Tuesday, September 16, 2014

CHEUPE MJUMBE MPY A ZFA

Chama cha waandishi wa habari za michezo Zanzibar ZAWA kimempongeza  raisi wa ZFA kwa  kuteua mtu mwenye taaluma ya habari kuingia katika kamati tendaji ya chama hicho kukamilisha nafasi alizopewa rais huyo na katiba ya chama chake.

Akizungumzia uteuzi huo Naibu Katibu Mkuu wa ZASWA, Salum Vuai Issa alisema hatua hiyo itasaidia kupatikana kwa ufanisi hususan taarifa za masuala mbali mbali za kiutendaji wa chama hicho na kupunguza urasimu wa upatikanaji wake.

Vuai alisema hatua ya Rais huyo kuona umuhimu wa kamati hiyo kuwa na mjumbe mwenye taaluma ya uandishi wa habari kutasaidia katika kufanikisha shughuli mbali mbali za kiutendaji katika chama hicho na kudhihirisha kukubali kubadilika kwa chama hicho ingawa muda uliobakia kumalizika kwa uhai wa kamati hiyo ni mdogo.

“Ni vyema kuwa ameona umuhimu wa kumuingiza mtu kama 'Cheupe' katika kamati yake, naamini atasaidia sana ingawa muda uliobakia sio mkubwa hadi kufikia uchaguzi mkuu mwisho wa mwaka huu”, alisema Vuai na kuongeza kuwa kwa kumtaka mteule huyo kuzingatia ueledi alionao ili kuleta mabadiliko yatakayosaidia chama hicho badala ya kujali maslahi binafsi.

“Tunamfahamu kwa uwajibikaji na kujituma kwake ndani ya chama chetu hivyo ni vyema akasimamia misingi hiyo ili kukisaidia chama hicho katika kufikia malengo yake kwa ufanisi unaotakiwa”, alisisitiza Naibu Katibu huyo.

Mwishoni mwa wiki iliyopita Rais wa ZFA Ravia Idarous Faina alimteua mtangazaji kituo cha redio ya Zenji FM, Ali Bakari ‘Cheupe’ kuwa mjumbe wa kamati tendaji ya chama hicho kuanzia Septemba 12. 

Rais huyo alifanya uteuzi kwa mujibu wa kifungu cha 31(1) L ambacho kinamruhusu kiongozi huyo kuteua wajumbe wanne kuunda kamati tendaji kuungana na wajumbe wengine ambao hupatikana kwa kuchaguliwa.

Aidha aifungu cha 31(2) iv cha katiba ya ZFA  kinafafanua kuwa katika uteuzi wa nafasi hizo ni lazima kuwe na uwiano sawa wa wajumbe kutoka pande zote mbili za visiwa vya Unguja na Pemba ambapo toka kuingia madarakani mwezi juni 2013 Rais huyo aliwateuwa Omar Ahmed na Nassor Ali kutoka Pemba na Hashim Salum wa Unguja.

Ali Bakari ‘Cheupe’ (37) ambae pia ni mjumbe wa kamati ya utendaji wa ZASWA kwa nyakati tofauti alikuwa akitumika katika kazi mbali mbali za ZFA kama vile utoaji na usambazaji wa taarifa za chama hicho kwa waandishi wahabari hasa pale alipoambatana na timu ya taifa ya Zanzibar katika mashindano ya chalenji nchini Uganda mwaka 2012 ambapo pia hivi karibuni aliteuliwa kuwa mjumbe wa kamati ya mashindano ya majimbo Taifa yanayosimamiwa na chama hicho.

Monday, September 15, 2014

ZINGATIENI MASHARTI YA MIKATABA YEYU - ATTAI


Manahodha wa vilabu vinavyoshiriki ligi kuu ya Zanzibar na ligi daraja la kwanza taifa wametakiwa kuwaelimisha wachezaji wao juu ya umuhimu wa kuzingatia masharti ya mikataba wanayoingia na vilabu vyao ili kuepusha migogoro kati yao.

Mjumbe wa kamati tendaji ya chama cha soka Zanzibar ZFA Masoud Attai, alitoa rai hiyo hivi karibuni alipokua akiwasilisha mada juu ya umuhimu wa mikataba ya wachezaji wakati wa usajili katika semina iliyowajumuisha manahodha wa vilabu vinavyoshiriki ligi kuu ya  Zanzibar na daraja la kwanza Taifa.

Aliwataka manahodha hao kuanzisha utaratibu utakaowawezesha wachezaji wenzao kuelewa masharti na matakwa ya mikataba wanayoingia na vilabu vyao ili kuepuka kuingia katika migogoro ambayo kwa kiasi kikubwa inachangia kushusha viwango vyao vya uchezaji.

