"TUSHIRIKIANE KUSAIDIA SEKTA YA ELIMU KWA MAENDELEO YA TAIFA" - BAUCHA
Wadau wa elimu nchini wametakiwa
kutoa mashirikiano kwa walimu ili kuinua kiwango cha ufaulu wa wanafunzi na
ubora wa elimu inayotolewa katika skuli za serikali na binafsi
nchini.
Akizungumza katika mahafali ya pili
ya wanafunzi wa skuli ya Fuoni Sekondari waliomaliza kidatu cha nne Mkurugenzi
wa biashara wa kampuni ya Zantel Moh’d Khamis Baucha alisema mashirikiano kati
ya pande hizo ndio njia pekee itakayoongeza kiwango cha kufaulu na kuleta
ufanisi kwa jamii nzima.
Alisema kuwa katika zama za sayansi
na teknolojia ni lazima kuwepo na njia mbadala zitakaziowezesha wanafunzi
kunufaika na elimu wanayoipata wakiwa skuli kama njia mojawapo ya kujikomboa na
umasikini na kujitegemea pindi wanapomaliza masomo.
“Zama zimebadilika sana, ipo haja kwa
wanafunzi, walimu, wazazi na wadau wengine kushirikiana na kuhakikisha
tunazingatia katika upatikanaji wa elimu bora na sio bora elimu tu”,
alisema.
Aidha aliwaasa wahitimu hao
kuhakikisha wanayatumia vyema mafunzo waliyoyapata wakati wanasubiri matokeo na
kuwa raia wema huku wakiwasaidia wanafunzi wanaoendelea situu kujua kusoma bali
pia kufahamu wanachosomeshwa.
“Wakati mkiondoka skuli ni vyema
mkayatumia masomo mliyoyapata na kuwasaidia wenzenu waliobaki kujua kusoma,
kufahamu wanachosomeshwa, na kuhesabu kama njia ya kujijengea uwezo wenu na wao
katika kufikiri na kupambanuua mambo,….. mkifikia hatua hiyo mtakuwa mmeelimika
kikamilifu”, aliongeza Meneja huyo.
Aidha aliahdi kuwa kampuni yake
italishughulikia tatizo la ukosefu wa vifaa vya maabara na kompyuta
linaloikabili skuli hiyo na kuwataka wadau wengine kujitokeza kusaidiaskuli hiyo
hususan uchakavu wa majengo ili kupata mazingira mazuri ya kujifunzia jambo
ambalo amedai lina mchango mkubwa katika upatikanaji wa elimu bora.
“Nimesikia kilio chenu, kwa kuanzia
nimekuja na ‘modem’ za ‘internet’ kwa ajili ya mtandao na nitakaa na wenzangu
katika kampuni kuangalia ni namna gani tunaweza kusaidia hasa masuala ya vifaa
vya maabara na kompyuta ili kuendana na wakati uliopo”, alisema Meneja
Baucha.
Akisoma risala ya walimu na
wanafunzi wa skuli hiyo, Mwalimu Sudi Mchenga alizitaja changamoto
za uhaba wa walimu hasa katika masomo ya sayansi, uchakavu wa majengo, uhaba wa
samani, vifaa vya maabara na kompyuta kuwa ni miongoni mwa mambo yanayokwaza
malengo yao ya kufaulisha, wanafunzi wengi zaidi kila mwaka.
“Pamoja na kupiga hatua za mafanikio
mwaka hadi mwaka, bado uchakavu wa majengo, samani na nyenzo nyengine za
kujifunzia na kufundishia zimekuwa ni matatizo yanayotukwaza kufikia malengo
yetu, hivyo tunawaomba wadau wote kutusaidia ili tutimize wajibu wetu
kikamilifu”, alisema Maalim Mchenga.
Mapema akimkaribisha mgeni rasmi
Kaimu Mkurugenzi wa idara ya elimu sekondari Zanzibar, Maalim Ali
Hamdani aliwataka wanafunzi wanaofaulu kuendelea na elimu ya juu nchini kufanya
maombi mapema katika bodi ya mikopo ya elimu ya juu ili kuepusha malalamiko ya
kunyimwa mikopo.
“Idadi ya wanafunzi wanaohitaji
mikopo imekuwa ikiongezeka kila mwaka hivyo basi wale watakaobahatika kuendelea
na masomo hasa ya elimu ya juu ni vyema wakafanya maombi mapema kabla bajeti
haijapitishwa ili kuweza kutoa mikopo kwa wanafunzi wengi zaidi”, alisema afisa
huyo akijibu ombi la kupatiwa mikopo kwa walimu wanaokwenda kusoma.
Aidha aliwataka walimu wanaopata
nafasi ya kwenda kusoma kurudi maskulini mwao ili kupunguza uhaba wa walimu
ambao amedai unachangiwa na baadhi yao kutorudi katika vituo vyao wanapomaliza
masomo na wengine kubadilisha kada kwa kisingizio cha maslahi duni jambo ambalo
alisema linachangia kupunguza idadi ya walimu.
Skuli ya Fuoni ni miongoni mwa skuli
kongwe zilizopo Zanzibar iliyoanzishwa mwaka 1952 ikitoa elimu ya awali ,msingi
ha kati kabla ya kubadilishwa kuwa ya sekondari, katika mahafali hayo
wanafunzi 129 wanaume 58 na wanawake 71 walikabidhiwa vyeti vya
kumalizia masomo idadi ambayo ni ziada ya wanafunzi 16 ya wanafunzi 113
waliomaliza mwaka jana ambapo kati yao wanafunzi 11, wanawake 7 na
wanaume 4 walifaulu na kuendelea na kidato cha tano katika skuli mbali
mbali.
No comments:
Post a Comment