NA MWINYIMVUA NZUKWI, ZANZIBAR
WAJUMBE wa mkutano mkuu wa klabu ya Malindi inayoshiriki ligi kuu ya Zanzibar wamemchagua Mohammed Abdallah Mohammed ‘Aljabri’ kuwa Mwenyekiti wa klabu hiyo kwa kipindi cha miaka minne ijayo.
Uchaguzi wa viongozi uliofanyika Jumapili Septemba 9, 2018 katika ukumbi wa zamani wa sinema ya Empire Mkunazini, Mwenyekiti huyo aliyebaki peke yake baada ya mgombea mwenzake katika nafasi hiyo Jaffar Hussein Babu ‘Jeff’ kuondoa jina lake, alipata kura 100 kati ya 101 zilizopigwa baada ya kura moja kuharibika.
Akitangaza matokeo Msimamizi wa uchaguzi huo, Katibu Msaidizi wa chama cha soka (ZFA) wilaya ya Mjini Ali Abdullah Mohammed pia alimtangaza ‘Jeff’ kuwa mshindi wa nafasi ya Makamo Mwenyekiti baada ya kupata kura 92 na kumshinda Ramadhan Haji aliyepata kura 5 kati ya kura 100 zilizopigwa na kura 3 ziliharibika.
Katika nafasi ya katibu mkuu wa klabu, Mohammed Masoud aliyegombea peke yake nafasi hiyo alitetea nafasi yake kwa kujinyakulia asilimia 100 ya kura zote 101 zilizopigwa huku kocha Seif Mussa ‘Fagurson’ akichaguliwa kuwa Katibu msaidizi wa klabu hiyo kongwe katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Wajumbe wengine wanaounda Kamati tendaji ya klabu hiyo waliochaguliwa katika uchaguzi huo ni Abdullah Thabit ‘Dula Sunday’ (Katibu Mwenezi), Ali Majid (Mshika fedha), Rajab Said (Msaidizi Mshika Fedha), Amir Saleh (Mhasibu Mkuu) na wajumbe Nassir Seif, Mussa Ramadhan na Mahmoud Hamza.
Aidha mkutano huo umeidhinisha uteuzi wa wajumbe wa baraza la wazee na bodi ya wadhamini wa klabu hiyo na kumthibitisha kiongozi wa muda mrefu wa klabu hiyo Howingkao Hojofat kuwa meneja mkuu wa klabu hiyo yenye mastakimu yake ndani ya Mji Mkongwe wa Zanzibar.
Wanaounda baraza la wazee litakalokuwa na kazi ya ushauri na usuluhishi wa migogoro ndani ya klabu hiyo ni Msadik Abdallah, Abdi Basha, Abdallah Mzee na Ali Mwinyi wakati bodi ya wadhamini inaundwa na mchezaji na kiongozi wa zamani wa klabu hiyo Zahor Salum, sheha wa zamani wa shehia ya Malindi Himid Omar, kiongozi wa zamani wa klabu hiyo Mzee Boti, Ramadhani Haji na mwanachama wa klabu hiyo aliegombea nafasi ya umakamu mwenyekiti katika uchaguzi huo Ali Rajab.
Akitoa shukrani kabla na baada ya kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti Mohammed Abdallah ‘Aljabri’ aliwataka wanachama wa klabu hiyo kuendeleza ushirikiano waliouonesha kabla na wakati wa mkutano huo na kufuata taratibu wakati wa kutekeleza masuala yanayohusiana na klabu yao.
Alisema iwapo mshikamano huo utaimarishwa kuna uwezekano mkubwa wa kufikiwa kwa malengo yaliyowekwa ya kurudisha hadhi ya timu hiyo kama ilivyokuwa katika miaka ya 80 wakati timu hiyo ilipofanikiwa kutwaa ubingwa wa Zanzibar na Tanzania kwa wakati mbali mbali.
Aidha aliahidi kuwa ataendelea kushirikiana na wanachama wote bila ya kujali hadhi au nafasi zao na kwamba ataendelea kusimamia mipango ya kuiendeleza timu hiyo.
