BALOZI SEIF ASITISHA UMILIKI WA ARDHI
- ATAKA MASLAHI YA WANYONGE YAZINGATIWE
- ATAKA WANANCHI, MAMLAKA KUHESHIMU SHERIA
Hatua hiyo imefikiwa kufuatia mgongano unaoendelea kujitokeza kati yake na wanakijiji
wa eneo hilo ambao unaashiria uvunjifu wa amani
baina ya mmiliki huyo na wanakijiji hao.
Aidha hatua hiyo pia inauzuia uongozi wa kituo cha kujiendeleza kielimu katika shehia hiyo kufanya shuguli
yoyote ya ujenzi kwa kile kilichogundulika kuwa umiliki wa eneo hilo hauko kihalali katika
vyombo vinavyosimamia masuala ya Ardhi.
Zuio hilo limetolewa hivi karibuni na Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipofanya
ziara fupi katika eneo hilo baada ya malalamiko ya muda mrefu ya wananchi wanaotumia maeneo hayo hao dhidi ya watu wanaodaiwa kumilikishwa mashamba hayo ambayo yalikuwa yakitumiwa na wizara ya kilimo.
Naibu katibu mkuu wa Wizara Kilimo na
Maliasili Juma Ali Juma alimthibitishia Makamu wa Pili wa Rais kwamba mmoja ya watu wanaodai kumiliki eneo hilo Kassim Hassan hakuwa na nyaraka halali za eneo hilo
ambalo ni lilikuwa ni milki ya Wizara ya Kilimo walilopewa baada ya mapinduzi ya ya Zanzibar ya 1964.
Juma alisema kutokana na maombi
na umuhimu wa ardhi kwa mahitaji ya jamii, serikali imeiagiza wizara hiyo
kupima eneo hilo ili baadae ligaiwe kwa wananchi kwa
lengo la kuendeleza mahitaji ya kilimo na ujenzi kazi ambayo alisema kuwa imeshakamika.
Malalamiko ya wanachi yalikwenda sambamba
na ule mzozo unaofukuta kati ya wakulima waliokuwa wakiendeleza shughuli za Kilimo
katika shamba la Bwana Abeid Said wakidai kwamba mmiliki huyo alikuwa akionyesha
dalili mbali mbali za kuhatarisha maisha ya mifugo
yao pamoja na vipando vyao.
Akitoa ufafanuzi wa kadhia hiyo
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliiagiza wizara ya kilimo kumtafutia shamba jengine Bwana Abei Said Shankar ili kuepuka shari.
“Nakuagizeni Wizara ya Kilimo
mhakikishe kuwa mnampatia eneo la kujenga nyumba mwananchi huyu masikini wa Mungu, mnampimia eneo la ujenzi Bwana Kassim kwa ajili ya kituo chao
waweze kumiliki kihalali pamoja na kumpatia shamba jengine bwana Abeid" aliagiza balozi Iddi na kuongeza kuwa hatua
hii itaondoa mvutano bila ya
migongano miongoni mwa jamii.
“Kama mtu anashindwa kuishi na jamii
inayomzunguka katika maeneo ya umiliki wa serikali mtu huyo inafaa aondoshwe na
mamlaka zinazosimamia umiliki huo wa Serikali ili kuepuka shari”. Alisisitiza
Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar.
Aidha Balozi Seif aliiasa jamii kuheshimu sheria na taratibu zilizowekwa ili kuepuka mizozo
isiyokuwa na lazima na kutahadharisha kwamba ardhi itaendelea kuwa
mali ya serikali na haitasita kuitumia kwa maslahi ya umma.
Eneo hilo la ekari sita lililopo
katika kijiji cha Selemu, wilaya ya Magharibi, Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja kilichojaaliwa utajiri wa ardhi yenye rutba lililomilikishwa kwa wizara ya kilimo na mali asili Zanzibar tokea mwaka
1964.
CHANZO: OMPR
CHANZO: OMPR