anakuwa mkali pale anapohojiwa. Huu si uendeshaji mwema wa nchi kwani kila mmoja anawajibu wa kuchangia ujenzi wa taifa sasa kama hawajui namna mambo yalivyo watachangiaje?" , alihoji nguli huyo katika fani ya uandishi wa habari.

Mbali ya ubinafsi na ukiukwaji wa taratibu za utawala wa nchi unaofanywa na viongozi wa taasisi mbali mbali za serikali, wachangiaji wengi katika mkutano huo walilitaka Baraza la Habari Tanzania (MCT) kuchepuza mchakato wa upatikanaji wa sheria ya haki ya kupata habari ambayo katika rasimu yake sehemu ya tatu inaelezea haki ya habari na majukumu ya mamlaka za umma katika kustawisha mwenendo wa utoaji na upatikanaji wa habari.

Bila shaka hapo ndipo nchi itakuwa inatekeleza kwa vitendo azimio la umoja wa mataifa la kuanzishwa kwa siku hii ya haki ya kujua kwa kila mmoja katika jamii kutekeleza wajibu wake ipasavyo kwa kupata, kutoa na kusambaza habari kwa wote na kwa wakati.

Baadhi ya wadau wa habari waliohudhuria maadhimisho ya siku ya haki ya kujua yaliyofanyika 28/9/2012 katika ukumbi wa Hoteli ya Mazson mjini Zanzibar wakifuatilia kwa makini mada ya umuhimu wa kujua iliyotolewa na Katibu Mtendaji wa tume ya utangazaji zanzibar Chade Omar (hayupo pichani). Kutoka kushoto mstari wa mbele ni Mwalim, Juma Seif kutoka idara ya elimu mbadala, Mulhat Said Mtangazaji Chuchu FM redio na Masudi Saanani mwandishi Mwananchi Communication.

Meneja wa Baraza la Habari Tanzania (MCT) ofisi ya Zanzibar, Suleiman Seif Omar akitoa maelezo ya utambulisho kwa wadau wa habari (hawapo pichani) waliohudhuria maadhimisho ya siku ya haki ya kujua yaliyofanyika 28/9/2012 katika ukumbi wa mikutano wa hoteli ya Mazson, Shangani mjini Zanzibar, wengine kutoka kushoto ni Katibu mtendaji wa Tume ya Utangazaji Zanzibar Chande Omar Omar, Makamo mwenyekit mstaafu wa MCT Maryam Hamdan na afisa wa fedha na usuluhishi wa MCT Alan Nlawa

Tuesday, October 16, 2012

NIPENI MUDA KUTATUA MGOGORO HUU - BALOZI SEIF


  • MGOGORO WA ARDHI KATI YA JWTZ, WANANCHI NGOMA BADO MBICHI
  • TUME YA TAKRIMA YASHINDWA KUTOA RIPOTI
Na: Mwinyimvua Nzukwi, Zanzibar.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeeleza kuwa inakusudia kutoa uamuzi wa moja kwa moja katika kutafuta suluhu juu ya mgogoro wa ardhi uliopo kati ya Wananchi wa Vijiji vya Fuoni, Maungani , Kombeni na Diiman kwa upande mmoja na Kambi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kambi ya Kisaka saka wilaya ya magharibi, unguja.

Kauli hiyo imetolewa na makamo wa pili wa rais wa Zanzibar, Balozi Seif Aili Iddi alipokuwa akizungumza na wananchi wa Maeneo hayo katika Kituo cha Afya cha Fuoni Kibondeni baada ya Tume aliyoiunda mwezi Julai mwaka huu kushindwa kuwasilishwa ripoti yake tokea mwishoni mwa mwezi Agosti.

Balozi Iddi aliwataka Wananchi hao kuendelea kuwa na subra wakati Serikali inalitafakari suala hilo kwa ajili ya kulipatia ufumbuzi wa kudumu utakaoleta afueni kwa pande zote mbili.

Aidha aliekleza kusikitishwa kwake kwa kutotekelezwa kwa maagizo aliyoyatowa katika Kikao cha pamoja kati ya pande mbili za mzozo huo mnamo  Julai 7 mwaka huu ambapo mbali na kuunda kamati ya kuchunguza na kupendekeza hatua za kutatua mgogoro huo pia aliuagiza Uongozi wa Kambi ya Kisakasaka kulirejesha Bambo waliloliondoa mahali walipokubaliana na Wananchi katika mazungumzo ya awali.
“ Hakukuwa na haja ya kutoa maamuzi ya haraka kuhusiana na Mgogoro huo, ndio maana nikaunda Tume hiyo lakini cha kusikitisha hadi sasa sijaletewa ripoti hiyo kama nilivyoagiza kuletewa mwishoni mwa Mwezi wa Agosti mwaka huu.” Aliswema Balozi Seif.

