Chama cha waandishi wa habari za michezo Zanzibar ZAWA kimempongeza raisi wa ZFA kwa kuteua mtu mwenye taaluma ya habari kuingia katika kamati tendaji ya chama hicho kukamilisha nafasi alizopewa rais huyo na katiba ya chama chake.
Akizungumzia uteuzi huo Naibu Katibu Mkuu wa ZASWA, Salum Vuai Issa alisema hatua hiyo itasaidia kupatikana kwa ufanisi hususan taarifa za masuala mbali mbali za kiutendaji wa chama hicho na kupunguza urasimu wa upatikanaji wake.
Vuai alisema hatua ya Rais huyo kuona umuhimu wa kamati hiyo kuwa na mjumbe mwenye taaluma ya uandishi wa habari kutasaidia katika kufanikisha shughuli mbali mbali za kiutendaji katika chama hicho na kudhihirisha kukubali kubadilika kwa chama hicho ingawa muda uliobakia kumalizika kwa uhai wa kamati hiyo ni mdogo.
“Ni vyema kuwa ameona umuhimu wa kumuingiza mtu kama 'Cheupe' katika kamati yake, naamini atasaidia sana ingawa muda uliobakia sio mkubwa hadi kufikia uchaguzi mkuu mwisho wa mwaka huu”, alisema Vuai na kuongeza kuwa kwa kumtaka mteule huyo kuzingatia ueledi alionao ili kuleta mabadiliko yatakayosaidia chama hicho badala ya kujali maslahi binafsi.
“Tunamfahamu kwa uwajibikaji na kujituma kwake ndani ya chama chetu hivyo ni vyema akasimamia misingi hiyo ili kukisaidia chama hicho katika kufikia malengo yake kwa ufanisi unaotakiwa”, alisisitiza Naibu Katibu huyo.
Mwishoni mwa wiki iliyopita Rais wa ZFA Ravia Idarous Faina alimteua mtangazaji kituo cha redio ya Zenji FM, Ali Bakari ‘Cheupe’ kuwa mjumbe wa kamati tendaji ya chama hicho kuanzia Septemba 12.
Rais huyo alifanya uteuzi kwa mujibu wa kifungu cha 31(1) L ambacho kinamruhusu kiongozi huyo kuteua wajumbe wanne kuunda kamati tendaji kuungana na wajumbe wengine ambao hupatikana kwa kuchaguliwa.
Aidha aifungu cha 31(2) iv cha katiba ya ZFA kinafafanua kuwa katika uteuzi wa nafasi hizo ni lazima kuwe na uwiano sawa wa wajumbe kutoka pande zote mbili za visiwa vya Unguja na Pemba ambapo toka kuingia madarakani mwezi juni 2013 Rais huyo aliwateuwa Omar Ahmed na Nassor Ali kutoka Pemba na Hashim Salum wa Unguja.
Ali Bakari ‘Cheupe’ (37) ambae pia ni mjumbe wa kamati ya utendaji wa ZASWA kwa nyakati tofauti alikuwa akitumika katika kazi mbali mbali za ZFA kama vile utoaji na usambazaji wa taarifa za chama hicho kwa waandishi wahabari hasa pale alipoambatana na timu ya taifa ya Zanzibar katika mashindano ya chalenji nchini Uganda mwaka 2012 ambapo pia hivi karibuni aliteuliwa kuwa mjumbe wa kamati ya mashindano ya majimbo Taifa yanayosimamiwa na chama hicho.