Alisema wachezaji wengi wa soka visiwani humo wamekuwa wakiingia mikataba kiholela na wakati mwengine bila ya kuisoma mikataba ili kujua maudhui na matakwa ya mkataba husika jambo linalopelekea usumbufu kwa chama chake kila msimu mpya wa usajili unapoanza.

“Mara nyingi wachezaji wakishakabidhiwa fedha huwa hawana haja ya kujua matakwa mengine yaliyomo ndani ya mkataba wake, jambo hili ni la hatari na mara nyingi huwa ndio chanzo cha migogoro inayofikishwa FA na kusababisha mahusiano mabaya baina ya mchezaji na timu au viongozi wa timu zao”, alisema Maalim Attai.

Aliongeza kuwa ili mkataba uwe halali ni lazima pande zote mbili ziridhie baada ya kukubaliana hivyo ni vyema wachezaji wakaisoma mikataba yao kikamilifu na kuelewa matakwa ya mikataba hiyo hususan ukomo wa mikataba hiyo ili kumlinda mchezaji pindi anapotaka kuhamia katika timu nyengine.

“Kuna wakati mchezaji  anajua kuwa mkataba wake umeisha kama walivyokubaliana lakini kwa kuwa hakuangalia maandishi anajikuta bado ana mkataba unaomfanya aendelee kubakia na timu yake ya zamani akiwa hana furaha”, alisema mjumbe huyo ambae pia ni mjumbe wa kamati ya ufundi ya Baraza la vyama vya soka la Afrika Mashariki, CECAFA.

Akifungua semina hiyo mjumbe wa kuteuliwa na rais ktaika kamati hiyo Hashim Salum aliwaasa manahodha hao kutambua nafasi zao na umuhimu wao katika timu ili waweze kuwaunganisha wachezaji wenzao na viongozi kama njia moja wapo ya kudumisha  nidhamu ndani na n je ya uwanja.

“Mkitambua nafasi na umuhimu wenu katika vilabu vyenu mtaumisha amani na maelewano ndani nan je ya vilabu vyenu na kama mtadumu na hilo bila shaka viwango vya uchezaji wenu vitakua na kuleta mafanikio ya timu zenu”, alisema.

Naye daktari wa timu ya taifa za Zanzibar ‘Zanzibar Herois’ Mohammed Said ambaye alitoa mada juu ya umuhimu wa tiba kwa wachezaji, aliwataka wachezaji kuchukua tahadhari wakati wote ili kuimarisha viwango vyao vya uchezaji na kutumikia vilabu vyao kwa muda mrefu zaidi.

“Utafiti unaonesha kuwa ‘injuries’ (majeraha) nyingi hutokea mazoezini na hii inatokana na kuwa wachezaji mara nyingi hupuuza na kuacha kuchukua tahadhari ikiwemo kuvaa vifaa vya kujikinga”, alisema Dk. Said.

Aliongeza kuwa ni vyema wachezaji na vilabu vya soka nchini kuwa na utaratibu wa kuchunguza afya za wachezaji wao kabla na wakati wa msimu ili kuwa na uhakika wa kujua utimamu wa mwili na akili za wachezaji ambalo ni jambo muhimu kwa walimu katika kuteua aina ya mafunzo kwa wachezaji.

Katika semina hiyo pia mada ya mahusiano kati ya wachezaji na vyombo vya habari iliwasilishwa na mjumbe wa kamati ya utendaji wa chama cha waandishi wa habari za michezo Zanzibar ZASWA, Ali Bakari ‘Cheupe’ ambaye aliwaasa manahodha hao kuwa na mahusiano mema na vyombo vya habari kama njia moja wapo ya kukuza soka la Zanzibar na kuwavutia wafadhili kudhamini michezo.

“Mkumbuke kua ‘media’ (vyombo vya habari) ni daraja muhimu katika kukuza michezo, hivyo kuna umuhimu kwenu kuwa na mahusiano mema wakati wote na katika mazingira yeyote kwani  kuna baadhi yenu mnakuwa wagumu kutoa ushirikiano hasa pale timu zenu zinapopoteza mechi”, alisisitiza Cheupe.

Semina hiyo ambayo ni mwendelezo wa maandalizi ya ligi kuu ya Zanzibar iiliyoaanza kutimua vumbi lake Septemba 15 ililenga katika kujenga uelewa na dhamana ya viongozi hao kwa wachezaji wenzao katika kuepusha mizozo kabla, wakati na baada ya mchezo kama njia mojawapo ya kukuza soka la Zanzibar.