SERIKALI ITWASAKA WALIOMUUA ASKOFU MUSHI
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imewataka wananchi wa imani zote kutoa ushirikiano kwa vyombo vya ulinzi na usalama ili kuviwezesha kufanya uchunguzi wa kifo cha Askofu Varistus Gabriel Mushi kilichotokea jana asubuhi.
Akitoa taarifa ya serikali, Waziri wa nchi Afisi ya Makamo wa Kwanza wa Rais Muhammed Aboud Muhammed ofisini kwake Vuga, alisema serikali italiwezehsa jeshi la polisi na vyombo vyengine ulinzi na usalama ili kubaini chanzo cha matukio hayo yanayoonekana kushamiri siku hadi siku.
Abuod alisema katika wakati huu wa majonzi wananchi na waumini wa dini zote wanapaswa kutulia na kuviacha vyombo hivyo vifanye kazi zao kwa utaalamu na mafunzo yao.
"Serikali haiwezi kuacha matukio kama haya yaendelee kwani yanaibua hofu kwa jamii na kuathiri jina la nchi yetu na uchumi wetu kwa ujumla", alisema Aboud.
Aliongeza kuwa serikali ya Zanzibar inaunga mkono tamko lililotolewa na serikali ya muungano linalovitaka vyombo vya usalama vya ndani na nje ya nchi ili kubaini chanzo cha matukio hayo na kama kuna watu au kundi lolote linalofadhili matukio hayo.
Kuhusu suala la uwezekano wa kuzagaa kwa silaha, Aboud alisema hali hiyo inatokana na mazingira ya Zanzibar yanayowezesha kuwepo kwa bandari zisizo rasmi (bubu) jambo ambalo serikali inalifanyia kazi na kuwataka wananchi kutoa taarifa juu ya watu wanaowatilia shaka kuhusika na vitendo vya uhalifu.
Aidha aliwataka viongozi wa dini kuendelea kuhubiri amani , utulivu na kuvumiliana miongoni mwa waumini wao ili kuiepusha nchi na matatizo ya kijamii na kiuchumi.
"Kwa miaka mingi watu wa dini tofauti wamekuwa wakiishi pamoja kwa mafahamiano na mshikamano hivyo bado kila mmoja wetu anapaswa kutimiza wajibu wake ili kuendeleza mshikamano uliodumu kwa muda mrefu", aliongeza Aboud.
Askofu Mushi aliuawa kwa kupigwa risasi tatu kichwani asubuhi ya Jumapili wakati akienda kuendesha misa ya Jumapili katika kanisa la mtakatifu Theressa liliopo Beit el Ras nje kidogo ya mji wa Zanzibar ambalo ni sehemu ya kanisa Katholiki jimbo kuu la Zanzibar.
No comments:
Post a Comment