Alieleza kuwa Serikali isingependa kuona Jeshi lililoundwa kwa ajili ya kutumikia Jamii linaendelea kuwa na mifarakano na Wananchi katika utekelezaji wa majukumu yake.
Makamu huyo wa Rais wa Zanzibar ambaye ndiye mtendaji na msimamizi mkuu wa shughului za serikali ya Zanzibar aliwaahidi Wananachi hao kwamba mambo yote waliyokubaliana na Uongozi wa Jeshi yanatekelezwa kikamilifu huku ufumbuzi wa kudumu ukitafutwa.
“Nipeni muda, hivi sasa nimetingwa na shughuli za Baraza la Wawakilishi na nadhani mnaelewa kuwa mimi ndie msimamizi mkuu wa kazi za serikali shughuli za Serikali …….. nikimaliza tu jibu la suala hili nitajuka kulitoa hapa hapa”. Alifafanua Balozi Seif.
Mapema Mwenyekiti wa Kamati ya Wananchi hao Khamis Vuai Makame, aliiomba Serikali kuyachukulia hatua za haraka mambo waliyokubaliana na uongozi wa jeshi hilo ili kutatua mgogoro huo na kuepusha madhara yanayoweza kutokea.
Khamis alisema bado wataendelea kulalamikia kutokuwepo kwa uhalali wa ramani ya kambi hiyo wakati wananchi hao ndio wenye hati ya umiliki wa ardhi hiyo kwa mujibu wa sheria na taratibu za mamlaka inayohusika na ardhi hapa nchini walizopatiwa miaka kadhaa iliyopita.
Mwenyekiti huyo alimuelezea Balozi Seif kuwa jeshi hilo limeingia katika mgogoro huo kwa utashi wa baadhi ya watu maslahi yao na si maslahi ya jeshi au jamii inayolizunguka kambi hiyo.
Khamis alisema wanaamini kuwa utatuzi wa mgogoro huo utapatikana kwa kutumia vikao halali na kumpongeza Balozi Seif kwa hatua anazoendelea kuchukuwa katika kutafuta ufumbuzi wa mgogoro huo toka ulipozuka.
“Hapa hapana tatizo kubwa kama tutatumia vikao na kulizungumza kwani mwisho wa yote naamini suluhu itapatikana ”, alisema mwenyekiti huyo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliunda tume ya kuufuatilia Mgogoro huo wa ardhi kati ya JWTZ  kambi ya Kisakasaka na wananchi wanayoizunguuka kambi hiyo Julai mwaka huu chini ya uenyekiti wa Mkuu wa Wilaya ya Magharibi, tume ambayo imeshindwa kuwasilisha ripoti yake katika muda uliopangwa kama iliyoagizwa. .
Mgogoro huo umezuka baada ya wananchi wa vijiji hivyo kulalamikia ramani mpya ya JWTZ inayoonesha maeneo hayo kuwa ni sehemu ya jeshi hilo kambi ya Kisakasaka huku wananchi hao wakiwa na hati halali za umiliki jambo linalodaiwa ni utashi wa baadhi ya watu kwa maslahi yao na si ya taasisi hiyo, madai ambayo yanapingwa na viongozi wa jeshi.
 
551.jpg569.jpgBaadhi ya wananchi wa vijiji vya Fuoni, Maungani , Kombeni na Dimani Wilaya ya Magharibi, Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja wakimsikiliza Makamo wa pili wa Rais wa Zanzibar (hayupo pichani) katika mkutano ulioandaliwa kwa lengo la kutafuta suluhu ya mgogoro wa ardhi kati ya wananchi wa vijiji hivyo na JWTZ kambi ya Kisakasaka.

Balozi Seif akisisitiza jambo kwa wananchi wa vijiji vya Fuoni, Maungani, Kombeni na Dimani Wilaya ya Magharibi, Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja katika mkutano wa kutafuta suluhu ya mgogoro wa ardhi kati ya wananchi wa vijiji hivyo na JWTZ kambi ya Kisakasaka. (Picha na OMKPR)