Nae Makamu Mwenyekiti Jaffar Hussein ‘Jeff’ aliwashukuru wadau mbali mbali waliofanikisha kukamilia kwa mkutano huo hususan Mkuu wa mkoa wa Mjini Magharibi Ayoub Mohammed mahamoud ambae licha ya kushindwa kuhudhurui katika mkutano huo alitoa baraka za kufanyika ikiwa ni pamoja na ulinzi uliopelekea wanachama wa klabu hiyo kutumia haki yao ya kidemokrasia bila ya hiofu au ukiukwaji wa sheria.
Aliwaasa baadhi ya wanachama, washabiki na wapenzi wa klabu hiyo waliokuwa wakiupinga mkutano huo, kuacha kufanya hivyo na badala yake kuungana na uongozi uliochaguliwa ili kuhimiza maendeleo ya timu hiyo kongwe nchini.
Akiwasilisha mapendekezo ya Kamati hiyo mara baada ya kuchaguliwa Katibu Mkuu Mohammed Masoud alisema watahakikisha kuwa klabu hiyo inakuwa chachu ya maendeleo ya soka nchini na kuzitaka timu nyengine za mitaani kuimarisha timu zao ili kuongeza ushindani.
Alisema iwapo vilabu vikongwe kama Ujamaa, Small Simba, Miembeni na vyenginevyo vitaimarishwa vitaongeza hamasa ya watu wa Zanzibar kwenda viwanjani jambo ambalo litaongeza ushindani kama ilivyokuwa siku za nyuma.
Aidha katibu huyo alikipongeza chama cha soka Zanzibar (ZFA) kwa kurejesha mfumo wa ligi kuu ya pamoja kwa vilabu vya Pemba na Unguja jambo alilosema litasaidia kukuza umoja, ushindani na maelewano miongoni mwa klabu za ligi kuu.
Masoud ambae aliwahi kugombea nafasi ya urais wa Zanzibar na ZFA katika chaguzi zilizopita aliitaka Kamati teule ya chama hicho kukamilisha taratibu za kupatikana kwa viongozi wa chama hicho baada ya viiongozi wake wakuu kujiuzulu na kupelekea Mrajisi wa vyama na klabu za michezo Zanzibar kuunda Kamati ya muda inayosimamia maswala yote ya ZFA taifa.
Mkutano huo wa uchaguzi uliohudhuriwa na wanachama 101 kati ya 126 wa klabu, ulisimamiwa na Kamati maalum ya uchaguzi iliyoongozwa na Makamo Mwenyekiti wa chama cha soka (ZFA) wilaya ya Mjini Juma Mohammed ‘Kocha Juma’ pia wanachama walimtunukia uanachama wa heshima Mkuu wa mkoa wa Mjini Magharibi Ayoub Mohammed Mahmoud kutokana na mchango mkubwa wa kiongozi huyo katika michezo ndani na nje ya mkoa wake.
Wanachama wakipiga kura wakati wa zoezi la uchaguzi
Makamo Mwenyekiti wa ZFA Wilaya ya Mjini Juma Mohammed (kushoto) akibadilisha mawazo na Sheha wa shehia ya Mkunazini Fuad Abdallah (mwenye kofia) na Makamu Mwenyekiti wa klabu ya Malindi Jaffar Hussein 'Jeff' mara baada ya kuahirishwa mkutano mkuu wa uchaguzi wa klabu ya Malindi.
Wanachama wakipiga kura wakati wa zoezi la uchaguzi
Makamo Mwenyekiti wa ZFA Wilaya ya Mjini Juma Mohammed (kushoto) akibadilisha mawazo na Sheha wa shehia ya Mkunazini Fuad Abdallah (mwenye kofia) na Makamu Mwenyekiti wa klabu ya Malindi Jaffar Hussein 'Jeff' mara baada ya kuahirishwa mkutano mkuu wa uchaguzi wa klabu ya Malindi.
Wanachama wa klabu ya malindi wakiidhinisha mapendekezo ya kamati tendaji baada ya kuwateua wajumbe wa bodi ya wadhamini, baraza la wazee na meneja wa klabu hiyo mara baada ya kukamilika kwa uchaguzi wa viongozi.