Monday, November 26, 2012

AFUTA HATI YA UMILIKI WA ARDHI

BALOZI SEIF ASITISHA UMILIKI WA ARDHI
  • ATAKA MASLAHI YA WANYONGE YAZINGATIWE
  • ATAKA WANANCHI, MAMLAKA KUHESHIMU SHERIA
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imefuta hati ya umiliki wa eneo la shamba la serikali alilomilikishwa  Abeid Said Shankar liliopo katika kijiji cha Selemu wilaya ya magharibi Unguja.

Hatua hiyo imefikiwa kufuatia mgongano unaoendelea kujitokeza kati yake na wanakijiji wa eneo hilo ambao unaashiria uvunjifu wa amani baina ya mmiliki huyo na wanakijiji hao.
Aidha hatua hiyo pia inauzuia uongozi wa kituo cha kujiendeleza kielimu katika shehia hiyo kufanya shuguli yoyote ya ujenzi kwa kile kilichogundulika kuwa umiliki wa eneo hilo hauko kihalali katika vyombo vinavyosimamia masuala ya Ardhi.
Zuio hilo limetolewa hivi karibuni na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipofanya ziara fupi katika eneo hilo baada ya malalamiko ya muda mrefu ya wananchi wanaotumia maeneo hayo hao dhidi ya watu wanaodaiwa kumilikishwa mashamba hayo ambayo yalikuwa yakitumiwa na wizara ya kilimo.
Naibu katibu mkuu wa Wizara Kilimo na Maliasili Juma Ali Juma alimthibitishia Makamu wa Pili wa Rais kwamba mmoja ya watu wanaodai kumiliki eneo hilo Kassim Hassan hakuwa na nyaraka halali za eneo hilo ambalo ni lilikuwa ni milki ya Wizara ya Kilimo walilopewa baada ya mapinduzi ya ya Zanzibar ya 1964.
Juma alisema kutokana na maombi na umuhimu wa ardhi kwa mahitaji ya jamii, serikali imeiagiza wizara hiyo kupima eneo hilo ili baadae ligaiwe kwa wananchi kwa lengo la kuendeleza mahitaji ya kilimo na ujenzi kazi ambayo alisema kuwa imeshakamika.
Malalamiko ya wanachi yalikwenda sambamba na ule mzozo unaofukuta kati ya wakulima waliokuwa wakiendeleza shughuli za Kilimo katika shamba la Bwana Abeid Said wakidai kwamba mmiliki huyo alikuwa akionyesha dalili mbali mbali za kuhatarisha maisha ya mifugo yao pamoja na vipando vyao.
Akitoa ufafanuzi wa kadhia hiyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliiagiza wizara ya kilimo kumtafutia shamba jengine Bwana Abei Said Shankar ili kuepuka shari.
“Nakuagizeni Wizara ya Kilimo mhakikishe kuwa mnampatia eneo la kujenga nyumba mwananchi huyu masikini wa Mungu, mnampimia eneo la ujenzi Bwana Kassim kwa ajili ya kituo chao waweze kumiliki kihalali pamoja na kumpatia shamba jengine bwana Abeid" aliagiza balozi Iddi na kuongeza kuwa hatua hii itaondoa mvutano bila ya migongano miongoni mwa jamii.
“Kama mtu anashindwa kuishi na jamii inayomzunguka katika maeneo ya umiliki wa serikali mtu huyo inafaa aondoshwe na mamlaka zinazosimamia umiliki huo wa Serikali ili kuepuka shari”. Alisisitiza Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar.
Aidha Balozi Seif aliiasa jamii kuheshimu sheria na taratibu zilizowekwa ili kuepuka mizozo isiyokuwa na lazima na kutahadharisha kwamba ardhi itaendelea kuwa mali ya serikali na haitasita kuitumia kwa maslahi ya umma.
Eneo hilo la ekari sita lililopo katika kijiji cha Selemu, wilaya ya Magharibi, Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja kilichojaaliwa utajiri wa ardhi yenye  rutba lililomilikishwa kwa wizara ya kilimo na mali asili Zanzibar tokea mwaka 1964.

CHANZO: OMPR

No comments:

Post a Comment