Thursday, July 4, 2013

UJENZI BARABARA YA CHEJU WAANZA



WAKANDARASI WATAKIWA KUZINGATIA UTAALAMU, VIWANGO UJENZI WA BARABARA
 Na Mwinyimvua Nzukwi, Zanzibar
KAMPUNI na  wataalamu wa ujenzi wa barabara nchini wametakiwa kuhakikisha wanazingatia utaalam ili kuzifanya barabara hizo kuwa  katika kiwango kinachokubakila Kimataifa na zinadumu kwa muda mrefu.

Wito huo umetolewa na makamo wa pili wa Rais wa Zanzibar balozi seif ali iddi alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa barabara ya Jendele – Cheju - Kaebona yenye urefu wa kilomita 11.7 unaofanywa na kampuni ya D.P Shapriya +Co. Ltd ya Dara es salaam  ambayo ni miongoni mwa bara bara iliyomo katika mradi wa ujenzi wa bara bara tatu za vijijini katika kisiwa cha Unguja.

Alisema serikali inatambua kuwepo kwa wahandisi na wasimamizi wa ujenzi wa barabara wasio waaminifu ambao baadhi ya wakati hufanya kazi kwa kuondoa njiani miradi wanayopewa bila ya kuzingatia masharti na mikataba ya ujenzi.

Alisema hali hiyo huleta kero kwa wafadhili wa miradi na wakati mwengine kuyatia hasara mataifa yenye miradi hiyo ambayo yanayoshindwa kuihudumia na kuiendeleza miradi husika kutokana na ufinyuna ukuwaji mdogo wa uchumi wa nchi zao.

“Baadhi ya makandarasi wamekuwa na tabia ya kuondosha njiani kazi wanazopewa  tabia ambayo huwakera wafadhili na kwa upande mwengine kuyaongezea mzigo mataifa yenye kusaidiwa ufadhili wa miradi hiyo”, alisema Balozi Seif.

Akizungumzia suala la fidia kwa vipando na mali za wananchi walioathirika na miradi hiyo, Makamo huyo wa Rais aliiagiza Wizara ya Miundo Mbinu na Mawasiliano Zanzibar kufanya upembuzi yakinifu ili kuepukana na baadhi ya watu wajanja wenye tabia ya kujipandikiza katika madai ya fidia na kuwakosesha haki watu wanaohusika jambo ambalo amedai kuwa ni chanzo cha migogoro kati yao na serikali.

“Kuna tabia imekuwa ikijichomoza mara kwa mara wakati wa uanzishwaji wa miradi kama hii kwa baadhi ya watu wasiohusika kudai fidia katika maeneo mbali mbali nchini na kuitia hasara serikali kwa vile wanakuwa hawamo katika jabeti iliyokubalika kabla ya kuanza kwa mradi na kuisababishia hasara serikali na kupunguza kasi ya utekelezaji wa miradi hiyo hivyo ni vyema mkawa makini zaidi”, alisistiza.

Aidha Balozi Seif aliipongeza kampuni ya D.P Shapriya +Co. Ltd ya Dara es salaam inayonga barabara hiyo kwa hatua iliyofikia katika utekelezaji wa mradi huo licha ya kuchelewa kutokana na mvua za masika jambo ambalo linatia moyo ya kuweza kukamilika kwa mradi huo katika muda uliopangwa.

Mapema Msimamizi wa Mradi huo Wizara ya Miundo Mbinu na Mawasiliano Zanzibar, Mhandisi Suleiman Abdulla Ali alisema serikali kupitia wizara husika tayari imeshawalipa fidia wananchi wote waliohusika katika mradi huo na kwamba tathmini  imeshafanywa kwa ajili ya waathiria wa mradi wa barabara ya Koani – Jumbi yenye urefu wa Kilo Mita 6.3 na  wizara husika italipa fidia mara tuu fedha zitakapopatikana.

Aidha alifahamisha kuwa kutokana na ufinyu wa bajeti ya kazi za ujenzi wa barabara hizo umepelekea kutolewa kwenye mradi huo ujenzi wa barabara ya Kizimbani hadi Kiboje yenye urefu wa kilomita 7.

Akitoa maelezo ya utekelezaji wa miradi hiyo Mshauri muelekezi wa Mradi huo kutoka kampuni ya Newtech Consulting Group ya Sudan, El-Tayeb Rabah Mohammed alisema kuwa mradi huo umepangwa kuchukuwa  miezi 17 hadi kukamilika kwake mnamo mwezi Mei mwakani.

El – Tayeb alimuhakikishia Balozi Seif kwamba ana matumaini ya kupatikana na kukamilika kwa ujenzi huo kwa  kiwango kizuri kitakachokidhi mahitaji yaliyokusidiwa kwa pande zote mbili.

Alieleza kuwa Wataalamu hao wa ujenzi wameshasafisha eneo la wastani wa kilomita 10 hadi sasa na kufanya kazi za kutengeneza tabaka la chini kwa wastani wa kilomita 2 kwa Bara bara ya Cheju –Jendele – Kaebona.

Mkataba kati wa utekelezaji wa mradi huo kati ya SMZ kupitia wzara ya miundombinu na mawasiliano na Kampuni ya DP Shapriya + Co Ltd ya Dar es salaam kwa kazi za utekelezaji mnamo tarehe 11 Septemba mwaka 2012na ujenzi wa kazi hiyo kuanza mapema Januari mwaka huu umegharamiwa na Benki ya Maendeleo ya Kiislamu (BADEA) kwa kushirikiana na SMZ ambapo zaidi cha shilingi za kitanzania bilioni 14.8 zitatumika .

Kukamilika kwa barabara hizo inatarajiwa kupunguza kwa kiasi tatizo la usafiri kwa wakulima wa zao la mpunga katika bonde la Cheju ambao walikuwa wakipata usumbufu kwa miaka kadhaa sasa wakati wa kusafirisha mazao na kuwaunganisha wanachi wa maeneo ya wilaya ya kati na kusini Unguja kwa unafuu.